Friday, 10 June 2016

KUTOKA JF: PROF. HAROUB OTHMAN, MWALIMU NYERERE NA KUMBUKUMBU ZA ALI MUHSIN BARWANI






Kwezisho,
Nashukuru kuwa umesoma kitabu.
Hayo matundu usemayo mimi siyajui.

Nimejitahidi kutafiti na kuandika kadri ya uwezo wangu.

Mara nyingi hupata maswali ya sampuli yako na mimi
huwa najibu kuwa labda Nyerere angeliandika historia
yake na vipi alikutana na Abdul Sykes tungeweza kupata
mengi.

Lakini kwa bahati mbaya sana Nyerere hakuandika.

Kwa nini hakuandika historia hii muhimu katika maisha yake
hatutoweza kujua kwa uhakika ila tutafanya, ''speculation,'' tu.

Miaka michache iliyopita katika ukumbi huu huu palifumuka
vumbi kubwa niliposema kuwa hotuba ya Nyerere aliyosoma
UNO 1955 ilikuwa imetayarishwa 1950 na jopo la Abdul Sykes,
Hamza Mwapachu, Sheikh Hassan bin Amir, Stephen
Mhando, Dr.Vedasto, Kyaruzi 
na timu nzima ya TAA Political
Subcommitee ambayo Abdul alikuwa katibu wake.

Waliofuatilia mnakasha ule watakumbuka.
Kwa wengi hii ilikuwa habari mpya.

Kuna baadhi walikuwa hawajasikia hata hilo jina la Abdul na
majina mengine niliyotaja kama Sheikh Hassan bin Amir na
Said Chaurembo.

Ilikuwa kama vile nimemtukana Mwalimu Nyerere.

Na kila nilipojaribu kueleza historia ya TANU kama niijuavyo
ndivyo nilivyozidisha ghadhabu za baadhi ya watu.

Sishangai kukuona unahangaika na kuwa katika hali ya kutotosheka
na niliyoandika.

Hauko peke yako katika hili.
Mwalimu wangu Prof. Haroub Othman yeye alikwenda mbali zaidi.

Prof. Haroub alimkabili Mwalimu Nyerere uso kwa macho kutaka
kusikia kutoka kinywani kwake ukweli katika yale niliyoandika.

Je ungependa kujua jibu la Mwalimu Nyerere?



Onyx,
Mwaka wa 1974 Ali Muhsin Barwani alifunguliwa kutoka jela za Bara ambako
Nyerere alimfunga kwa miaka 10 baada ya serikali ya Zanzibar kupinduliwa
mwaka wa 1964.

Hakupita muda Ali Muhsin alitoroka kwa kuvuka mpaka wa Horohoro kwa njia za
panya kwa miguu usiku wa manane akisaidiwa na wasamaria wema na hivyo
kuweza kufika Mombasa kisha Nairobi na kupata msaada wa UNHCR waliomsaidia
kufika Cairo kuungana na familia yake.

Ali Muhsin alitoroka Tanzania mwezi Mtukufu wa Ramadhani kama huu.
Mwaka wa 1997 aliandika kitabu, ''Conflicts and Harmony in Zanzibar.''

Unaweza kumjua Ali Muhsin kwa kuingia hapo chini:
Mohamed Said: KUTOKA JF: KUMBUKUMBU ZA ALI MUHSIN BARWANI: ''CONFLICTS AND HARMONY IN ZANZIBAR''
Mohamed Said: TUJIKUMBUSHE: SHEIKH ALI MUHSIN BARWANI MMOJA WA WAPIGANIA UHURU WA ZANZIBAR
Mohamed Said: MAISHA YA SIASA YA SHEIKH ALI MUHSIN BARWANI (1919 - 2006) - KUMBUKUMBU YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR

[​IMG]
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa U Thant akisalimiana na
Waziri Mkuu wa Zanzibar Mohamed Shamte na Waziri wa
Mambo ya Nchi za Nje Ali Muhsin Barwani New York


Katika kitabu chake hicho Ali Muhsin alimueleza Nyerere kwa namna
ambayo haikuwahi kufanywa kabla.

Kitabu hiki kilipigwa marufuku kimya kimya kuingia Zanzibar lakini photo
copy ya kitabu iliweza kupenyezwa na kuwafikia baadhi ya watu.

Kila aliyekisoma alipata mshtuko wa aina yake na mmoja wa wasomaji
wa kitabu hiki alikuwa Prof. Haroub Othman.

Mara tu baada ya kutoka kitabu cha Ali Muhsin ndipo kikatoka kitabu
cha Abdul Sykes mwaka wa 1998.

Kama ilivyokuwa kwa kitabu cha Ali Muhsin, kitabu hiki nacho kilikuja
na mengine ambayo yalionekana kuwataabisha baadhi ya watu na
mmoja katika hao waliotaabika alikuwa Prof. Haroub Othman.

Hakuweza kustahamili ndipo alipofunga safari hadi nyumbani kwa
Mwalimu Nyerere na kumuomba akijibu kitabu cha Ali Muhsin
Barwani 
na kitabu cha Mohamed Said kwani vikiachiwa bila majibu
vitaharibu ''legacy'' yake.

Mwalimu Nyerere alikuwa kasoma vitabu vyote viwili na jibu alilompa
Prof. Haroub ni kuwa yeye Haroub atengeneze kamati na yeye atakuja
kueleza yote ili wao waandike historia yake.

Kamati ilitengenezwa lakini hakuna kilichofanyika hadi Mwalimu Nyerere
alipofariki dunia mwaka 1999.

Kitabu cha Ali Muhsin Barwani kinapatikana Tanzania Publishing House,
Ibn Hazm Media Centre Msikiti wa Mtoro na Manyema na Elite Bookshop
Mbezi Samaki kwa bei ya shs: 10,000 hadi shs 13,000.

No comments: