Sunday, 16 February 2014

TANU Ilivyovunja Ngome ya Kanisa Katoliki Jimbo la Kusini, 1955 Sehemu ya Nne


TANU Ilivyovunja Ngome ya Kanisa Katoliki Jimbo la Kusini, 1955
Sehemu ya Nne

DC mkoloni alikataa kutoa kibali kwa TANU kufanya mkutano wa hadhara. Akiwa amekasirika sana, Shabaan Msangi aliitisha mkutano wa dharura wa tawi uliohudhuriwa na Nyerere na Tambwe. Baada ya mkutano huo Tambwe alikwenda kumwona DC. Ruhusa ilitolewa, na adhuhuri hiyo siku ya Jumapili, katika kiwanja ambacho Wazungu walikuwa wakicheza gofu, ambako mwaka mmoja uliopita Gavana Edward Francis Twining alitoa hotuba iliyowavunja moyo Waafrika, Nyerere alihutubia mkutano wa hadhara. Kamwe haijapata kutokea kabla ya siku ile katika historia nzima ya Jimbo la Kusini, watu wengi kiasi hicho kujumuika mahali pamoja. Wazungu na Wahindi pamoja na askari, watu wakiwa wamekaa na wengine wamesimama katika  ya jua kali walikuja kumsikiliza Nyerere akihutubia. Ili kuhakikisha amani na usalama pale mkutanoni serikali iliweka askari waliouzunguka uwanja mzima wa mkutano. Nyerere aliwafikishia watu ule ujumbe wa TANU wa kuwa, kutawaliwa ni fedheha, na Waafrika wa Tanganyika lazima wadai uhuru wao. Uingereza ilikuwa ikiitawala Tanganyika chini ya udhamini kwa niaba ya Umoja wa Mataifa, na wakati ukiwa muafaka inabidi Uingereza ikabidhi nchi kwa wananchi wenyewe. TANU ilikuwa imewasili Jimbo la Kusini.

Tangu mwaka 1954 tetesi za chama cha siasa kilichoanzishwa Dar es Salaam kupigania uhuru zilikuwa zimepenya na kufika Mikindani, mji mdogo kusini mwa Lindi. Huko Mikindani kama ilivyokuwa mjini Lindi, harakati za utaifa zilianzia kwa wakazi wa mjini, Wamakonde wengi wao wakiwa Waislam. Kinyume na imani ya watu wengi kuwa Wamakonde ni wapagani, Wamakonde pekee waliokuwa si Waislam walikuwa wale waliokuja kutoka Msumbiji, koloni la Wareno. Hawa ni Wamakonde waliovuka mto Ruvuma kuingia Tanganyika kutafuta kazi katika mashamba ya mkonge kama manamba. Uislamu ulikuwa umeimarika Kilwa na sehemu nyingine za pwani kwa zaidi ya miaka elfu moja. Wamakonde wasio Waislam wanaweza kutambulika kwa chale walizochanja  katika nyuso zao na ndonya kwa wanawake wao. Wamakonde wa Tanganyika kutoka Lindi, Mikindani na Mtwara katika mwambao wa ukanda wa pwani wa kusini ni kabila la Waislam wengi. Wamakonde Wakristo wanatoka katika maeneo yanayozunguka Masasi ambayo hadi sasa ni eneo la Wamishonari. Wamishonari wa UMCA waliingia Masasi, nchi inayokaliwa na Wamakua na Wamakonde katika mwaka 1876.

Mikindani haikuwa kama Lindi. Lindi ilikuwa kituo cha biashara na utawala wa kikoloni katika Jimbo la Kusini. Lindi ilikuwa na uwanja wa gofu, sinema na kilabu mahususi kwa Wazungu ambayo hakuna Mwafrika au Mhindi aliyekanyaga hapo bila sababu ya maana. Lindi ilikuwa na barabara za lami na mitaa yake iliwashwa taa usiku kuondoa giza. Kadhalika mji ulikuwa na idadi ya kutosha ya Waafrika waliokuwa katika utumishi wa serikali. Wakati huo Lindi ilikuwa manispaa iliyokuwa ikikua na yenye shughuli nyingi. Ikilinganishwa na Lindi Mikindani ilikuwa kijiji kikubwa cha uvuvi kisichokuwa na mambo ya mjini na wakazi wake bado walitumia taa za kandili. Si watu wengi waliokuwa wakihamia Mikindani kutoka sehemu nyingine kuja kutafuta kazi. Uhamiaji wa watu kutoka sehemu nyingine  kuja mjini Mikindani ulikuwa katika kiwango cha chini sana. Watu pekee waliokuja Mikindani walikuwa Wamakonde kutoka Newala na Masasi ndani ya Tanganyika na wale kutoka upande wa pili wa mpaka toka Msumbiji. Hawa walikuja kufanya kazi katika mashamba ya mkonge yaliyokuwa yakimilikiwa na ukoo wa Karimjee. Hawa Wamakonde wahamiaji walikuwa wakidharauliwa na wenyeji na kwa ajili hii Wamakonde wakiwa hawana dini walijitenga na wenyeji. Hakukuwa na maingiliano baina ya Wamakonde kutoka koloni la Wareno la Msumbiji na Wamakonde Waislam wa Tanganyika. Wakiwa mbali na nyumbani ambako maisha chiini ya Wareno yalikuwa magumu sana hawa Wamakonde  waliangukia chini ya ulezi wa  Kanisa.

