Saturday, 15 February 2014

BAKWATA Sehemu ya Nane


BAKWATA
Sehemu ya Nane

Uchambuzi wa Dhulma
Tasnifu ya Kiwanuka toka ilipochapishwa mwaka 1973 imesimama kama ndiyo ukweli kwa yale yaliyotokea katika ''mgogoro'' wa Waislam. Msimamo wa Kiwanuka ni kuwa Nyerere na serikali ilikuwa imefanya sawa kwa yale yaliyofanyika ili kudumisha umoja wa taifa la Tanzania. Yeye anaunga mkono dhana ya kuwa siasa na dini zisichanganywe. Vitu hivi viwili lazima vitenganishwe. Kami ilivyokuwa katika maandishi mengi kuhusu historia ya siasa ya Tanganyika, tasnifu imeshindwa kabisa kuunganisha mchango wa Waislam katika kuleta umoja wa Waafrika wa Tanganyika wakati wa kudai uhuru na kwa ajili hii tasnifu imeshindwa kueleza mategemeo ya Waislam katika Tanganyika huru. Tasnifu ya Kiwanuka haielezi ni vipi hawa Wakristo ambao wameshika madaraka katika siasa nyanja nyingine jinsi walivyoyapata na nini msingi wa madaraka hayo. Kiwanuka katika tasnifu yake anawaonyesha Waislam wakiwa katika mapambano na serikali na haonyeshi nafasi ya vyombo vya dola katika mfarakano huo. Kama angelikuwa anaielewa historia ya uhuru wa Tanganyika asingeshindwa kujua sababu za Waislam kupambana na serikali ya Tanganyika huru iliyokuwa imehodhiwa na Wakristo. Halikadhalika angelijua sababu kwa nini serikali ilikuwa inataka sana kuwa na jumuiya ya Waislam ambayo ingekuwa na mamlaka nayo na kuiamrisha kama ilivyokuwa katika taasisi nyingine za umma kama vyama wafanyakazi. Kama Waislam wangekuwa hawataki umoja wa wananchi wangemuunga mkono Sheikh Suleiman Takadir mwaka 1958 alipompinga Nyerere na AMNUT mwaka 1959. Walichokuwa wanakidai Waislam ilikuwa ni fursa sawa kati ya Waislam na Wakristo katika kugawana madaraka ya kuendesha nchi na kuwepo kwa fursa sawa katika kutoa elimu. Huku si kuchanganya dini na siasa. Huku ni kutafuta haki ili taifa lijingengeke katika misingi hiyo.

Mwaka 1963 walimu Wakristo Bukoba wakiungwa mmkono na Kanisa Katoliki, waliwapinga wagombea Waislam walioteuliwa na TANU katika uchaguzi wa serikali za mitaa. Wagombea Waislam walishindwa katika uchaguzi ule. Kanisa lilikuwa limechanganya dini na siasa kwa kuwapinga Waislam wasichaguliwe kushiriki katika kuongoza nchi. Hakuna taarifa zozote zinazoonyesha kama serikali ya Nyerere ilichukua hatua yoyote dhidi ya Kanisa au dhidi ya wale wagombea Wakatoliki. Lakini Waislam walikamatwa na kuwekwa kizuizini kwa kukataa utawala wa Kikristo katika TANU ñ chama ambacho Waislam walikiianzisha na kukijenga ili kiondoe dhulma. Halamshauri Kuu ya Taifa TANU ilifuta katika TANU Baraza la Wazee wa TANU lililokuwa na wajumbe Waislam watupu kwa kile kilichoitwa ëkuchanganya dini na siasaí.

Kanisa Katoliki Bukoba lilikosa ujanja kwa hiyo njama zake zikaweza kugundulika mapema. Nguvu mpya dhidi ya Uislam na Waislam ilitumia ujanja na mbinu za hali ya juu na hivyo ikafanikiwa kuihujumu EAMWS na kuiweka BAKWATA kuwaongoza Waislam. Vipi serikali ambayo sifa yake ni kupinga ubaguzi wa rangi na kutetea umoja wa kitaifa, itawaruhusu kikundi kisichozidi watu watano kutumia magazeti ya TANU- The Nationalist, Uhuru, Radio Tanzania, polisi na Usalama wa Taifa , vyombo vilivyo chini ya vya dola kuamrisha utengano wa watu na kueneza siasa za ubaguzi  wa rangi. Vipi itaundwa jumuiya ya Waislam ambayo licha kuwa  haina ridhaa ya Waislam wenyewe vilevile haina ulamaa hata mmoja ndani ya uongozi wake. BAKWATA haikuundwa kwa maslahi ya kumtumikia Allah. Uongozi wa Kikristo uliokuwa madarakani ulikuwa na hofu ya hali yake ya baadae huku wakikabiliana na Waislam walio huru chini ya jumuiya yao wenyewe iliyo huru na mbali na serikali na Kanisa.

Kwa kuwa serikali haikuonyesha dalili zozote za kutaka kuleta fursa sawa kwa wote katika elimu na kugawana madaraka, ikijizatiti katika kuiacha dhulma ya kikoloni iendelee, ilikuwa wazi awamu ya pili ya harakati itaanzishwa dhidi ya serikali iliyohodhiwa na Wakristo kama vile Waislam walivyopambana na udhalimu wa Kikristo ndani ya ukoloni wa Waingereza. Dalili zilikuwa wazi kuwa harakati zilikuwa zimeenza na hazitakuwa kupitia TANU kwa sababu ndani ya TANU Waislam walikuwa wameshaanza kupigwa vita. Harakati hizi za pili zilikuwa ziwe chini ya umoja wa Waislam wote. Hii ilisababisha hofu kuu kwa serikali na kwa ajili ya woga ule ikawa imejiweka tayari kujikinga na jambo kama hilo lisitokee. Kwa ajili hii serikali ikawa inavamia kila Muislam aliyedhaniwa ni tishio kwa Kanisa. Ni katika hofu hii ndiyo maana hata historia ya kweli ya uhuru wa Tanganyika inaogopwa kuandikwa. Hii ni moja ya njia ambayo serikali inadhani inaweza kujikinga dhidi ya hisia za Waislam.

Wakati kundi lililojitenga kutoka EAMWS huku likiungwa mkono na serikali, likimshutumu Aga Khan kwa kuwa Muasia, hakuna aliyethubutu kuonyesha kidole kwa taasisi za Kikristo katika Tanzania zinazoongozwa na Wazungu na kufadhiliwa na mataifa kadhaa ya Ulaya. Hakuna aliyethubutu kuonyesha kidole kuelekeza kwa Kanisa Katoliki ambalo lina uwakilishi wa kibalozi wa Papa nchini Tanzania. Kwa kuwa inafahamika kuwa Kanisa Katoliki linalazimisha utiifu kwa Kanisa kutoka kwa waumini wake, na kwa kuwa Kanisa lina mawakala wake katika TANU na utumishi wa serikali, ingelikuwa ni Ukristo ambao   ungehatarisha usalama wa nchi na wala si Uislam. Wakati Nyerere anawadhoofisha Waislam kwa hila za wagawe uwatawale, Wakristo walikuwa wanazidi kupata nguvu kila kukicha.

Hadi ilipofika mwaka wa 1970 vumbi la mgogoro wa EAMWS likawa limetulia. Mwaka huo Nyerere alihudhuria semina kwa ajili ya dini na viongozi wa siasa. Semina hii kwa ujanja ilitayarishwa na Tanzania Episcopal Conference kamati ya juu kabisa ya Kanisa Katoliki inayotunga sera zote za Kanisa. Katika semina ile kwa mara ya kwanza hadharani Nyerere alizungumza kuhusu TANU na sura yake ya dini. Nyerere alisema, ‘’Chama chetu, TANU, hakina dini. Ni chama cha siasa tu na hakuna mipango au makubaliano na dini maalumi.’’ Maneno haya yanaweza kuwa na maana moja tu, nayo ni kuwa TANU jinsi miaka ilivyokuwa inapita, imepoteza taswira yake ya Uislam. Kuanzia mwaka 1954 TANU ilikuwa na dini na dini ya TANU ilikuwa Uislam. Historia ya TANU na harakati za kudai uhuru wa Tanganyika ndiyo shahidi wa ukewli huu. Juu ya haya yote, Waislam wanakataa kudhalilishwa na serikali na Kanisa. Waislam hawajaacha harakati za kupambana na serikali na Kanisa kwa njia mbalimbali ambazo serikali inadai ni ëkashfa na matusií kwa Ukristo. Serikali imeshindwa kutuliza hasira za Waislam dhidi yake na dhidi ya Kanisa. Sababu ni kuwa wakati umebadilika. Waislam wamepoteza imani na serikali. Waislam hawaamini kuwa serikali haina dini. Waislam wametambua kuwa wanadhalilishwa na kunyimwa haki kwa kuwa serikali ni ya Wakristo. Salama yao na dini yao kama ilivyokuwa wakati wa ukoloni, ipo katika kuondoa dhulma inayotawala nchi kwa kuwa hivi sasa Ukristo umechukua nafasi ya ukoloni.

Kulia Kwenda Kushoto: Sheikh Abdallah Idd Chaurembo, Julius Nyerere


Mwisho
Waislam waliikataa BAKWATA na kukawa na harakati za chini kwa chini kuipinga BAKWATA na viongozi wake kuanzia ilipoasisiwa mwaka 1968. Ilipofika mwaka 1991 juhudi hizi zilizaa matunda kwa Waislam kuiteka BAKWATA...

Kwa atakae kujua mengi kuhusu juhudi hizi na aingie hapa chini:
http://www.mohammedsaid.com/2013/12/the-founding-of-baraza-kuu-supreme.html

No comments: