TANU Ilivyovunja Ngome
ya Kanisa Katoliki Jimbo la Kusini, 1955
Sehemu ya Tatu
Nyerere
na msafara wake ulipokelewa na uongozi wa TANU wa Lindi huko Mbanji, kijiji
kidogo nje ya mji. Msafara wa Nyerere ulipowasili Mbanji ilikuwa kiasi cha saa
moja jioni hivi na giza lilikuwa linaanza kutanda. Mbali na Mpunga na wale
wajumbe wawili waliokutana na Nyerere mjini Dar es Salaam mwezi uliopita,
hakuna hata mtu kati ya umma ule uliokuja kupokea ujumbe kutoka makao makuu ya
TANU aliyekuwa anajua Nyerere anafanana vipi. Mpunga, dereva wa lori,
alijibagua kutoka kwa lile kundi la watu akawa amesimama pembeni ili Nyerere
apate kumuona. Baada ya Nyerere kumtia Mpunga
machoni, Mpunga alimwendea kumsalimu Nyerere, Tambwe na Diwani; kisha
aliligeukia lile kundi la watu kumtambulisha Nyerere kwa wananchi akilitaja
jina lake kwa sauti kubwa. Baada ya hapo aliutambulisha ule ujumbe wa Nyerere.
Nyerere na ujumbe wake ulisindikizwa kwa shangwe na kundi la watu hadi ofisi ya
TANU kwenye nyumba ya Mnonji. Kupakana na ofisi ya TANU ilikuwepo nyumba ya
seremala mmoja, Issa bin Ali Naliwanda. Hii ndiyo nyumba iliyochaguliwa alale
Nyerere na ujumbe wake, si kwa sababu ilikuwa nzuri kupita zote. Ilichaguliwa
na kupewa heshima hii kwa sababu ilikuwa karibu sana na ofisi ya TANU na hivyo
basi ilirahisishia TANU kazi ya ulinzi wa Nyerere. Siku iliyofuata ilikuwa
Jumapili na Nyerere aliwaomba wenyeji wake apelekwe kanisani kwa ajili ya
ibada.
Kanisa
Katoliki mjini Lindi ni jengo la fahari lililoko ufukweni katika Bahari ya
Hindi. Lindi ulikuwa mji wa Waislam. Mbali na mlio wa kengele za kanisa hakuna
mtu pale mjini aliyekuwa akishughulishwa na kile kilichokuwa kikifanyika kwenye
viwanja vya kanisa. Watu wachache waliokuwa wakienda kusali kanisani walikuwa
Wakristo waliokuja Lindi kutoka sehemu nyingine za Tanganyika kufanya kazi
katika ofisi za serikali. Ghafla mahala hapa palipokuwa pweke, palipopuuzwa kwa
miaka na Waislam wa mjini, pakawa muhimu kwa sababu rais wa TANU ambae alikuwa
Mkatoliki alikuwa na haja ya kuhudhuria ibada pale kanisani. Hakuna mtu katika
uongozi wa TANU wa Lindi aliyejua ndani ya kanisa lile kulikuwa vipi wala
hapakuwa na yoyote kati yao aliyewahi kuingia ndani ya kanisa, si Lindi wala
mahali popote pale. Uongozi wa TANU wa Waislam mjini Lindi haukumwamini Mkristo
yoyote kumsindikiza Nyerere kanisani ili kumpa ulinzi. Baada ya kujadili suala
hilo kwa urefu hatimaye iliamuliwa kuwa
Mpunga na wanachama wachache Waislam wenye kuaminika lazima wamsindikize
Nyerere kanisani na wengine wabakie nje kulinda mlango.
Jumapili
hiyo Nyerere aliingia ndani ya kanisa Katoliki mjini Lindi akifuatwa nyuma na
walinzi wake Waislam wakiongozwa na Salum Mpunga, dereva wa lori shupavu. Misa
hii maalumĂ ilidumu katika fikra za wale Wakristo waliokuwepo pale kanisani kwa
miaka mingi kwa kuwa tukio hilo liliwagusa sana Wakristo walioshuhudia mkasa
ule ndani ya kanisa la Lindi. Hii huenda ilikuwa mara ya kwanza na ya mwisho
kwa Nyerere kumsalia Mungu wake huku akiwa amesimamiwa na Waislam.
No comments:
Post a Comment