Showing posts sorted by date for query Kumbukumbu ya Mapinduzi ya zanzibar. Sort by relevance Show all posts
Showing posts sorted by date for query Kumbukumbu ya Mapinduzi ya zanzibar. Sort by relevance Show all posts

Thursday, 12 April 2018


TAAZIA: SHEIKH SAUD BIN AHMED AL BUSAIDI
HAKUKATA TAMAA NA REHMA ZA ALLAH
Sheikh Saud bin Ahmed Al Busaid
(Picha kutoka katika kitabu chake)


Nimepata taaarifa ya msiba wa Sheikh Saud bin Ahmed Al Busaidi jana usiku kutoka Abu Dhabi kwa rafiki yangu Abdul Aleem Attas. Mara ya mwisho tulionana Dar es Salaam yapata zaidi ya miaka 20 iliyopita na tukapoteana hadi siku tatu zilizopita bada ya mmoja wa jamaa zake kuniunganisha na yeye baada ya kusoma historia fupi niliyoandika ya harakati za kudai uhuru wa Tanganyika na nikamtajaa baba yake mdogo Shariff Abdallah Attas, mtu maarufu katika Dar es Salaam ya 1950. Akijua mapenzi yangu ya vitabu Abdul Aleem akaniambia kuwa kaninunulia kitabu cha marehemu mzee wetu, ‘’Memoirs of an Oman Gentlemn from Zanzibar.’’ Nilimfahamisha kuwa kitabu ninacho toka kilipotoka na alinipa mwandishi mwenyewe na kina sahihi yake.

Nawapa pole wafiwa wote khasa Dr. Rawya Saud Al Busaidi. Allah awape subra wafiwa wote na Allah amweke baba yetu mahali pema peponi.

Hakika ni vigumu sana kuandika taazia ya mtu ambae hukupata kumjua kwa karibu. Lakini juu ya ukweli huu naamini nina dhima ya kusema kitu kidogo kuhusu msomi huyu wa Chuo Kikuu Cha Oxford kutoka Zanzibar ingawa lazima nikiri kuwa nimemjua Sheikh Saud kwa kusoma kitabu chake, ambacho kwa ukamilifu si tu ni histori ya maisha yake binafsi bali pia ni historia ya Zanzibar inayorudi nyuma kiasi cha karne moja hivi sasa.  Kitabu hiki ninacho na namshukuru Allah kuwa alinipa mwenyewe kupitia rafiki yangu Dr. Harith Ghassany na kama nilivyokwisa kusema kina sahihi yake. Kitabu hiki kipo katika Maktaba yangu. Nina furaha ya kusema pia kuwa kitabu hiki nilikifanyia pito (book review) ili wasomaji wafahamu umuhimu wa kukisoma.



Kama ilivyo kawaida ya kumbukumbu zilizoandikwa na wa wale ambao walishuhudia mainduzi na kisha walikimbia Zanzibar baada ya mapinduzi, historia ya Sheikh Saud bin Ahmed Al Busaidi inafuata mkondo ule ule wa kuanza kuelezea Zanzibar iliyokuwa imetulia na mahali pazuri pa kuishi kisha ikafuatia maisha ya shida, wasiwasi, vifungo na mauaji na mwisho kwa wale waliiobahatika kukimbia nchi wakiwa hai, maisha ya uhamishoni na mwisho kuishia takriban wengi wao, katika faraja na ustawi katika nchi mpya walizohamia, iwe ni UAE au Oman.  Haya nimeyasoma katika kitabu cha Sheikh Ali Muhsin, ‘’Conflict and Harmony in Zanzibar,’’ na katika kitabu cha Muhammad Al - Marhuby kuhusu maisha ya baba yake Sheikh Amor Ali Ameir Al Marhubi, ‘’Amor Ali Ameir His Life and Legacy My Father.’’ HIstoria hii kwa wengi ni faraja.

Kumbukumbu hizi zimatuachia elimu ya kutosha ya kuweza kuijua kwa undani historia ya kweli ya Zanzibar. Historia ya maisha ya Sheikh Saud bin Ahmed Al Busaidi unaweza ukaipa jina, ‘’A Tale of Two Revolutions.’’ Aliondoka Zanzibar baada ya mapinduzi ya mwaka wa 1964 kisha akaondoka Libya baada ya mapinduzi ya 1969 yaliyomuingiza Muammar Gadafi madarakani. Kati ya mapinduzi haya Sheikh Saud hakukata tamaa katika maisha yake alifanya kazi kwa juhudi kubwa na hakutaka kuangalia nyuma na kujisikitikia. Kila siku yake ilikuwa siku mpya iliyompa nafasi ya kuangalia mbele na kushinda changamoto mpya zilizojitokeza ama akiwa Kenya baada ya kukimbia Zanzibar, Misri, Libya au Oman.

Mwaka wa 1970 Sultan Qaboos alichukua uongozi wa Oman na akafungua milango kwa Waomani waliokuwa nje warejee kwenye nchi yao ya asili, Oman na watapokelewa kwa mikono miwili. Sheikh Saud bin Ahmed Al Busaidi alifunga mizigo na kwenda Oman mwaka wa 1971 na huu ukawa mwanzo wa maisha mapya ya furaha na umafanikio makubwa akiwa Oman akishiriki katika kutumikia nchi yake mpya kwa juhudi na mapenzi makubwa.

Mzee wetu katika kitabu chake kwa furaha amehitimisha kwa nukuu kutoka kwa William Shakespeare, ‘’All’s well that ends well.’’ Ameandika maneno haya akirudi nyuma kuiangalia nchi yake Zanzibar aliyoikimbia miaka 50 iliyopita lakini kwa rehma zake Allah amejikuta yuko tena Zanzibar kwa mapumziko akitokea Oman akiwa visiwani na wanae na wajukuu zake. Hii ilikuwa kwa hakika moja ya ndoto zake kuwa ifike siku arudi nchini kwake na aweze kukanyaga ardhi ambayo aliikanyaga akiwa mtoto mdogo akicheza katika vichochoro vya Mji Mkongwe.

Napenda kuhitimisha k kusem kuwa Sheikh Saud ameishi maisha yaliyokamilika akipanda milima na kushuka mabonde akiwa na ustahamilivu na mategemeo mema. Katika maisha yake ukisoma kitabu chake kunzia maisha yake Zanzibar hadi kuishia Oman yapo mazingatio mengi sana.

Allah ampanulie kaburi lake alijaze nuru na amweke mahali pema peponi.
Amin

Wednesday, 4 April 2018

Mwandishi amesimama Lincoln Memorial aliposimama
Dr. Martin Luther King alipotoa hotuba yake, ''I Have a Dream.''

Siku kama ya leo Martin Luther King aliuliwa Memphis kwa kupigwa risasi na hii leo imetimia miaka 50 toka Martin Luther King auliwe mwaka wa 1968.

Martin Luther King alikuwa mpigania haki za watu weusi Marekani.

Kumbukumbu hizi zinanirudisha mimi miaka 50 nyuma nikiwa kijana mdogo nina umri wa miaka 18 na mwanafunzi wa St. Joseph’s Convent, Dar es Salaam.

Shule yetu ilikuwa katikati ya mji karibu na Bahari ya Hindi, Bridge Street.

Kutoka shule ilipokuwapo na nyumbani kwetu Libya Street ilikuwa inanichukua kama dakika 20 au zaidi kidogo kufika shule.

Nyumba yetu ilikuwa no. 10 na kwa ajili hii tukaipa jina No. 10 Dawning Street, makazi ya Waziri Mkuu wa Uingereza.

MIaka ile ya 1960 Wamarekani walikuwa na ushawishi mkubwa sana kwa sisi vijana na safari ya Mwalimu Nyerere Amerika mwaka wa 1963 wakati wa John Kennedy akiwa rais wa Marekani ilizidisha pia uhusiano mwema katika ya Marekani na Tanganyika. 

Miaka hii ya 1960 Waingereza wakiita, ‘’Roaring 60s’’ kwetu vijana katika ‘’teens.’’ hasa wa Dar es Salaam hakika ilikuwa miaka ya wazimu khasa na tukiiga kila kitu cha Kimarekani, kuanzia mavazi hadi muziki wake.

Hizi zilikuwa enzi za ‘’Soul Music’’ na Apollo Theatre, Harlem, New York na Broadway tukizijua kwa kuzisoma na kuangalia picha.

Kuwa iko siku Allah atanifkisha huko kote ilikuwa ndoto ya mbali sana.

''Soul,'' ulikuwa muziki maalum na makhsusi kwa watu weusi wa Marekani na nje yake.


Apollo Theatre, Harlem, New York
Si rahisi kwa leo kueleza na mtu akaelewa wazimu uliotukumba wakati ule tukiwa vijana wadogo tukisikiliza nyimbo za James Brown, Wilson Picket, Ray Charles, Stevie Wonder, Ottis Redding kuwataja wachache  katika miziki ya vijana, yaani ‘’Pop.’’

Lakini ilikuwa pia enzi za miziki ya jazz ya wapigaji kama Duke Ellington na waimbaji bingwa kama Nat King Cole, Frank Sinatra, Louis Armstrong,muziki uliokuwa ukipendwa na watu ''sophisticated,'' wenye umri wa kati, na hapa sitaki kuwagusa wanamuziki kutoka Uingereza kama The Beatles, Eric Burdon and The Animals, Erick Clapton kwa kuwataja wachache.

Magazeti tuliyokuwa tukipenda kusoma yalikuwa Newsweek, Time na Ebony gazeti la watu weusi Marekani.

Wengi wetu nami nikiwa katika kundi hilo tulikuwa na ndoto kuwa iko siku tutakwenda Marekani kusoma katika moja ya vyuo vikuu vya huko na wako ambao ndoto zao zikaja kuwa kweli na tuko pia ndoto zikabakia ndoto.

Wamarekani walikuwa na kituo chao cha utamaduni katikati ya mji ambacho ndani mlikuwa na maktaba ya vitabu, muziki na ‘’theatre,’’ sehemu wakionyesha filamu.

Kwa kuwa na vitu hivi Wamarekani walituteka na mimi nilinasa katika dema lile kwani nilikuwa mwanachama wa maktaba ile na nilipofikia makamu ya kuwa naandika katika magazeti ya Uingereza kama Africa Events na New African Mkurugenzi wa United States Information Service  (USIS) alinipa uanachama wa Library of Congress, Washington nikiweza kuazima kitabu au jarida kutoka huko na nikaletewa Dar es Salaam.

Mwandishi akiwa Library of Congress, Washington DC

Sasa tuje kwa Martin Luther King na mimi.

Mwalimu wangu wa English Language alikuwa mama mmoja wa Kingereza jina lake Mrs. Grant.

Mume wake alikuwa anaitwa Grant na wote walikuja Tanzania katika mpango wa British Council wa kusomesha Kiingereza.

Bwana Grant alikuwa alikuwa akisomesha Chuo Cha Ualimu Chang’ombe.


Class of 1970
Nyuma ni St. Joseph's Cathedral
Mwandishi waliosimma wa kwnaza kulia
Mrs. Grant sijui kwa vipi lakini alikuwa mwalimu aliyenipenda labda kwa kuwa nilikuwa na mapenzi makubwa na somo lake lililokuwa linaitwa, ‘’Reading Labaratory,’’ tukifunzwa kusoma kwa haraka, yaani kwa ‘’speed,’’ akiweka, ‘’time clock,’’ kupima unasoma maneno mangapi kwa dakika ngapi kisha kuna maswali unajibu kuonyesha kuwa umeelewa ulichosoma.

Nilisoma mahali kuwa John Kennedy alikuwa ''fast reader,'' akisoma wastani wa maneno 300 kwa dakika, basi nami nikataka kuwa kama yeye.

Kulikuwa na mashindano ya Elocution Kiingereza na Kiswahili kwa shule zote za Dar es Salam na shule yetu kila mwaka ikishinda katika English Elocution na kuna mwaka tuliwahi kushinda kwa pamoja English na Swahili Elocution.

Mrs. Grant akaniambia kuwa mwaka ule nitafute ''passage,'' yeyote niihifadhi kichwani niingie katika mashindano ya English Elocution.

Mwaka wa 1963 ndiyo mwaka ambao Martin Luther King alitoa hotuba yake maarufu, ‘’I Have a Dream,’’ Lincoln Memorial, Washington DC.

Lincoln Memorial Washington DC

Nilikuwa nimehifadhi mengi kutoka michezo ya William Shakespeare kama ‘’Julius Caesar,’’ ‘’Merchant of Venice,’’ ambayo wala nisingehitaji kujifunza kwani tayari nilikuwa nimeshahifadhi mengi kutoka vitabu hivyo na ningeweza kusoma wakati wowote hata nikiamshwa usiku wa manane.

Lakini haya yalikuwa mashindano na nilitaka niingie katika mashindano yale na mtu mashuhuri kama Martin Luther King siyo na Cassius katika ‘’Julius Caesar,’’ au Shylock katika ‘’Merchant of Venice,’’

Niliamua kumsoma Martin Luther King na hotuba yake ‘’I Have a Dream.’’

Nikitoka nyumbani asubuhi nakwenda shule njia nzima naisoma kimya kimya hotuba hiyo na tulikuwa wanafunzi wengi tunawania nafasi hiyo ya kuwakilisha shule na kila mtu kachukua chake anachotaka kusoma na sote tutasoma mbele ya mwalimu wetu na mbele ya wanafunzi wenzetu na yule aliye bora ndiye atakaewakilisha shule latika mashindano yale.

Nilishindwa kwa hiyo sikuweza kuiwakilisha St. Joseph’s Convent katika English Elocution.
Kwa nini nilishindwa?

Wenzangu walikuwa wanasema Kiingereza kwa ‘’accent,’’ nzuri ya Kiingereza wengi wao wakiwa wameanza kusoma Kiingereza toka darasa la kwanza katika shule kama Salvatorian, St. Xavier na wengine kutoka hapo hapo St. Joseph's. Mimi Mswahili wa Kariakoo niliyesoma shule ya kawaida, ‘’accent,’’ yangu haikuwa imetulia ndicho kilichonifanya nishindwe.

Lakini ile tu kukubali kupambana na wenzangu wale ilihitaji kidogo ushujaa na ubishi wa Kimanyema.

Miaka mingi imepita na leo huwa wakati mwingine nacheka kimoyomoyo nikiwasikia wanangu wanazungumza Kiingereza kwa mbwembwe nyingi na wakati mwingine nashindwa kabisa kuziweka mahali hizo ‘’accent’’ zao au hata kuzitambua.

Lakini kwangu mimi ile kuchagua ile hotuba, ‘’I Have a Dream,’’ hotuba ile na ujumbe uliobebwa mle ndani uliniathiri sana.

Kila nilipokuwa napita katika mistari ya hotuna ile nilikuwa kama vile nawaona Wamarekani Weusi siku zile wakiitwa, ‘’Negros,’’ wanavyoteswa na Wamarekani Weupe.

Nilikuwa kama vile naisikia moja ya nyimbo maarufu katika ‘’Negro Spirituals,’’ nyimbo ambayo ukiisikilizaza inakutia huzuni, ‘’Go Down Moses Let My People Go,’’ iliyopigwa na Louis Armstrong.

Ilikuwapo na nyimbo nyingeni ya Sam Cooke, '' A Change is Gonna Come,'' ikiimbwa pia kwa maombolezo na mategemeo kuwa iko siku ubaguzi utaondoka Amerika na hali za watu weusi zitakuwa bora.

Hakuna mtu katika miaka ile aliyewaza hata kwa mbali kuwa iko siku mtu mweusi atatawala Amerika.

Hotuba ya Martin Luther King na muziki wa Louis Armstrong vilikuwa vikinitoa katika mji wa Dar es Salaam na kunipeleka Marekani ya karne ya 18, Deep South ambako utumwa ulikuwa umeshamiri na Wanegro wakifanyishwa kazi wakiwa watumwa katika mashamba ya pamba.

Wakati mwingine ndoto na mawazo yanayotawala akili huwa kweli ingawa si mara nyingi.

NIlisafiri kwa barabara ndani ya gari ya rafiki yangu James Brennan tukitoka Iowa City akinileta Chicago kupanda ndege kuelekea New York. 

Tulipita Mississippi ambayo mto wenye jina hilo ulinikumbusha Tom Sawyer  na Huckleberry Finn, ''characters,'' niliowapenda wakati nikiwa mtoto mdogo nikiwasoma katika kitabu cha Mark Twain - ''Tom Sawyer and Huckleberry Finn.''

Hawa walikuwa marafiki wawili waliokuwa watu wa mikasa mingi na kupitia watoto hawa wawili niliweza kujua maisha ya shamba Amerika ile ya Deep South yakoje.

Wakati ule wala haikunipitikia kuwa nitakuja kuisoma historia ya America nikiwa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam nikisomeshwa na bingwa wa historia Prof, Fredrick Kaijage, mwalimu aliyenifunza mengi na nina deni kubwa kwake.

Wala haikunipitia kuwa nitakuja kuiona kwa macho yangu Mississippi River niliyoijua zaidi kwa mikasa ya Tom Sawyer and Huckleberry Finn. 

Prof.  Kaijage kama walimu wengi katika maisha yangu, alinipenda kiasi siku nilipokuwa kwa sababu yoyote ile sikufika darasani au kwenye semina atajua na ataniulizia kwa wanafunzi wenzangu.

Miaka ya 1960 haikuwa tena miaka ya watumwa kulimishwa pamba bali ilikuwa miaka ya James Meredith aliyekataliwa kuingia Chuo Kikuu Cha Mississipi na Gavana mbaguzi wa Alabama, George Wallace kwa kuwa tu alikuwa na ngozi nyeusi.

Sasa mimi ni mtu mzima na wakati mwingine huwa nazungumza na wanangu kuhusu raha na elimu inayopatikana ndani ya kitabu.

Huwa nawaambia kuwa nilipokuwa mtoto nilikuwa nikifika Tanganyika Library siku hizo iko Mtaa wa Mkwepu nilikuwa nikiinamia kitabu kusoma basi huwa naondoka kabisa Dar es Salaam.

Ikiwa ni kitabu cha Spaniards wanaikata Bahari ya Atlantic kwenda Amerika ya Kusini katika nchi ya Aztec mimi nakuwa mmoja wa mabaharia wale nasafiri na wao ndani ya meli yao nafanya yale wanayofanya.

Katika hali hii ya raha nikinyanyua kichwa jua limezama na nje taa zinawaka, Maghrib imeshaingia.

Naondoka maktaba narudi nyumbani, Libya Street mwendo mfupi tu kutoka Mkwepu Street.

Nawaambia wanangu kuwa hawatoweza kuyapata haya hadi wahame kwenye kuangalia DVDs waje kwenye kusoma kitabu.

Huwa nahitimisha nasaha zangu siku zote kwa kuwaambia, ‘’Nothing can replace the book.’’
Kama sik kusoma vitabu nisingeijua haya niliyokuja kuyajua.

MIaka ikaenda nikafika Washington DC Lincoln Memorial nikiwa na mwenyeji wangu Dr. Harith Ghassany mwandishi wa kitabu mashuhuri kuhusu historia ya mapinduzi Zanzibar, ''Kwheri Ukoloni Kwaheri Uhuru,''  ambae katika kunionyesha mji akanipeleka Lincoln Memorial.

Mwaka wa 2011 nikiwa Lincloln Memorial nilisimama pale aliposimama Martin Luther King miaka 48 iliyopita na kutoa hotuba yake maarufu, ‘’I have a Dream,’’ akiwa kijana mbichi wa miaka 34.

Nikiwa pale fikra zangu zikirudi nyuma kwa haraka nikiwa nami nimesimama mbele ya darasa nikiwahutubia wanafunzi wenzangu, ‘’I Have a Dream,’’ Mrs. Grant mwalimu wangu wa Kiingereza akinisikiliza.

Tuesday, 13 February 2018


Masheikhe wetu: Sayyid Omar Abdalla (Mwinyi Baraka)
Sehemu ya (3)
Na Ben Rijal


Mwinyi Baraka

Makala haya nitamalizia juu ya kusoma kwake, kufanya kazi kwake na misukosuko ya hapa na yapale aliokumbana nayo. Tunaona katika nyakati mbalimbali wasomi wa Kiislamu hupata misukosuko ya kila aina hasa kwa kufanyiwa fitna na wengi wao humalizikia kuwekwa korokoroni na kuonekana kama ndio shahada ya kuwa mlinganiaji wa dini ya Kiislamu. Wengi wao huwekwa korokoroni na Waislamu wenzao. Kuna maandiko yanaonyesha kuwa Sayyid Omar Abdalla kafungwa mara mbili kwa misimamo yake, lakini unapopitia kumbukumbu mbalimbali na kufanya mahojiano na mtu ambaye alibahatika kuwa naye Zanzibar, Uiengereza na kufungwa pamoja naye anathibitisha kuwa kafungwa mara mmoja tu.

          Katika makala iliopita nilijaribu kuonyesha kusoma kwake na tumeona kuwa Sayyid Omar Abdalla kwanza alikwenda kusoma Chuo cha SOAS na kupata shahada ya Diploma ambayo ndio aliokuja nayo na kuwa sasa kishakuwa msomi anayotakiwa kuwa anaongoza Chuo cha Kiislamu “Muslim Academy” ingawa mwenyewe alikuwa akiona kuwepo na pengo na kuwa hajaaelimika atakavyo.
          Bada ya kurudi masomoni na kuwa anashirikiana na watawala katika kuweza kukiendeleza Chuo cha Muslim Academy, Sayyid Omar alihudhuria mikutano mingi na hata ikajiri afike Nigeria kwenda kuweza kuangalia namna wao wanavyoendesha masomo ya Kiislamu katika nchi ambayo Kiengereza kinatawala na kipo juu.
          Unapopitia nyaraka mbalimbali saa nyengine unahangaishwa kufahamu mtawala Muiengereza katika utawala wake namna ambavyo alivokuwa anaziangalia dini kuu mbili na kuhakikisha kuwa hazipishani na wakati huo huo anakuja na upendeleo kwa upande mmoja halafu upendeleo huo unakuja unafichwa na kuonyeshwa juhudi za kuwaweka waumini wa dini kuu mbili Afrika ukiwa Uislamu na Ukiristo kuwa upo sawa.
          Muiengereza alikuwa amejaribu katika nchi ya India, Sudan na Nigeria kuweka mtaala wa elimu ya dini ya Kiislamu ambao unafahamika na utaweza kutumika unavyostahiki, aidha alifanya katika nchi hizo kuwa na Makadhi pamoja na Mahakama zake ambazo Waislamu hawatakuwa na shida na ili kuweza kuyatolea ithibati hayo, utayaona katika kumbukumbu za kuanzishwa kwa Muslim School mkolini alijaribu kukaa na viongozi mbalimbali wa dini na wasomi wa kuiweka Ofisi ya Kadhi na Mahkama yake, na akahakikisha kuwa wale wasomi wanaofahamika na wenye ujuzi ndio wakupewa nafasi ya kuongoza kuanzia Kadhi na watendaji wake.
          India na Sudan walifanya vizuri sana katika kujipanga kwa mitala ya dini ya Kiislamu,  utaona hadi leo Sudan wana taratibu nzuri ya kuwanisha baina ya uongozi wa dunia na akhera.
          Sayyid Omar bin Abdalla alipata fursa yakwenda Nigeria na alivutiwa kuona mpangilio wa mitala ya Madrasa namna ilivyopangiliwa namna walimu walivyofunzwa namna ya kumsomesha mtoto kujua kusoma Qur’an na Sheria na hapo hapo kufunzwa msingi wa mwanzo wa lugha ya kiarabu, kujua vitu mbalimbali vinaitwaje kwa Kiarabu hasa vile vilivyomzunguka, haya yalimvutia sana Sayyid Omar Abdalla na safari yake hio ya Nigeria ilikuwa akipenda kuielezea katika mihadhara yake na kuanza kuandaa mipango ya utekelezaji kwa Zanzibar na Afrika ya Mashariki kwa jumla.
          Sayyid Omar aliporudi Ulaya akawa anasoemsha dini katika Skuli ya Teacher Training na akaja kuwa mwalimu Mkuu wa Skuli ya Muslim Academy kwa hakika alikuwa anaposemesha dini mara zote akipenda kuingiza na taaluma yake alioipata Chuo cha Makerere College ikiwa elimu ya viumbe (Biology).
          Ilipofika mwanzo wa miaka ya 60 Sayyid Omar Abdalla alifanikiwa kupata Scholarship nyengine kwenda Uiengereza. Wakati huo akiwa Muiengereza akijua makoloni yanamtoka lakini alianza kujisafisha na kuweka nidhamu ambayo kila mwaka akijaribu kuhakikisha wanafunzi wangapi wanakwenda nje kusoma masomo ya juu na Zanzibar kwa wakati wake ikiwa na idadi ya watu 300,000 ukichukua na asilimia na uwastani wake ilikuwa na wanafunzi wasiopungua 400 wakiwa wapo nchi za kigeni wanasoma, wengi wao walikuwepo Misri kwa program ya Gamal Abdulnasir na wengine wakiwepo Uiengereza, Iraq, Marekani, India na kwengineko.
          Sayyid Omar Abdalla alijiunga na Chuo Kikuu cha Oriel College, Oxford na safari hii akafanya shahada ya Masters ambayo somo lake lilikuwa juu ya Falsafa na hapa ndipo mkanganyiko nitajaribu kuweka sawa na haya ninayosema nasema kwa kupitia Faili lake na mazungumzo nna  murid wake Sheikh Ahmed ambaye kawa naye hapa Zanzibar kama katika wanaohudhuria mihadahara yake na kuwa naye kwenye rubaa za kheri na wakawa pamoja Uiengereza na wakafungwa jela pamoja.
          Katika Chuo cha Oxford Sayyid Omar Abdalla alisoma somo la Falsafa (Philosophy) alipokuwa anajifunza somo hili alionyesha maajabu mengi namna alivyokuwa akiweza kuona wana Falsafa watangulizi wa Kiyunani kina Aristotle na wengineo walivyokuja kuwa athiri wasomi wa Kiislamu kama Ibn Sinna (Avicenna) na kuweza kuwafahamu wana falsafa wa Kiislamu ambao wengine hata roho walikua wakielezea katika kitu chengine ambacho kitabaki na kuondoka na kurejea kwa njia nyengine.
          Sayyid Omar alivutiwa na Mwanafalsafa Ibn Bajja na Imam Ghazali na unaposoma Risala yake ya mwisho Chuwomi Oxford (Thesis) alioipa jina “Some Felicity in Medieval, Islamic Philosophy” ndio utapofahamu kwanini alishikana na Ibn Bajja akawa tafauti na Ibn Rushd, hawa kina Ibn Rushd na Ibn Sinna waliuweka pembeni Uungu na wakenda katika nadharia ambayo mwanadamu ameiasisi.
          Sayyid Omar alivutiwa zaidi na Imam Ghazali ambaye akiweza yeye kumfahamu zaidi, Imam Ghazali alianza kuzama na nadharia za kina Aristotle, kisha akazama kuona Uungu na umoja yaani sii umoja huu lakini upweke wa Allah kuwa hakuna mwengine wa kuabudiwa ila ni yeye tu katika mamlaka yake na uongozi wake.
          Leo katika elimu ya Ikolojia (Ecology) kunazungumzwa juu ya mwindaji na  mwindwaji na haya Imam Ghazali katika kitabu chake cha Ihya Ulumu Deen anagusia na utafahamu utapomsikia Sayyid Omar Abdalla alivomfahamu Imam Ghazali, naye kuwa na uelewa wa somo la ilimu ya viumbe.
          Imam Ghazali akifahamisha namna ya ndege Allah alivyomjaalia kuwa kila saa awe anakula kisha anakitoa chakula kama kinyesi, anakula tena na kurudia kula, Imam Ghazali anaeleza kuwa kuumbwa kwa ndege kuwa na umbo dogo w ni kwasababu awe yupo natunaendelea kuwaona kwa dahar, lakini kuweza kubakia kwake ndege kuepukana na maadui awe kila akila akikaa awe hashibi bada ya muda mdogo anataka kula tena na hio inamfanya kuwa kwa udogo wake angekuwa anakula na kushiba basi maadui wake kina nyoka na wengine wangewamaliza kirahisi, hapa ndipo kunakazi kufahamu na inataka malinganisho ya ilimu ya dunia na akhera.
          Katika somo la Ikolojia  haya maingiliaano wanayaita “Predator prey relation) na Sayyid Omar Abdalla nilimsikia anamuelezea Imam Ghazali kwa wigo wa Ikolojia na namna wanyama wanavyopotea kutoonekana tena (Extinct) ni namna Allah alivyopanga vipi viumbe viweze kupambana na wengine na kujihami na kuendelea kukuwepo, Falsafa ya Imam Ghazali ilimvaa vya kutosha na Sayyid Omar Abdalla alifika hadi hawezi kutoa mhadhara bada ya kutoa aya chache na kuja na hadithi za Mtume Muhammad (SAW) asimgusie Imam Ghazali.           Bahati nzuri hii risala yake ya Oxford imechapishwa na vyema ukaipata ukaisoma.
          Sayyid Omar Abdalla alirejea Zanzibar mwaka wa 1963 bada ya kumaliza masomo yake hapo Oxford na alifika kuwa na kasi kubwa ya kutoa mihadhara na akipata nafasi iwe kwenye hitima, majlisi, radio au popote pale akichukua nafasi hio kuweza kutoa mawaidha mazito ambayo ni zaidi yalikuwa ulinganisho wa dini ya Kiislamu na Kikiristo.
          Yalipotokea Mapinduzi ya 1964 alikuwa ni mwalimu bado hakuyapa kisogo aliendelea kufanya kazi na kwenda sambamba na mabadiliko yaliotokea, ithibati ya hio ni hio picha ya ujenzi wa uwanja wa Amani, akiwa yumo katika ujenzi wa taifa na huku ana shoka anachanja mnazi.
Sayyid Omar Abdalla na Maalim Zubeir Rijal katika ujenzi wa taifa
          Matokeo machache juu ya Sheikhe huyu: Sayyid Omar Abdalla ilikuwa kila siku ya Ijumaa akipenda kuwa na rubaa na wenzake ya kumuomba Mungu katika zile taratibu ambazo Mola anasema “Niombeni nikujibuni” yeye na wenzake  waliweka taratibu ya kuleta maombi au tuite Nyiradi siku za Alkhamisi na Ijumaa, katika mwaka wa 1968 alikamatwa na wenzake kama 25 kwa kuambiwa wanapanga njama ya kupindua Serikali, akawekwa korokoroni kwa mwezi mmoja badaye ilikuja  kuelekweka kuwa ilikuwa ni fitna tu, tena hapo Mzee Abeid Amani Karume akaamua kuwachia, afya yake iliathirika sana kwani akisumbuliwa na kisukari na akawa hapati dawa ya kupiga shindano ya Insulin. Sayyid Omar bada ya kutolewa jela alikuwa akiishi na khofu akaona asije akafungwa tena akaamua kuhama Zanzibar huku  tayari kapatiwa nafasi ya kurudi Uiengereza lakini aliona vyema kwenda kusihi katika visiwa vya Comoro ambavyo ana nasaba navyo.
          Safari mmoja akiwa anasafiri kutokea Kenya anaelekea Ulaya, amesimama kwenye foleni, binti wa Kikenya alio katika kupima mizizigo na kutoa namba ya viti kwenye ndege kumuona mzee na majuba na kashika bakora akamshika kumwambia “eeh muzee nenda kwenye foleni ile ya kwenu Mombasa, ndege itakukimbia.” Sayyid Omar alikaa kimya lakini jeuri ya kitoto ikazidi kwa kumtaka mmoja ya wafanyakazi kumtoa kwenye Foleni, Sayyid Omar akatoa Pasi ya kusafiria ikiwa na hadhi ya kidiplomasia na mrundo wa tiketi, mpaka akaiona tiketi yake anayokwenda Ulaya, aliyotumwa akamjibu yupo pahali sawa, binti akasema haiwezi kuwa, akawa anajipanga sasa kwenda kumtoanyeye mwenyewe kilichomudhi hakifahamiki, lakawa anamuhudumia msafiri wa Kifaransa ambaye hajui Kiengereza, ikawa vuta ni kuvute na wakati unakwenda Sayyid Omar akamsogelea yule bibi wa Kifaransa na kumuamikia kwa Kifaransa na kutaka kujua nini shida yake, akawa Sayyid Omar sasa anatafsiri kutoka Kifaransa anapeleka kwa Kiengereza kwa mratibu wa Tiketi, binti wa Kikenya hakuamini, alivyoyasuluhisha binti akataka kujua wapi aliposoma kujua Kiengereza na Kifaransa, Sayyid Omar Abdalla akamwambia “You better asked Kibaki, he knows me better, we were together at Makerere College” Binti wa Kikenya  alitahayari bali aliogopa asije kushtakiwan kwa wakubwa wake na Sayyid Omar alipomuona anatetemeka huku hana raha akamwabia “Jitahidi kuwaona watu wote ni sawa.”
          Alifika Chuo Kikuu cha DaresSalaam akatoa uwaidh juu ya umuhimu wa kujiendeleza kiroho kwa kuwa na dini, wakati wa masuala kijana akaona aaah, huyu mzee ndio watu wa kizamani Wakoloni waliwafundisha lugha ndio katuhutubia kwa Kiengereza, akamvaa akamwambia unajua nini Karl Marx kasema? “Religion is the opium of the mass” kwa maana ya kuwa “Dini ni kasumba kwa umma.” Sayyid Omar Abdalla kwa mshangao wa wengi aliusoma ukurasa mzima wa Das Capital juu ya maneno hayo na kusema ukurasa gani upo wenye manerno hayo ambayo aliyasoma  kwa ghibu, na akamtaka kijana huyo amsome Maurice Bucaile katika kitabu “What is the Origin of man na The Qur’an, The Science and the Bible.” Kijana badala ya kutaka kumshushua Sheikhe alijikuta kajishusha hadhi na kujuta aliyotaka kuyafanya.
          Sayyid Omar Abdalla akipenda kuurejea na kurejea msemo wa mwana sayansi wa Fizikia maarufu kwa jina la Albert Einstein usemayo “Science without religion is lame, religion without science is blind.” Somo la sayansi pasi kujuwa dini ni sawa na kilema na sayansi pasi kujuwa dini ni mithili ya kipofu.” Sheikhe huyu alikuwa na elimu zote mbili hizo na akiweza kufahamisha na kutowa ujumbe kwa watu wa rika zote wakiwa wasomi na wale wasiokuwa wasomi.
          Yapo mengi ambayo ningeweza kumzungumza Sheikhe huyu, nategemea haya machache yanatosha, fatwana na mie wiki ijayo umjua Sheikh Abubakar Bakathir. Tumuombe Allah nasi tufwate nyayo za Sayyid Omar Abdalla (Mwinyi Baraka), Ameen.


Wednesday, 10 January 2018





Kulikuwa na ukumbi ukiitwa ZANZINET nilikuwa mwanachama wa ukumbi huo ambao ulikusanya Wazanzibari waliokuwepo Zanzibar na waliokuwa nje ya Zanzibar, humo watu wakijadili maudhui mbalimbali yawe ya Dini, Kisiasa, Jamii na mengineo. Kulikuwa a wachangiaji mahiri kina Al Marhoum Ali Baucha, Dr. Amour, Houd Houd na wengineo. Mie Pangu Pakavu nilikuwemo humo na nikichangia baadhi ya nyakati.

Mwaka wa 2009 Dr. Amour aliandika kutoka tarehe 11 hadi 12 January 1964 alioyakumbuka na mie nikaona niseme yangu lakini kwa jazanda nyengineo, nimeyagundua leo katika pekura zangu huku na kule.

ASALAMA ALAYKUM!

Utangulizi

Nilipoandika Nakumbuka Miaka 45 iliyopita fikra ilinijia pale nilipokuwa nimekaa bure sina la kufanya sina wakuzungumza naye na kitabu nilichokuwa nakiosma cha Baraka Obama The Audacity of Hope nishakimaliza, basi hapo afkar zikawa zinazunguka magenzi yangu yanakumbuka nyuma ikiwa huku nishatembelea maeneo mbalimbali ambayo wakati mzee alipokuwa hai tukipita na kuwatembelea marafiki na hata wale aliokuwa akiwadai.

Niliyoandika yalikuwa ni juu ya mimi na wakati huo wala sijataka kuandika yale ambayo yalikuwa ni mengi mno yaliokizunguka kitandawili kizima cha Mapinduzi kwani hayo yanaandikwa kila kukicha kwa kila aina ya kalamu, nikimaanisha vile muandishi apendavyo kuandika juu ya suala hili.

Bahati Dr. Amour ameleta yale ambayo anayakumbuka kuelekea January 12, 1964. Dr. Amour kenda mbali mno kwa zile kumbukumbu na mie kanielimisha mengi katika uandishi wake, kwani siku zote hutakiwa tuwe tumo kwenye kujifunza “Elimu kuanzia kwenye kitanda cha mbeleko hadi uingiapo kaburini,” hutakiwa tuwe tunaendelea kujifunza na kusoma isiwe yale ya Rabi wa Kiyahudi aliposema maneno haya katika mwaka wa 1949:

Wasilamu Hawasomi;

Wakisoma hawafahamu;

Wakifahamu Hawatekelezi.

Hayo ni matusi tena yenye kuamsha hisia (Kutoachangamoto) tuwe sio hivyo huyo Mwanakharashi alivyosema.

Dr. Amour anazitaja Jezi ambazo Malindi wakivaa miaka ya 40 hadi 70 ambazo kwasasa zinavaliwa na Team ya Premiership ya Uiengereza Stoke City. Wenyewe Malindi wakizita Bakora, wakizivaa hizo hatoki mtu, mie nilipojiunga na Malindi na kuchezea First Division katika mwaka wa 1970 tukizivaa hizo lakini sio kwa kila mchezo na hakika tukizivaa alikuwa hatoki mtu. Katika michezo ya kawaida sare tuliyokuwa tukiivaa ni ya kijani na mikononi na ukosini ilikuwa na rangi ya njano na sare nyengine ilikuwa ya buluu ya bahari.

Nakumbuka mchezo mmoja tukicheza na Abaluhya ya Kenya baadaye ikaja kuitwa Leopards akiwemo Angana mchezaji mahiri ambaye kwasasa namfananisha na Michael Essein wa Ghana na Chelsea huyu ingekuwa anaishi nyakati hizi basi pakuchezea kunakomnasibu ni Real Madrid, AC Milan au Man Utd.

Leopards ilikuwa haifungiki na sisi tulipocheza nao watu wakiamini kuwa tutalala tena sio chini ya mabao 5, hatutoka chini ya mabao hayo, lakini mwalimu wetu Al-Marhum Seif Rashid alitufundisha mbinu za kuweza kukabiliana na team hiyo kubwa na tukaweza kuwazuia. Marehemu Seif Rashid alikuwa hodari kwa kupanga mbinu.

List yetu siku hiyo ilikuwa 1. Amiri 2. Hamza Zubeir/Abdalla Mwanya 3. Ali Fereji 4. Mzee Boti 5. Mustapha Kassim 6. Mohammed Magram 7. Mohammed Issa 8. Mansab Abubakar 9. Seif Mohd (Tornado) 10. Ahmeid Baba 11. Farouk. Tulivaa bakora ndani ya dakika 15 Ali Fereji alifanya kama anarejesha Mpira kwa Amiri, asiurejeshe halafu akaurejesha bila ya kutizama hapo tena Angana akaufumania mpira na kuweka bao. Baada ya bao hilo Mpira ulipelekwa Center na alianza Seif Tornado akampasia Baba, Baba akampa Mansab, hapo tena Mansab akapiga krosi ikamkuta Mohd Issa akakimbia nao sehemu ya Winga ya kulia akamimina krosi iliyomkuta Tornado na hapo Tornado akapiga mkwaju wa hali ya juuu na bao kusawazisha hapo hapo baada ya kufungwa, mchezo ulimalizikia 1-1 yaliofikiriwa hayajawa.

Bakora ikivaliwa ilikuwa hatoki mtu, kutoka zama za kina Kassim bin Mussa, Saidi Nyanya, Issa Juma, Boti Senior, Ramadhan Saleh, Khalid Keis, Mohd Kassim, Seif Rashid, Zaghalouli, kina Abdimout, Ahmed Ajmy, Mzee Boti, Saad, Bahbeish, Murtaza, hadi kina Mansab, Muniri beki papua niliyokuja kumrithi, Mohd Issa, Mohd Magram na Omar Magram na Hamza. Bakora ikivaliwa huwa hutoki.

Dr. Amour saa nyengine mtu akikumbuka hulia, sawa na Marehemu Bwamkubwa Bata Shoes alipokuwa anatajiwa Marehemu Islanders, alikuwa hastahamili huangua kilio, akimkumbuka Babu Ahmada, Taimuri, Marehemu Shioni Mzee, Mamdad, Marehemu Shebe na Clarinet yake na wengineo, na mie kwa kweli nasema Dr. Amour umeniliza kuitaja Bakora aaahhh, aaaah, aaaaaaah.

Kwa Dr. Omar Juma ambaye ambaye namletea nakumbuka zama hizo ambazo nilikwenda kupumzika Pemba skuli zimefungwa yeye alikuwa katika wanafunzi wa mwanzo wa Syd Abdalla Secondary School, akiwa na kina Dr. Ali Tarab, Miskir, mwenzao Head Prefect wakimwita Father, Nasim ambaye anakuja kuolewa na Dr. Jaffar Tejani, Dr. Omar ikiwa jina nimepopoa nirekebishe na wengi wengineo.

Dr. Omar amekuja na Wajiwaji ambayo ameona kwa upana na kwa upande wake. Palipokuwa na palipo lazima kuwe na mabadiliko, sawa namti huanzia mbegu ukaja mche na kisha ukaja mti na kisiki na mzizi wake, lakini vipi huo mti unapokua hakika unakua kupitia njia mbalimbali hapo ndipo pakujiuliza. Mti wenye kushughulikiwa hukuwa haraka na kutoa matawi na matunda mazuri makubwa-makubwa, naule uwachiwao na ukuwe bila kushughulikiwa basi usitegemee kupata matunda mazuri na hata mara nyengine hufikia kufa, sasa kwa mantiki hiyo ndio nililokuwa nalizungumzia kwa kuwa nipo nyuma ya pazia nakuuzunguka mbuyu au nuite kama mzee wangu alioita Mbuu siko wazi.

Hood hood anauliza verejee ikawa bakora nikaita mchapo au upupu nikauita muwasho? Hood hood ameyataka mambo yawekwe ben ben lakini mie nimekuwa nikitambaa sijapiga chubwi itategemea wengineo ambao wanaweza wakazamia kwa kupiga chubwi lakini isiyokuwa “Aaaah, Chubwi, Ndani? Aaaah, Chubwi, Ndani? Katumbukia aaah, katumbukia aaaah, Aaaaah Chubwi Ndani, Aaaah Chubwi Ndani.”

Ya Jana

“Mla Mla Leo, Mla Jana Kalani, Muulize Jirani,” Wala sio uwongo lakini wengine wanasema “Mla Mla Jana, Mla Leo Hajala Kitu,” kwani wengine huona “Mla Jana ni Mithili ya Chungu aliona Ganda la Mua la Jana ni Kivuno.” Watrib wa Malindi wameimba “Ganda la Mua la Jana Chungu kaona kivuno, aaah, kwa Mbwembwe na Kujivuna........”  Sasa Jee ni Jana au leo?

Naiwe itavyokuwa kwenye kula na kwenye jana kuna raha zake na wale ambao ukiwapeleka jana hustaladha koliko ukawaweka kwenye leo, yaani ukiwapeleka zamani wao huona ndiko na ukiwaweka sasa huwachafua na kukirihika khasa wakaazi wa Zimbabwe au kuleeee.

Jana ni Jana na Leo ni Leo iwe itavyokuwa, Jana ikipotea ikaja leo huwa haiji tena lakini ipi jana na ipi leo? Vyote hivi hukimbia na kutoweka na kuja kama leo na jana lakini sio leo iliyopita na jana iliyopita (You can’t turn the clock back-V. I. Lenin.)

Jana asubuhi, jana ilikuwa Ijumamosi nilielekea Marikiti kujinunlia mahitaji yangu ya wiki na huku afkar za miaka 45 iliyopita inanizonga baada yakusoma mails za wenzangu kuhusu hili. Napita soko la Mboga nakutana na Mzee Abdalla Habeish huyu mzee ni hazina mie nikikutana nae hupenda kumuuliza yaliopita nayeye huwa simchoyo na hakosi kunitupia chochote kile.

Kama kawaida yangu nilimtupia suala juu ya miaka 45 iliyopita kuanzia 10 December 1963 hadi January 12 1964 anakumbuka nini? Alinijibu kuwa anakumbuka mengi lakini yanataka wasaa nikae naye kuzungumza ikiwa wakati huo anaelekea kazini Masomo Bookshop. Juu ya hayo akanambia bora nikupe moja nalo “Tarehe 4 January 1964, napita Vikokotoni nakuta Umma wa watu nilipoingia kati kuyasafi mambo niliambiwa Ofisi za Umma Party zilifungwa rasmi siku hiyo.” Alisitia hapo na mie kuanza kujiuliza mengi, kwanini zilifungwa? Wao hao Umma Pary idadi yao ilikuwa haizidi watu 3,000 wakitisha kitu gani? Nikawa najiambia kuwa kulikuwa kunanukia kitu ambacho kilijificha mficho wa mbuni, ingawa kitu hicho kilikuwa kimejificha lakini kilikuwa kipo wazi.

Angalia kila mtu alikuwa na dhana kuwa kuna kitu kitatokea kwanini kikawachwa kitokee? Labda kilikuwa kimeandikwa kitoke kwayo kulikuwa hakuna nguvu ya kukizuwia. Au matokeo yaliokuwa yakingojewa yalikuwa maridhawa, Dr. Harith yuwasemaje?

Bwana Ali ni mzee rafiki wa familia yangu na kaja kuwa rafiki yangu mkubwa nazungumza naye sana na huyu mzee bingwa wa kukisarifu Kiswahili basi aliniambia kuwa kwenye tarehe 10 January 1964 alipita kwenye moja ya Makao ya ASP hapo Kijangwani akamsalim Mzee Faraji ambaye alikuwa rafiki yake, jawabu ya Mzee Faraji badala yakuitikia salamu alimjibu “Siku zenu zinahesabika, mtakiona,” Bwana Ali alimjibu “Mashudu,” hii inanijia kama al-Marhum Ali Muhsin alivyosema kwenye kumbukumbu za BBC za miaka 50 iliyopita alipoulizwa kuwa jamaa watazuia Uhuru usiwe-ndivyo wasemavyo, jawabu yake ilikuwa “Labda wanaota,” hapa mie kunanipa mtihani, aaah kwanini kulikuwa na dharau? Doto ni doto lakini ndoto huja zikawa ni yaliootwa yakawa ni kweli.

Nikiendelea na Bwan Ali aliniambia kuwa kila akikutana na Mzee Faraji akimkariria kwa uhakika kuwa wakati wao umekwsiha na watakiona.

Mzee wangu Zubeir Rijal akipenda kuweka kumbukumbu juzi katika kuchungulia moja yaFile naikuta barua ya mwanafunzi wake Dr. Zamil Suleiman  Al-Alawy amabye akimtaka mzee awe Referee wake na mzee kishampelekea hiyo barua na Dr. Zamil anamjibu natoa sehemu ya barua hiyo nayo ambayo ameiweka kwa kumbukumbu:

Dear Mr Rijal,

Thank you very much for your letter and the letter of recommendation in 6 copies. I do hope that the authorities concerned with Common Wealth Scholarship will not suspect your extravagancy in praising me. Believe me I do not possess even half the qualities mentioned in your letter of recommendation.     

I think I am not quite sure that the political tension in Zanzibar is over and things run smoothly. But to be frank, I do not know that people of Zanzibar will accept the new form of government as mentioned in your letter to me without any opposition.

You’re faithfully
Zamil Suleiman Al-Alawy

Dr. Zamil yupo Ulaya na khofu inamjia hapa nikitandawili kikubwa nataka nikionana naye nikenda Mrima au akija Unguja nijadiliane naye Dr. Zamil nimuulize juu ya hisia hizo alizokuwa nazo zilitokea wapi?

Nazungumza na Maalim M. Maalim ananiambia kuwa kwenye mwezi wa December kueleka January 1964 kulikuwa kumegubikwa juu ya kitu cha khatari kitatokea, vipi na lini hawakujua. Marehemu Nabwa moja ya makala yake alikwenda kwa undani juu ya Mapinduzi yalivyokwenda labda aambiwa Virus 99 apekue pekue atafute makala ya Nabwa juu ya Mapinduzi tuipate kuisoma hapo tena ndipo Hood hood alipopatafuta atapadasa.

Najiuliza na kujiuliza Inspector Aboud Saidi kipi kilichompelekea amwambie mzee wangu kuwa tukisikia fujo tuondoke Vitongoje tuje mjini? Kulikuwa na jambo ambalo lilikuwa ndani ya nafsi za watu lakini hakuna aliyofahamu kuwa ni jambo gani na mwisho jambo lilikuwa nalo ni MAPINDUZI Tarehe 12 January 1964.

Nakuachia hapo nitaendelea na kumbukumbu hizi kila akili itavyokuwa inanipeleka ndani ya kitandawili hichi kilichojificha hadi leo na kila mweledi kuelezea vyake.

Nakumbuka Miaka 45 Iliyopita.
Ngaridjo Onana
Ben Rijal

Tuesday, 27 June 2017

Chief Makwaia Mohamed Mwandu

Nimeona tangazo la Busiya Chiefdom katika mitandao ya kijamii na nikaangalia, ‘’clip,’’ yake. Hili ni tamasha linalofanyika hapo Busiya kulipokuwa na uchifu wa Makwaia. Mwalimu Nyerere alifuta uchifu katika baada ya uhuru wa Tanganyika lakini taratibu uchifu unarejea kwa kuona umuhimu wa kuenzi asili za watu na utamaduni wao. Uchifu huu hauna mamlaka ya utawala ila heshima na kumbukumbu.


Chief Michael Lukumbuzya

Historia ya Mwalimu Nyerere na machifu waliokuwapo Tanganyika toka enzi na enzi, kama baba yake Chief Edward Makwaia, Chief David Kidaha Makwaia, Chief Abdallah Said Fundikira, Chief Haruna Msabila Lugusha, Chief Thomas Marealle, Chief Makongoro, Chief Abdiel Shangali, Chief Kunambi, Chief Majebele, Chief Adam Sapi Mkwawa, Chief Ngua na mkewe Mwami Theresa Ntare, Chief Mang’enya, Chief Michael Lukumbuzya na wengineo ni historia yenye msisimko wa kipekee kabisa.


Chief Thomas Marealle

Nimebahatika katika maisha yangu kufahamiana na baadhi ya hawa machifu katika siku zao za mwisho wa maisha yao na pia kufahamiana na watoto wao kwa karibu na kutoka kwao nimejifunza mengi katika yale yaliyokuwa katika fikra za wazee wao na yale waliyokuwanayo wao wenyewe binafsi.


Kulia: Abraham Ally Sykes na Kibo Marealle nyumbani kwa Mwandishi Tanga1999



Kuwa hivi sasa uchifu wa Makwaia wa Busiya Usukumani umerejea hakika ni kitendo cha kupigiwa mfano.

Kumbukumbu nyingi za machifu waliokuwapo aidha zimekufa kabisa au hazipo na zile zilizokuwapo ziko taabani.

Chief Abdallah Said Fundikira

Labda nieleze kwa nini nimeguswa na uchifu Mkwaia wa Busiya.

Nimeguswa na uchifu wa Busiya kwa kuwa kiongozi wa uchifu huu ni rafiki yangu toka utotoni.
Nimejuana na Chief Edward Anthony Makwaia mwaka wa 1967 sasa imepita miaka 50, yaani nusu karne.

Nilimfahamu Edward pale nilipoingia St. Joseph’s Convent mwaka wa 1967 kujiunga na elimu ya sekondari na tulisoma darasa moja hadi mwaka wa 1970. Yeye alikuwa anatolea Salvatorian College na mimi Kinondoni Primary School.

Katika miaka hii minne ya shule tuliingiliana sana na Edward akawa rafiki yangu kipenzi na kupitia kwake nikajuana na jamaa zake wengi kama akina Mwapachu na akina, Yunge na Gordon. Lakini katika maajabu ya maisha ni kuwa hata kabla sisi hatujazaliwa wazee wetu kwa njia za ajabu kabisa walikuwa na uhusiano wa hapa na pale.

Mmoja katika ukoo wa kina Yunge aliingiliana sana na wazee wangu katika miaka ya 1950 na nina picha nilipiga na Kapufi Yunge sote tukiwa watoto ingawa Kapufi alikuwa kanitangulia labda kwa miaka miwili hivi. Picha hii ninayo katika maktaba na nikiitia mkononi nitaiweka hapa. Picha hii ilikuwa ukutani kwa mama yangu mkubwa Bi. Mwanaisha bint Mohamed kwa kipindi chote cha maisha yake na kila alipokuwa akiizungumza ile picha alikuwa akimwita Kapufi, ‘’Chapa Ng’ombe,’’ kwa ajili ya ule Usukuma wake kwani Wasukuma ni wafugaji wakubwa wa ng’ombe.

Picha hii ilipigwa mwaka wa 1956 katika studio ya Gomes, iliyokuwa Acacia Avenue (Baada ya uhuru 1961 mtaa ukaitwa Independence Avenue na sasa ni Samora Avenue. Huyu Gomes ndiye aliyepiga ile picha maarufu ya waasisi wa TANU mwaka wa 1954). 


Waasisi wa TANU
Picha iliyopigwa na Gomes 7 Julai, 1954


Katika mwingiliano huu nikamkuta Edward ambae siku zile tulizoea kumwita Teddy akiwa na udugu na jamaa zangu wengi, mmoja wa ‘’cousin sister,’’ wake Lilian amabe tulizoea kumwita Lilly akiwa ni binti ya Abbas Sykes. Mimi, Teddy, Lily (ambae tulikuwa sote St. Josephs), Kleist Abdul Sykes, Ebby Abdul Sykes, Monalisa na Alma Ally Sykes ikawa sote tumekuwa pamoja utotoni tukiwa  na watoto wa koo mashuhuri katika Dar es Salaam ya wakati ule kama akina Lyabandi, Abbas Max, Sykes, Tsere, Singano, Bizuru, Msikinya, Lukindo, Mkwawa, Maharage, Masayanyika, Mang’enya, Muhuto, Fritsch, Kondo, Kafumba, Mzena, Bomani, Kahama, Kharusi na nyingineo nyingi. Kundi hili ambalo ndilo rika langu sasa sote sisi ni watu wazima na umri wetu wastani ni miaka 60.


Kulia: Balozi Mohamed Maharage Juma, Balozi Anthony Cheche, Balozi Patrick Tsere (mtoto wa Dr. Luciano Tsere)
Dr. Tsere ni mmoja wa madaktari watano ambao walisaidia sana kuijenga TAA baada ya Vita Kuu ya Pili, wengine ni Dr Vedasto Kyaruzi, Dr Wilbard Mwanjisi, Dr Michael Lugazia na Dr Joseph Mutahangarwa

Nyuma kulia ni Haitham ''Angela Davis'' Rashid, Mwandishi na Kamili Mussa.
Kushoto waliokaa ni Stella Emanuel. Esther Mzena na Wendo Mwapachu hii ilikuwa picnic tulifanya
Kigamboni kwenye nyumba ya mapumziko ya Rais Nyerere na aliyetupeleka hapo ni Magombe Makongoro, 1968
Katika familia hizi kuna historia kubwa ambazo kwa wakati ule wa utoto sikuzijua hadi nilipofika utu uzima. Historia ambazo zinakwenda na historia ya Tanganyika kuanzia kupigania uhuru wa Tanganyika na Zanzibar hadi kufikia mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka wa 1964. Historia ya mauaji kwa Zanzibar hadi vifungo vya siasa na kudhulumiwa kwa mali kote Tanganyika na Zanzibar.



Kulia: Ali Muhsin Barwani, Dr. Idarus Baalawy, Mohamed Shamte, Juma Aley na Ibun Saleh


Ilinichukua miaka mingi kuja kuijua historia ya ukoo wa Kharusi, Ibun na Shamte wa Zanzibar ingawa marafiki wawili wa baba yangu, Abdulaziz Twala na Jaha Ubwa walikuwa wameuawa baada ya mapinduzi. Ilinichukua miaka mingi pia kuja kuijua historia ya Chief Kidaha Makwaia. Nilipigwa na bumbuazi siku nilipoambiwa kuwa Abdul Sykes alimtaka Chief Kidaha Makwaia awe Waziri Mkuu Tanganyika itakapokuwa huru kwa Chief Kidaha kuwa rais wa TAA kisha waunde TANU yeye Chief Kidaha akiwa rais wa TANU. Hii iikuwa katika miaka ya 1950 wakati ule Chief Kidaha mjumbe wa LEGCO.


Kulia: Chief Edward Anthony Makwaia wa Busiya alipokwenda kumpa pole Kleist Sykes (kushoto) alipofiwa na mdogo wake Adam Abdulwahid Sykes. Kiasi cha nusu karne iliyopita baba zao watu hawa walikaa mara kadhaa wakijadili namna bora ya kuwaondoa Waingereza Tanganyika. Wakati ule Chief David Kidaha Makwaia alikuwa mjumbe wa LEGCO na Abdul Sykes alikuwa Katibu na Kaimu Rais wa TAA. Mengi ya mazungumzo haya yakifanyika nyumbani kwa baba yake Kleist.  Hakika dunia inazunguka.

Ilinichukua pia miaka mingi kuijua kwa undani historia ya ukoo wa Sykes lau kama hawa walikuwa jamaa wa karibu sana na wazee wangu kuanzia mababu zangu katika miaka ya 1920. Kwa hakika ilinichukua miaka mingi kuijua historia ya babu yangu mwenyewe katika kupigania uhuru wa Tanganyika na kupigania haki za wafanyakazi kupitia vyama vya wafanyakazi. Wakati ule sikuweza kutambua kuwa ule urafiki niliyokuwa nashuhudia baina ya Edward Makwaia na Kleist Sykes umetoka mbali kwa baba zao wakati wa harakati za kudai uhuru wa Tanganyika. Sikuweza kwa wakati ule kujua kuwa ule ukaribu wa Wendo Mwapachu na Kleist ulitoka huko nyuma pia.


Kulia: Asya Kharusi na Sambayawo Nyirenda hawa wote ni madaktari wa binadamu.
Baba yake Sambayawo, Alexander Gwebe Nyirenda ndiye aliyepandisha bendera ya Tanganyika Mlima
Kilimanjaro usiku wa uhuru
Kwa miaka ile ya utoto sisi watoto kutoka familia hizi sote tulikuwa wamoja tukicheza pamoja wakati mwingine watoto wa washindi na washindwa au ukipenda watoto wa waliodhulumu haki za watu na wadhulumiwa tukiwa wamoja bila kujua yale yaliyopitikana siku za nyuma kati ya wazee wetu na watawala waliokuwa madarakani.Ilinichukua miaka mingi kujua kuwa eneo lote la Upanga hadi kufikia Selender Bridge hadi Ikulu ilikuwa hodhi ya ukoo waTambaza hadi kufikia miaka ya 1800 na wakanyang'anywa na Wajerumani na hadi leo kuna makaburi ya mababu zao ndani ya Ikulu. Katka miaka ya 1980 waliamua kutoa ardhi iliyokuwa makaburi ya wazee wao Upanga ujengwe msikiti uliopewa jina, ''Masjid Maamur.'' Huu uliongeza misikiti inayowahusu Dar es Salaam kuwa mitatu wa kwanza ukiwa Masjid Mwinyikheri Akida ambao (una zaidi ya miaka 100 na ndiyo msikiti wa kale kupita yote Kariakoo) na Masjid Tambaza.

Kama ulivyo wastani wa umri wetu miaka 60 na miaka ya utoto wetu ilikuwa katika 1960s na Waingereza waliipa jina miaka hii wakaiita, ‘’The Roaring 60s,’’ na kwa hakika hii ilikuwa miaka ya aina yake. Tulikulia katika mazingira na utamaduni wa aina yake. Waingereza walikuwa wameondoka na wamewaachia utawala wazee wetu. Wazee wetu waliathirika na sisi watoto wao pia. 


Waliokaa kulia: Yusuf Zialor, Wendo Mwapachu
Kulia waliosimama ni Abdallah Tanbaza Abdul Mtemvu na Abdallah Mggambo

Palikuwa na aina mpya ya maisha ambayo kwa kiasi fulani yalitia afueni kwa wazee wetu kwa kukamata nafasi za kazi ambazo zamani zilikuwa zikishikiliwa na Wazungu na Waasia.




Wazee wetu walikuwa wanapumua kutokana na kazi ngumu ya kupigania uhuru katika miaka ya 1950.


|Chief David Kidaha Makwaia

Hata hivyo katika hali hii palikuwapo pia na majeruhi ya harakati za ukombozi wa Tanganyika. Baadhi ya majeruhi hawa walikuwa machifu ambao jana tu walikuwa watu wenye hadhi zao katika jamii lakini ghafla baada ya uhuru kupatikana na Mwalimu Nyerere kufuta uchifu, machifu hawa wakajikuta katika hali ambayo hawakuitegemea kamwe.

Hii ni historia ya pekee inayohitaji ipatiwe nafasi iandikwe.

Juu ya haya yote mmoja kati yetu watoto tuliolelewa katika miaka ya 1960 wakati Tanganyika inapata uhuru wake kutoka kwa Waingereza, leo ni Chief wa Busiya, utawala uliokuwa na nguvu katika wakati wake.

Vipi Edward na watu wa Busiya wameweza kurejesha uchifu wa mababu zao, vipi waliweza kumtawaza  Chief Edward Anthony Makwaia na mengi mengine nadhani iko siku yataelezwa.

Kwa sasa muhimu ni kuwa kila mwaka wakati wa Saba Saba, Wasukuma wa Busiya huwa wanafanya tamasha kuhuisha utamaduni wao na uchifu uliozaliwa upya wa Busiya.


Chief Edward Anthony Makwaia katika vazi la kichifu

Chief Edward Anthony Makwaia akicheza ngoma ya Kisukuma
2016

Kushoto aliyepiga magoti ni Mama Mary Mackeja mama yake Edward Makwaia
siku ya sherehe ya kuzaliwa kwake kulia wa kwanza ni Mwandishi, William Mfuko, Juma Volter Mwapachu na nyuma ya Mama Mackeja ni Wendo Mwapachu
1967

Kulia waliochutama: Edward Anthony Makwaia, Salma Bhatia, Asya Kharusi, Razia Bhatia, Iddi Mvule, David Gabba,
Waliosimama kulia: Mwandishi, Shayo, Maximillian Mafuru
Kulia waliosimama: Gulamabbas Jivraj, Israel, Charles Mesquita


Picinic Form One D St. Joseph's Convent 1967 Kigamboni Beach
Kulia waliokaa: Iqbal Bapumia, Salma na Razia Bhatia wengine majina sikumbuki
Kulia waliosimama: David Gabba nyuma ya Daivid ni Edward Makwaia anefatia jina sikumbuki baada yake ni Sambayawo Nyirenda, Fortunata, Zariha Juma, Wun Siang Chou, Shenaz na wa mwisho ni mwalimu wetu wa darasa Miss Kindy.
Nyuma kabisa baada ya Edward Makwaia ni Khalid Abdallah

Kulia: Edward Makwaia, Willliam Mfuko, Mwandishi na Khalid Abdallah

Kulia: Mwandishi, Yusuf Zialor, Kleist Abdulwahid Sykes, Bubby, Abdallah Tambaza waliokaa kulia ni Abdul Mtemvu, Wendo Mtega Mwapachu na Kessy 

Kushoto Lilian Abbas Sykes akizungumza na Jaji Mark Bomani mwisho kulia ni Mohamed Chande Jaji Mkuu Mstaafu
Kulia waliokaa: Shayo, Iqbal Bapumia
Kulia waliosimama: David Gabba, John Gondwe, Sambayawo Nyirenda, Khalis Abdallah, Abdul Yusuf, Shaib Salum
Nyuma: Maxmillian Mafuru, Asya Kharusi Jennnifer Gordon, Mwandishi na Edward Makwaia

Mwandishi katika sherehe ya siku za kuzaliwa Iqbal Bapumia ''class mate,'' 1969
Picha kapiga Iqbal