Monday, 8 June 2015

Nyerere Alipomzungumza Abdul Sykes



Katika hotuba hii ya Mwalimu Nyerere kuna jambo kakosea. Anasema safari ya kwanza kutangaza TANU alikwenda Mbeya. Hapana safari ya kwanza alikwenda Morogoro akiongozana na Zuberi Mtemvu 1954 na hii safari ya Mbeya aisemayo alozungumza na wanachama mkutano wa ndani ilikuwa mwaka 1955 alipokwenda Lindi akifuatana na Ali Mwinyi Tambwe na Rajab Diwani. Mbeya TANU ilikuja baadae sana. Ukisoma kitabu cha Abdul Sykes utayakuta haya na ithibati yake ni nyaraka nilizosoma katika majalada ya akina Sykes.

''Nyerere na msafara wake ulipokelewa na uongozi wa TANU wa Lindi huko Mbanji, kijiji kidogo nje ya mji. Msafara wa Nyerere ulipowasili Mbanji ilikuwa kiasi cha saa moja jioni hivi na giza lilikuwa linaanza kutanda. Mbali na Mpunga na wale wajumbe wawili waliokutana na Nyerere mjini Dar es Salaam mwezi uliopita, hakuna hata mtu kati ya umma ule uliokuja kupokea ujumbe kutoka makao makuu ya TANU aliyekuwa anajua Nyerere anafanana vipi. Mpunga, dereva wa lori, alijibagua kutoka kwa lile kundi la watu akawa amesimama pembeni ili Nyerere apate kumuona. Baada ya Nyerere kumtia Mpunga  machoni, Mpunga alimwendea kumsalimu Nyerere, Tambwe na Diwani; kisha aliligeukia lile kundi la watu kumtambulisha Nyerere kwa wananchi akilitaja jina lake kwa sauti kubwa. Baada ya hapo aliutambulisha ule ujumbe wa Nyerere. Nyerere na ujumbe wake ulisindikizwa kwa shangwe na kundi la watu hadi ofisi ya TANU kwenye nyumba ya Mnonji. Kupakana na ofisi ya TANU ilikuwepo nyumba ya seremala mmoja, Issa bin Ali Naliwanda. Hii ndiyo nyumba iliyochaguliwa alale Nyerere na ujumbe wake, si kwa sababu ilikuwa nzuri kupita zote. Ilichaguliwa na kupewa heshima hii kwa sababu ilikuwa karibu sana na ofisi ya TANU na hivyo basi ilirahisishia TANU kazi ya ulinzi wa Nyerere. Siku iliyofuata ilikuwa Jumapili na Nyerere aliwaomba wenyeji wake apelekwe kanisani kwa ajili ya ibada.

Kanisa Katoliki mjini Lindi ni jengo la fahari lililoko ufukweni katika Bahari ya Hindi. Lindi ulikuwa mji wa Waislam. Mbali na mlio wa kengele za kanisa hakuna mtu pale mjini aliyekuwa akishughulishwa na kile kilichokuwa kikifanyika kwenye viwanja vya kanisa. Watu wachache waliokuwa wakienda kusali kanisani walikuwa Wakristo waliokuja Lindi kutoka sehemu nyingine za Tanganyika kufanya kazi katika ofisi za serikali. Ghafla mahala hapa palipokuwa pweke, palipopuuzwa kwa miaka na Waislam wa mjini, pakawa muhimu kwa sababu rais wa TANU ambae alikuwa Mkatoliki alikuwa na haja ya kuhudhuria ibada pale kanisani. Hakuna mtu katika uongozi wa TANU wa Lindi aliyejua ndani ya kanisa lile kulikuwa vipi wala hapakuwa na yoyote kati yao aliyewahi kuingia ndani ya kanisa, si Lindi wala mahali popote pale. Uongozi wa TANU wa Waislam mjini Lindi haukumwamini Mkristo yoyote kumsindikiza Nyerere kanisani ili kumpa ulinzi. Baada ya kujadili suala hilo kwa urefu hatimaye iliamuliwa kuwa  Mpunga na wanachama wachache Waislam wenye kuaminika lazima wamsindikize Nyerere kanisani na wengine wabakie nje kulinda mlango.

Jumapili hiyo Nyerere aliingia ndani ya kanisa Katoliki mjini Lindi akifuatwa nyuma na walinzi wake Waislam wakiongozwa na Salum Mpunga, dereva wa lori shupavu. Misa hii ‘’maalum’’  ilidumu katika fikra za wale Wakristo waliokuwepo pale kanisani kwa miaka mingi kwa kuwa tukio hilo liliwagusa sana Wakristo walioshuhudia mkasa ule ndani ya kanisa la Lindi. Hii huenda ilikuwa mara ya kwanza na ya mwisho kwa Nyerere kumsalia Mungu wake huku akiwa amesimamiwa na Waislam.

DC mkoloni alikataa kutoa kibali kwa TANU kufanya mkutano wa hadhara. Akiwa amekasirika sana, Shabaan Msangi aliitisha mkutano wa dharura wa tawi uliohudhuriwa na Nyerere na Tambwe. Baada ya mkutano huo Tambwe alikwenda kumwona DC. Ruhusa ilitolewa, na adhuhuri hiyo siku ya Jumapili, katika kiwanja ambacho Wazungu walikuwa wakicheza gofu, ambako mwaka mmoja uliopita Gavana Edward Francis Twining alitoa hotuba iliyowavunja moyo Waafrika, Nyerere alihutubia mkutano wa hadhara. Kamwe haijapata kutokea kabla ya siku ile katika historia nzima ya Jimbo la Kusini, watu wengi kiasi hicho kujumuika mahali pamoja. Wazungu na Wahindi pamoja na askari, watu wakiwa wamekaa na wengine wamesimama katika  ya jua kali walikuja kumsikiliza Nyerere akihutubia. Ili kuhakikisha amani na usalama pale mkutanoni serikali iliweka askari waliouzunguka uwanja mzima wa mkutano. Nyerere aliwafikishia watu ule ujumbe wa TANU wa kuwa, kutawaliwa ni fedheha, na Waafrika wa Tanganyika lazima wadai uhuru wao. Uingereza ilikuwa ikiitawala Tanganyika chini ya udhamini kwa niaba ya Umoja wa Mataifa, na wakati ukiwa muafaka inabidi Uingereza ikabidhi nchi kwa wananchi wenyewe. TANU ilikuwa imewasili Jimbo la Kusini.''

Huenda mkutano aliokusudia Mwalimu Nyerere kuufanya Mbeya ni huu aliofanya Mkindani nyumbani kwa Ahmed Adam baada ya kutoka Lindi:

''Julius Nyerere, Ali Mwinyi Tambwe na Rajabu Diwani waliwasili Mikindani kutoka Lindi siku ya Jumamosi. Kabla ya kuwasili ujumbe huo, kazi kubwa kuliko zote waliyokuwanayo uongozi wa TANU Mikindani ilikuwa kutafuta mahali pa kumlaza Nyerere. Walimwendea Ahmed Adam, Mnubi mmoja tajiri na mtu wa makamo, aliyemiliki nyumba moja ya fahari. Nyumba hii ilikuwa ya ghorofa moja na ilijengwa kwa mawe na chokaa. Ahmed Adam aliombwa awe mwenyeji wa Nyerere na ujumbe wake. Nyumba hii tayari lilikuwa na kisa chake. Ilijengwa na hayati kaka yake Ahmed Adam baada ya Vita Kuu ya Kwanza. Kaka yake alikuwa askari wa Kinubi aliyekuwa katika jeshi la Wajerumani. Huenda alichukuliwa Misri mwishoni mwa  mwa karne ya kumi na tisa na Wajerumani kuja Tanganyika kama mamluki katika jeshi la Wajerumani wakati wa vita vya Maji Maji. Baada ya vita alilipwa kiinua mgongo na serikali ya Ujerumani na kwa kutumia fedha hizo alijenga nyumba hiyo. Katika Vita Kuu ya Kwanza yeye alipigana katika jeshi la Wajerumani dhidi ya Waingereza. Baada ya vita Wajerumani wakiwa wameshindwa vita,  Waingereza waliitikadi nyumba hiyo kama mali ya adui wa himaya ya Kiingereza na kwa hiyo ilibidi itaifishwe. Hii ilikuwa ndiyo nyumba pekee iliyokuwa nzuri yenye kumilikiwa na Mwafrika na kwa ajili hii haikuweza kukosa kuhusudika.


Utawala wa Waingereza ulikuwa katika taratibu ya kuitaifisha nyumba hiyo wakati ilipofahamika kwamba serikali isingeweza kufanya hivyo kwa sababu ya kifungu cha sheria ambacho kilisema kuwa mali ya Waafrika waliokuwa wakitumika katika majeshi ya watawala wao haiwezi kutaifishwa.  Hii ilinusuru nyumba hiyo na hivyo ilibakia mikononi mwa mwenyewe mpaka alipofariki na nyumba hiyo ikaja kuwa katika miliki ya mdogo wake, Ahmed Adam. Ahmed Adam alikubali kumpokea Nyerere na ugeni wake nyumbani kwake. Nyumba hiyo ilikuja kuwa tawi la kwanza la TANU Mikindani. Siku hiyo hiyo ya Jumamosi, usiku Nyerere aliitisha mkutano na  wanachama kama thelathini hivi walihudhuria. Nyerere aliwaeleza kwa ufupi juu ya ile safari yake ya Umoja wa Mataifa na hali ya siasa kwa ujumla mjini Dar es Salaam. Nyerere aliwahakikishia waskilizaji wake kuwa kulikuwa na uwezekano mkubwa sana kuwa Tanganyika itakuwa huru katika uhai wao.''

No comments: