Kumbukumbu:
Sheikh Yahya Hussein
Na
Alhaj Abdallah Tambaza
![]() |
Sheikh Yahya Hussein |
MWEZI kama huu miaka minne iliyopita, Rais Jakaya Kikwete ilibidi
akatishe ziara nchini Botswana na kurudi nyumbani kuongoza maelfu ya waombolezaji
jijini Dar es Salaam katika mazishi ya mmoja wa watu mashuhuri kupata kutokea katika ukanda wa Afrika
Mashariki na Kati. Alikuwa bingwa wa usomaji Qur’an; bingwa wa unajimu; bingwa
wa tiba asilia; mtaalamu wa nyota (horoscope); msomi bobezi wa dini ya Kiislamu
na pia mwanasiasa nguli. Mazishi yake yalikuwa makubwa kupita kiasi, kwani
ilibidi barabara ya Morogoro kuanzia eneo la Magomeni Mikumi hadi makaburini
kwa Tambaza isipitike kuanzia saa 7:00 mpaka saa 9:00 mchana kutokana na wingi
wa watu. Rekodi yake ya mahudhurio—ukiacha ya Nyerere na Sokoine—bado haijavunjwa
mpaka wakati huu. Jeneza lilikuwa halikamatiki; lilionekana kwa mbali mithili
ya kishada kilichokuwa kikienda arijojo!
Namzungumzia Almarhum Sheikh Yahya Hussein, aliyefariki Mei 20,
2011 na kuzikwa siku iliyofuata kwenye Makaburi ya Tambaza, Upanga, Dar es
Salaam. Jina lake halisi ni Yahya Hassan, lakini alijulikana zaidi (adopted
name) kwa jina la Yahya Hussein. Hussein ni jina la pacha wa babake mzazi, Mzee
Hussein Juma ambaye ndiye aliyekuwa babake mlezi. Wazee hawa mapacha walikuja jijini Dar es Salaam, miaka mingi
nyuma, wakitokea Bagamoyo baada ya kuombwa na wazee wa ‘ki-Dar es Salaama’,
waje kufundisha watoto dini ya Kiislamu.
Hassan na Hussein Juma Karanda, waliasisi madrassa mashuhuri iliyojulikana
kama Al-Hassnain Muslim School, katika Barabara ya Msimbazi, Kariakoo, Dar es
Salaam. Neno al—Hassnain, kwa Kiarabu maana yake ni Hassan wawili au mbili.
Hivyo wao mapacha wawili walimiliki kwa pamoja madrassa hiyo. Kwa maksudi nimekielezea
kisa hiki cha wazee wale wawili—Hassan na Hussein—walivyomlea mtoto Yahya kama
walikuwa wamemzaa pamoja, kwa sababu ni jambo la kupigiwa mfano. Si watu wengi
wa kileo wanaoweza kufanya mambo ya namna hiyo. Ni utamaduni mzuri ambao
umepotea kabisa katika familia nyingi nchini mwetu. Mwandishi huyu, alilelewa
na baba yake mkubwa Bwana Yahya Saleh kwa ‘staili’ hiyohiyo aliyopitia Sheikh
Yahya, katika malezi ambayo mpaka leo yamemwachia athari ya kudumu maishani mwake. Madrassa ya al- Hassnain
inatajwa kama moja ya vituo maalumu kidini katika kipindi hicho, kwani vijana
wengi wa wakati huo wa miaka ya 1950 walipitia hapo. Ilikuwa inatoa elimu zote
mbili— ‘secular’ and Islamic — kinyume kabisa na uzushi unaoenezwa kwamba Waislamu
hawashughulishwi—wanapuuza— na elimu dunia. Madrassa nyingine zilizokuwa
zikifuata mitaala ya namna hiyo hapa jijini ni, Habib Punja Ilala, Al-Jamiatul
Islammia (sasa Lumumba Primary School) na Maalim Mzinga & Sons Muslim
School ya Kariakoo, ambako mwandishi huyu alipata elimu yake ya awali.
