Muhammad YussufNamshukuru sana rafiki na ndugu yangu mpenzi, Mohamed Said, kwa utafanuzi wake mwanana alioutowa kwa ufasaha mkubwa kuhusu Mapinduzi ya Zanzibar na hasa juu ya washirika katika Mapinduzi hayo.
Nimefarijika sana na pale alipoandika kuwa "Ikiwa tutachukulia kuwa hii ndio historia ya kweli, basi Kassim Hanga hawezi kuwa kinara wa Mapinduzi ya Zanzibar".
Isitoshe, Hamza Rijal katika mchango wake amemuelezea Hanga kuwa ni mtu mzuri na ambaye ameshiriki kwa vitendo kuzuia mateso na mauaji ya watu wasiokuwa na hatua wakati wa Mapinduzi. Hata kaka yangu, Abdulla Al Harthy, hakumzunguzia Hanga kwa ubaya kadri alivyomjua.
Na kwa kweli, huyo ndiye Hanga niliyemjua mimi. Na ndio maana wema wake na wema wa wenzake, akina Othman Sharif, Twala na wengineo, uliwaponza na kusababisha wanamapinduzi kudhulumu roho zao.
Kwa upande mwengine, nakubaliana kabisa na hoja inayoashiria kuwa hatuwezi kuzungumzia Mapinduzi ya Zanzibar bila ya kumjadili Hanga na ushiriki wake, lakini ni ukweli usiofichika kuwa popote pale yalipofanyika Mapinduzi, roho za watu wasiokuwa na hatia zilipotea. Hanga alilijua hilo; na ndio maana alitumia ushawishi wake kujaribu kuzuia mauaji na mateso yasiyo ya lazima.
Ikiwa hivyo ndivyo, hivi itakuwa sahihi kumnyooshea kidole Hanga kwa kuhusika na mauaji ya watu waliopoteza maisha bila ya sababu za msingi? Hivi tunasahau kuwa katika utekelezaji wa zoezi la Mapinduzi, siku zote kuna mchanganyiko wa watu wazuri na wenye nia njema ya kutaka kuleta mabadiliko ya kweli kwa maslahi mema ya Wananchi; na wale wenye nia mbaya ya kutaka kujinyakulia madaraka kwa maslahi yao binafsi na kulipiza visasi.
Kwa bahati mbaya, Mapinduzi ya Zanzibar yamegubikwa na kumililkiwa na watu wengi waliokuwa waovu na wenye nia mbaya kwa maslahi mapana ya Zanzibar; Mapinduzi ambayo athari zake mbaya bado tunaendelea kuziona zikijitokeza zaidi ya miaka 50 tokea kufanyika kwake.
Kwa muktadha huu, hapana shaka yoyote ile kuwa Abdulla Kassim Hanga na wahanga wenzake watakumbukwa zaidi kwa wema wao na mchango wao adhimu katika jitihada za kuwaletea Wananchi wa Zanzibar mabadiliko ya kweli na yenye Faida na maslahi kwao na kwa vizazi vijavyo.
Mohamed Said Mzee Issa bin Nasser Al - Ismaily mwandishi wa kitabu "Zanzibar: Kinyang'anyiro na Utumwa," ni katika watu walioathirika sana na mapinduzi. Baada ya mapinduzi alihamia Dar es Salaam. Siku moja alimuuliza Abdulwahid Sykes ilikuwaje Zanzibar? Abdul Sykes alimwambia Issa Nasser kuwa tusizungumze yaliyotokea Zanzibar yatatuvunjia udugu wetu.

Habari hii ipo katika kitabu cha Dr. Harith Ghassany "Kwaheri Ukoloni Kwaheri Uhuru.'' Abdul Sykes hakutaka walizungumze tatizo la Zanzibar kwa kuwa wengi katika jamaa walishiriki kwa namna moja au nyingine kufanikisha yale Mapinduzi. Ila kitu ambacho kabisa hawakukitegemea ni mauaji yaliyotokea katika Mapinduzi na baada ya Mapinduzi. Mauaji haya na wao mikono yao ilikuwa imeloa damu kwa kule kushiriki kwao kuiangusha serikali ya Mohamed Shamte. Huenda wengi wasijue kuwa usiku ule wa mapinduzi Karume alikuwa mgeni nyumbani kwa Abbas Sykes, mdogo wake Abdul Sykes, Wakati ule Abbas alikuwa Regiona Commissioner wa Eastern Regional na akiishi Mtaa wa Shaaban Robert. Ali Mwinyi Tambwe alikataa kuzungumza na Prof. Haroub Othman kuhusu mchango wake katika Mapinduzi na kaingia kaburini bila kufungua kinywa chake kuhusu Mapinduzi. Abbas Sykes alikaa kimya miaka yote hakutaka kueleza lolote alilojua kuhusu Mapinduzi hadi alipokutana na Dr. Ghassany wakati akitafiti kuhusu kitabu chake. Abdul Faraj alizungumza na Dr. Ghassany kuhusu Mapinduzi kwa heshima ya Abbas Sykes rafiki yake toka utoto.Hapa nimewataja wazee wetu wachache tu. Wote hawa leo wakiangalia kilichotokea baada ya Mapinduzi wanajiuma vidole vyao na hii ndiyo sababu ya wao kujiweka mbali na historia hii. Hawataki kuingia katika historia hii ya Zanzibar.
|
![]() |
Masheikh Maarufu wa Dar es Salaam na Zanzibar Wakiwa Nyumbani kwa Abbas Sykes Mtaa wa Shaaban Robert 1962 alipoteuliwa kuwa Regional Commissioner wa Easter Province Walifika Pale Kumuombea Dua |
![]() |
Kushoto: Ibun Saleh, Juma Aley, Mohamed Shamte, Dr. Baalawy, Ali Muhsin |
No comments:
Post a Comment