TANU Ilivyovunja Ngome
ya Kanisa Katoliki Jimbo la Kusini, 1955
Sehemu ya Pili
Baada
ya kuandikisha wanachama waasisi mkutano wa siri uliitishwa katika Welfare
Centre ambako ndiko alikokuwa akifanya kazi Chembera. Chembera aliwaeleza kwa
ufupi wale wanachama wa mwanzo kuhusu malengo na madhumuni ya chama hicho kipya
cha siasa. Mkutano huo ulichagua kamati ya watu watatu yaani, Makopa, Chembera
na Faraj ili kuwakabili Mnonji na Waziri kuwaleza kuwa TAA haipo tena nchini
Tanganyika. Lengo lilikuwa kuwasadikishia kuwa ilikuwa kazi bure na kupoteza
wakati kujaribu kuihuisha TAA mjini Lindi wakati ambapo Tanganyika nzima
ilikuwa ikisonga mbele na TANU. Baada ya mjadala mrefu sana na mkali wa wale
vijana watatu na ule uongozi wa TAA wa wazee, walikubaliana TANU lazima
isajiliwe mjini Lindi.
Uchaguzi
ulifanyika na Shaaban Msangi, kijana wa Kipare akifanya kazi kwa Smith Mc
Kenzie, alichaguliwa rais na Ahmed Seif, katibu. Mpunga, Chembera, Mnonji na
Idd Toto walichaguliwa wajumbe wa kamati. Ahmed Seif alikuwa kijana ambaye
ndiyo kwanza amemaliza shule, yeye alikabidhiwa kuendesha ofisi kwa niaba ya
uongozi. TANU mjini Lindi ilimwajiri ili
kukiandaa chama kiweza kufanya kazi zake kwa ufanisi. Hassan Mohamed Kinyozi
aliajiriwa kama mhudumu wa ofisi. Hawa wawili walikuwa ndiyo wafanyakazi wa
kwanza wa TANU waliokuwa wakilipwa mshahara katika Jimbo la Kusini na wakawa
miongoni mwa wafanyakazi wachache sana walioajiriwa na TANU kwa wakati ule.
Mnonji alitoa nyumba yake katika mtaa wa Makonde kuwa ofisi ya kwanza ya TANU
Jimbo la Kusini. Baada tu ya kuanzishwa kwa TANU, Athumani Mussa Lukundu,
kiongozi wa Lindi Dockworkersí Union, aliunganisha chama chake na TANU. Jambo
hili, kwa TANU lilikuwa la kuitia moyo sana kwa sababu Dockworkersí Union
ilikuwa na wananchama wengi na hatua ile iliongezea TANU nguvu.
Baada
ya muda mfupi tu toka kufunguliwa kwa TANU Mkutano Mkuu wa Kwanza wa TANU wa
mwaka 1955 ulifuatia. Tawi la Lindi lilikuwa tayari lina uhusiano na makao
makuu ya TANU mjini Dar es Salaam, na lilikuwa likitarajia kuhudhuria mkutano
huo na kukutana na Julius Nyerere na uongozi mzima wa TANU pale makao makuu Dar
es Salaam. Mpunga, mwanachama muasisi wa TANU, na Ali Ibrahim Mnjale
waliteuliwa kuhudhuria mkutano huo kama wajumbe kutoka Jimbo la Kusini.
Halmashauri ya TANU ya Lindi iliwaelekeza wajumbe hawa wafikishe ombi rasmi kwa
makao makuu ili Julius Nyerere aje kufanya ziara kusini kwanza, kukutana na
wananchi na kufanya kampeni kwa ajili ya TANU na pili aje kupambana na
propaganda dhidi ya TANU zilizokuwa zikitawanywa na Yustino Mponda. Mponda akitumia uhusiano wake na serikali ya
kikoloni na nafasi yake kama mjumbe wa Baraza la Kutunga Sheria kutoka Newala;
na vilevile akitumia ushirikiano wake wa muda mrefu na kanisa ambao bila shaka
yoyote lilikuwa serikali ndani ya serikali kule kusini, alikuwa ameanza kampeni
yake ya kuipinga TANU. Hili lilikuwa likiathiri msukumo wa uanachama. Mponda
alikuwa mmoja wa wajumbe waliotumwa na Gavana Twining kwenda Umoja wa Mataifa
Februari, 1955 kwa niaba ya serikali ya kikoloni kwenda kuipinga. Uongozi wa
TANU huko Lindi ulitaka Nyerere aende kupambana na Mponda akiwa katika uwanja
wake mwenyewe, ndani kabisa ya ngome ya Ukristo wa Kikatoliki katika
Tanganyika.
Mkutano
mkuu wa mwaka wa TANU ulifanyika katika ukumbi wa Hindu Mandal mjini Dar es
Salaam. Siku kabla ya mkutano TANU ilimwalika Gavana Edward Twining kwenye
tafrija katika Ukumbi wa Arnatouglo lakini alikataa kistaarabu na akamtuma
Chief Secretary, Bruce Hutt, kumwakilisha. Baada ya mkutano, wakati wajumbe
wengine wanaondoka kurudi kwenye majimbo yao, Mpunga na Mnjawale walibakia
nyuma kukutana na uongozi wa makao makuu wa Julius Nyerere, Sheikh Suleiman
Takadir, John Rupia, Ali Mwinyi Tambwe, Said Chamwenyewe, Oscar Kambona na
wengineo. Mpunga na Mnjawale waliwafahamisha viongozi wa makao makuu kuhusu
hali mbaya ya siasa Jimbo la Kusini. Mbali na kampeni za kuipinga TANU za
Mponda, katika ziara yake Lindi Gavana Twining aliwatahadharisha Waafriika wa
Tanganyika wasijihusishe na ëwafaanya fujo wanaotaka kuzusha vuruguí. Twining
alikuwa akitoa onyo hili akiikusudia TANU ambayo ilikuwa imeanzishwa mwaka
uliopita. Hotuba hii ya Gavana iliwatisha wananchi kujiunga na TANU. Mpunga na
Mnjawale walisisitiza kuwa kuja kwa Nyerere mjini Lindi kulitakiwa haraka sana
kukabiliana na vyote viwili, kwanza ile hotuba ya gavana na pili zile kampeni
za kupinga TANU zilizokuwa zikiendeshwa na Liwali Yustino Mponda.
![]() |
| Mkutano wa Kwanza wa TANU 1955 |
Wakati
huo Abeid Amani Karume aliyehudhuria ule mkutano alimwalika Nyerere afanye
ziara Zanzibar. Kitu cha kustaajabbisha ni kuwa, Nyerere alionekana kuiafiki
zaidi ziara ya Zanzibar kuliko ile safari ya kwenda kusini kuiimarisha TANU.
Mpunga alimsisitizia Nyerere umuhimu wa yeye kwenda Lindi ambako kunaweza kuwa
ndiyo chanzo cha TANU kupata ufanisi Newala, Songea, Tunduru na Masasi ambako
kulikuwa na upinzani mkubwa dhidi ya TANU. Kanisa lilikuwa likiwazuia Wakristo
kujiunga na TANU. Sheikh Suleiman Takadir, Said Chamwenye, John Rupia, Ali
Mwinyi Tambwe wote waliunga mkono ule ujumbe wa Lindi juu ya suala hili. Baada
ya kufikia makubaliano, Mpunga na Mnjawale walipewa barua ya kuthibitisha
safari ya Nyerere. Ziara ya Nyerere
ilikuwa ianze muda mfupi kutokea hapo kwa kuwa ilikuwa ndiyo siku za mwisho za
kiangazi. Barabara sehemu ya kusini ya Tanganyika zilikuwa hazipitiki wakati wa
masika, zikiitenga kabisa kusini toka sehemu zilizobaki za nchi. Ali Mwinyi
Tambwe na Rajab Diwani walifuatana na Nyerere kwenda Jimbo la Kusini kuondoa
wasiwasi na woga uliozushwa na Gavana Twining na kibaraka Yustino Mponda.
| Ali Mwinyi Tambwe |

No comments:
Post a Comment