![]() |
Kushoto: Mohamed Seif Khatib na Mzee Omar Suleiman |

Kibao Mbele ya Nyumba ya Mwalimu Nyerere
Makumbusho ya Kumbukizi ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere
Cherahani ya Mzee Omari Suleiman Aliyokuwa Akiitumia Kumshonea Mwalimu Nyerere Nguo. Cherahani hii Mzee Omar Suleiman Alimpa Nyerere Kama Zawadi Kutoka Kwake ili iwe Kumbukumbu ya Wakati Wao Walipokuwa Wakipigania Uhuru wa Tanganyika Cherahani hii Imehifadhiwa Katika Kumbukumbu ya Nyumba ya Mwalimu Nyerere Magomeni
...historia ya Mzee Omar Suleiman haiwezi kukamilika bila ya kumtaja rafiki yake shujaa wa uhuru na muasisi wa TANU marehemu Haruna Taratibu. Mwaka wa 1953 Haruna alikuwa na umri wa miaka 23 na akifanya kazi Public Works Department (PWD) kama mwashi. Haruna Taratibu alijaribu kuunda chama cha wafanyakazi kwa kuwahamasisha na kuwakusanya vibarua walioajiriwa katika kazi za ujenzi. Kwa sababu ya harakati hizo za kutaka kuanzisha chama cha wafanyakazi, Taratibu alionekana na wakoloni kama mtu mkorofi na mzusha vurugu. Hata hivyo Taratibu hakufanikiwa kuanzisha chama hicho na matokeo yake akapewa uhamisho kwenda Singida kama adhabu. Taratibu alivutiwa sana na harakati za Mau Mau nchini Kenya na alizoea kufuatilia matukio yake katika gazeti lake alilokuwa akilipenda sana, “Baraza,” gazeti la Kiswahili la kila wiki kutoka Kenya.
Ilikuwa katika Novemba 1954 wakati Taratibu alipokuwa akipekuapekua gazeti hilo ndipo alioposoma habari kuhusu TANU. Taratibu aliuliza pale Singida mjini kama kuna tawi la TANU. Taratibu alifahamishwa kukuwepo kwa tawi la TANU pale mjini na katibu wake alikuwa mzee mmoja kwa jina la Mzee Kinyozi. Taratibu alikata kadi yake toka kwa huyo mzee na akawa mwanachama wa chama cha siasa. Asubuhi iliyofuata Taratibu aliingia ofisini kwake na akaiweka kadi yake ya uanachama wa TANU yenye rangi nyeusi na kijani juu ya meza yake, kila mtu aione. Ofisa Mzungu wa PWD Singida hakuweza kuvumila ufedhuli kama ule, alishauri Taratibu apewe uhamisho kurudi Dodoma alikotoka, kabla hajaeneza sumu yake kwa Waafrika wengine. Hapo ndipo alipokuja kuungana na Mzee Omar Suleiman.
Mwaka 1955 wakati wimbi la utaifa wa Tanganyika lilipokuwa limepamba moto Tanganyika, Omari Suleiman alikuwa na umri wa miaka 43. Omar Suleiman alikuwa fundi cherahani akifanya shughuli zake katika nyumba moja katikati ya mji wa Dodoma. Mkabala na nyumba ambamo Suleiman alikuwa amepanga chumba kimoja ilikuwa nyumba aliyopanga Taratibu. Mara baada ya kupewa uhamisho kutoka Singida, Taratibu alimuuliza jirani yake, Suleiman, kama kuliwepo na tawi la TANU pale mjini. Suleiman alimwambia Taratibu kuwa hapakuwepo na tawi la TANU mjini Dodoma na alimjulisha kuwa kulikuwa na tetesi mjini kuwa Hassan Suleiman amemuahidi na kumhakikishia DC kuwa yeye, akiwa katibu wa Jimbo wa TAA, hatairuhusu TANU kusajiliwa katika Jimbo la Kati bila ya idhini yake. Lakini ukweli ulikuwa Hassan Suleiman akitokea katika uongozi wa TAA alikuwa tayari ameisajili TANU lakini hakumfahamisha mtu yoyote wala kufanya juhudi yoyote kuitisha uchaguzi au kufanya mkutano. Hassan Suleiman kama, Omar Suleiman alikuwa pia na umri wa miaka 43 mwaka 1955. Tofauti na Omari Suleiman, Hassan Suleimani alikuwa ameelimika na alikuwa mwanasiasa mwenye uzoefu akiwa amekiongoza chama cha African Association kuanzia miaka ya 1940 na alikuwa amehudhuria mikutano ya African Association Tanganyika na Zanzibar.
Haruna Taratibu, Omari Suleimani na marafiki zake wachache waliunda kamati ndogo kisha wakaandika barua kwenda makao makuu ya TANU Dar es Salaam kuomba ruhusa ya kufungua tawi la TANU. Katibu mwenezi wa TANU, wakati ule Oscar Kambona, aliwaandikia kuwaeleza kuwa Hassan Suleiman tayari alikuwa ameshaisajili TANU na ikiwa uchaguzi wa viongozi haujafanyika basi waonanena na yeye pamoja na Ali Ponda. Omari Suleiman na Haruna Taratibu hawakuridhika na majibu kutoka makao makuu ya TANU kwa hiyo walikwenda kutafuta ushauri kwa Edward Mwangosi, aliyekuwa mwanachama mkongwe wa African Association. Mwangosi aliishauri kamati ile iitishe mkutano Community Centre ili kujadili ufunguzi wa tawi la TANU, na Hassan Suleiman na Ali Ponda waalikwe kuhudhuria. Kadhalika Mwangosi aliishauri kamati ile kuwaalika walimu waliokuwa wakifundisha Kikuyu Secondary School, wengi wao wasomi kutoka Makerere kuhudhuria mkutano huo. Mwangosi aliwaambia wajumbe wa kamati ile ndogo kuwa wasomi wa Makerere walikuwa ni muhimu sana kwenye chama kwa kuwa wangetoa uongozi uliokuwa unatakiwa.
![]()
Mzee Job Lusinde Kama Alivyo Hivi Sasa
Karibu ya watu arobaini pamoja na wale wasomi wa Makerere, miongoni mwao Job Lusinde walihudhuria mkutano ule. (Lusinde alikuja kuwa waziri, na Amon Nsekela, alikuja kushika nyadhifa muhimu katika serikali na vilevile kuwa Balozi wa Tanzania nchini Uingereza). Hassan Suleiman na Ali Ponda hawakutokea mkutanoni. Wakati wanakusanyika kwa ajili ya mkutano, afisa wa Community Centre aliwaambia kuwa alikuwa amepokea amri kutoka kwa DC kuwa mkutano huo usifanyike. Kufuatia amri ile watu walitawanyika mara moja. Alexander Kanyamara aliyekuwa Mwafrika tajiri mjini Dodoma na rafiki wa John Rupia, wakati ule makamu wa rais wa TANU, aliwataka kuahirisha mkutano huo kwa sababu ya kutokuwepo kwa viongozi wa juu wa TAA, Hassan Suleiman na Ali Ponda. Kutokana na sababu hii na vile vitisho vya DC, mkutano uliahirishwa bila kupanga tarehe ya mkutano mwingine. Asubuhi iliyofuata Taratibu alikamatwa na polisi na kupelekwa kwenye ofisi ya DC, (hivi sasa ofisi hiyo ni ofisi ya Waziri Mkuu). Taratibu alimkuta Hassan Suleiman pale ofisini akizungumza na DC, Bwana Smith. DC alianza kumsaili Taratibu kwa kumuuliza kama alikuwa akijua kuzungumza Kiingereza. Taratibu alijibu kuwa yeye hakusoma. Akizungumza Kiingereza Hassan Suleiman alimwambia DC kuwa yeye ndiye katibu wa TANU mjini Dodoma. DC, Bwana Smith, alimshutumu Taratibu kwa kuunda chama haramu na kwa kuitisha mkutano usio na idhini ya serikali katika Community Centre jana yake ambao ulielekea kuvuruga amani. Bila woga Taratibu alijibu kwamba yeye alikuwa na mamlaka ya kuitisha mkutano kwa sababu alikuwa mwanachama wa chama cha siasa kilichosajiliwa kihalali. Taratibu aliichomoa kadi yake ya TANU kutoka mfukoni kwake yenye rangi nyeusi na kijani na kumwonyesha DC. Bwana Smith alimuuliza Hassan Suleiman kama ikiwa na yeye pia alikuwa na kadi ya TANU. Hassan Suleiman hakuwa nayo. Hassan Suleiman na DC walizungumza Kiingereza kwa muda baada ya hapo aliwataka wote wawili kuandika maelezo yao. Baada ya kuandika maelezo yake Taratibu aliruhusiwa kurudi nyumbani. Inasadikiwa kuwa wakati ule mwanachama pekee wa TANU mjini Dodoma walikuwa Haruna Taratibu na Alexander Kanyamara ambae yeye alikata kadi yake Dar es Salaam.
Kushoto: Iddi Faiz Mafongo, Sheikh Mohamed Ramia, Julius Nyerere, Saadan Abdu Kandoro na Haruna Taratibu
Dodoma Railway Station 1956
Wasomi wa Makerere, ambao Mwangosi aliwaamini sana katika kuunda TANU, walipopata habari kuhusu mkasa wa Taratibu na DC, Bwana Smith, waliogopa. Waliamua kujiweka mbali kabisa na TANU na mambo ya siasa na kuendelea na kazi yao ya kufundisha. Haruna Taratibu na Omari Suleiman sasa waliamua kugeuza mbinu, waliitisha mkutano wa siri usiku nyumbani kwa Swedi bin Athumani. Mkutano huu uliamua kuwa Taratibu lazima aende makao makuu ya TANU Dar es Salaam akazungumze na Nyerere ana kwa ana kuhusu matatizo yaliyokuwa yakiikabili TANU Dodoma. Mahdi Mwinchumu aliyekuwa mwanachama wa TANU Dar es Salaam alijitolea kufuatana na Taratibu hadi makao makuu ya chama Dar es Salaam kwa kuwa alikuwa akijuana na viongozi wa TANU. Said Mussa mjumbe mwingine wa ile kamati ya siri alijitolea vilevile kufuatana na Taratibu na Mwinchumu hadi Dar es Salaam. Siku ya kuondoka Job Lusinde alikwenda stesheni ya gari moshi kuagana na ule ujumbe uliokuwa ukielekea Dar es Salaam, makao makuu ya TANU. Lusinde aliuambia ule ujumbe kuwa jamaa wa Makerere wanaunga mkono maamuzi yote yatakayoamuliwa na ile kamati ya siri.
(Kutoka kitabu: "Maisha na Nyakati za Abdulwahid Sykes (1924 - 1968)...")
Kusoma habari zaidi ingia hapa:
http://www.mohammedsaid.com/2013/12/mzee-omar-suleiman-1910-2012-mwasisi-wa.html
|
No comments:
Post a Comment