Friday, 15 May 2015

Mchango wa Waislamu Katika Maendeleo ya Dunia Ibn Al-Haytham na Ben Rijal


Unapozisoma makala hizi za mchango wa Waislamu katika Maendeleo ya Dunia utaona kama zinajirejea, lakini kama utakuwa unasoma baina ya mistari utafahamu kuwa ninayomzungumzia katika makala hizi ni tafauti ya mwengine.

Ibn al-Haytham huyu ndio gwiji aliokuja kuzama na kuelewa juu ya muangaza na vipi mtu anaweza kuona. Mwalimu wangu Maalim Abeid Marine nilipokuwa Form IV alinifundisha somo la mwangaza (light) katika Fizikia na makala hii nitamtunuku na kutaka amjue Ibn al-Haytham nje ya alivyomsoma Sir, Issac Newton.

Unapowasoma wanazuwoni wa Kiislamu waliopita utaona kila mmoja katoa mchango wake na kila mmoja anamwambia mwenzake nipishe lakini kati ya wote hao anayewekwa juu zaidi ni Ibn al-Haytham alioishi baina ya mwaka wa 965 hadi 1040.

Ibn al Haytham alizaliwa katika mji wa Basra nchini Iraq aliishi katika Ukhalifa wa Bani Abass, alikuja miaka 100 baada ya kuasisiwa kiginge cha elimu kilichokuja kujulikana kwa jina la Jengo la Hekima ambapo tafsiri za kisomi mbalimbali zikifanyika.

Ibn al Haytham alijifunza Sayansi kwa magwiji wa wakati huo, umahiri wake katika taaluma na kufanya tafiti alichaguliwa kuwa Meya wa mji wa Basra lakini juu ya kupatiwa kazi hio hakukumzuwia kuendelea kusoma na kufanya tafiti, khulka ambayo imeawondoka wasomi wengi wa miaka hii ambapo akipewa cheo mtu iwe uwaziri, ubunge, utibabu, uhandisi,ukurugenzi, uwalimu basi tena ile taaluma huwekwa pembeni na  kujipweteka na kusahau taaluma aliojifunza na kuwa mwenye kuhubiri siasa, lakini Ibn al-Haytham ilikuwa ni kinyume chake kwani aliendelea kufanya tafiti na huku akishikilia cheo cha Umeya, inafaa tufwate nyayo zake.

Ibn al Haytham jambo jengine ambalo lilikuwa halimshughulishi lilikuwa madhehebu na utengamano wa kimadhehebu, wakati wa uongozi wa al-Hakim huko Misri ambao kiongozi wake alikuwa mwenye kufwata madhehebu ya Shia Ismaili akiwa hakubaliani na kiongozi wa Sunni wa Iraq lakini hakuwa na tafauti baina ya Shia na Usuni alimwalika Ibn al Haythim huko Misri kusaidia kufanya tafiti na kazi kubwa aliotakiwa kuifanya ilikuwa namna ya kuuzuwia mto Nile kwa kuwekea kingo.

Ibn al Haytham aliifanya kazi aliotakiwa kwa kusafiri katika mto wa Nile hadi kwenye kingo zake nakuangalia wapi panopoweza kujengwa bwawa amabalo alilipendekeza al-Hakim. Ibn al Haytham akaona kuwa ujzui wa nyakati zake kwa jambo hilo halitowezekana kwa hio kwa kumjua Ibn al-Hakim ukali wake na kutokubali kufanyiwa istihzai, Ibn al Haytham akajipa ugonjwa wa Uwandazimu kwani kwa kufanya hivyo kutamuepusha kuuliwa na kiongozi huyo aliokuwa hataki upuuzi lake lazima liwe, uwazimu aliojipa ulimchongea kufungwa kifungo cha nyumbani kwa miaka 10 na alifunguliwa kifungo hicho baada ya al-Hakim kufariki.

Miaka yake ya kifungo cha nyumbani hakukaa bure kwani alipata utulivu mkubwa na wengi waliofungwa jela huko nyuma waliweza kupata utulivu kuanzia Mtume Yussuf, tuje kwa Abuu Hanifa,  Ibn Taymiyah, Maulana Abula ala Maududi, Syd Qutub na wengi wengineo, jela iliwatuliza na kuzichemsha akili zao lakini sio jela za siku hizi hasa Afrika ukiwa na utulivu uliotoka nao nje ya jela uyapata upungwani utapoingia jela kwa idhilali zinazotolewa.

 Ibn al-Haytham kwahivo alijishughulisha kutaka kujua juu ya muangaza, vipi unavyofanya kazi, vipi mwanadamu anaona na kwanini anaweza kuona vitu mbalimbali. Ingawa kufanya kwake huku tafiti kulikuwa ni Mapinduzi ya kisayansi na mchango wake  ulikuwa mkubwa mno katika maendeleo ya dunia.
Mbinu za Kisayansi

Kabla ya Ibn al Haytham wajuzi wa sayansi hasa Wayunani walikuwa wakitoa jawabu za kisayansi kwa kufikiria na kudhania au kusema jambo Fulani limetokana na Mungu, alikuwa ni mtu wa mwanzo aliopinga hoja hizo na akaamini lolote lile la kisayansi ni lazima ulihakikishe kwa kulifanyia utafiti na kupata jawabu yake kisha ndio likiubalike na hii ndio mbinu iliobaki na kukubalika hadi hivi sasa.

Unaposoma vitabu vilivyoandikwa na watu wa Magharibi somo la sayansi na mchango wake mara zote huwataja Wayunani na kufwatiwa na magwijii kama Roger Bacon, Galilei na Issac Newton, ikiwa hao wote waliegemea na taaaluma ya Ibn al-Haytham, ambaye mawazo yake na uthibitisho wa matokeo ya utafiti na kufanya majaribio kwa kupata jawabu ndio uliokuja kuwaongoza.

Katika kitabu chake alichokiita Muangaza au Buku la Mwangaza alizipinga nadharia za Kiyunani ambazo zikiamini kuwa mwangaza unakuja nje ya macho, kisha hudunda kwenye kitu kisha hurejea kwenye macho ndio mtu anpoaweza kuona.

Ibn al-Haytham alizama kwenye utafiti akiwa yupo kwenye kifungo cha nyumbani kuangalia mwangaza unavyopenya na unavyopotea na kaweza kuelezea vipi muangaza unavyoingia katika macho. Ile dhana ya “Pinhole camera” alikuwa mtu wa mwanzo kuijaribu na kuiandikia matokeo yake aliyafanya hayo ikiwa miaka 100 baadaye ndio kukaja kutenegenezwa kamera ya kupigia picha. Ibn al Haytham alitaka kujua namna mwangaza unapotembea katika maji au hewa na akaja kuelezea namna mawingu yanavyobadili rangi, aliweza kuhesabu ukubwa wa hewa (atmosphere) miaka alfu baadaye kazi hio ikaja kuwezekanana kupanuliwa na kufanyiwa majaribio. Tafiti zake za kisayansi alizoziandika katika kitabu chake cha mwangaza ndio ikasaidia baadaye katika nchi za Ulaya wanasayansi wao  kutengeneza viyoo vya miwani, kiyoo cha kuongezea ukubwa wa hati, darubini ya kuoenea mbali na kamera za kupigia picha.

Ibn al-Haytahm alitoa mchango mkubwa katika ilimu ya nyota, aliweza kuitengua taratibu iliokuwa ikifwatwa ya Ptolematic ambayo ikielezea juu ya nyota na sayari zinavyozunguka na kufanya kazi, badala yake alikuja na maelezo yaliosawa kabisa juu ya nyota na sayari zinavyofanya kazi. Ilimu ya upigaji bao alifiuta kabisa kuwa sio sayansi na hakuwa akiamini kabisa kama bao husibu.

Sir, Isaac Newton aliathirika sana na kazi za Ibn al-Haytham, kwani Ibn al-Haytham alijifunza somo la Calculus ambalo ndio lilochangia kufanywa formula mbali za uhandisi tunaojivunia hivi sasa. Ibn al Haytham aliandika juu ya Kanuni inayoelezea kusogea kwa vitu (movement of bodies) ikiwa hivi sasa tunaambiwa ni ‘Newton law of motion.” Sir Issac Newton aliona tunda la “apple” lilianguka na kujiuliza kwanini lisende juu na ndipo akajua kuwa kuna nguvu ya mvutano “gravity” unaposoma kitabu cha mwangaza cha Ibn al-Haytham alikuwa tayari kishaelezea juu ya “Gravity” na soma kitabu chake uone kuwa baada ya yeye kufa kwa zaidi ya miaka 100 ndio akaja Sir, Issac Nnewton.

Ibn al-Haytham alipinga sana mambo ya kichawi na upigaji bao na aliweza kuandaa mpango wa kujua kuingia nyakati za Sala kwa kueleka Makka, aidha Ibn al-Haytham alifanya tafiti katika uga wa “psychology” kuweza kutumia muziki kuponya wanadamu na wanyama kwa baadhi ya maradhi.

Kama wenzake waliomtangulia na waliomfwatia kazi zao nyingi zilipotea. Ibn al-Hytham aliandika vitabu 200 kati ya hivyo ni 50 tu ndio vilivyobaki na kufanyiwa kazi.

Ibn al Hatham akiishi kidarweshi, kazi zake kutosifiwa ni kutokana na namna alivyokuwa akiishi. Kazi zake zilivyokuja kufanyiwa tafsiri kwa lugha ya Kilatino waliofanya kazi hizo wakalibadilisha jina lake na kumwita Alhazen mbinu iliotumiwa na watu wa Magharibi kuficha majina ya waliokuwa sio wazungu kwa kuwa kila ujuzi uwe kwa mzungu tu.

Inakubalika kuwa kazi zake alizozifanya ndiozo zilochangia kuiweka Sayansi kuwa juu katika zama zetu hizi. Makala ijayo itamueleezea

Pitia rejea zilizo orodheshwa hapo chini kuweza kumfahamu zaidi Ibn al-Haytham. Makala ifwatayo itamzungumzia Ibn Zuhr aliokuwa tabibu na akifanya upasuaji alioandika kwa kina katika kitabu chake "Al-Taisir Fil-Mudawat Wal-Tadbeer."

Rejea
Morgan, M. (2007). Lost History. Washington D.C. : National Geographic Society.
Masood, E. (2006). Science and Islam. Icon Books.
“Ibn al-Haytham.” The Columbia Encyclopedia, 6th ed.. 2012. Retrieved October 01, 2012 from Encyclopedia.com:http://www.encyclopedia.com/doc/1E1-IbnalHay.html
Steffens, B. (2007). Ibn al-Haytham : first scientist. Greensboro, N.C. : Morgan Reynolds Pub.







No comments: