YALIYOTOKEA KIFO CHA ABDALLAH KASSIM HANGA


1 Vote

WAKATI Dk. Harith Ghassany anaandika kitabu chake, ”Kwaheri Ukoloni Kwaheri Uhuru,” siku moja usiku alinipigia simu kutoka Washington. Wakati ule mimi naishi Tanga. Dk. Ghassany akaniuliza kuhusu Abdallah Kassim Hanga aliyewahi kuwa Waziri baada ya Mapinduzi ya Zanzibar. Nadhani katika mazungumzo yetu siku za nyuma nilipata kumweleza kuwa nilimfahamu Hanga katika utoto wangu.
Baada ya kumpa kisa hiki sikumaliza akanikatisha na kuniambia angependa anirekodi katika kinasa sauti ili atumie maelezo yangu kwenye kitabu. Hapa chini ndiyo niliyosema kuhusu Hanga na ndivyo yalivyo katika kitabu:
Picha hii iliyochukuliwa tarehe 16 Januari 1968 inamuonesha Mwalimu Julius Nyerere akihutubia mkutano wa kumuumbua Abdullah Kassim Hanga (aliyekaa baina ya maaskari wawili) na hiyo inaaminika kuwa siku ya mwisho Hanga kuonekana hadharani.
Picha hii iliyochukuliwa tarehe 16 Januari 1968 inamuonesha Mwalimu Julius Nyerere akihutubia mkutano wa kumuumbua Abdullah Kassim Hanga (aliyekaa baina ya maaskari wawili) na hiyo inaaminika kuwa siku ya mwisho Hanga kuonekana hadharani.
”Mimi nikiishi na baba yangu mtaa wa Somali, namba 22. Klabu ya mwanzo maarufu ya Kilwa Jazz Band ilikuwa kwenye nyumba ya mama yake Abdu Kigunya. Mbele ya nyumba yao ikifika kama saa tisa, kumi, laasiri, wazee walikuwa wanaweka jamvi pale, wanacheza bao. Sasa hivi ukienda pamejengwa majumba ya maghorofa.
“Hanga akija pale mtaa wa Gogo, kona na Mtaa wa Mchikichi, nyumba ya kona barazani wazee wametandika majamvi wanacheza bao. Mimi nilimjuwa Hanga kwa sababu nikimuona kwenye magazeti. Na wakati ule mawaziri wakitembeya na yale magari meusi yakiitwa “Humber.” Sikumbuki kumuona Hanga kuja pale na gari.
Na Mohamed Said
Na Mohamed Said
“Basi ikapita, Mapinduzi Unguja yakatokea sisi wadogo, hatujui nini kinachotokea. Mwaka 1967 nadhani, pale Mnazi Mmoja, Dar es Salaam, Anatoglou Hall, tukicheza mpira wa miguu pale. Mambo yalianza Mnazi Mmoja katika mkutano wa hadhara. Hanga katolewa jela Ukonga kaletwa pale kuadhiriwa na Nyerere. Sisi ni watoto, mambo yale na nyimbo zile lazima tujumuike. Hanga akaletwa pale. Namuona Hanga mimi kwa macho yangu ya kitoto na miwani yake ile.
“Hanga alikuwa mwembamba na mrefu na alikuwa na thick hair. Alikuwa mtu mwenye kupendeza. Kaja pale na uso ulionyong’onyea. Lakini sisi hatujui kinachotendeka. Watoto wa Kiswahili miaka 14, 15, 16, ni wadogo. Hatujui kinatendeka nini. Lakini mimi najua kuwa yule pale Hanga namuona kuwa ni mfungwa.
“Hanga miwani iko puani uso umemparama kama jiwe la kiama, madevu yamemjaa. Anaadhiriwa! Jua la saa sita mchana linampiga vizuri. Kwa pale kukaa na kajiinamia nilijuwa kuwa mambo si mazuri. Nyerere pale anazungumza na wote wanasikiliza. Nyerere unajua. Nyerere alikuwa ni orator (mzungumzaji mzuri).
“Na kuna kumuuwa mtu kiungwana. Nakumbuka incident moja Nyerere anamuonyesha kidole Hanga anasema “hili, hili, hili. Hana lolote. Hakuna lolote anaweza kufanya huyu. Afadhali huyu mwanzake [Babu].” Ukitizama kwenye Tanganyika Standard, wakati ule bado halikuchukuliwa na serikali, wakati ule mhariri ni yule Muingereza, Brandon Grimshaw.
“Utakuta full page. Mimi kwa jicho langu nimeona kwa sababu baba yangu mimi akinunua lile gazeti. Picha ya Hanga iko mbele na madevu na miwani yake ile. Si mimi tu, watu wengi wanakumbuka hiki kisa. Mimi baba yangu rafiki zake walikuwa Jaha Ubwa, Twala…Wakitembeleana zamani wakati wa pasaka. Baba yangu alikuwa memba wa band ya Black Birds ya Bwana Ally Sykes.
“Nadhani kule ndo walikofanya urafiki na hawa jamaa wa Zanzibar. Picha yangu mimi ya Mzanzibari, wakija kule nyumbani, unamuamkia na suala lilikuwa “wewe umeshahitimu wewe.” Na ile ”sophistication” ya wake zao wakija nao pale, yale mavazi, mabuibui, uturi ule, vile vyakula wakiandaa nyumbani pale.
“Hii ndo picha yangu ya Mzanzibari. Palikuwa na picha pale ukutani ya marahemu father wangu na kina Jaha Ubwa. Ile picha ikapotea pale ukutani. Ikawa haionekani tena. Lakini palikuwa mzee akizungumza habari za akina Twala alikuwa akinong’ona. Nahisi mzee alikuwa ana khofu. Ile ni dalili ya woga. Kitu kibaya kimetendeka.
“Lakini lazima aulize. Vipi mkewe. Watoto vipi? Lakini hawezi kusema kwa sauti. Siku nilipokuja kukutana na Ali Nabwa aliponielezeya habari za Zanzibar, nikamwambia mimi baba yangu alikuwa ana masikilizano na akina Twala na yeye akaanza ku open up sasa. Nikasema duu! Alipotoka jela Ali Nabwa alikuja pale mtaa wa Narungombe na Skukuu.
“Pale palikuwa na baraza maarufu sana ya Saigon Football Club. Nabwa alikuwa anakuja pale. Tukitoka tukikaa pembeni tukizungumza chamber. Nilijua baadaye sana kuwa kumbe alikuwa ametoka jela. Pale ndo nilipoanza kuwaona Wazanzibari kwa sura nyingine sasa. Kumbe zile bashasha zinadanganya?
“Kuwa Hanga ndiye aliyekuwa kinara wa Mapinduzi ya Zanzibar hili si jambo lenye utata tena. Ikiwa hivyo ndivyo Hanga hatoweza kuutua mzigo wa roho zilizopotea katika mapinduzi hayo. Ikiwa Hanga atalaumiwa kwa vifo vya maelfu ya Wazanzibari nani alaumiwe kwa mauti yaliomfika Hanga tena kwa kuuliwa kikatili kwani hapana neno zaidi ya hilo linaloweza kutosheleza kuelezea jinsi Hanga alivyouliwa.
“Kichekesho kikubwa ni kuwa wale waliopoteza roho na kutangulia mbele ya haki yao yalikuwa yamekwisha. Lakini kwa wale wajane na mayatima waliobakia nyuma na kuhangaika, kifo cha Hanga na wenzake katika wale waliofanikisha mapinduzi kuuliwa kwao kulikuwa miujiza ya aina yake, uchawi usioelezeka nani fundi wake. Ilikuwa vigumu kueleza. Ingeeleweka vyema endapo kisasi cha kuitoa roho ya Hanga kingetimizwa kwa mikono ya maadui zake waliopinduliwa. Haikuwa hivyo.
“Wale wajane na mayatima walililipiziwa kisasi na watu waliokuwa maadui wakubwa wa hao waliopinduliwa. Vipi Hanga kiongozi mkuu wa mapinduzi aje kuwa adui wa mapinduzi yenyewe kiasi cha kuwa hukumu ya kumtosheleza haikuwa kifo tu bali kifo cha kishenzi?
“Fikra za Hanga zilikuwaje pale alipokuwa peke yake ndani ya selo Ukonga Prison…usiku ukimpita bila ya hata lepe la usingizi akiwaza yanayomkabili. Nini kilikuwa kikimpitikia katika ubongo wake wakati wauaji wake walipomtoa katika selo yake na yeye akawakabili ilhali akijua kuwa walikuwa wamekuja kuitoa roho yake. Fikra yake ilikwenda wapi?
“Ilikwenda kwa Sultan Jamshid bin Abdullah na Masultani wengine waliopita ambao wameiaga dunia mikono yao ikiwa haina damu, au kwa Abeid Amani Karume aliyeingia madarakani kwa mapanga ya Wamakonde wakata mkonge kutoka Sakura na Kipumbwi? Fikra ya Hanga ilielekea wapi? Kwa Nyerere aliyemsaliti? Hakika ni wazi hakutegemea mapinduzi aliyoyaasisi yangemgeukia na kuwa sababu ya yeye kutolewa roho kwa kuuliwa kishenzi.
Jambo la kusikitisha ni kuwa hadi pale alipokamatwa na kuwekwa jela Ukonga na kufikishwa mbele ya mkutano wa hadhara na kuadhiriwa na Julius Nyerere tayari alikuwa keshapoteza kila kitu achilia mbali dira ya mapinduzi aliyokusudia ingeongoza Zanzibar. Hanga hakuwa kamwe na uwezo wa kumfanya Karume lolote kwani Karume tayari alikuwa chini ya mbawa za Nyerere, ngome ambayo Hanga asingeweza kuitikisa achalia mbali kuibomoa.
Muungano baina ya Tanganyika na Zanzibar ilikuwa hirizi tosha ya kumkinga Karume. Katika mkasa wa kuuliwa kwa Hanga ndipo msemaji mmoja akasema, “Maiti toka makaburini mwao walionyesha ujuzi wa kufanya miujiza na uchawi wao kwani laiti kifo cha Hanga kingesababishwa na wale waliyopinduliwa kisasi chake kingekuwa cha kutisha.
Ilibidi Hanga kwa miujiza ya maiti zile auliwe na wale wale aliowaweka madarakani watu ambao hapakuwepo na sababu ya wao kumuona adui.
Itaendelea wiki ijayo.