BAKWATA
Sehemu ya Tatu
Mkutano uliamua kuunda Tume ya Uchunguzi ya watu saba kuchunguza chanzo cha mgogoro na kisha itoe taarifa. Mussa Kwikima kijana mwanasheria alichaguliwa kuwa katibu wa tume ile ya uchunguzi. Wakati huo mikoa tisa ilikuwa tayari imeshajitenga na EAMWS na magazeti ya TANU yakawa tayari yamejenga mgogoro ule kufikia hali ya kuonekana kuwa ni mgogoro wa taifa zima ambao kila mtu anaweza kuuingilia na kusema atakalo. Magazeti ya TANU yakawa yanaandika na kuchapisha mambo ya EAMWS kama wanavyotaka, wakizidi kutia chumvi katika ugomvi ambao tayari ulikuwa umeshaleta hofu na farka kubwa katika jamii. Inasemekana viongozi wengine wa EAMWS walikuwa wanaambiwa wajitoe huku wameshikiwa bunduki.
Pambano kati ya Nyerere,
Tewa na Bibi Titi, 1968
Ili
tume ya uchunguzi ya Waislam iweze kufanya kazi yake vyema na bila upendeleo,
ilikuwa lazima ile tume ya Waislam iiombe serikali izuie propaganda iliyokuwa
ikiendeshwa na wale waliokuwa wamejitenga na EAMWS, wakitumia jukwa la radio ya
serikali na magazeti ya TANU. Tume ya Waislam ilikutana na Waziri wa Habari na
Utangazaji, Hasnu Makame, ofisini kwake tarehe 20 Novemba, 1968, kujadili
tatizo lile.
Hii
haukusaidia kitu. Propaganda dhidi ya uongozi wa EAMWS iliendelea kwa nguvu
zote. Mashambulizi kutoka pande tatu yaliyopangwa vyema yalikuwa kazini.
Benjamini Mkapa akitumia gazeti la Nationalist ataandika habari yoyote ya Adam
Nasibu, Martin Kiama akitumia Radio Tanzania atatumia habari ile kama habari
muhimu katika radio na habari hiyo itatangazwa kutwa nzima huku ofisi ya rais
ikiwa kimya kwa fitna ile. Lile kundi la waliojitenga na umma wa Waislam Adam
Nasibu akiwa kama msemaji wao mkuu wakawa wakati mwingine kwa mastaajabu
makubwa wakawa wanakiuka hata misingi ya akida ya Tanzania, wakitoa madai ya
ubaguzi wa rangi, wakikazania lazima EAMWS ivunjwe. Adam Nasibu alinukuliwa na
The Nationalist akisema kuwa:
Waislam lazima wafahamishwe kwa nini East
African Muslim Welfare Society iwe na katiba ambayo inaendana na mwelekeo wa
nchi. Hatujui nafasi ya Aga Khan katika nchi yetu na ndiyo maana tunamkataa.
Lakini
cha kushangaza zaidi ilikuwa ule ukimya wa serikali kuhusu matakwa ya kundi la
Adam Nasibu lililokuwa likidai kuwa Waislam wachanganye dini na siasa katika
suala hili, wakati ilikuwa ikijulikana wazi kuwa kufanya hivyo ni mwiko mkubwa
katika siasa za Tanzania. Haya yote
mbali, lile la kushangaza hasa na kitu ambacho kilikuwa kigeni katika Tanzania
ilikuwa yale madai ya kuingiza ubaguzi wa rangi katika siasa za Tanzania.
Ilikuwa inastaajabisha kuona magazeti ya TANU yaliyokuwa na sifa ya kuheshima
haki za binadamu yakichapisha na kuzipa uzito wa hali ya juu habari za kundi
dogo la Waislam waliokuwa wanawalaumu Waislam wenzao wa Kiismailia kwa
kutozaliwa weusi. Miaka kumi iliyopita watu wa Tanganyika, Waislam wenyewe
waliokuwa ndiyo walioanzisha na kuijenga TANU, walipambana vikali dhidi ya
siasa za kibaguzi za Zuberi Mtemvu na chama chake cha African National
Congress. Mtemvu alishindwa na matokeo yake ikawa Tanganyika kuwa na serikali
ya watu wote isiyobagua rangi na ikitawala raia wa rangi zote kwa misingi ya
haki. Kwa ajili hii nchi ikawa haina msuguano kwa ajili ya ubaguzi wa rangi.
Haya matokeo mapya yalikuwa hayaendani na misingi ya TANU.
Ilipofikia
hali hii, rais wa EAMWS, Tewa Said Tewa na makamo wake Bibi Titi Mohamed,
waliamua kulipeleka suala hili kwa Juluis Nyerere, Rais wa Tanzania na mwenyekiti
wa TANU, chama tawala. Watu hawa walikuwa wakichekeana jino pembe. Lakini ili
tuelewa chanzo cha uadui huu inatulazimu turudi nyuma hadi mwaka wa 1963,
katika siku za mwanzo za uhuru, katika mkutano wa Halmashauri Kuu ya TANU
uliofanyika Ukumbi wa Karimjee.
Kama
ilivyokwishaelezwa hapo mwanzoni kuwa mwaka 1963 ulikuwa mwaka wa mambo mazito.
Ilikuwa ndiyo mwaka ambao Kanisa Katoliki liliteua wagombea wake wapambane na
wagombea wa TANU waliokuwa Waislam katika uchaguzi wa serikali za mitaa kule
Kigoma na Bukoba. Ulikuwa ndiyo mwaka ambao Rais wa TANU, Nyerere alipopambana na
EAMWS kupitia Bilali Rehani Waikela. Mwaka wa 1963 ndiyo ulikuwa mwaka ambao
Halmashauri Kuu ya TANU ilivunja Baraza la Wazee wa TANU lililokuwa
limetawaliwa na Waislam kwa madai kuwa baraza hilo lilikuwa likichanganya dini
na siasaí. Mwaka 1963 ulikuwa mwaka muhimu kwa Halmashauri Kuu ya TANU kwa
sababu ilikuwa mwaka ambao ilifanya maamuzi nyeti ya kidini. Mwaka ule Bibi
Titi na Nyerere walishambuliana kwa maneno ndani ya Halmashauri Kuu ya TANU
kuhusu jambo jingine tena la dini lililokuwa likihusu EAMWS.
Wanakamati
wawili wa Halmashauri Kuu ya TANU, Selemani Kitundu na Rajab Diwani, waliiomba
Halmashauri Kuu ya TANU imjadili Aga Khan na nafasi yake kama patroni wa EAMWS.
Kitundu na Diwani walidai kuwa wana habari Aga Khan anataka kuitawala
Tanganyika kupitia Waislam na EAMWS. Kwa ajili hii basi wakapendekeza EAMWS
ifungiwe. Nyerere aliwaunga mkono Selemani Kitundu na Rajab Diwani. Bibi Titi
akasimama kishujaa dhidi ya Diwani, Kitundu na Nyerere, akasema hakuna kati yao
aliyekuwa na haki ya kuifungia jumiaya yoyote ya Waislam. Kama walikuwepo watu
ndani ya EAMWS ambao walikuwa wanakwenda kinyume na sheria basi watu hao
wapelekwe mahakamani na sheria ichukue mkondo wake. Bibi Titi akaendelea na
kusema kuwa EAMWS imekuwepo kabla ya TANU na siku zote imekuwa ikitoa huduma
kwa Uislam. Inasemekana hasira zilipanda na kukawa na kutoleana maneno kati ya
Bibi Titi na Nyerere. Bibi Titi akamwambia Nyerere yeye hamuogopi yeyote ila
Allah.
Tuhuma
zile dhidi ya Aga Khan na EAMWS hazikuweza kuthibitishwa na Halmashauri Kuu ya
TANU ikaliacha jambo lile kwa wakati ule. Lakini Nyerere alikuwa amefedheheka.
Kuanzia hapo akajenga chuki dhidi ya Bibi Titi na kumweka Rajab Diwani na
Selemani Kitundu karibu yake. Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1965 Bibi Titi na
Tewa wakapoteza viti vyao kwa watu ambao walikuwa hata hawafahamiki A.M.
Mtanga na Ramadhani Dollah. Iliaminika kuwa Nyerere alikuwa anahusika na
kuanguka kwa Bibi Titi na Tewa. Kuanzia hapo mambo yakawa dhahiri. Nyerere
alikuwa amewatangazia vita wote wawili, Bibi Titi na Tewa. Nyerere alikuwa sasa
ana imani kuwa wale maadui zake wawili walikuwa wamekwisha kisiasa. Lakini
kilichokuwa kikimuudhi Nyerere zaidi ilikuwa taarifa ambazo alikuwa akizipata kuwa
Tewa alikuwa akipewa mapokezi makubwa sana na Waislam katika ziara zake huko
mikoani kama rais wa EAMWS.
Sasa
mwaka wa 1968, Bibi Titi na Tewa walipokwenda kumuona Nyerere kuhusu jambo
lililokuwa linawahusu Waislam, Nyerere alikuwa amejitayarisha vyema. Kiwanuka
ameueleza mkutano huu vizuri sana:
‘’Viongozi hawa wawili wa Waislam walimueleza
Mwalimu masikitiko yao jinsi radio ya serikali na magazeti ya TANU yalivyokuwa
yakiandika habari kuhusu matatizo yale ya Waislam. Walidai kuwa TANU ilikuwa
ikichanganya dini na siasa. Waliokuwa wakimtahadharisha kuhusu jambo hilo
hawakuwa wengine ila marafiki zake wa zamani na wa kutumainiwa, Tewa na Bibi
Titi. Marafiki wa kutumainiwa kwa sababu ilikuwa Titi aliyemuunga mkono Nyerere
katika siku za mwanzo za TANU, pale Suleiman Takadir mmoja wa wazee wa TANU aliposema kuwa TANU ilikuwa na Ukristo kama Mwalimu na Rupia, rais na makamo
wake walivyokuwa Wakristo. Yeye mwenyewe
akiwa Muislam hasa, aliipatia TANU ushindi kwa kuthibitisha kuwa Tanzania,
Tanganyika kama ilivyokuwa ikijulikana wakati ule, ilikuwa mbele, na Uislam
unafuata nyuma. Leo, alikuwa anazungumzia jambo ambalo yeye mwenyewe
alilishinda katika miaka ya 1950. Jibu walilopata kutoka kwa Mwalimu lilikuwa
la kusisimua. Mpashaji wangu habari anasema lilikuwa jibu la mkato, ‘’Mmeamua
kunipiga vita, jiandaeni.’’
Mstari wa Nyuma Kulis Kwenda Kushoto wa Pili ni Tewa Said Tewa
Mstari wa Mbele Katikati ni Julius Nyerere
Baraza la Kwanza la Mawaziri Tanganyika
No comments:
Post a Comment