Ili kuepuka mgongano na Waislam wamishonari walikuwa wamejenga kanisa kubwa sana juu ya kilele cha mlima maili chache toka Mikindani sehemu moja ikijulikana kama Mchuchu.  Karibu na kanisa walikuwa wamejenga shule ambayo Alfred Omari alikuwa akifundisha. Baba yake Alfred alikuwa Mmakua Muislam lakini mwanae alibatizwa kwa ajili ya kupata elimu. Inasemekana Mwafrika wa kwanza kusoma shule ya misheni kule kusini alikuwa Charles Suleiman. Huyu alikuwa kijana wa Kiislamu aliyebatizwa na wamishonari. Alikuja kuwa Mwafrika wa kwanza kufuzu ualimu katika miaka ya mwishoni ya 1800.

Mbali na changamoto hii kwa Uislamu kutoka kwa wamishonari, Mikindani ilibakia kuwa chemchemu ya elimu ya Kiislamu. Mikindani ilijivunia mchanganyiko wa wanachuoni wenye sifa kubwa ndani na nje ya Tanganyika. Elimu ya dini ya Kiislamu ilifundishwa  Mikindani na Sheikh Suleiman bin Said na mdogo wake Ali, Wagunya kutoka Mombasa; Kenya; Sheikh Saleh Maondoa kutoka visiwa vya Comoro; Sheikh Hassan bin Hassan Mchendange, Mmakonde kutoka Mikindani; Sheikh Ahmed Mohamed Ghazal, Mwarabu kutoka Mombasa; Sheikh Abdallah wa Mwalimu; Mohamed bin Abdallah na Sheikh Fumai bin Silim, Mmakonde wa Mikindani. Kutokana na hawa usufi uliota mizizi na tariqa za Kadiria na Shadhly zilidumu katika sehemu zote za Waislam huko kusini. Kadiri miaka ilivyopita wenyeji wa sehemu zile za kusini, Wamakonde, nao wakaipata elimu hii ya Kiislam kutoka kwa wageni na mabadiliko haya yalikuja kukutana na kuibuka kwa harakati za kudai uhuru mara baada ya vita kuu ya pili.

Wanachuoni wa Kiislamu mjini Mikindani hawakuwa wakipendeza machoni mwa Waingereza kama vile walivyokuwa hawapendezi kwa Wajerumani. Mbali na chuki dhidi ya utawala wa kikoloni kufuatia Vita Vya Maji Maji, Waislam walikuwa na chuki zao binafsi dhidi ya Waingereza kutokana na amri waliyotoa ya kumfukuza mwanachuoni mashuhuri wa Kiislamu, Sheikh Abdallah wa Mwalimu. Sheikh Abdallah aligombana na Waingereza juu ya jambo la akida na uadilifu. Sheikh Abdallah  alikuwa liwali akihukumu kwa mujibu wa sharia za Kiislam pale Mikindani. Katika wadhifa huu, afisa wa kikoloni aliamuamuru kutekeleza wajibu ambao Sheikh Abdallah aliuchukulia kuwa ulimvunjia hadhi yake, heshima na itibari kwa Uislamu. Sheikh Abdallah, kutokana na ugomvi huu, alihamishiwa Kondoa Irangi, sehemu yenye Waislam watupu katika Tanganyika, jimbo la kati. Sheikh Abdallah aliishi Kondo Irangi katika miaka yake ya mwisho na kufariki huko. Waislam mjini Mikindani hawakuweza kuwasamehe Waingereza wala kusahau ule udhalimu dhidi ya Sheikh Abdallah. Mwanae, Sheikh Mohamed bin Abdallah wa Mwalimu aliitwa kutoka Lindi kuja kuongoza Tariqa ya Kadiria mjini Mikindani baada ya kifo cha baba yake. Mohamed bin Abdallah, alisoma elimu ya Kiislamu mjini Kondoa. Mjini Lindi alianzisha zawiyya, akahuisha Tariqa ya Kadiria na akawa na madras yake mwenyewe. Alipofariki Sheikh Suleiman bin Said na mdogo wake, Mikindani, nyumbani kwa Sheikh Abdallah wa Mwalimu kukawa hakuma khalifa wa kuongoza tariqa. Hatua ya Sheikh Mohamed kuja Mikindani ilisadifiana na kuibuka kwa TANU. Sheikh Mohamed akiwa khalifa wa Kadiria na murid wake ndiyo walikuwa watu wa kwanza kujiunga na TANU pale Mikindani.


1 comment:

Unknown said...

Tunaelezwa na wazee pale UHURU ulipopatikana katika Mikutano ya hadhara khasa DaresSalaam waliokuwa wakihudhuria kwa wingi walikuwa ni Waislamu. Nyeyere akitamka mambo ambayo yakiwagusa Waislamu wakisema, Pasuaaaaaaaaa! Siku Nyerere akasema "Ikija kuchanika asilie mtu, " Taib, iliwachanikia Waislamu kuanza kupigwa pande na mwisho kutumiliwa Waislamu wenzao kuiua EAMWS.

Mie lakini nitaitumia Pasuuuuuuuu, kwa kwetu hapa Visiwani, anapoelezea kitu mtu, kikakuna na ikiwa sehemu ya kurusha madongo, hunena, Pasuaaaa.

Ben Riajl