BAKWATA
Sehemu ya Nne

Mwalimu Nyerere alikuwa anawaambia Tewa Said Tewa na Bibi Titi Mohamed uso kwa macho wajiandae kwa kile kilichokuwa dhahiri: vita ya msalaba dhidi ya umoja wa Waislam. Sheikh Suleiman Takadir aliyaona haya na aliiomba TANU toka mwaka wa 1958 pawepo na uhakika kuwa Wakristo ambao walikuwa wanapanda migongo ya Waislam na kuchukua uongozi hawatakuja kuwafanyia uadui Waislam pale Waislam watakapokuwa sasa wanataka kugawana madaraka ya kuongoza nchi sawa na Wakristo baada ya uhuru. Tewa Said Tewa, muasisi wa TANU, waziri katika serikali ya kwanza ya uhuru, balozi katika Jamuhuri ya watu wa China na Rais wa baraza la Tanzania la EAMWS, pamoja na Bibi Titi, mwanamke aliowakusanya wanawake wote nyuma ya Mwalimu Nyerere na TANU, walikuwa wakisemwa na Nyerere kama vile watoto wadogo wa shule waliokuwa watukutu kwa sababu tu, walikuja kumfahamisha Rais kuhusu kukiukwa kwa maadili ambayo ilihitaji yeye ashughulikie mara moja na kutoa uamuzi.
Ulipofika
mwezi Oktoba, mgogoro ukachukua mwelekeo mpya pale Makamo wa Rais wa
Tanzania, Abeid Amani Karume, alipoishambulia EAMWS kuwa ni chombo cha
unyonyaji. Kutokea hapo Karume akawa
anafanya mashambulizi na kutoa shutuma kwa EAMWS, wakati mwingine akijaribu
kufafananisha uhusiano wa EAMWS na Waislam katika mtazamo wa Ki-Marxist, akidai
kuwa jumuiya ile kilikuwa chombo cha makabaila wakubwa na kilikuwa chini yao
kikiwanyonya watu wa chiniĆ. Mgogoro
ulipozidi kukua mashambulizi yakahama sasa kutoka EAMWS na kuhamia kwenye
mafunzo ya msingi katika Qur'an Tukufu. Katika mkutano wa hadhara Zanzibar,
Karume alitoa changamoto kwa Muislam yeyote ajitokeze bila ya woga kupinga
kauli zake mbili kuwa ''hakuna tofauti kati ya Uislam na Ukristo,'' na ''kufunga
siyo lazima.''
Lakini
juu ya mashambulizi dhidi ya uongozi wa Waislam
kutoka serikalini, Nyerere alikuwa hana uwezo wa kumgusa Mufti Sheikh
Hassan bin Amir. Sheikh Hassan bin Amir
alikuwa na nguvu sana kiasi cha kwamba si Nyerere au yeyote yule kuweza kumgusa
kwa wakati ule. Sheikh Hassan alikuwa kwenye siasa kabla ya vijana waliokuwa
katika TANU na nafasi yake katika umma wa Kiislam na uzalendo wake ulikuwa
hauna shaka. Sheikh Hassan bin Amir aliingizwa TAA kwa mara ya kwanza mwaka
1950 na Abdulwahid Sykes akiwa mwanakamati katika Kamati Ndogo ya Siasa ya TAA.
Kwa ajili hii basi, akawa mmoja wa wale waliotia sahihi ile memoranda iliyotayarishwa
na TAA kwenda kwa Gavana wa Tanganyika, Edward Twining kuhusu mabadiliko ya
katiba ya Tanganyika. TANU ilipoasisiwa, Sheikh Hassan bin Amir alikuwa
akikiwakatia watu kadi za TANU msikitini huku akidarsisha. Baadhi ya wanachama
shupavu wa TANU ambao Sheikh Hassan bin Amir aliwaingiza katika TANU ni Sheikh
Mussa Rehani ambae alipewa kadi yake ndani ya msikiti Kigoma. Wakati Nyerere
alipokuja TAA Dar es Salaam mwaka 1953, alimkuta Sheikh Hassan bin Amir
mwenyeji katika siasa. Baada ya uhuru Sheikh Hassan bin Amir alijiuzulu siasa,
kutokana na kauli yake alisema kuwa, ili awatumikie Waislam vyema.
Nyerere
alifahamu fika kuwa haitakuwa rahisi kwake kumweka Sheikh Hassan bin Amir
kizuizini kama alivyofanya kwa Waislam wengine. Sheikh Hassan bin Amir alikuwa
ndiyo Mufti wa Tanganyika na Zanzibar na kwa ajili hii alikuwa na hadhi kubwa
katika umma wa Waislam. Halikadhalika haikuwa rahisi kwa yoyote kumkiuka Sheikh
Hassan bin Amir na kuchukua uongozi wa Waislam.
No comments:
Post a Comment