Tuesday, 25 February 2014

YUSUF OLOTU 1927 - 1997: SHUJAA WA KURA TATU, 1958

 YUSUF OLOTU 1927 - 1997
SHUJAA WA KURA TATU

Utangulizi

Nilikwenda kumuona Mzee Yusuf Olotu nyumbani kwake Moshi nyakati za jioni baada ya L’ Asr.
Nilimkuta Mzee Olotu ndani amelala kwa kuwa hali yake ya afya haikuwa njema sana.

Baada ya ujitambulisha alichangamka kwani nilipomtajia wazazi wangu wote akawa anawafahamu ingawa ni miaka mingi hawajaonana.

Mtoto wa Mzee Olotu Ahmed ni makamo yangu na tulicheza pamoja utotoni kwa kuwa nyumba zetu zilikuwa jirani Moshi Mtaa Chini.

Mzee Olotu alifurahi kusikia naandika kitabu cha historia yao wapigania uhuru wa Tanganyika. Akanieleza kuwa walipita watu kwake miaka michache iliyopita wakitokea CCM na wakachukua nyarakza zake zote na picha wakidai kuwa wanakusanya nyaraka hizo na picha kwa ajili ya kuandika historia ya TANU na pia kutoa kifuta jasho kwa wale waliokuwa mstari wa mbele kupigania uhuru wa Tanganyika.

Kwa masikitiko alinieleza kuwa hakuna kilichofanyika na hata alipokwenda ofisi ya CCM kuomba angalau wamrudishie nyaraka na picha zake aliishia kuzungushwa.

Tukaanza mazungumzo huku kinasa sauti change kikizunguka taratibu.

Mzee Olotu alikuwa anasumbuliwa na kikohozi lakini alianza kuzungumza kwa utaratibu baada ya kuwaambia watoto wake waliokuwa nje kuwa ana mgeni muhimu na hataki kusumbuliwa.

Hatukufika mbali katika mazungumzo mvua kubwa ikaanza kunyesha ikasindikizwa na radi…

Kwa miaka mingi kila nilipokuwa namsikiza Mzee Olotu katika kinasa sauti changu na nikisikia vile akinyamaza kuzungumza kwa ajili ya kikohozi kisha akireja kueleza historia ya uhuru sauti yake ikiingiliana na radi nilikuwa najiuliza – ile radi ilikuwa inaashiria nini?

Nilikuwa Arusha baada ya miaka kupita ndipo nilipopata taarifa kuwa Mzee Olotu amefariki na kazikwa jana yake.

Niliondoka siku ya pili yake kwenda Moshi kuhani.

Nasikitika kuwa Mzee Olotu hakukiona kitabu ambacho kimemtaja yeye na wenzake katika kuunda TANU Kilimanjaro, mwaka wa 1955 na kupigania uhuru wa Tanganyika.
MS

Yusuf Olotu

Historia ya harakati za kudai uhuru wa Tanganyika kama walivyoshiriki wananchi wa Kilimanjaro haiwezi kamwe kukamilika bila ya kutaja jina la Yusuf Ngozi achilia mbali mchango wake katika kuipa TANU ushindi katika uchaguzi wa kura tatu. Jina hili la Ngozi alilipata kwa kuwa alikuwa akifanya kazi katika kampuni ya kuuza ngozi. Uchagga ilikuwa chini ya utawala wa machifu waliokuwa wakijulikana kama Mangi. Baadhi ya machifu hawa walikuwa katika Baraza la Kutunga Sheria na kwa ujumla wao walikuwa karibu na serikali ya kikoloni kuliko walivyokuwa na wananchi wanaowaongoza. Hali ya siasa katika Jimbo la Kaskazini ilikuwa ngumu na ya kukatisha tamaa. Wakati TANU inakabiliwa na Kura Tatu mgogoro wa ardhi ya Wameru ulikuwa umekwisha kwa wananchi kudhulumiwa haki yao. Japhet Kirilo alikuwa tayari amerudi mikono mitupu kutoka Umoja wa Mataifa alikopeleka madai ya Wameru.


Chief Marealle, Chief Maruma na Chief Shangali

Kirilo hakuwa na chochote cha kuwaonyesha Watanganyika. Ilikuwa Yusuf Ngozi ndiye aliyeweza kuifanya TANU iingie kwanza Moshi mjini kwa vishindo na kutoka hapo akaieneza vijijini. Kupitia kumbukumbu za Mzee Yusuf Ngozi ndipo unapokutana na historia za awali kabisa za wanasiasa maarufu waliopata majina na vyeo na wengine kuwa mawaziri katika Tanganyika huru. Mfano wao ni Lucy Lameck, Enesmo Eliufoo na wengineo. Ilikuwa ni Yusuf Ngozi pamoja na wazalendo wengine walioifanya TANU ishinde uchaguzi wa kura tatu mwaka 1958. Kupitia kumbukumbu zake halikadhalika ndipo kwa huzuni kubwa utakapokutana na mashujaa waliosahaulika kama yeye mwenyewe, mashujaa wa kike na wa kiume na wazalendo kama marehemu Mama Bint Maalim, Amina Kinabo, Halima Selengia, Juma Ngoma, Melkezedek Simon, Gabrieli Malaika na wengineo. Hawa ndiyo mashujaa ambao kwa muda waliamua wasahau nguvu na utawala wa machifu wao na kujiweka chini ya TANU.

Habari za kuenea kwa TANU Kilimanjaro na matatizo ya Kura Tatu zimeelezwa na Yusuf Olotu katika mahojiano aliyofanya na mwandishi nyumbani kwake Moshi tarehe 21 Januari, 1989. Yusuf Ngozi alimfahamisha mwandishi kuwa ofisi ya CCM Wilaya, miaka michache iliyopita walimuandikia barua kumuomba awape nyaraka zake zote za mwanzo kuhusu TANU na awaandikie historia ya jinsi chama kilivyoenezwa Kilimanjaro na mchango wake binafsi. Kazi hii aliifanya na akakabidhi nyaraka hizo kwa CCM. Yusuf Ngozi alimfahamisha mwandishi kuwa alidokezwa kuwa nia ya zoezi hilo ilikuwa ni kuweka kumbukumbu za mashujaa wa harakati za uhuru ili wapate kuenziwa na taifa na wale ambao hali zao za kimaisha si nzuri wasaidiwe na chama. Yusuf Olotu alifariki dunia tarehe 3 Juni, 1997 akiwa na umri wa miaka sabini.

Yusuf Ngozi hakuwa na elimu bali alikuwa mwananchi wa kawaida aliyethamini utu wa Mwafrika na mtu aliyechukia dhulma na fedheha ya kutawaliwa. Kilimanjaro ilikuwa inasifika kwa kuwa na Waafrika waliokuwa na elimu ya juu kabisa katika Tanganyika. Lakini wasomi hao walishughulishwa zaidi na maslahi yao binafsi. Wengi wao walikuja kujitokeza na kuingia chama cha TANU mwaka 1958 katika uchaguzi wa kura tatu. Wakati huo mambo yalikuwa shwari na Waingereza walikuwa wamesalimu amri. Yusuf Ngozi labda kwa kuelewa mazingira ya Kilimanjaro alianza kujenga msingi wa TANU si kwa wanaume bali kutoka kwa akina mama. Hiki ni kitu azizi sana katika historia ya kupigania uhuru. Katika historia ya TANU sehemu ambazo chama kilipata nguvu kubwa sana ni zile sehemu ambazo kulikuwa na utamaduni wa Kiswahili wa vyama vya akina mama kama hapo Moshi mjini, Dar es Salaam, Tanga, Lindi na kwingineko.

Joseph Kimalando aliogopa kuitumikia TANU lakini alijiona amesalimika kuifanyia kazi United Tanganyika Party (UTP) – chama cha Wazungu kilichoundwa kuipinga TANU. Kimalando alikuwa katibu wa UTP Moshi na Mohamed Kishikio Badi alikuwa mwenyekiti wake. Yusuf Ngozi aliwahamasisha wanawake wa Moshi chini ya Mama bint Maalim kuipiga vita UTP hadi ikafa. Wanawake wale walikuwa wakizikusanya kadi za UTP na kumpelekea Mzee Yusuf Ngozi kwenye ofisi ya TANU. Yeye kama njia ya kuwakatisha tamaa na kuwapiga vita vya kisaikolojia UTP alikuwa akichukua marundo kwa marundo ya kadi za UTP na kumpelekea rais wake Mohamed Badi kumhakikishia kuwa wananchi walikuwa hawakitaki chama chake cha vibaraka.

Yale masharti ya Kura Tatu yaani kipato, elimu na kazi ya maana, kwa wapiga kura na wagombea hayakuwasumbua Wachagga wengi kwani wao kama tulivyoona walikuwa ni watu waliokuwa na elimu na vipato vya kutosha. Kwa maneno mengine sheria ile (ambayo kwa sehemu nyengine kama vile Bagamoyo ilikuwa ngumu) kwa Wachagga ilikuwa nyepesi na hivyo kuruhusika kupiga kura pasi na pingamizi. Lakini kwa bahati mbaya sana iliingia fikra kuwa masharti yale ya kupiga kura na hasa kile kipengele cha kipato ilikuwa njama ya serikali ya wakoloni kutengeneza orodha ya Wachagga ili wawatoze kodi ya mapato. Wachagga ni wafanya biashara na wenye bidii katika kilimo.


Hiki kipengele cha kipato kiliwaweka wana - TANU wa Uchaggani – wafanyabiashara, wafugaji na wakulima wa kahawa katika hofu kubwa. Hulka ya kuthamini mali ilikuwa imefifilisha umuhimu mzima wa watu wa Kilimanjaro kupiga kura ili TANU ichukue viti katika Baraza la Kutunga Sheria. Tatizo la Uchaggani sasa likawa ni la kipekee. Kazi kubwa hapa ilikuwa ni kubadilisha fikra za watu na kuwatoa hofu ya kulipa kodi kwa mali zao na kuwafanya kuona ukweli na umuhimu wa kuishinda UTP na kumng’oa Mwingereza Tanganyika. Hili lilikuwa tatizo ambalo TANU hawakukutana nalo mahali popote katika Tanganyika. Hata katika mkutano wa Tabora kujadili juu ya Kura Tatu hakuna kumbukumbu yoyote inayoonyesha kuwa kuna Waafrika ambao watashindwa kutumia haki yao ya kupiga kura kwa kuwa na fedha nyingi. Tatizo ilikuwa ni kinyume chake. Tatizo la TANU katika majimbo mengine lilikuwa ni kuwafanya watu wakubaliane na masharti yale magumu ya kibaguzi katika kupiga kura ili chama kiingie katika uchaguzi.

Katika hali ya kawaida mtu angalitegemea kuwa watakaosimama ni wale wasomi wa Makerere kuwaeleza wananchi hali ya mambo na mwelekeo wa nchi. Katu hao hawakusimama. Alikuwa Yusuf Ngozi aliyehamasisha. Alitembea Kilimanjaro nzima na kuwaeleza watu kuwa kama hawatajiandikisha kuipigia kura TANU na kumuunga mkono Mwalimu Nyerere katika vita dhidi ya Waingereza basi wajue kuwa UTP itashinda na Waingereza wataendelea kuitawala nchi hii. Sehemu nyingine alikuwa akiwafahamisha Waafrika wenye biashara ndogondogo kuwa wao vilevile wana kazi na kipato kinachokidhi masharti ya upigaji kura kwani hesabu zao za mwaka zilikuwa zinapita kile kiwango cha pauni mia nne (400). Aliikuta hali hii kwa mafundi cherehani huko Kahe – kijiji kidogo nje ya Moshi. Mafundi hawa walijihesabu hawana kazi ya maana wala kipato cha pauni 400 kwa mwaka. Mzee Yusuf Ngozi aliwasomesha na kuwaonesha kuwa walikuwa na kazi ya maana na kipato cha kutosha. Hivyo aliwanasihi wasiache kujiandikisha na kuipigia kura TANU. Sehemu nyingine Yusuf Ngozi alikuwa na propaganda yake ya kutisha. Alikuwa akiwauliza wananchi kama wao walikuwa wako tayari kuishi katika nchi yenye bendera tatu. Katika Jimbo la Kaskazini TANU ilimsimamisha Enesmo Elufoo.


Sophia Mustafa


Eliufoo kwa kiti cha Moshi na Sophia Mustapha alisimamishwa Arusha. Yusuf Ngozi aliifanyia kampeni TANU kwa ufanisi mkubwa na TANU iliweza kushinda kwa kura nyingi sana na wajumbe wake kuingia katika Baraza la Kutunga Sheria.TANU ilishinda ule uchaguzi wa kura tatu. UTP ambayo ilikuwa na nguvu sana huko Tanga ilikiri kushindwa. David Emmanuel mwenyekiti wa UTP akitambua ukweli kuwa hakukuwa na mategemeo yoyote kwa chama hicho pale Tanga na kama ishara ya pekee kabisa ya ukarimu na moyo wa kutaka maelewano mema, alikusanya samani yote iliyokuwa ndani ya ofisi ya UTP na kuitunukia TANU.

NB
Kwa maelezo kamili kuhusu Uchaguzi wa Kura Tatu angalia The Tanganyika Gazette Vol. XXXIV No. 48 26 September, 1958. Vilevile Sauti ya TANU No. 25 Septemba, Uchaguzi wa mwaka 1958 ulifuatiwa na uchaguzi mwingine mwaka 1959 ambao TANU ilishinda.



No comments: