Tuesday, 25 February 2014

Mkakati wa Tanga Kupambana na Wapinzani wa Kura Tatu, 1958


Mkakati wa Tanga Kupambana na Wapinzani wa Kura Tatu, 1958

Mwaka 1958 serikali ya kikoloni iliandaa uchaguzi wa Baraza la Kutunga Sheria ambao viti vilikuwa vishindaniwe kwa misingi ya utaifa. Kulikuwa na viti kwa ajili ya Wazungu, Wahindi na Waafrika. Masharti mengine ya kumwezesha Mwafrika kupiga kura yalimtaka awe na kipato cha paundi mia nne za Kiingereza kwa mwaka, awe na kiwango cha elimu ya darasa la kumi na mbili na awe ameajiriwa katika kazi maalum. Haya yalikuwa masharti magumu na yaliyoonekana kama hayataweza kukubalika na TANU. TANU ilifanya mkutano wake mkuu wa mwaka wa 1958 mjini Tabora kuanzia tarehe 21-26 Januari kujadili miongoni mwa mambo mengine ikiwa ishiriki katika uchaguzi chini ya masharti haya ya kibaguzi yaliyowekwa au wasuse. Mkutano ule ulitishia kuigawa TANU katika kambi mbili hasimu. Kambi moja ni ile ya wenye siasa za wastani waliopendelea kushiriki katika uchaguzi na ile ya pili ni ile ya wenye msimamo mkali waliotaka uchaguzi ususiwe kabisa. TANU ilinusurika na kile ambacho kingeweza kuwa mgogoro ndani ya chama ambao ungewafanya wale wenye msimamo mkali kama Sheikh Suleiman Takadir, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa TANU katika makao makuu, na Zuberi Mtemvu, wakati huo katibu mwenezi wa TANU, kufanya mapinduzi ambayo yangekigawa chama kama isingelikuwa busara ya Julius Nyerere, Rais wa TANU.

Lakini ili kuzielewa hisia za wanachama wa TANU, fikra za uongozi wake na nguvu zilizokuwa zikidhibiti siasa Tanganyika wakati ule wa ukoloni, na ili kuelewa kwa nini kura tatu ilileta mgogoro na kutoelewana katika uongozi, inatubidi turudi nyuma tufuatilie mwanzo wa siasa mjini Tabora, mahala ambapo TANU ilifanya uamuzi wake ya kihistoria na kuwanasa Waingereza katika mtego wao wenyewe. Tunahitaji kuyatazama mambo kwanza kuanzia Tanga mahali ambapo Nyerere na uongozi wa TANU pale Tanga walikutana kwa siri kuweka mikakati ya mkutano wa Tabora. Baada ya kufanya hivyo tufichue jambo moja baada ya jingine katika ule mkutano ambao wajumbe wa TANU walikutana katika ukumbi wa Parish wa Kanisa Katoliki, Tabora. Hii itatuwezesha kujua kwa nini mkutano mkuu huu ulikuwa muhimu na kwa nini kutokana na mkutano huu Waislam ambao walijitoa mhanga sana katika kudai uhuru, mara tu baada ya uchaguzi huo walianza kupoteza nguvu yao katika siasa hatimaye kutupwa nje na katu hawakuweza kurejesha tena nguvu hiyo hadi hivi sasa. Akiiandikia Fabian Colonial Bureau, katibu mwenezi wa TANU, Zuberi Mtemvu ambae alikuwa amelichambua jambo hili la utatanishi aliandika:

‘’Katika nchi kama Tanganyika, utajiri na elimu vimo mikononi mwa wageni. Mwafrika ni maskini na hana elimu. Upigaji kura wenye masharti magumu yaliyoegemezwa kwenye mali na elimu utawaathiri Waafrika peke yao bila kuwagusa Wazungu na Waasia hata kidogo.’’ 

TANU kwa hakika kilikuwa chama cha Waislam; kwa hiyo ilikuwa ni dhahiri kuwa kuyakubali masharti yale ya kibaguzi ya upigaji kura ilikuwa sawasawa na kuwasukuma Waislam ambao ndiyo walikuwa wafuasi wakubwa wa chama nje ya wigo wa siasa. Nimtz ameandika kwa ufupi hali ya Waafrika katika uchaguzi wa mwaka wa 1958 na 1959 katika mji wa Bagamoyo, mji ambao ni wa Waislam: 
  
‘’...kutokana na sifa za wapiga kura na masharti magumu ambayo serikali ya kikoloni iliweka, upigaji kura ulibakia kwa asilimia ndogo sana ya Waafrika ambao ndiyo waliokuwa wengi. Katika Wilaya ya Bagamoyo ambako uchaguzi ulifanyika mnamo Septemba, 1958, watu 630 tu, katika idadi ya watu 89,000, ndiyo waliyojiandikisha. ‘’

Ujumbe wa Nyerere mwenyewe kutoka makao makuu ulikuwa na watu wengi ambao wasingeweza hata kidogo kusimama kama wagombea katika uchaguzi chini ya masharti yale. Makao makuu ya TANU yalikuwa yanawakilishwa kwenye mkutano mkuu na Julius Nyerere, Sheikh Suleiman Takadir, Bibi Titi Mohamed, John Rupia, Elias Kissenge, Dossa Aziz, Julius Mwasanyangi, Michael Lugazia, Ramadhani Chaurembo, Hussein Mbaruk, Clement Mtamila, Idd Tulio, Mzee Salum, Idd Faiz Mafongo, Idd Tosiri, Haidari Mwinyimvua na Rajabu Diwani. Hii ilikuwa na maana uongozi wa Waislam kule Dar es Salaam, Tanga, Tabora, Dodoma na mahala pengine nchini Tanganyika usingeweza kusimama kama wagombea uchaguzi ili wachaguliwe kuingia katika Baraza la Kutunga Sheria wala wasingeweza kuwapigia kura wagombea wanaowataka. Kwa hiyo ilikuwa ni jambo la wazi kabisa kuwa TANU ingesusia uchaguzi. Serikali ya kikoloni, ikishirikiana na wamishionari, walikuwa wamewanyima Waislam elimu, sharti lile lile ambalo sasa linawekwa kuwazuia Waislam kushiriki katika siasa. Mkutano wa Tabora ulikuwa uamue ikiwa TANU itashiriki katika uchaguzi na kushindana na UTP au ingesusia uchaguzi huo na hivyo kumpa mshindani wake mkubwa na hasimu wake ushindi wa bure.

Hakuna kumbukumbu zozote zinazoeleza mawazo ya Nyerere katika suala la kura tatu wala hakuna nyaraka inayoweza kueleza kuwa alipata hata kuzungumza suala hili kwa faragha pale makao makuu na viongozi wenzake kama Sheikh Suleiman Takadir, Zuberi Mtemvu, Rajab Diwani, Idd Faiz, Haidar Mwinyimvua, Dossa Aziz au Bibi Titi Mohamed. Kwa ajili hii ni vigumu kuweza kujua ni kwa kiasi gani Nyerere alikuwa amejizatiti katika msimamo wa TANU kuingia katika kura tatu chini ya masharti yale. Lakini ikiwa utafanya tathmini kutokana na hali ya hewa ya siasa kama ilivyokuwa katika miezi ya mwisho ya mwaka 1958, si vigumu kuona kwa nini Nyerere ilibidi afiche msimamo wake katika suala la kura tatu kama TANU lilivyotwishwa na serikali. Nyerere alikuwa anafahamu hatari iliyokuwa ikinyemelea TANU kutokana na kura tatu. Alijua wazi ili kukinusuru chama na mgawanyiko kulikuwa na haja kubwa ya yeye kufanya uamuzi haraka na kwa makini kabla ya kuenda kwenye mkutano Tabora.

Siku kadhaa kabla ya kusafiri kwenda Tabora kwenye ule mkutano mkuu wa mwaka wa TANU, Nyerere na Amos Kissenge, Kaimu Katibu Mwenezi wa TANU, walisafiri kwenda Tanga kushauriana na uongozi wa Kamati Kuu ya Taifa ya TANU Tanga kuhusu matatizo yaliyoletwa na uchaguzi wa kura tatu. Mkutano huu baina ya Nyerere, Kissenge na ule uongozi wa Tanga ulikuwa wa siri sana. Tanga iliwakilishwa na Hamisi Heri, Mwalimu Kihere, Abdallah Rashid Sembe, NgĂ­anzi Mohamed, Mustafa Shauri na Abdallah Makatta. Nyerere alizungumza waziwazi na kwa ithibati ya moyo wake. Nyerere alikiambia kikao kile kuwa amekuja Tanga kuomba wamuunge mkono kwa sababu ilikuwa ni matakwa yake TANU lazima ishiriki katika ule uchaguzi wa kura tatu uliokuwa unakaribia hata masharti yakiwaje. Nyerere aliuambia uongozi wa Tanga uliokuwa ukimsikiliza kwa makini kuwa alikuwa amekuja kwao kwa sababu watu wa Tanga wanajulikana kwa ufasaha wa lugha na kwa uwezo wao wa kuzungumza vizuri. Nyerere alisema angehitaji hiki kipaji adimu cha watu wa Tanga kuunga mkono msimamo wake huko Tabora. Nyerere alitoa hoja kwamba TANU lazima iingie katika uchaguzi kwa sababu kuususia ni sawasawa na kukipa chama hasimu, UTP ushindi bila jasho kuingia katika Baraza la Kutunga Sheria. TANU ingedhoofika na hivyo ingekosa sauti katika maamuzi yatakayotolewa na serikali katika  siku zijazo.

Kufichuka kwa msimamo wa Nyerere wa kutaka TANU iingie kaatika kura tatu kulishtua uongozi wa Tanga. Majadiliano makali yalifuata uongozi wa Tanga ukionyesha upinzani wao kwa msimamo wa Nyerere. Baada ya majadiliano ya muda mrefu Nyerere alifanikiwa kuwashawishi wote wawili, Hamisi Heri na Mwalimu Kihere ambao ndiyo walikuwa wapinzani wakubwa wa msimamo wa Nyerere na uchaguzi wa kura tatu. Nyerere aliutahadharisha uongozi wa Tanga kuwa agenda ya kura tatu itakapokuja anatabiri kupata upinzani mkali kutoka katika majimbo. Huko Tanga kwenyewe, TANU ilikuwa ikikabiliwa na upinzani mkali kutoka UTP na serikali.

Matawi kadhaa yalikuwa yamepigwa marufuku. [1]  UTP ilikuwa na nguvu Tanga kwa sababu wanachama wake wengi walikuwa wakimiliki mashamba ya mkonge katika jimbo hilo. Kwa ajili hii chama kilikuwa kinaelemewa na mashambulizi kutoka wa wapinzani. Wakati huo Tanga ilikuwa imetoa viongozi wenye uwezo lakini wote walikuwa wamehamishiwa makao makuu mjini Dar es Salaam. Wapangaji mikakati wazuri kama Peter Mhando alikuwa amehamishiwa Dar es Salaam na kutoka hapo alipelekwa Tabora ambako si muda mrefu akafa. Elias Kissenge vilevile alihamishiwa makao makuu kushika nafasi ya Katibu Mkuu wa TANU baada ya Oscar Kambona aliyekuwa ameshika nafasi hiyo kwenda Uingereza kwa ajili ya masomo. Uongozi wa TANU Tanga hata baada ya kujadili mbinu waliyopanga na huku Nyerere akielekeza mikakati ambayo Mwalimu Kihere na Abdallah Rashid Sembe wataitekeleza Tabora, bado uongozi ule ulikuwa na wasiwasi wa mafanikio ya mpango huo. Kwa ajili ya wasiwasi huu, viongozi wa TANU wa Tanga walimuomba Nyerere wawe pamoja ili ifanywe tawaswil waombe msaada wa Allah awape ushindi dhidi yaa vitimbi vya Waingereza. 

Maili tatu kutoka Tanga kipo kijiji cha Mnyanjani ambako kulikuwako na tawi la TANU lililokuwa na nguvu sana likiongozwa na Mmaka Omari kama mwenyekiti na Akida Boramimi bin Dai akiwa katibu. Mmaka alikuwa kijana aliyekuwa akiendesha mgahawa pale kijijini na Akida bin Dai alikuwa mwashi. Akida aliongoza tawi la vijana wa TANU ambalo baadae lilikuja kujulikana kama Tanga Volunteer Corps (TVC). TVC ilikuwa sawasawa na Bantu Group, ambayo wakati huo ilikuwa imekwishaanzishwa huko Dar es Salaam na Tabora. Vikundi hivi mbali na kufanya shughuli za propaganda na kuhamasisha wananchi halikadhalika viliifanyia TANU ujasusi. Nyerere na Kissenge walichukuliwa hadi Mnyanjani na tawaswil ikasomwa. Waliohudhuria kisomo hicho  walikuwa Abdallah Rashid Sembe, Sheikh Dhikr bin Said, Mzee Zonga, Hemed Anzwan, Salehe Kibwana aliyekuwa mshairi maarufu, Akida Boramimi bin Dai na Mmaka Omari. Aliyechaguliwa kusoma Quran Tukufu alikuwa mjomba wa Mwalimu Kihere, Sheikh Ali Kombora.


No comments: