Friday, 15 May 2015

Majanga, Matokeo na Imani Na Ben Rijal


Makala mbili mfululizo nitazungumzia juu ya majanga, makala ya mwanzo ityazungumzia majanga kwa jumla na makala ya pili nitajaribu kuangalia katika majanga na matokeo yake hali ya kiroho inakuwaje?

Wataalamu wanatufahamisha kuwa kuna aina mbili kuu za majanga, kuna majanga ya kimaumbile na kuna majanga yanayochangiwa na mkono wa mwanadamu.

Majanga ya kimaumbbile ni yale ambayo yanatokea bila ya mwanadamu kuwa ni sababu, ingawa wengine wanasema kuwa hata haya majanga ya siku hizi ya kimaumbile bado mkono wa mwanadamu unachagia kwamfano wa majanga ya ukame unaosababishwa na kukosekana mvua, ukiangalia kwa undani ni janga la kimaumbile lakini kutokanana uchangiaji wa mwanadamu katika suala la mabadiliko ya tabianchi na uchocheaji wa uongezekaji wa gesi za nyumbani (Green House Gasses) kunafanaya baadhi ya maeneo duniani kukabiliana na mvua zenye kuleta mafariko na maafa wakati maeneo mengine hupata ukame wa muda mrefu au kuendelea kuwa wanapata ukame wa mara kwa mara.

Majanga ya Kimaumbile

Haya huwa katika umbile la dunia, hewani au kuhusiana na maji. Mara nyingi husikia matokeo ya matetemeko ya ardhi (earthquake) kama hili tokeo la karibuni lilotokea nchini Nepal. Matetemeko ya ardhi yamekuwa mengi duniani. Matetemeko ya ardhi ardhini na matetomeko ya ardhi yanayotokea baharini mfano wa Tsunami. Matetemeko ya ardhi ni janga kubwa ambayo huathiri maisha, mali, miundo mbinu n.k. Tsunami iliotokea mwaka wa 2004 na chehche zake kufikia hata huku maeneo ya kwetu katika ukanda wa Afrika Mashariki lilihesabiwa kuwa ni janga la tatu kwa ukubwa kutokea duniani na lilichukua roho za watu 229,000 kwa mara mmoja. Katika mwaka wa 2011 Tetemeko la ardhi lilokuwa na ukubwa wa kipimo cha Ritchr 9.0 huko Tohuku inakadiriwa kuchukua roho za watu 15,889 na watu kama 6,152 kujeruhiwa na watu wasiopungua 2,014 wamepotea hadi leo hawajulikani walipotelea wapi? Mwaka wa 2010 nchini Chile kulitokea tetemeko la ardhi lilichukua roho za watu wasiopunguwa 525, mwaka wa 2008 huko China katika mji wa Sichuan tetemeko la ardhi lilichukua roho za watu 61,150. Matetemeko ya ardhi hutokea kwa sekunde tu lakini athari zake huwa ni kubwa mno.

Mafuriko

Mafuriko hutokanana mvua kubwa na maji kujaa na kwa kasi kubwa na kuvamia maeneo ya nchi athirika na kuharibu miundo mbinu ya barabara, njia za umeme, mabawa ya kuzalishia umeme n.k. Katika majanga ya mafuriko ambayo bado yamo katika kumbukumbu na kuwafanya wanahistoria kuyaandika na kutowa kumbusho kwa wanadamu ni kama yafwatayo: Mafuriko ya Johnstown yaliotokea mwaka wa 1889 na kuchukua roho za watu 2,200, mafuriko ya Huang He katika mto wa njano katika mwaka wa 1931 inakisiwa kuwa zilipotea roho za watu baina ya watu 800,00 na 4,000,000, mafuriko yaliosababishwa kufurika kwa mto Yangtze nchini China yalisababisha watu milioni 14 kukosa makazi, mafuriko ya Pakistan katika mwaka wa 2010 yaliathiri watu zaidi ya milioni 20 kwa njia mbalimbali. Sote tunayakumbuka mafuriko ya Msumbuji yalioandikwa hasa kwa kutokeo tokeo la ajabu la mzazi kujifungua juu ya paa la nyumba kuepuka kusombwa na maji, mafuriko hayo yaliizamisha nchi ya Msumbiji ya eneo lake kwa thuluthi kwa kugubikwa na maji na kukadiriwa watu wasiopungua 465,000 kukosa makazi na kuhitajia misada ya kila aina.

Vimbunga

Vimbunga ni kati ya majanaga ya kimaumbile na vimbunga vinavyopiga athari zake ni kubwa mno, vimbunga vya karibuni ambavyo vilileta athari kubwa mfano ni kimbunga Katrina kilochotokea Mrekani, kimbunga cha mwaka wa 1970 Bhola cyclone na kile kimbunga kilichotokea mwaka wa 1780 na kuvivuruga viiswa vya Martinique, St. Eustatius na visiwa vya Barbados.

Majanga Yanayosababishwa na Mwanadamu

Mbali na majanga ambayo hutokea kwa njia ya maumbile hivi sasa kuna majanga mengi ambayo husababishwa na mwanadamu na athari zake nazo ni kubwa pale zinazpotokea. Majanga yanayotokea na kusababishwa na mwanadamu ni watu kukanyagana katika mkusanyiko mkubwa wa watu, matokeo ya ajali za viwandani, umwagikaji wa mafuta, miripuko ya nuklia, vita na silaha zinazotumiwa n.k.

Uvujaji wa gesi katika kiwanda cha rangi nchini India mji wa Bhopal athari zake zipo hadi leo kutokanana eneo hilo liloathirika katika matokeo yake aidha watoto wanaozaliwa kuzaliwa na vilema na ardhi kukosa rutba na matokeo mengine ya Kimazingira.  Kiwanda caha Union kilichopo Bhopal nchini India ni kwanda cha rangi kilichokosa viwango nchini Marekani badala yake kilihamishiwa nchini India, msiba ulitokea katika kiwanda cha  Union Cabide mwaka wa 1984, inakisiwa kuwa watu 500,000 waliathiriwa moja kwa moja na gesi hatari ya methyl isocyanate (MIC) na kemikali nyenginezo, kutokana na takwimu za Serikali watu 2,259 walifariki mara tu tokeao lilipotokea, watu 3,787 walifariki kutokana na vifo vilivyosababishwa na maradhi mbalimbali kutoakana na uvujaji huo wa gesi. Ilipofika mwaka wa 2006 Serikali ya India ilitoa takwimu nyengine zilioelezea kuwa watu ambao waliathirika kutokana na kuvuja kwa gesi na kemikali ni watu 558,125, wengine wakiwa wameathirika lakini sio kwa kiwango kikubwa idadi yao ilifikia 38,478 na kuna waliopata vilema vya maisha idadi yao ilifikia watu 3,900.
  
Nishati ya mafuta ni muhimu kwa maisha ya mwanadamu kwani mafuta tangu kuvumbuliwa hadi hii leo yamekuwa yanapatikana katika nchi zilizokuwa kidogo kwa idadi duniani kwahio mafuta hubidi kusafirishwa kutoka nchi moja hadi nchi nyengine kwa njia ya baharini. Kumetokea ajali mbalimbali katika nyakati tofauti na kusababisha umwagikaji wa mafuta kwa wingi na kuathiri mfumo wa maisha katika bahari.

Moja katika tokeo kubwa lilitokea mwaka wa 1976 wakati meli ya Torrey Canyon iligonga mwamba na kumwaga mafuta yanayokisiwa mageloni milioni 38 katika kisiwa cha Scilly, tokeo hili ni moja katika majanga makubwa yanayohesabiwa yaliosababishwa na mwanadamu, aidha katika mwaka wa 2000 nchini Brazil bomba la kusafirishia mafuta lilipasuka nakumwaga mafuta mazito yanayokadiriwa kufikia galoni 343,200 katika ghuba ya Guanabara. Huko Marekani katika mwaka wa 2000 meli ya mafuta ijulikanayo Westchester ilimwaga mafuta yalikadiriwa kufikia kiwango cha galoni 567,000. Janga la umwagikaji wa mafuta ambalo lilishuhudiwa na watu wengi lilitokea Pakistan wakati meli iliyopewa jina la Tasman Spirit ilipasuaka pande mbili ikiwa imeshatia nanga bandarini ilimwaga mafuta ghafi yanayokadirwa kufikia tani 28,000.

Majanga yaliotokea viwandani na kusababisha athari kubwa la hivi karibuni ni lile tokeo la  kiwanda cha nuklia cha Fukushima Daiichi nchini Japan,  tokeo lilotokea mwaka wa 2011 lilikuwa ni  tokea baya zaidi baada ya lile la  Chernobyl liliotokea nchini Urusi.

Kuvuja  kwa miale ya nuklia kwenye kiwanda cha nuklia cha Chernobyl miale yaliovuja kutoka kiwandani hapo yalisafiri masafa marefu kufika hadi katika maeneo ya Mediterranean.

Majanga ni mengi mno ambayo yanatokea kila siku kuna majanga madogo madogo ambayo athari zake nazo huwa ni ndogo na kuna majanga makubwa yenye athari kubwa duniani. Majanga ambayo mengi yanayosababishwa na mwanadamu huweza kuzuilika lakini ukaidi wake mwanadamu na kukwepa taratibu alizoziweka yeye mwenyewe ndio huchangia pakubwa kutokea ajali ambazo husababisha vifo, kuharibika kwa miundo mbinu na kuchangia hasara ambayo mataifa hushindwa baadaye kuyamudu.

Majanga yaliokuwa sio ya maumbile mara nyingi yanaweza kuepukika pale tu taratibu zilizowekwa katika nchi, kanda na duniani kama zitafwatwa.

Makala ya wiki ijayo, majanga yanapotokea na hali ya kiroho inatakiwa iweje?


No comments: