Saigon Club iliasisiwa mwaka wa 1967 kutoka club ya Everton. Mtaa mmoja pakawa na club mbili zilizotengana na hii ikaleta uhasama mkubwa wa kimichezo baina yao. Nakumbuka Saigon na Everton walipata kucheza mechi tatu mbili Mnazi Mmoja na nyingine Kidongo Chekundu. Mechi hizi zilikuwa ngumu na zilijaa kila aina ya ubabe. Mimi nakumbuka nilicheza mechi ya kwanza Mnazi Mmoja na nilikatika jino la mbele la chini lakini si kwa ugomvi. Jumanne Hassan tukimtania kwa jina la "Guu la Ngamia" yeye alikuwa Saigon alipiga shuti kali golini na mimi nilikuwa nimesimama katikati ya "goal line," nikauzuia kwa kichwa na kwa nguvu ya shuti lile meno yakajigonga na jino likakatika kidogo. Alama hii ninayo hadi leo kutoka mwaka wa 1967 nikiwa na umri wa miaka 15. Jumanne baadae alikuja kuwa maarufu kwa jina la Jumanne Masimenti akicheza mpira Cosmopolitan chini ya kocha Mansour Magram ambae alimchukua kutoka Saigon. Baada ya hapo Simba wakamchukua kutoka Cosmo kisha alipokuwa akicheza kama mshambuliaji Timu ya Taifa wakati wa kocha Mjerumani Trutman huyu kocha akampa jina lingine la utani akamwita, "Tarzan." Jina hili nadhani kocha wake alimpa kutokana na tambo lake kwani Jumanne Allah alimjalia tambo kubwa na alikuwa ana nguvu sana lakini juu ya sifa hizi Jumanne alikuwa mpole. Jumanne ni marehemu. Jumanne alipatapo kunambia kuwa nisingeweza kucheza mpira wowote wa maana kwa kuwa yeye toka zamani alishaniona kuwa akili yangu ilikuwa zaidi katika vitabu kwa sababu hata mazoezini nikifika wakati wenzangu wanapiga danadana na kupasha mili moto mimi nakuwa nimeinamia kitabu nasoma. Jumane alikuwa akisema hivi kwa njia ya kichekesho na wale wenzetu tuliokuwa sote enzi zile za utoto watacheka sana na wengine wataniita kwa jina langu la mpira, "Eusobio." Haya mambo ni kumbukumbu ya miaka ya 1960. Eusobio alikuwa mchezaji wa Portugal kutoka Msumbiji katika Kombe la Dunia la mwaka wa 1966 mashindano yalipofanyika Uingereza. Siku zile tulipokuwa wadogo kila mtu alikuwa na jina lake la kupanga kutoka wacheza senema nyota hadi wachezaji mpira. Kulikuwa na majina kutoka Brazil na Saigon alikuwapo Rashid Vava, Garincha na kutoka Italy alikuwapo Mashaka "De Stefano." Mashaka yeye baada ya shule alisoma ukutubi (Librarian) na alikujakufanya kazi Maktaba Kuu. Miaka mingi sana sijamuona Mashaka. Wakati mwingine mtu anachukua jina la mcheza senema lakini yeye ni mchezaji mpira kama Juma Abeid Spencer. Huyu Spencer alikuwa mchezaji wa Everton ya Uingereza na alishabiana na Juma Abeid kwa tambo na kwa ajili hii Juma akapewa jina la Spencer; Hamis Marlon Brando, Selemani Jongo (Rory Calhoun). Abdallah Mkwanda yeye anacheza mpira lakini alichagua jina la mcheza masumbwi kutoka Sweden - Ingemar Johansson. Jongo alicheza timu ya mtaani ikiitwa Brazil kisha akenda Morogoro ambako alicheza na kuwa kapteni wa timu ya Mororgoro iliyochukua Taifa Cup katika miaka ya 1970 na Yanga wakamsajili na kumrudisha Dar es Salaam. Katika hawa wengi wameshatangulia mbele ya haki. Miaka mingi sasa imepita na kila miaka inavyozidi kusonga mbele ndivyo waasisi wa Saigon wanavyozidi kupungua na si kwa ajili ya kufariki tu bali mihangaiko ya maisha imewatoa wengi katikati ya mji wa Dar es Salaam na Kariakoo na kuwapeleka mbali.
Kwa kipindi kirefu sasa Saigon Club imekuwa ikisoma khitma kila mwaka kuwarehemu waliotangulia mbele ya haki. Hii imekuwa moja ya kalenda muhimu sana katika shughuli ya club hii na imekuwa ikihudhuriwa na watu wengi. Shuguli hii huwakutanisha wapenzi wa mpira masheikh na watu wa kawaida wengine huwa hawajakutana kwa kipindi kirefu. Huwa ni shughuli ya furaha na wakati mwingine kwa kiasi kidogo huwa na majonzi kwani katika kuwarehemu waliotangulia huwa wakati yakitajwa majina ya watu ambao khitma ya mwaka uliopita walikuwa hai. Kama ilivyo ada huwa jina la kwanza kurehemewa huwa linatajwa jina la Sheikh Hassan bin Amir kisha yanafuata masheikh wengine wengi, kisha wazee maarufu, kisha wanachama na wapenzi wa Saigon na mwisho ni mama zetu waliotangulia ambao kwa njia moja au nyingine walifungamana na Saigon katika uhai wao. Katika moja ya ibra za Saigon ni kule kupendeka na watu wa aina zote. Yanapotajwa majiina ya masheikh waliotangulia wengi wao katika uhai wao walikuwa hawakosi kufika katika khitma kila mwaka na masheikh hawa walipokuwa na shughuli zao katika misikiti yao waliwaeka Saigon mstari wa mbele kwa kila jambo. Marehemu Sheikh Kasim bin Juma ndiye kwa hakika alikuwa sheikh wa Saigon. Nakumbuka Sheikh Kassim alikuwa haipiti siku mbili tatu atapita club na kutoa maneno mawili matatu ya kutuhimiza katika dini. Katika Maulid ya kila mwaka ya Mfungo Sita Msikiti wa Mtoro Sheikh Kassim aliwachukua Saigon na kuwapa kazi ya uandazi katika karamu ambayo ilikusanya watu wengi sana khasa vijana wa Kariakoo. Leo nikiangalia nyuma ilikuwa kama vile Sheikh Kassim anatufunza namna ya kufanya shughuli. Katika khitma ya Saigon huwa yanatajwa majina ya watu ambao rika lao bado hai na wanakuwa na kumbukumbu nyingi za utoto wakati Saigon ilikuwa ni club ya kucheza mpira vijana wa Kariakoo ambao umri wao ulikuwa kuanzia miaka 12 hadi 20 na zaidi kidogo wakati wakisakata kabumbu katika Uwanja wa Mnazi Mmoja kwa mazoezi na Viwanja vya Jangwani kwa mechi na club pinzani kama Dundee au Young Kenya. Nimeitaja club ya Dundee kwa kuwa ilituchukulia mchezaji wetu mmoja Yakub "Gowon" Mbamba na siku ya mechi na Dundee Yakub alikuwa na wakati mgumu sana kuwaangalia machoni rafiki zake wa Saigon. Kisa hiki Yakub amenihadithia siku chache zilizopita.
Katika moja ya mambo yanayovutia hisia khasa kwa wanachama wenyewe wa Saigon ni pale katika khitma yanaposomwa majina ya vijana waliokufa wakiwa na umri mdogo sana katika miaka ya 1960 na 1970 ambao walivaa jezi ya Saigon. Mathalan Khalid Fadhili maarufu kwa jina la mpira la "George Young'' aliyekuwa mchezaji wa Uingereza. Khalid alifariki akiwa hata miaka 20 hajatimiza. Yeye alikuwa "half back" mzuri sana na wa kutegemewa na club. Mwingine aliyefariki bado mbichi ni Ahmada bin Sheikh Digila kwa jina la mpira "Benchflour" jina la mchezaji mwingine kutoka club za Uingereza. Ahmada ni mtoto wa Sheikh Digila mmoja wa mashekh maarufu Dar es Salaam na alikuwa mmoja wa wanafunzi wa Sheikh Hassan bin Amir. Katika khitma huwa napata simanzi linapotajwa jina la Sheikh Digila kisha likatajwa jina la mwanae Ahmada Digila. Katika sisi Ahmada alitushinda sana kwa elimu ya dini na usomaji wa Qur'an. Namkumbuka sana Ahmada jinsi katika khitma zikigawiwa juzuu alivyokuwa na ulimi mwepesi wenye kasi katika kusoma. Ahmada alikuwa "half back six" hodari akigombea namba na Hassan "Gilbert." Hassan yeye hakutaka kuchukua jina kutoka Ulaya. Yeye alichukua jina lake la utani kutoka kwa Gilbert Mahinya aliyekuwa mchezaji wa Sunderland (sasa Simba) akicheza "half back six," kisha akenda Yanga. Siku si nyingi nilikutana na Hassan Gilbert Mlimani City kavaa "Bermuda Pence," anafanya shopping na mabinti zake. Hassan alikujakuwa mtaalamu wa "computer," na alinifahamisha kuwa ameshastaafu kazi. Nilishangaa kwani Hassan alikuwa na taarifa zangu kuwa nami nilimtangulia katika kustaafu.
Wakati mwingine utalisikia jina la marehemu linarehemewa ingawa yeye hakuwa mwanachama wa Saigon. Hii ni katika kuonyesha mapenzi na urafiki uliopo kwa wazawa wa Dar es Salaam. Mfano nilisikia jina la Rashid Mnyika likitajwa. Mnyika kama alivyozoeleka hakupata kuwa mwanachama wa Saigon lakini ni katika vijana wa mtaani kwa wakati ule wa 1960. Mnyika alikuwa "centre forward," hatari wa Young Boys na sifa yake kubwa ilikuwa kufunga magoli kwa kichwa inapopigwa kona. Mnyika alikuwa mkubwa kwa umri kwangu na sasa katika ujana wetu akajakuwa muongeaji wangu sana nikikutananae Msikiti wa Manyema na katika mazungumzo nilikuwa sishi kumkumbusha jinsi alivyokuwa akizongwa na mabeki wakati kona ikipigwa na cha ajabu Mnyika ataruka kuwapita mabeki wote na atafunga goli. Yeye alikuwa akishangaa jinsi nilivyokuwa nakumbuka mambo mengi madogo madogo ya zamani. Mnyika alikuwa hodari hata shule na alikwenda Ujerumani kusoma mambo ya uchoraji ramani akiwa mfanyakazi wa Wizara ya Ardhi. Mnyika alifariki kiasi cha kama miaka mitatu iliyopita. Kumbukumbu yangu ya mwisho tulikutana Msikiti wa Manyema na nilipomwambia mbona kapotea akanambia alikuwa Uingereza kuwatembelea watoto wake.
Tusafiri kwa picha turudi nyuma miaka mitano iliyopita kabla hatujaangalia khitma ya mwaka huu wa 2015.
KHITMA YA SAIGON CLUB MWAKA WA 2010
 |
Dr. Gharib Bilal Akiwasili Katika Khitma 2010 Akiwa Amefuatana na Sheikh Ahmed Haidar Akipokelewa na Viongozi wa Saigon Club Mwisho Kulia ni Mussa Shagoo na Juma Simba |
 |
Dr. Gharib Bilal Makamu wa Rais Mgeni wa Heshima Kushoto Kwake ni Sheikh Ahmed Haidar Kutoka Zanzibar Aliyemsindikiza |
 |
Kushoto: Sheikh Katungunya, Sheikh Abdallah Mzee Mwita, Ustadh Adam Bingwa wa Tajwid |
 |
Mohamed Mzee Mwita Mhandisi wa Ndege Government Hangar Sasa ni Mstaafu Mmoja wa Wanafunzi Waliosoma
Shule ya Sheikh Hassan Juma Al Hassanain Muslim School |
 |
Kushoto: Marehemu Awadh Juma Maarufu "Mrido wa Chuma" na Said Ally Abbas Hawa ni Katika Waasisi wa Saigon Club 1967 Mrido amefariki Kiasi cha Kama Miaka Miwili Iliyopita na Tulimzika Makaburi ya Mwinyimkuu Magomeni. Jina la Mrido Alipewa kwa Ajili ya Ukakamavu Wake Said Ally Abbas Alikuwa Akicheza Nafasi Yoyote Mbele
|
 |
Abraham Sykes, Kaka Shomari, Kaka Hussein na Balozi Cisco Mtiro |
 |
Katikati ni Marehemu Athmani Kilambo Mchezaji wa Young African na Timu ya Taifa Kilambo Alikuwa Katika Timu ya
Tanganyika Iliyochukua Kikombe ch Gossage Miaka Miwili Mfululizo 1964 na 1965 Chini ya Kocha Myugoslavia Celebic |
 |
Katikati Brigadier Simba Waziri Simba Nyumbani Kwa Wazee Wake ni Mtaa wa Mshume Kiyate (Tandamti) |
 |
Sheikh "Rocket" Sheikh Maarufu wa Tarika Kutokea Mtwara |
 |
Kushoto: Juma Abeid (Spencer), ? Sheikh Issa Auisi Marehemu Ally Sykes Katika Khitma ya Saigon Mwaka 2010
Sheikh Issa Ausi Amesoma Shule ya Kitchwele Wakati Mmoja na Abbas Sykes Miaka ya 1930

Mwandishi Akiwa Katika Khitma ya Mwaka 2010
KHITMA SAIGON 2015
 |
Kushoto Sheikh Alhad Mussa, Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi na Iddi Simba
 |
Sheikh Mahdi Imam wa Msikiti wa Mwinyikheri Kisutu |
 |
Kushoto: Sheikh Zuberi Mmoja wa Viongozi Msikiti wa Manyema na Hamza Kasongo |
Sheikh Zuberi bin Yahya Imam Mkuu Msikiti wa Mtoro
Kushoto: Beki Na. 2 Mkali Atika Kombo Mmoja wa Waasisi wa Saigon 1967 na Harudiki Kabunju Kiongozi wa Mpira Dar es Salaam wa Miaka Mingi
 |
Katikati Aliyevaa Kofia ni Juma Abeid Spencer |
Kushoto: Balozi Paul Rupia na Mdogo Wake Stephen Rupia
Kushoto: Stephen Rupia, ? Babu Mzee mwita na Abraham Sykes
 |
Kushoto: Sheikh Walid Bin Sheikh Alhad Omar na Sheikh Ali Basaleh |
 |
Mohamed Chaurembo |
 |
Kushoto: Ayub Sykes, Kaka Hussein na Hussein Shane |
 |
Omar Zimbwe Mmoja wa Wachezaji Mpira wa Timu ya Taifa Katika Miaka ya 1960 na 1970 Akisalimia Jamaa Sheikh Zubeir katika Kumueleza Omari Zimbwe Alisema Alipiga Penalti 160 na Hakuwahi kukosa Hata Moja |
 |
Wasimamizi wa Shughuli Kushoto: Muharam Mkamba na Kulia Pembeni ni Abdulbari |
 |
Kushoto: Nusura Faraj, Abdallah Tambaza na Sheikh Rashid |
 |
Kushoto: Paul Rupia, Aliyeinama ni Mdogo Wake Stephen Rupia, ? Babu Mzee Mwita na Abraham Sykes
|
No comments:
Post a Comment