Showing posts with label nyakati. Show all posts
Showing posts with label nyakati. Show all posts

Saturday 24 February 2018


IKO WAPI TANGA ILE?




Tanga ya zamani zile, ya jagina Shaabani
Aliyesifika kule, na kote Uswahilini
Mbona kama izamile, haipo kwenye ramani
Iko wapi Tanga ile?

Tanga yake Jinamizi, Sheikih Ali Zakuwani
Ilo ikikaza uzi, kwa mambo yenye thamani
Imegota zake mbizi, nani wa kuiauni?
Iko wapi Tanga ile?

Tanga ya Mwalimu Pera, Pera bin Ridhiwani
Zama zake iling'ara, na kushika usukani
Doro leo yadorora, haitajwi midomoni
Iko wapi Tanga ile?

Tanga ya Sheikh Mdanzi, wa Hanasa muhisani
Iloenea mapenzi, na baraka tani tani
Ya sasa ni kama bunzi, makaziye jalalani
Iko wapi Tanga ile?

Tanga ya Mwinyihatibu, Mohamedi nambawani
Aloandika vitabu, vizuri vyenye maani
Mbali imejitanibu, haipo hatuioni
Iko wapi Tanga ile?

Tanga ya Sheikh Ghulamu, Mwabondo mtu makini
Aloifunza kaumu, ushairi pamwe dini
Umekwisha umuhimu, Tanga sasa Tanga duni
Iko wapi Tanga ile?

Tanga ya Sheikh Hemedi, Buhry wa Mnyanjani
Ilolea auladi, kwa kumcha Rahmani
Imeenda hairudi, imakeni hii shani
Iko wapi Tanga ile?

Tanga ya Sheikh Salimu, Kibao niambieni
Iko wapi waadhamu, nikaishufu kwa mboni
Nikajifunze nudhumu, nikiwamo Tanga ndani
Iko wapi Tanga ile?

Tanga ya Sheikh Saidi, Nuru aso mshindani
Ilopendwa ja waridi, au vile asumini
Hae! Imezama sudi, bahati si mara thani
Iko wapi Tanga ile?

Tanga yake Sheikh Ali, Hemedi mwanachuoni
Iliyotajika mbali, Ulaya na Arabuni
Leo imelala chali, waruka watu na nyuni
Iko wapi Tanga ile?

Tanga yake Mohamedi, Ali Buhry mwendani
Aliyekuwa stadi, na fasaha wa uneni
Ilo sasa si ya jadi, ya jadi i wapi kwani?
Iko wapi Tanga ile?

Tanga ya Sheikh Kigamba, gwiji la Chongoleani
Iliyotoa miamba, waloongoza safuni
Kwa umbuji walitamba, kilugha hata kifani
Iko wapi Tanga ile?

Tanga ya Sheikh Kihere, Kihere wa Vibambani
Ilotamba si kwa sare, ingiapo shindanoni
Hadi wakaona gere, kina fulani fulani
Iko wapi Tanga ile?

Tanga yake Abdalla, wa Baruwa Baruwani
Iliyokosa kulala, kwa kukirimu wageni
Watu wakanywa na kula, kindugu na kijirani
Iko wapi Tanga ile?

Tanga ya Mwalimu Mbega, yeye kwake ujombani
Wa kuiga wakaiga, kwa mazuri kusheheni
Tangu yahame mafiga, hakuna chungu jikoni
Iko wapi Tanga ile?

Tanga ya bin Matunga, Abdi alo rubani
Ilojaliwa malenga, mwambao huu wa Pwani
I wapi nende ienga, nikumbukie zamani
Iko wapi Tanga ile?

I wapi ile i wapi, Tanga ile nijuzeni
Imebadilika vipi, toka juu kuwa chini
Na warithiwe wa kupi, walipo nionesheni
Iko wapi Tanga ile?

Hassan R Hassan

Saturday 11 March 2017

Ofisi Ndogo ya Chama Cha Mapinduzi Patrice Lumumba Avenue

Nina hakika si wengi hata humo ndani ya CCM wamepata kusikia jina la Alexander Tobias. Hawajapata kuisikia jina hili kama vile walivyokuwa hawajapata kusikia majina ya wazalendo wengi walipigania uhuru wa Tanganyika. Tufatane katika kisa hiki utakisikia kisa cha Alexander Tobias vile alikisaliti chama cha TANU hata kabla hakijazaliwa.

Ilikuwa mwaka wa 1987 niko ofisi ya Mzee Germano Pacha katika jengo la Biashara ya Wazee Tabora nikiwa nimesindikizwa na wenyeji wangu wawili, ­­­­Ali Salum Mkangwa na Ilunga Hassan Kapungu. Ofisi hizi za wazee wa TANU zilikuwa takriban kila mkoa khasa sehemu za mijini.­ Kazi yao kubwa ilikuwa kushughulika katika maduka yao na bidhaa adimu kama vile mafuta ya kupikia, mchele, sukari na wakati mwingine vitu kama sabuni nk. Hizi zilikuwa ni zile nyakati za hali ngumu sana ya uchumi Tanzania kila kitu kiliadimika. Huyu Germano Pacha ni mmoja katika watu 17 waliounda pamoja na Mwalimu Nyerere chama cha TANU 1954. Nilikuwa niko katika utafiti wa historia ya TANU na Sheikh Abubakar Mwilima aliniambia kuwa ni muhimu nikamuhoji Mzee Germano Pacha kwani alikuwa anajua mengi katika historia ya uhuru wa Tanganyika. Hakuwa Sheikh Mwilima peke yake aliyenipa ushauri huu. Hassan Upeka aliyekuwa katika Idara ya Usalama ya TANU toka mwaka wa 1956 na yeye pia alinishauri na kutia mkazo kuwa ni lazima niende Tabora nikazungumze na Mzee Pacha. Alikuwa Mzee Germano Pacha ndiyo aliyonifahamisha kwa mara ya kwanza kufukuzwa kwa kiongozi katika TAA wakati wa harakati za kudai uhuru wa Tanganyika.

Mzee Pacha anasema katika mkutano wa  mwaka wa 1954 wa TAA mkutano ulioasisi TANU walimfukuza chama Alexander Tobias aliyekuwa Katibu Mtendaji wa TAA Makao Makuu New Street kwa kosa la usaliti. Alexander Tobias alichukua majalada ya TANU ya siri akawapa Waingereza kupitia idara yao ya ujasusi Special Branch. Inasemekana Waingereza walimuhonga fedha nyingi kwa kazi ile. Huyu Alexander Tobias alianza kazi pale New Street June 1953 wakati Mwalimu Nyerere anachukua uongozi wa TAA. Alexander Tobias alikuwa mfanyakazi wa kwanza kuajiriwa na TAA kama katibu wa kudumu pale Makao Makuu ya TAA. Uamuzi huu wa kuwa na sekretariati pale Makao Makuu ulifanyika Nansio baada ya mashauriano kati ya Abdul Sykes na Hamza Mwapachu wakati wanashauriana na wanafanya mipango ya kumtia Nyerere katika uongozi wa TANU kupitia uchaguzi wa TAA wa April 1953.

Alexander Tobias akaanza kazi June 1953 Nyerere akiwa Rais wa TAA na Abdul Sykes Makamo wa Rais na hapo inaaminika ndipo alipodakwa na Special Branch na akawa sasa anawapa siri za TAA na mwisho akawakabidhi majalada yenyewe. Ukipitia nyaraka za Sykes za mwaka wa 1953 hiki ndicho kipindi ambacho TAA walikuwa wako katika muendelezo wa mawasiliano na vyama vingine vya siasa nje ya mipaka ya Tanganyika. Nimesoma barua kadhaa katika nyaraka za Sykes ambazo Alexander Tobias alikuwa anaandika kwa niaba ya TAA kuiandikia serikali ya Kiingereza. Katika barua hizo ziliyonivutia sana ni zile ya kumuombea ruhusa Ally Sykes kama kiongozi wa TAA kusafiri kwenda Lusaka, Northern Rhodesia kuhudhuria mkutano wa Pan African Congress uliokuwa umeitishwa na Kenneth Kaunda akiwa kiongozi wa African National Congress. Mkutano huu ulikuwa ujumuishe vyama vya siasa vilivyokuwa Kusini ya Sahara kuzungumzia ukombozi wa nchi zao.

Ni wazi Alexander Tobias kwa nafasi yake katika kipindi kile cha mpito kuelekea kuunda TANU mwaka unaofuatia, alijua siri nyingi za chama na kwa kiasi kikubwa kwa usaliti wake aliwadhoofisha sana wazalendo wa TAA. Yale ambayo alifanya hakika ulikuwa ni usaliti mkubwa ambao usingeweza kustahamilika ila yeye kufukuzwa chama na hicho ndicho kilichofanyika siku ya kwanza tu katika mkutano wa TAA wa 1954. TANU isingeweza kuwa na wanachama wasaliti wa mfano wa Alexander Thobias.

Nimekileta kisa hiki baada ya kusoma katika mitandao ya kijamii kuwa  kimepita kimbunga ndani ya mkutano wa CCM Dodoma kinakumba wanachama waliokwenda kinyume na matakwa ya chama. Chanzo kikiwa Uchaguzi Mkuu wa 2015. Baadhi wamefukuzwa chama, wengine wamepewa karipio kali na wengine wamesamehewa.  Ni muhimu sana kwa chama kuijua historia yake. Bahati mbaya CCM haina historia ukiacha ile ya kuundwa kwake mwaka wa 1977. CCM haina moja walijualo katika historia ya TANU na ukombozi wa Tanganyika. Ndipo pale mwanzo nikasema tufuatane ili tumjue msaliti Alexander Tobias. Ikwa huijui jana yako huwezi ukaijua leo yako. Ndiyo leo hii bado tunapapasa kama vipofu katika mengi ambayo laiti tungeijua historia yetu bila shaka tungeijua na mila ya siasa zetu katika vyama vya siasa.

Alexander Tobias aifukuzwa chama kwa usaliti dhahiri. Swali la kujiuliza ni hili. Hawa waliofukuzwa CCM wamefukuzwa kwa usaliti? Kisa chao kinajulikana na kinatokana na uteuzi wa nafasi ya mgombea urais katika CCM. Tofauti zao zilitokea hapa. Yawezekana kweli msimamo wa kumuunga mkono huyu na kumpinga yule katika chama cha siasa ikawa kosa kiasi kupelekea watu kufukuzana chama? Ikitokea mathalan Katibu Mtendaji wa CCM akaiba majalada pale Makao Makuu Dodoma akayauza kwa wapinzani kama alivyofanya Alexander Tobias 1953, kosa hili ni wazi ni la mwanachama kufukuzwa chama kwani ni usaliti. Hili la wanachama kugongana katika uchaguzi wa nani apeperushe bendera kugombea urais wa nchi kupitia CCM hukumu yake inahitaji utulivu wa fikra. 

Nampa pole ndugu yangu Ramadhani Madabida kwa yaliyomfika.

Nakumbuka kama jana vile siku nilipomuona Madabida katika TV akizungumza pale Lumumba akajaribu kumnadi alyedhaniwa ni mgombea wake wa urais mbele ya vyombo vya habari. Mashaallah Madabida ni mzungumzaji hodari anaejua kuchagua maneno yake kwa uzito unaostahili. Madabida alizungumza vizuri sana hadi akafika kuinukuu Qur’an.  

Zamani sana nilimuazima Madabida kitabu kinaitwa, ‘’Khrushchev Remembers.’’ Katika kitabu hiki utamu unakuja pale Stalin alipokufa na pakawa na ombwe zito na ombwe hilo likazua mvutano kati Nikita Khrushchev na Lavrenty Beria. Kati ya kambi mbili hizi ipi ichukue uongozi? Mwisho wa kinyang’anyiro kile mshindi alipatikana na damu nyingi ilibaki sakafuni. 

Nawafananisha Madabida, Sophia Simba na wenzao waliofukuzwa pamoja na wale viongozi wa Chama Cha Kikomunisti cha Urusi waliopoteza maisha yao kwa kukimbilia kupanda jahazi lililokuwa liashapangiwa kuzamishwa. 

Naamini Madabida anakikumbuka kitabu hiki na yale yaliyomfika Beria na wenzake.

Friday 10 March 2017


Utangulizi

Nilipokuwa nasoma hizo beti za Kibatari nimepata faraja kuona kuwa Wazanzibari wamejifunza kujicheka na hii ni ishara nzuri. Huku kunashusha shinikizo la damu na huleta kicheko moyoni na kicheko huleta nuru katika uso. Nuru nayo huangaza pote.

Kibatari
Ewe wangu kibatari 
Utulize moyo wako 
Wewe bado u mzuri
Liondowe sononeko 
Umeme ulinighuri 
Kukusahau mwenzako 
Lakini sasa tayari
Takutafuta uliko

Na mie takugomeya
Nitoe kiburi chako
Wa Zeco ushazoweya
Huo ndo kiasi chako
Sasa kaka subiriya
TANESCO kiboko yako

Kibatari kibatari 
Sikama sijakikubali
Kimelea wasomi  mahiri 
Hata huwezi amini
Swali langu jamani 
Naomba mnijibuni
Wenye kosa ati ni walipaji kwani?

Suali hili ni kubwa
Liende mbele sambamba
Siku, wiki Na mwezimbamba
Mifuko yetu mwairamba

Tuelezwe kwa makini Kosa hili ni la naniiii?
Mbona mwababaisha sana huku mkifunga goli porini
Kibatari nakupenda Ila utaua jamaniiiii
  
Ndugu yenu kibatari
Sitaki chenu kiburi
Mlinitupa duhuri
Kwa hiyo yenu ghururi

Na nyingi zenu shururi
Niliweza zisubiri
Nikawa kama kaburi
Wala hamnidhukuri

Mlikuwa mwafikiri
Kuwa mimi ni faqiri
Wapi wenu uhodari
Na ule ujemedari

Nawapeni tahadhari
Kosa msilikariri
Munitundike vizuri
Kwenye uzi wa hariri



Tuesday 27 September 2016


 

Inawezekana kabisa kuwa hata kwa mbali au hata kwa ndoto mbaya ya kutisha ya jinamizi Mh. Ahmed Katani alipatapo kufikiri kuwa itatokea siku yeye atasoma tamko la uamuzi wa kumfukuza Prof. Ibrahim Haruna Lipumba kutoka CUF. Kama wasemavyo wanasiasa wenyewe, siku ni muda mrefu sana katika siasa. Mwandishi alikutana na Mh. Katani siku chache zilizopita alipofika nyumbani kwake akiongozana na Mh. Riziki Shahari Mbunge wa Mafia Viti Maalum wakitokea Bungeni Dodoma. Mazungumzo aliyofanya na Mwandishi kwa muda mfupi kama ungewasikiliza utadhani wawili hawa walikuwa wanajuana kwa muda mrefu. Msomaji anaweza kusoma utangulizi hapo chini wa ukurasa ambao Mwandishi aliandika kama ufunguzi wa matumaini kuwa iko siku Mh. Katani atakuja na historia ya maisha yake katika siasa za upinzani. Mh. Katani Ahmed Katani tayari keshaingia katika jedwali la historia kwa kusoma tamko la kumfukuza Prof. Lipumba kutoka CUF. 

Hivi yawezekana kwa Prof. Lipumba kumtazama usoni kijana wake Mh. Katani na akasema maneno aliyosema Julius Caesar, ''Et tu Brute?''

Msikikilize Mh. Katani hapo chini:






Utangulizi

Mheshimiwa Katani Mbunge wa Tandahimba ni kijana kwa maana halisi ya neno lenyewe. Katika muda mfupi wa kuzungumza nae kwa mara ya kwanza akisubiri kikombe cha kahawa alipopita nyumbani kwa Mwandishi, Mwandishi amegundua kuwa Mh. Katani amekalia kitabu ambacho ikiwa atakiandika kinatosha kuwa rejea ya kueleza adha za siasa za upinzani khasa wakati wa uchaguzi mkuu. Ukurasa huu umefunguliwa rasmi kumsubiri Mh. Katani afunguke kwa faida ya wapenda demokrasia...


Mheshimiwa Katani Mbunge wa Tandahimba

Monday 26 September 2016




Mahujaji nje ya Uwanja wa Julius Nyerere

Sheikh Abdallah Jabir




Katikati Prof. Mussa Assad kulia Ramadhani Sengati na Kushoto Masasi



Kulia ni Sheikh Salim Mtambo




Mtemi Ramadhani






Prof. Mohamed Bakari


Kulia Prof. Mohamed Bakari na Said Mohamed

Sunday 18 September 2016


Photo: Balozi Dr. Ramadhani Kitwana Dau safarini Malaysia kuwakilisha nchi
Dr. Ramadhani Kitwana Dau akiwa Uwanja wa Julius Kambarage Nyerere
Dar es Salaam akielekea Kuala Lumpur Malaysia jioni ya leo kwenda kushika
nafasiyake ya Ubalozi Nyuma akimsindikiza ni Mh. Mbaraka Dau Mbunge wa 
Mafia na aliyevaa kofia ni Bwana Lumba pia kutoka Mafia

Friday 16 September 2016


Hakika isiyo shaka
Yakini metajika
Ukumbini imefika
Ya Bwana Msifika

Humpa anomtaka
Fadhila zake Rabbuka
Hujawa bila mipaka
Zikatimu na kufika

Viumbe tuakitika
Amina Rabbi labeka
Alhamdu twatamka
Kukiri kufadhilika

Ewe kiumbe kumbuka
Mja ulositirika
Uendako hujafika
Mola wako hajkwita

Tenda ulowajibika
Jiepushe na pirika
Usije kughafilika
Dunia ikakupita

Sije pitwa na niaka
Ukaja vuka mipaka
Kaingiwa na mashaka
Ukabaki unajuta

Twakuomba wetu Mola
Ewe Subhana Taala
Ni wewe Jalla wa ‘Ala
Kwa sifazo tunakwita

Utukinge na balaa
Zilizo kwenye mitaa
Maovu yalozagaa 

Maneno huwa muhibu...
Yalonenwa na sahibu...
Uwe karibu...
Tungo zipate khatibu...



''Msomi Bwana Saidi..
Pokea mkono wa Idi..
Leo kwako mefaidi..
Kunifukiza kwa udi..

Zangu hini shukrani..
Hakika sikuamini..
Kujiona hadharani..
Humo mwako sebleni...''

Sunday 11 September 2016


Ewe Mola Mtukufu
Twakuomba ya Raufu
Waja wako dhaifu
Dua zetu zipokea


Ndugu zetu Isilamu
Walotimiza la muhimu
Nguzo ilio adhimu
Dua tunawaombea


Kufika kwao Makka
Hilo halina shaka
Uwezo wake Rabbuka 
Pasi na kutegemewa


Wageni wa sharafu
Katika miji mitukufu
Kwa Hijja na kutufu 
Makka na Madina pia

Zijaalie zao Hijja
Ziwe na nzuri tija
Pasiwe na hoja
Au kasoro kuingia

Wajaalie ya wepesi 
Pasiwe hata tetesi 
Kama nyeupe karatasi
Ibada zao zitoke doa

Uwape pia nguvu
Na akili Tulivu 
Waepushie maovu 
Manasiki kukamilia

Kwa salama na kheri 
Waja wako wazuri
Uwarejeshe safari
Hijja zao kutimia

Sala na salamu 
Zimfikie Hashimu 
Mtume Akiramu 
Muhammad Nabiyya


Mola wetu Rabbana 
Yailahi Subhana 
Dua Twaomba sana 
Mikono juu twainua

Khkitani

*Allahuma  Rabil Alamina
Twaitika Maalim  Duana
Tena twakushuru sana 
Kwa Dua kwa wetu Subhana
Azipoke ya Manani Maulana
Amina Yarabil Amina


Ahmed Al Brazil

Tuesday 6 September 2016

Fuatilia ukurasa huu In Shaallah tutaweka picha kila tuzipatapo za mahujaji kutoka Tanzania...

Photo
Kulia: Imam wa Msikiti wa Mtoro Sheikh Zuberi Yahya, Ustadh Mussa, Hafidh Mohamed
Ali Hassan (Kibabu), Sheikh Othman Maalim na Ustadh Hassan
(Picha kwa hisani ya Sheikh Zuberi Yahya)

Photo
Photo
Sala ya Ijumaa Makka

Photo

Saturday 13 August 2016

Maalim Seif akizungumza na Mwandishi (haonekani kwenye picha) nyumbani kwake
Dar es Salaam

Mwandishi akimkabidhi Maalim Seif  kitabu cha Kumbukumbu za Ali  Muhsin
Barwani ''Conflict and Harmony in Zanzibar.''

Kumtembelea Maalim Seif nyumbani kwake ni mfano Waingereza wangesema ‘’a walk in the park,’’ Kiswahili chake labda mtu ungesema unatoka chumbani kw.ako unakuja sebuleni yaani ni wepesi usiomithilika. Maalim nimefahamiananae kwa mara ya kwanza 1992 nilionananae Starlight Hotel Titi Street, Dar es Salaam. Hizi zilikuwa siku za mwanzo za siasa za vyama vingi. Miaka mingi imepita na hapa katikati tukionana kwa mbali sana na kwa muda mfupi mfupi ile ya kupeana salaam, Waswahili wanausemi, ‘’salaam ya Mungu,’’ ikiwa na maana mnasalimiana kisha mnapitana kila mtu na hamsini zake. Lakini namini Maalim akinisoma na wakati mwingine akinisikia katika vyombo vya habari, pia wakati mwingine akipata salaam zangu kupitia jamaa na marafiki. Lakini mimi Maalim nimenfuatilia kwa karibu na nimempiga picha nyingi sana kwa kiasi ya miaka ishirini na zaidi. 

Leo nimepata bahati ya kumfikia nyumbani kwake Sharif Shamba nje na mbali na matarumbeta na shamrashamra za mikutano na mengineyo. Ilikuwa starehe tukinywa kahawa na kucheka mfano tuko barzani tunapumzika. Lakini tabu kukutana na mtu kama Maalim Seif ukaacha kumdodosa lau kwa mbali kwa namna ya maskhara. Najua kitabu cha Ali Muhsin kakisoma kilipochapwa tu mwaka wa 1997 lakini niliona nimepelekee kuchokoza upya fikra zake. Mimi binafsi katik kitabu cha Ali Muhsin moja ya sehemu iliyokamata fikra zangu ni pale anapohadithia yale aliyokutananayo katika jela mbalimbali za Tanganyika wakati alipofungwa baada ya mapinduzi. Nikamrushia Maalim swali, ''Maalim tupate basi kitabu makhsusi ulipokuwa kifungoni.'' Kacheka kidogo. Nilikuwa nimemkumbusha mbali. Jibu lake lilikuwa, ''In Shaallah.'' Sikumuacha karibu nikaongeza na ''Memoirs...'' yaani kumbukumbu za maisha yake.  Mara ya mwisho kuwa jirani sana na Maalim ilikuwa mwaka wa 2012 Bwawani Hotel nikiwa na TV Imaan tulikokwenda kumsikiliza Maalim akizungumza kuhusu hali ya Zanzibar na mategemeo ya wananchi. 

Maalim alikuwa sasa yuko serikalini. Nakumbuka shida niliyowapa walinzi pale nilipoingia katika chuma cha faragha alipokuwa Maalim Seif, Mzee Hassan Nasoro Moyo na viongozi wengine. Mimi nilikuwa nje na wala sikuwa na nia ya kuingia ndani ya chumba kile kwani mtangazaji na mtu wa kamera tayari walikuwa ndani ya chuma kile wakishughulika. hawa vijana wote wana vitambulisho shingoni vinaning'inia na watu wa usalama weshawaruhusu. Mimi sina chochote lakini Ismail Jussa ndiye kanishika mkono tunazunguma basi hadi mle chumbani nikawa sasa uso kwa uso na Maalim. Ikawa sasa tunazungumza hili na lile, ''easy.'' Sasa nimefungua ''tablet,'' yangu nampiga picha Maalim na wakati mwingine kumwelekeza ''pose,'' niitakayo. Kumbe jamaa wa Usalama kidogo weshafanya wasiwasi wa kutaka kunijua mie nani. Mara niko kwa Mzee Moyo tunazunguza na kucheka. Lakini jamaa wa Usalama bado hawajanijua mie nani. Mara nimerukia Eddy Riyami basi ikawa kwao wao ni tafrani kidogo. Nilipotoka nje tu wakanifikia kwa maswali...

Jicho halisahau kile ambacho jicho la kamera liliona. Naomba kamera yangu ikuchukue katika barabara ya kumbukumbu turudi nyuma zaidi ya miaka ishirini iliyopita pale nilipoanza kufuatilia nyayo za Maalim na wale aliokuwa pamoja na yeye...

Fatilia ukurasa huu...In Shaallah tunautengeneza.... 


Mwandishi akiwa Viwanja Vya Jangwani akifuatilia mkutano wa CUF na kupiga picha
mwaka wa 2000
Historia mpya ya Zanzibar bila shaka watakapokuja kuandika watafiti wa historia ya visiwa hivi itatoa umuhimu wa pekee katika uchaguzi wa mwaka 1995. Kwa mara ya kwanza wananchi wa Zanzibar walitikisa na pengine mtu unaweza kusema walivunja ngome ya dhana ya, ''Mapinduzi Daima.'' CCM Zanzibar walishindwa uchaguzi ule. Imewezekana vipi kwa kipindi cha miaka mitatu tu ya uhai wa CUF ikaweza kuwa na nguvu ya kupambana kukishinda katika sanduku la kura  chama kilicho na dola na  fursa zote zinazokwenda na dola. Tume ya Uchaguzi Zanzibar ilishindwa kutoa matokeo ya uchaguzi kwa siku tatu. Yaliyobakia ni historia. Endapo Maalim ataandika kumbukumbu zake sura hii ya uchaguzi wa mwaka wa 1995 utakuwa na mengi ya kusisimua. Mwandishi alikuwapo Zanzibar kipindi kile na aliiona hali ya Zanzibar kwa jicho lake. Kitu ambacho anakikumbuka ni siku baada ya matokeo kucheleweshwa akiwa amekaa Malindi akamuona Baraka Shamte katika magwanda ya kijani akipita barabarani huku akipiga makelele mathalan ya mtu aliyepagwawa akisema, ''We have won the election we are going to form the government.'' Lakini kitu cha ajabu hata wale CCM waliokuwa wamezagaa katika vikundi vidogo vidogo walikuwa kama wamenyeshewa na mvua.  Walikuwa kimya wakizungumza kwa sauti za chini. Taarifa zilikuwa zimewafikia kuwa Maalim Seif Sharif Hamad kashinda uchaguzi na kamwangusha Komando Salmin Amour.


Photo
Kalenda ya Maalim Seif kuingia Ikulu Zanzibar 1995 ilikuwa imewekwa kwenye
maskani maarufu CUF  ''Jaws,'' Stone Town

Mwaka wa 2012 baada ya miaka 17 kupita na hali ya siasa za Zanzibar kubadilika, Maalim na CUF wakipata nguvu kila kukicha nilifanya mahojiano ya televisheni na Baraka Shamte, kada mkubwa wa CCM na mwana ASP. Wakati huu Maalim alikuwa Makamu wa Rais wa Zanzibar. Nimepata kumjadili Baraka Shamte mara kadhaa katika mitandao ya kijamii. baraka Shamte ni mtu mwenye histroia kubwa katika historia ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka wa 1964. Baraka Shamte ametunukiwa nishani ya miaka 50 ya mapinduzi.


Mwandishi Akifanya Mahojiano na Baraka Shamte Kada Maarufu wa CCM Nyumbani 
Kwake Mkunazini Zanzibar Kuhusu Historia ya Mapinduzi. Baraka Shamte ni Mtoto wa
 Mohamed Shamte Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kwanza wa Zanzibar 
Aliyepinduliwa Katika Mapinduzi ya 1964
Uchaguzi wa Mkuu Zanzibar 1995 Mwandishi akiwa nje ya kituo cha kupiga kura
Darajani siku ili mvua kubwa ilipiga

Shaaban Mloo na Kabourou kampeni za uchaguzi wa 2000


Photo
Kushoto: Prof. Ibrahim Lipumba, Shekue, Mama Ummie na Ummie biti yake.


Nilipokutana na Maalim kwa mara ya kwanza aliniuliza uwezekano wa CUF kupata wanachama Bara. Fikira ya Maalim ilikuwa ni kuwapata wazee wetu wa Dar es Salaam kuunga mkono chama. Mimi nikamwambia kuwa wazee wetu tuwaache kwa sasa tulenge vijana. Nakumbuka nilirudi tena kwa Maalim na baadhi ya vijana wachache viongozi na tukabadilishana mawazo. 

Vijana hawa walikuwa wametokea chama cha National Reconstruction Alliance ambako mwenyekiti alikuwa Prof. Malima na alipokufa ikawa vijana wamepwelewa. Sasa Alipopatikana Prof. Lipumba moto ukawaka upya na matumaini mapya yakaibuka. Mwandishi ndiye ailiyemtambulisha Prof. Lipumba katika mkutano mkuu wa CUF. Tulikuwa tunaingia katika uchaguzi mkuu wa 1995. Mwandishi ndiye ailiyemtambulisha Prof. Lipumba katika mkutano mkuu wa CUF. Tulikuwa tunaingia katika uchaguzi mkuu wa 1995. Kwa kuwa mwandishi hakuwa mjumbe katika mkutano ule alisubiri nje ya ukumbi pale Star Light hadi usiku wa manane ndipo alipoingizwa mkutanoni kwa kazi hiyo tu kisha akatoka nje kupisha mkutano uendelee. Siku zile kwa shida ya fedha CUF  wakifanya mikutano yao usiku na asubuhi wajumbe wanapanda mabasi kurejea makwao. Naamini Maalim hakujuta kwa kuletewa vijana badala ya wazee wetu kwani kila alipopita mikoani na vijijini alipokelewa na vijana hawa. Baadae zilitufikia taarifa kuwa wapinzani wetu walishangazwa ni lini tulijenga mtandao ule wa nchi nzima na bila shaka swali hili pia lilikuwa kichwani kwa Maalim. Iko siku In Shaallah tutaelezana ni vipi hawa vijana walipatikana na tulikuwa na hadi anuani zao pamoja na nyumba na mtaa...ni hadithi ya kusisimua sana...


[​IMG]
Vijana wanachama wa NEMA mstari wa mwisho wapili kutoka kushoto waliosimama 
ni Shaaban Mzuzuri, mwandishi, Salehe Yongo (marehemu) na Adam Juma.

Tulikuwa sisi ndiyo waasisi wa ''mtandao.''

Mtandao wa Kikwete, Lowassa, Rostam wa 2005 uliomtia madarakani Jakawa Kikwete ulikuja miaka kumi baada yetu ila tofauti ilikuwa moja tu. Sisi ni watu masikini ya Mungu hatukuwa na fedha kilichokuwa kikitusukuma ni mapenzi ya nchi yetu na ari ya kupigania usawa na haki kwa kila mwananchi bila ya ubaguzi.

Photo: Abdul Sykes Book at IDM Mzumbe 1999



Mwandishi akiwa IDM Mzumbe akikitangaza kitabu cha Abdul Sykes 1999

Uchaguzi. wa mwaka wa 1995 ulitufunza mengi na kilipotoka kitabu changu, ''The Life and Times of Abdulwahid Sykes (1924- 1968) The Untold Story of the Muslim Struggle Against British Colonialism in Tanganyika,'' kitabu kilifungua mlango mwingine wa kuwafikia vijana wa Kiislam wasomi. Kitabu kilifungua historia mpya haijapatapo kuandikwa popote na kubwa zaidi ya yote mchango wa Waislam katika uhuru wa Tanganyika..Vijana walipatwa na butwaa kusoma kuwa TANU haikuasisiwa kama walivyokuwa wakifundishwa katika historia na Nyerere bali na marehemu Abdulwahid Sykes. Historia waliokuwa vijana wakisomeshwa toka shule ya msingi hadi chuo kikuu ikaporomoka kwa kasi ya ajabu. Harakati hizi mpya za chama kingine nje ya CCM ikapata wafuasi wapya.



Photo

Sasa likazuka tabaka lau kama ni dogo la wasomi vijana wa Kiislam ambao kwa yale waliyoyasoma katika kitabu kile wakahisi wao na wazee wao ni jamii iliyodhulumiwa kwani haiwezekani Waislam wapiganie uhuru kwa kiasi kile kisha mwishowe uhuru wenyewe usiwanufaishe kitu. Hapa ndipo nilipogundua kosa nililafanya la kuandika kitabu kwa Kiingereza badala ya Kiswahili na hivyo kukosa wasomaji wengi. 


Photo
Sheikh Hassan bim Amir akipeana mkono na Julius Nyerere katika
sherehe ya kuweka jiwe la msingi la Chuo Kikuu Cha Waislam 1968

Kwa upande wa vijana wa Kizanzibari nao walishangazwa kusikia kuwa Sheikh Hassan bin Amir Mzanzibari alipigania uhuru wa Tanganyika bega kwa bega na Julius Nyerere na akina Abdul Sykes. Mwandishi akaalikwa Chuo Kikuu Cha Zanzibar akatoe mada kuhusu Sheikh Hassan bin Amir. CUF haikuwa na tabu kwa vijana wasomi Zanzibar. Lile lilikuwa jimbo lao salama. Shida ilikuwa katika vyuo vikuu Bara. Katika uchaguzi wa 1995 tulimsindikiza Prof. Lipumba aliyekuwa mgombea urais wa Bara kwa tiketi ya CUF. Hivi vyuo vikuu Bara ni ngome ya Ukristo kwani Waislam hawajaweza kufikia hata asilimia kumi. Wanafunzi waliokuja kumsikiliza Prof. Lipumba walikuja zaidi katika kumkejeli kuliko kumsikiliza kama mgombea urais na mchumi bingwa. Lakini uchaguzi wa mwaka wa 2000 umma uliojitokeza katika mikutano ya Prof. Lipumba ulitisha CCM. Hasa mapokezi ambayo hayajapata kuonekana siku alipotoka Mwanza kuja Dar es Salaam wakati wa uchaguzi.