BAKWATA
Kilichobakia
baada ya kuvunjika kwa EAMWS ilikuwa ni kujaribu kuiweka BAKWATA katika mikoa
kama jumuiya inayowakilisha Waislam wote wa Tanzania Bara. Mwaka mzima wa 1969
Adam Nasibu na kamati ya watu wanne walitembea katika mikoa wakiahidi msaada wa
fedha kwa katibu yeyote wa zamani wa EAMWS ambae atashirikiana na BAKWATA makao
makuu kuisaidia kufungua ofisi katika mkoa wake. Waislam waliipuuza BAKWATA.
Tabora
ambayo haikujitoa katika EAMWS, serikali iliwaruhusu Adam Nasibu na kikundi
chake kufanya mkutano wa hadhara. Kabla Adam Nasibu hajahutubia Waislam, Maulid
Kivuruga mmoja wa wakongwe wa African Association na muasisi wa TANU Tabora,
alipanda jukwaani kwa niaba ya Waislam wa Tabora na kuweka sharti kuwa Waislam
watakuwa tayari kumsikiliza Adam Nasibu endapo Waikela mjumbe wa Tume ya
Waislam iliyokuwa ikitafuta sulhu na yeye ataruhusiwa na serikali kuwahutubia
Waislam ili aeleze upande wa pili wa kisa kile. Kivuruga alisema kuwa Waislam
wanaomba sharti hili likubaliwe kwa sababu katika Uislam panapotokea mgogoro
basi mpatanishi ni lazima asikilize pande zote mbili. Sharti hili lilikataliwa
na BAKWATA na serikali. Palepale mbele ya waheshimiwa wa serikali na viongozi
wa BAKWATA, Waislam wakaanza kuzomea huku wakitawanyika wakipiga takbir na
wengine wakiitikia, ''Allahu Akbar.''
Siku
chache baada ya tukio hili Waikela aliitwa na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai
kusailiwa kwa nini anaipinga BAKWATA. Wakiwa ndani ya chumba cha Tabora Hotel,
Geoffrey Sawaya, Mkrugenzi wa C.I.D, alimpiga maswali Waikela na kutaka kujua
kwa nini yeye hayuko tayari kushirikiana na serikali kuipa nguvu na kuieneza
BAKWATA. Sawaya akatoa hongo ya shilingi elfu arobaini kwa Waikela ili asaidie
kuimarisha BAKWATA. Waikela kama istizai alimuuliza Sawaya kama fedha zile
zilikuwa zimetoka bait mal. Waikela alikataa kupokea hongo ile. Sawaya
akamtisha lakini Waikela hakutishika. Waikela aliwekwa ndani ya chumba kile
akiulizwa maswali kwa kiasi cha saa nne na kisha akaamrishwa kuweka sahihi yake
katika makaratasi fulani. Hili alilifanya. Waikela hakufuatwa tena na serikali.
Ingawa kulikuwepo na juhudi za chinichini za kuipinga BAKWATA, juhudi hizi
hazikushinda kwa kuwa BAKWATA iliweza kufungua matawi yake nchi nzima pamoja na
Tabora. Wapo baadhi ya viongozi ambao hawakuweza kuhimili vishawishi vya
kupokea ile hongo ya serikali na kwa ajili hii walishirikiana na serikali hivyo
kuwezesha ofisi za BAKWATA kufunguliwa, hata kama zipo pale kwa jina tu.
Kuangushwa kwa EAMWS kulisababishwa na watu watatu ambao wao ndiyo walikuwa
mstari wa mbele kabisa - Adam Nasibu, Sheikh Kassim Juma na Sheikh Abdallah Chaurembo aliyepata kuwa mwanafunzi hodari wa Sheikh Hassan bin Amir; na njama hii ikaungwa mkono na Rashid Kawawa na Abeid Amani Karume. Mkono wa
Julius Nyerere na Kanisa Katoliki katika njama hii haukuonekana kabisa kama
ilivyo kawaida katika njama zote za kupiga vita Uislam na Waislam Tanzania.

No comments:
Post a Comment