TANU Ilivyovunja Ngome
ya Kanisa Katoliki Jimbo la Kusini, 1955
Sehemu ya Tano
Tukio
dogo la kiburi cha askari mpumbavu wa mkoloni ndiko kulisababisha watu wa
Mikindani wafungue tawi la TANU. Askari mmoja mpita njia aliingia katika ubishi
na kijana mmoja wa pale mjini, akiitwa Hassan Masudi Vuni. Akitumia mamlaka
yake ya kukamata mhalifu, askari huyo alimpiga Vuni kwa kumuonea. Miongoni mwa
watazamaji wa tukio hilo alikuwa Rashid Ali. Rashid Ali alikwenda kusimulia
tukio hili kwa Mohamed Ali Abdallah. Alipokuwa akisimulia mkasa ule, pamoja
naye alikuwa Suleiman Hassan Msepele. Walipokuwa wakijadiliana Msepele alitamka
kwamba tukio kama hilo kamwe lisingeweza kutokea Dar es Salaam kwa sababu
Mwafrika mmoja kwa jina lake Julius Nyerere alikuwa ameanzisha chama cha siasa
kupigania uhuru. Rashid Ali na Mohamed Ali Abdallah walitamani kujua mengi
zaidi kuhusu Mwafrika huyu aliyekuwa akijulikana kwa jina la Nyerere na chama
chake cha siasa, lakini Msepele hakuwa na mengi ya kueleza kuhusu Nyerere na
chama chake. Kwa hiyo basi, hawa watu watatu waliamua kumtuma mtu Dar es Salaam
kupata habari zaidi kuhusu chama hicho. Mohamed Ali aliandika barua na kumpa
Msham Awadh na Ali Muhidin kumpelekea Nyerere. Ndani ya barua hiyo Mohamed Ali
alimweleza Nyerere kwamba ukoloni ulikuwa bughudha kubwa katika Jimbo la
Kusini, na wangependa kufungua tawi la TANU mjini Mikindani ili kupigania
uhuru.
Mwaka
1955 Mohamed Ali alikuwa na umri wa miaka 45. Alikuwa hana elimu kama elimu
inavyojulikana kwa kuwa hakusoma shule yoyote. Alipokuwa kijana mdogo baba yake
alimpeleka Zanzibar kusoma elimu ya dini. Wakati huo Zanzibar ilikuwa ndiyo kituvu
cha elimu ya Kiislamu. Huko Zanzibar kijana Mohamed Ali alisoma kwa Sheikh
Mohamed LĂKhamus. Kisha aliendelea na masomo yake mjini Dar es Salaam kwa
Sheikh Wazir bin Said, mwanafunzi wa Sheikh maarufu sana na aliyekuwa khalifa
wa Tariqa ya Askariyya, Sheikh Idrissa bin Saad. Baada ya kumaliza masomo yake
mjini Dar es Salaam alisafiri hadi Belgian Congo na halafu alirudi Ujiji nchini
Tanganyika kufanya biashara ndogo ndogo. Katika mwaka 1947 alirudi Lindi na
kutoka hapo alikwenda Mikindani na kuwa fundi cherahani.
Msham
Awadh alikuwa akijulikana Lindi nzima na Mikindani kwa sababu ya biashara yake. Mshama Awadh
alikuwa alikuwa muuza uzuri, yaani vitu vya urembo kama vile uturi, dalia,
marashi, rangi na manukato mengine kwa wanawake wa hii miji miwili. Alikuwa
akiuza bidhaa zake kikapuni akipita nyumba hadi nyumba. Hawa walikuwa ndiyo
aina ya watu walioanzisha na kuongoza harakati za kumaliza utawala wa kikoloni.
Hawakuwa wajuzi wa lugha ya Kiingereza wala hawakuwa na ujuzi wa maisha ya
ulimwengu wa kimagharibi kama walivyokuwa baadhi ya Waafrika wengine waliyopata
elimu ya kimagharibi. Msham Awadh na Ali Muhidin walikwenda hadi Dar es Salaam
kukutana na Nyerere, Rupia, Chamwenye, Kambona na Dossa katika makao makuu ya
TANU, New Street. Msham Awadh na Ali Muhidin walipewa kadi za TANU na
wakaambiwa wafungue tawi Mikindani. Wakati Msham Awadh na Ali Muhidin wakiwa
njiani kwenda Dar es Salaam kukutana na Nyerere, Mohamed Ali alisafiri kwenda
Lindi kukutana na Mnonji na kumweleza kuwa Mikindani walikuwa wamekusudia
kufungua tawi la TANU. Mnonji alimpa kadi Mohamed Ali na akawa mwanachama na
akamwambia arudi Mikindani na kuanza kufanya kampeni kwa nguvu kwa ajili ya
TANU na awafahamishe watu kuwa Nyerere yupo njiani kuja Jimbo la Kusini.
Julius
Nyerere, Ali Mwinyi Tambwe na Rajabu Diwani waliwasili Mikindani kutoka Lindi
siku ya Jumamosi. Kabla ya kuwasili ujumbe huo, kazi kubwa kuliko zote
waliyokuwanayo uongozi wa TANU Mikindani ilikuwa kutafuta mahali pa kumlaza
Nyerere. Walimwendea Ahmed Adam, Mnubi mmoja tajiri na mtu wa makamo,
aliyemiliki nyumba moja ya fahari. Nyumba hii ilikuwa ya ghorofa moja na
ilijengwa kwa mawe na chokaa. Ahmed Adam aliombwa awe mwenyeji wa Nyerere na
ujumbe wake. Nyumba hii tayari lilikuwa na kisa chake. Ilijengwa na hayati kaka
yake Ahmed Adam baada ya Vita Kuu ya Kwanza. Kaka yake alikuwa askari wa Kinubi
aliyekuwa katika jeshi la Wajerumani. Huenda alichukuliwa Misri mwishoni
mwa mwa karne ya kumi na tisa na
Wajerumani kuja Tanganyika kama mamluki katika jeshi la Wajerumani wakati wa
vita vya Maji Maji. Baada ya vita alilipwa kiinua mgongo na serikali ya
Ujerumani na kwa kutumia fedha hizo alijenga nyumba hiyo. Katika Vita Kuu ya
Kwanza yeye alipigana katika jeshi la Wajerumani dhidi ya Waingereza. Baada ya
vita Wajerumani wakiwa wameshindwa vita, Waingereza waliitikadi nyumba hiyo
kama mali ya adui wa himaya ya Kiingereza na kwa hiyo ilibidi itaifishwe. Hii
ilikuwa ndiyo nyumba pekee iliyokuwa nzuri yenye kumilikiwa na Mwafrika na kwa
ajili hii haikuweza kukosa kuhusudika.
Utawala
wa Waingereza ulikuwa katika taratibu ya kuitaifisha nyumba hiyo wakati
ilipofahamika kwamba serikali isingeweza kufanya hivyo kwa sababu ya kifungu
cha sheria ambacho kilisema kuwa mali ya Waafrika waliokuwa wakitumika katika
majeshi ya watawala wao haiwezi kutaifishwa.
Hii ilinusuru nyumba hiyo na hivyo ilibakia mikononi mwa mwenyewe mpaka
alipofariki na nyumba hiyo ikaja kuwa katika miliki ya mdogo wake, Ahmed Adam.
Ahmed Adam alikubali kumpokea Nyerere na ugeni wake nyumbani kwake. Nyumba hiyo
ilikuja kuwa tawi la kwanza la TANU Mikindani. Siku hiyo hiyo ya Jumamosi,
usiku Nyerere aliitisha mkutano na
wanachama kama thelathini hivi walihudhuria. Nyerere aliwaeleza kwa
ufupi juu ya ile safari yake ya Umoja wa Mataifa na hali ya siasa kwa ujumla mjini
Dar es Salaam. Nyerere aliwahakikishia waskilizaji wake kuwa kulikuwa na
uwezekano mkubwa sana kuwa Tanganyika itakuwa huru katika uhai wao.
No comments:
Post a Comment