Friday 26 August 2016

SHEREHE YA KUWEKA JIWE LA MSINGI LA MAKAO MAKUU YA BAKWATA INAKUMBUSHA KUWEKWA NA NYERERE JIWE LA MSINGI LA CHUO KIKUU CHA WAISLAM CHANG’OMBE 1968

Kulia wa kwanza ni Tewa Said Tewa aliyekuwa rais wa EAMWS (Tanzania)

Mwaka wa 1968 Mufti wa Tanzania alikuwa Sheikh Hassan bin Amir. Mufti Sheikh Hassan bin Amir alikuwa mwanazuoni mkubwa, mwalimu, mwandishi na mwanasiasa kuanzia enzi za TAA akiwa mwaka wa 1950 mmoja wa wajumbe wa TAA Political Subcommittee. Sheikh Hassan bin Amir alipigana bega kwa bega na Mwalimu Nyerere ndani ya TANU kukielekeza chama katika mstari wa kuwaunganisha wananchi kuwa wamoja kwa mafanikio makubwa sana bila kujali tofauti za dini zao. Sheikh Hassan bin Amir aliweza kuanzia mwaka wa 1955 kutuliza hamasa za Uislam katika TANU ambazo laiti zingeliachiwa zimee zingelipanda mbegu mbaya sana ya ubaguzi kati ya Waislam waliokuwa mstari wa mbele na ndani kindakindaki dhidi ya Waingereza na ndugu zao Wakristo ambao hawakujitokeza kwa dhati kupambana na ukoloni.

Uhuru ulipopatikana mwaka wa 1961 Sheikh Hassan bin Amir akatangaza kupumzika siasa na akaanzisha Daawat Islamiyya (Wito kwa Waislam) nia ikiwa kutumikia Uislam khasa katika elimu kwa Waislam, elimu ambayo ilikuwa imehodhiwa na wamishionari wakati wa ukoloni. Katibu wa Daawat Islamiyya alikuwa Schneider Abdillah Plantan. Kufikia lengo hili Sheikh Hassan bin Amir akishirikiana na viongozi wa East African Muslim Welfare Society (EAMWS) Tewa Said Tewa na Aziz Khaki kwa pamoja waliweza kupata msaada kutoka Serikali ya Misri wa kujenga Chuo Kikuu Cha Kiislam. Mjenzi alipatakana, Al Nasr kampuni ya Kimisri na jiwe la msingi la chuo likawekwa na Mwalimu Julius Nyerere kwenye sherehe kubwa sana Chang’ombe iliyohudhuriwa na Waislam, Mabalozi wa Nchi za Kiislam waliokuwa Tanzania na viongozi wa serikali.


Ahmed Rashad Ali wakati ule Assistant Principal Secretary Ministry of Information anasema alikuwapo katika sherehe ile na alikuwa nyuma ya Nyerere alipokuwa anatembezwa kuonyeshwa michoro ya majengo na kupewa maelezo ya jinsi chuo kitakavyokuwa kikikamilika. Ahmed Rashad anasema alikuwa akimuangalia Nyerere kila hatua aliyokuwa akipiga na kupita huku akisindikizwa na Tewa Said Tewa na Sheikh Hassan bin Amir. Akiangalia kwa makini na kwa sura ya mshangao, akitikisa kichwa kuashiria kuwa anaelewa yote anayoelezwa. Anasema kulikuwa na mtangazaji wa Radio Tanzania Dar es Salaam aliyekuwa akirekodi sherehe ile na yeye kama afisa wa kutoka Wizara ya Habari jicho lake lilikuwa mara kwa mara akilitupa kwa yule kijana mtangazaji. Ahmed Rashad anasema ndipo katikati ya kutangaza kwake alipomuona yule mtangazaji akiviringisha ile tape ikanasa na akaivuta kwa nguvu na kuitoa yote katika mashine na kwa uzoefu wake Ahmed Rashad anasema alikuwa na uhakika ule mkanda ulishaharibika hautofaa tena kutiwa kwenye mashine kuweza kutoa sauti.

Alimfata kumwelekeza nini cha kufanya ili aendelee kurekodi lakini kijana alionyesha uzito wa kuelewa nini aliyokuwa akielezwa. Ahmed Rashad Ali anasema yale yaliyofuatia sherehe ile baada ya miezi michache ilimrudisha nyuma kwenye sherehe ile ya kuweka jiwe la msingi wa Chuo Kikuu Cha Kiislam na ikamjia kuwa huenda yule kijana aliharibu mkanda ule wa sherehe ile kwa makusudi. Nyerere baada ya kuweka jiwe la msingi wa chuo kile alipiiga marufuku EAMWS na Sheikh Hassan bin Amir akakamatwa usiku na maafisa wa Usalama wa Taifa kwa kuwa Mkuu wa Polisi (IGP) wa wakati ule Hamza Aziz alikataa kutii amri ya kumkamata Sheikh Hassan ikabidi Usalama wa Taifa ndiyo wamkamate kitu ambacho ni kinyume cha taratibu. Sheikh Hassan bin Amir akafukuzwa Tanzania Bara akarejeshwa kwao Zanzibar ambako alifariki mwaka wa 1979. Siku chache baadae  serikali ya Nyerere ikawaundia Waislam BAKWATA kuziba pengo la EAMWS.

Katika uwanja ule wa EAMWS serikali inapotaka kuwajengea BAKWATA Makao Makuu yao mwaka wa 1968 palikuwa na majengo mapya ya shule ya Kinondoni. Shule hii ilianza mwaka wa 1966 katika majengo ya Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika yaliyokuwa Mtaa wa Lumumba na Aggrey ambako wanafunzi wa kwanza wa kidato cha kwanza walianza kusoma hapo kisha mwaka huo huo wakahamia Kinondoni baada ya majengo yale kukamilika. Shule hii ilijengwa na EAMWS kutokana na maazimio ya Muslim Congress ya mwaka wa 1962. Mwaka huo iliamuliwa kuwa kwa kuwa uhuru ushapatikana na kwa sababu ukoloni uliwaathiri sana Waislam katika kuwanyima elimu juhudi za makusudi zifanywe za kujenga shule na mwisho chuo kikuu na ndiyo mwaka wa 1968 Nyerere akaalikwa kuweka jiwe la msingi wa chuo hicho.

Katika  moja ya madarasa ya shule hiyo ya Kinondoni mwaka huo wa 1968 mwezi Septemba, uongozi wa EAMWS ulikutana kujadili hatima ya EAMWS na hatima ya chuo kikuu kwa kuwa ghafla kulizuka kundi la viongozi wa EAMWS kutoka katika majimbo waliokuwa hawaitaki EAMWS kwa sababu ilikuwa ikiongozwa na Muhindi, Aga Khan wao walikuwa wanataka Uislam wa kizalendo. Kundi hili lilikuwa likipewa nguvu na serikali na katika moja ya nasaha za Tewa Said Tewa ambae ndiye alikuwa Rais wa EAMWS kwa upande wa Tanzania aliwaeleza Waislam kuwa, endapo EAMWS itavunjika huo ndiyo utakuwa mwisho wa ujenzi wa  chuo kikuu ambacho jiwe la msingi tayari lilikuwa limekwishawekwa na Nyerere.

Nimeandika haya hapa juu kwa kuwa baada ya Waislam kuelezwa kuwa serikali itawajengea BAKWATA Makao Makuu kumekuwa na maneno mengi katika mitandano ya kijamii kujadili jambo hili. Historia ya BAKWATA ina mengi na ni kisa kirefu. Ili mtu aweze kuelewa imefikaje hii leo BAKWATA baada ya miaka 48 inajengewa makao makuu na serikali ni vyema mtu akaijua kwanza historia ya BAKWATA. Atakae kuijua BAKWATA anaweza kuingia hapo chini:





No comments: