Ali Migeyo
Shujaa Kutoka Bukoba
![]() |
| Ali Migeyo |
Ali Migeyo alipigwa mabomu ya machozi na Waingereza Kamachumu mwaka 1953 wakati akidai haki ya Mwafrika. Akakamatwa na kufungwa jela ya Isanga, Dodoma. Uhuru ulipopatikana akafungwa tena na serikali kwa kupigania haki ile ile.
Kuna watu wawili walistahili kuwa katika orodha ya wale watu 17 walioasisi TANU. Mtu wa kwanza ni Hamza Kibwana Mwapachu na wa pili ni Sheikh Ali Migeyo. Hamza Mwapachu alikuwa ''kifungo cha siri' Nansio lakini Ali Migeyo alikuwa katika kifungo cha dhahir Isanga.
Fatilia ukurusa huu umsome shujaa huyu wa uhuru ambae leo hii hatajiki.
Vipande kutoka katika ''Maisha na Nyakati za Abdulwahid Sykes...''
Vipande kutoka katika ''Maisha na Nyakati za Abdulwahid Sykes...''
''Katika
majimbo ya ziwa katika miaka ya 1950 tawi la TAA lililokuwa na nguvu lilikuwa
tawi la Mwanza. Viongozi wake, Saadan Abdu Kandoro, Mmanyema na mtunga
mashairi, na Bhoke Munanka walikuwa wakitupiwa macho na serikali. Kandoro na
Munanka walikuwa wakijaribu kummunga mkono Ali Migeyo ambaye peke yake alikuwa
akijaribu kufungua matawi ya TAA sehemu za Bukoba. [1] Pale Bukoba
mwanasiasa mkongwe Migeyo, akiwa na umri wa miaka 53 alikuwa akihangaika
kufungua matawi katika jimbo la Ziwa Magharibi. Akiwa Kamachumu katika kampeni
hii, Migeyo alishambuliwa na mabomu ya kutoa machozi alipokuwa akihutubia
mkutano wa hadhara. Migeyo alikuwa na kipawa cha kuzungumza na hotuba zake
zilikuwa za kusisimua kiasi kwamba ilikuwa rahisi sana kwake kuwapandisha watu
jazba. Siku ile ya mkasa wa mabomu alikuwa akiwaandaa wananchi kuipokea TANU.
Alipokuwa akihutubu askari walikuja kuwatawanya watu kutoka kwa viwanja vya
mkutano. Mabomu ya machozi yalitupwa na Migeyo akatiwa mbaroni. Wakoloni kwa
ujanja wakamshtaki Migeyo peke yake bila ya kumuunganisha na TAA, chama
alichokuwa akikitumikia. Iliffe anaihadithia hali ilivyokuwa kanda ya ziwa:
Hatari iliyokuwepo ni kuwa katika kindibwindibwi
cha harakati za Mau Mau, vichwa maji wa kanda ya ziwa wangeweza kusababisha
vurugu ambayo ingevunja umoja wa TAA wakitekeleza 'mapinduzi' dhidi ya
wanasiasa wanaokubalika kama ilivyotokea Kenya, Senegal na Sierra Leone - au
kuichochea TAA katika mapambano ya waziwazi na serikali, na kuifanya kazi ya
kujenga utaifa kuwa ngumu.[1]
Dr
Lugazia alikuwa anatoka Bukoba, alitaka kuhakikisha kuwa viongozi wa TAA kutoka
nyumbani kwao hawapitwi na mkutano ule muhimu wa kuunda TANU. Dr Lugazia
alichukua juhudi za makusudi kupeleka rasimu ya katiba ya TAA kwa tawi la
Bukoba. Lakini baada ya kukamatwa kwa Migeyo, TAA ilikuwa imepoteza uhai wake.
Hakuna mtu aliyeweza kuwasha tena moto aliouwasha Migeyo. Barua muhimu ya
mwaliko iliyoandikiwa TAA Bukoba na Dr Lugazia ikiambatanisha katiba ya TANU ambayo
ilitakiwa kujadiliwa katika mkutano uliokuwa uitishwe Dar es Salaam
haikushughulikiwa. Hii ndiyo sababu katika mkutano wa kuasisi TANU mwaka 1954
Bukoba haikuwakilishwa.
Uongozi
wa TAA makao makuu uliona kuwa kukamatwa na kushtakiwa kwa Migeyo ilikuwa
sawasawa na vitisho dhahiri dhidi yao, ikichukuliwa kuwa wananchi katika
mkutano ule walikuwa wamejikusanya kwa amani. Kisa kile kilikuwa salamu za wazi
kutoka kwa Gavana Twining kuwa hakuwa tayari kuwaona watu wakihamasishwa dhidi
ya serikali. Abdulwahid aliwasiliana na Seaton na kumwomba amtetee Migeyo
ambaye alikuwa anashtakiwa Bukoba kwa kosa la jinai. Kamati ya TAA ya Mgogoro
wa Ardhi ya Wameru iliyokuwa ikitembelea kanda ya ziwa ilifika Bukoba kujionea
hali halisi ya mambo pale Kamachumu. Tarehe 14 Aprili, 1954 Migeyo alihukumiwa
kifungo cha miaka mitatu kwa kufanya mkutano bila ya kibali cha mkuu wa
Tarafa. Baadaye April 1954, Abdulwahid,
Nyerere na Rupia walikwenda Bugandika, nyumbani kwa Migeyo.[1]
TANU ilipoundwa tarehe 7 Julai, 1954, Migeyo alikuwa jela ya Butimba, Mwanza
akitumikia kifungo. Felix Muganda akitafakari tatizo la Bukoba alimwandikia
Nyerere kumfahamisha hali ya mambo ilivyo: ''Nimeuita uongozi wote wa Wahaya
kuwahamasisha ili wasije wakakata tamaa kutokana na yale yaliyompata Migeyo.''[1]
Hapo baadaye, uhuru ulipopatikana tutaona jinsi Ali Migeyo alivyoandamwa na
serikali ya Nyerere na mwisho kuwekwa kizuizini kwa kile kilichojulikana kama ‘’kuchanganya
dini na siasa.’’

No comments:
Post a Comment