Nilimfahamu Sheikh Yahya Hussein miaka zaidi ya hamsini iliyopita
nikiwa kijana mdogo nasoma madrassani kwa Maalim Mzinga jijini Dar es Salaam.
Wakati huo yeye akiwa mwalimu kwenye madrassa ya kwao ya Al-hassnain Muslim
School. Sheikh Yahya alikuwa rafiki wa mwalimu Abubakar Mzinga, pale chuoni
kwetu. Hivyo kila mara alikuwa akifika kufanya naye mazungumzo na kushauriana
kuhusu masuala mbalimbali ya dini, hasa kuhusu ile fani yake kuu ya usomaji
Qurani Tukufu kwa njia ya tajwiid. Maalim Mzinga naye alikuwa msomaji wa sifa. Nyumbani
kwao Sheikh Yahya, ni mtaa wa Mafia kona na Nyamwezi, eneo la Kariakoo. Mkabala
na nyumba hiyo alikuwa akiishi shangazi yangu. Hivyo niliweza kuwafahamu wengi
wa wanafamilia ya Sheikh Yahya. Dada zake Sophia, Husna na Zawadi tulikuwa
tukisoma darasa moja pale Shule ya Msingi Mnazi Mmoja kwenye miaka ya 60. Mmoja
wa wadogo zake wa kiume, Salum Hussein “Madegwa,” mchezo wetu ulikuwa mmoja
udogoni jina hili alilipata katika
uhodari wake wa kusakata kabumbu kwa hiyo akapewa jina la mcheza mpira mahiri
wa Kenya Livingstone Madegwa ambae alikuwa akichezea timu ya Kenya kwenye Kombe
la Gossage.
Marehemu Sheikh Yahya, alipata elimu yake ya ‘Kizungu’ katika
Shule ya Kitchwele Boy’s Middle School (sasa Shule ya Uhuru) jijini Dar es
Salaam, kwa wakati huo ikisomesha watu mpaka darasa la kumi tu. Sheikh Yahya
alikuwa hodari mno kwenye Hesabu na Kiingereza. Mtu hawezi kuamini ujuzi wa
Sheikh Yahya katika kuzungumza Kiingereza hadi amsikie kwa sikio lake mwenyewe.
Habari zinasema kwamba, akiwa shuleni, Sheikh Yahya alikipenda sana ‘Kimombo’
kiasi kwamba alikuja kumkosoa hata mwalimu wake Mwingereza, Mr. Monday, wakati
huo wa ukoloni— kwa madai kwamba alikuwa hawafundishi Kiingereza ipasavyo. Kitendo
kile kilichukuliwa kama utovu wa adabu wa mwanafunzi kwa mwalimu wake. Kijana
Yahya alifukuzwa shule, katika uamuzi ambao haukushangaza sana kwani wakoloni –
kwa hulka yao—hawajapigiwa walikuwa wanacheza; sikwambii ukiwapigia. Baada ya
kukaa nyumbani kwa zaidi ya miezi sita, babake, ambaye alikuwa akiheshimika sana,
alikwenda kumwombea ili alirudishwe apate nafasi ya kujiunga na masomo ya juu
Tabora School. Yahya, pamoja na kwamba alikuwa hayupo darasani kwa zaidi ya
miezi sita, bado aliweza kupata alama za juu kabisa kuliko wale wanafunzi
wenzake ambao walikuwa shule wakati wote. Habari zinasema, mwalimu mmoja Mzungu
hakuyakubali matokeo yale. Alimpa mtihani mwengine wa peke yake na yeye
mwenyewe akakaa hapo hapo akimwangalia. Mambo yakawa ni yale yale! Alipata tena
alama za juu kama mwanzo.
Kwa namna ambayo haikuelezwa vizuri mpaka leo, jina lake likakatwa
katika orodha ya waliofaulu kwenda Tabora School, wakimtuhumu kwamba pengine
alikuwa akitumia ‘tunguri.’ Ukoo huu ulitoa watoto hodari sana katika masomo.
Kulikuwa na Mansur Hussein ambae huyu hivi sasa ni Prof. wa Hisabati anasomesha
Nigeria. Alikuwapo Muhidin sasa ni marehemu ambae alikwenda hadi Makerere na
aliporudi Tanganyika alijiunga na Jeshi la Polisi.
Safari ya Sheikh Yahya kusaka elimu ilihamia Zanzibar. Kule
alikwenda kujiunga na Zanzibar Muslim Accademy iliyokuwa ikiongozwa na Mudir (Principal)
kutoka chuo cha Al-azhar Sharif cha Misri, Sheikh Mohammed Addahani. Yahya
hakupata nafasi, kwa sababu kwa mujibu wa mudir wa chuo, hakufikia vigezo vilivyohitajika
kujiunga chuoni pale.
Akisimulia kisa hicho, Sheikh Ahmed Haidar Mwinyimvua, Imam Mkuu
wa Masjid Mwinyikheri, Kisutu Dar es Salaam, aliyekuwa mwanafunzi chuoni pale
anasema:
“… Yahya aliondoka zake, lakini siku chache baadaye Mudir Addahani
aliisikia Quran Tukufu ikisomwa katika Sauti ya Unguja na mtu ambaye hakupatapo
kumsikia kabla; alitaka kujua alikuwa nani yule aliyesoma Qurani kwenye Sauti
ya Unguja. Akajibiwa,“Ah! …ni yule kijana Yahya ambaye ulimkataa kujiunga na Academy
yako, ‘’Alijiuma vidole, akasema yalikuwa ni makosa, atafutwe haraka aje
kujiunga na chuo mara moja,’’ anasema Sheikh Haidar.
Pamoja na
Sheikh Ahmed Haidar, wanazuoni wengine mashuhuri hapa nchini, ambao alikutana
nao pale Muslim Academy Zanzibar, ni Sheikh Harith bin Khelef (aliyekuja kuwa
Mufti na Kadhi Mkuu Zanzibar), Sheikh Mohammed Ali Gongabure, aliyetoka Mbwera,
Kusini mwa Tanzania na Khamis Said Khalfan wa Madrassa ya Mtoni jijini Dar es
Salaam. Hapa pia, mwanafunzi Yahya alikumbana na msukosuko mwengine; maana
alikuja kumkosoa Mudir Addahani, kwamba alikuwa akiwapendelea wanafunzi fulani
fulani katika utoaji wake wa maksi. Alifukuzwa chuo kwa utovu wa nidhamu.
Aliondoka na kwenda nchi za Uarabuni alikoasisi taasisi iliyojulikana kama
World Muslim Congress na baadaye kuwa Katibu Mkuu wa East African Muslim Welfare
Society (EAMWS) makao makuu nchini Kenya.
“Iliandaliwa hafla kubwa katika Continental Hotel mjini Cairo,
ambapo mbele ya maqarii (wasomaji) wakubwa kama Mustapha Ismail, Abdulbasit
Abdulsamad, Mahmud na nduguye Mohammed Alminshawi na Mufti wa al-Azhar… Yahya
alisoma Qurani ya hali juu (classical and mesmerizing) iliyosikika live redioni
Misri. “Lilikuwa ni tukio la aina yake, mimi pamoja na Watanzania wengine
tuliokuwa wanafunzi pale Cairo na wale wa ubalozini tulikuwapo ukumbini
tukimsindikiza ndugu yetu,” anasimulia Sheikh Haidar.
Safari ya
Sheikh Yahya haikuishia hapo. Alitembelea nchini Malaysia na kusoma Qurani
iliyomfanya kiongozi wa nchi hiyo siku hizo, Tunku Abdulrahman, amwalike Ikulu kula
naye chakula, ambako pia alimsomea ‘tajwiid’ kwa mara nyengine. Mjini Amman, Jordan alikaribishwa na Mfalme
Hussein, ambaye pia alipumbazika na sauti nyororo yenye mvuto na kuliwaza
aliyobarikiwa nayo hayati Sheikh Yahya. Msomaji zingatia kwamba halikuwa jambo
rahisi kwa mtu mweusi wa wakati huo, kusoma kwa kiwango cha Sheikh Yahya, tena elimu
yote hiyo akiwa ameipata nchini mwake.
Katika fani ya
tajwiid, Sheikh Yahya alibobea zaidi katika ‘ihkami, njia na mahadhi’; akiwa
mzuri zaidi katika mahadhi ya bayati, sika na razdi (usomaji wa Qurani una
namna namna, kama vile za waimbaji zilivyo na base, tenor, na aina ya mitindo
kama tango, rhumba, blues nk). Kuna majina mengine alikuwa ameyabuni mwenyewe
kama vile, ‘sika ya Bagamoyo’ ambayo imethibitika kwamba inapatikana Tanzania
tu:
“Ah! …hiyo ‘razdi gogo’…
hiyo ni ‘bayati mama’ ...ehe! …ehe! …hapo hebu rudia tena hapo kidooogo!” kila
mara alisikika Sheikh Yahya akisema wakati mtu mwengine akisoma Qurani na yeye
ni msikilizaji.
Katika safari
yake ya Uarabuni, Sheikh Yahya aliweza kupata fedha nyingi sana kwa maendeleo
ya dini ya Kiislamu pamoja na “scholarships” zizisokuwa na idadi alizowapatia
vijana wengine kwenda kusoma huko. Ukiacha
umaarufu wake katika kusoma Qurani, Sheikh pia katika kipindi fulani kabla ya uhuru
alijishughulisha na siasa.
Babake mkuu,
Sheikh Hussein Juma alikuwa kiongozi wa chama cha siasa cha UTP (United
Tanganyika Party) kama Makamu Mwenyekiti na yeye Yahya alijiunga na AMNUT (All
Muslim National Union of Tanganyika). Ingawa havikuwa vikikubaliana na TANU katika
masuala fulani, lakini madhumuni ya vyama hivyo yalikuwa ni yaleyale kama ya
TANU—kupigania uhuru. Sasa sijui ni kwa nini inasemwa uhuru uliletwa na TANU na
Nyerere tu? Chama cha TANU kilishinda uchaguzi tu kwenye ‘ballot box’ 1961 na
hivyo kuunda serikali; lakini kama ni mapambano dhidi ya mkoloni walifanya watu
wengi akiwamo Sheikh Yahya.
Wakati mmoja,
alipokuwa jukwaani akihutubia mkutano wa kisiasa kabla ya uhuru, Sheikh Yahya
aliwahi kumdhihaki (ridiculed) Nyerere na wenzake katika TANU, kama wapiga
makelele mfano wa wanamuziki wasiojua walitakalo! Mwanasiasa mwingine
machachari wakati huo alikuwa ni Zuberi Mtemvu wa African National Congress
(maarufu Congress). Katika uchaguzi kuelekea uhuru, Congress ya Mtemvu ilikuwa ya
pili baada ya Nyerere. Mikoa kama vile Bukoba, Tabora Congress iliibwaga TANU.
Yahya Hussein
alikuwa Mwafrika wa kwanza katika nchi za Afrika Mashariki kutoa Horoscope –
tafsiri ya nyota – kwenye magazeti ya Kiingereza na Kiswahili. Kabla ya hapo
kurasa hizo zilikuwa zikitoka kwenye magazeti ya London. Alikuwa mtu wa kwanza
kuwa na gari (saloon) lenye milango sita Tanzania. Alikuwa pia mtu wa kwanza
nchini kuwa na Mobile Van lenye TV screen ambalo alilitumia kwenye maonyesho au
nje ya nyumba yake pale Mwembechai na kuwapatia uhondo wa bure watu— hasa
watoto.
Mnamo miaka ya
mwanzo ya Mapinduzi ya Zanzibar, Sheikh Yahya alitembelea visiwani Zanzibar.
Akiwa huko alitiwa mbaroni na serikali ya Mzee Karume (hayati) kwa madai kwamba
alikuwa akionekana akizungumza na watu wenye asili ya Kiarabu. Akiwa gerezani
kule Zanzibar, Sheikh Yahya alikutana na mfungwa mwengine Mwarabu aliyetokea
nchi ya Bahrain. Habari zinasema, ilikuwa ni Mwarabu huyo aliyempa elimu ya
utabiri kufuatana na mwenendo wa nyota pamoja na uwezo wa kuzungumza na kupata
habari za majini.
“Mwarabu yule
alikuja kutoweka gerezani bila kuonekana na mtu mpaka leo kimazingaumbwe”
anasimulia Maalim Hassan Yahya, mtoto wa hayati Sheikh Yahya kwenye kipindi cha
Channel Ten on Monday kilichorushwa hewani Mei 30, 2011 siku chache baada ya
kifo cha baba yake. Mwaka 1965, Sheikh alihamishiwa Gereza la Ukonga Dar es
Salaam alikokaa kwa muda na baadaye aliachiwa huru na kuja mjini kujikita
katika fani hii mpya ya unajimu.
John Bwire,
Mhariri Mwandamizi wa Magazeti ya Raia Mwema, anasema hakuwa akimfahamu Sheikh
Yahya kabla ya kuanza kusoma magazeti ya Baraza na Taifa Leo kutoka Kenya:
“…nilikuwa mpenzi sana wa gazeti la Baraza la Kenya kwenye miaka
ya 60 na 70 na humo ndio nikawa nakutana na utabiri wa nyota za Sheikh Yahya…
hakuwa mtu wa Tanzania peke yake yule… ni hasara kwa ukanda mzima wa Maziwa
Makuu,”amesema Bwire.
Katika utabiri, alianzia kwenye kutabiri mpira
kabla ya kutoa utabiri wa nyota magazetini, wakati huo ambapo hakukuwa na mtu
mwengine aliyeijua fani hiyo hapa nchini.
Kwa mara ya kwanza, tulimshuhudia Sheikh Yahya akitabiri mpira katika mashindano makubwa ya Sunlight Cup (baadaye Taifa Cup) yaliyokuwa yakishindanisha timu za mikoa yote ya Tanzania Bara. Vipeperushi vyake alivyokuwa akivitawanya kabla ya mchezo pale uwanja wa Karume, si tu kwamba vilionyesha ni timu gani itaibuka mshindi, bali pia nambari za wachezaji na dakika mabao yatakapofungwa. Nakumbuka mwaka mmoja kwenye miaka ya 1960s, mashindano ya Gossage (sasa Challenge Cup) kwa nchi za Afrika Mashariki, yalifanyika jijini Dar es Salaam. Sheikh alikuwa akitoa utabiri wa michezo ile kadri ilivyokuwa inaendelea.
Siku moja
kulikuwa na mchezo baina ya Kenya na Uganda na hapo aliitabiria timu ya Kenya
kuibuka mshindi akitaja pia dakika na idadi ya mabao yatakayopatikana. Alibashiri
pia wachezaji wa Kenya Joe Kadenge, Chege Ouma, Livingstone Madegwa na John
Ambani ndio watakaong’ara mchezoni. Watu wa Kenya, wakiwamo viongozi wa nchi
ile, walianza kumfuatilia kwa karibu; hasa pale alipotabiri Kenya ndiyo
watakaochukua kombe mwisho wa mashindano. Utabiri ulipotimia; aliletewa mwaliko
maalumu na Serikali ya Kenya kwenda Nairobi kwenye sherehe za ushindi. Huo
ukawa ndio mwanzo wa Sheikh Yahya kufungua ofisi katika jiji la Nairobi, wateja
wake wakubwa wakiwa wanasiasa na viongozi mashuhuri nchini Kenya. Kadri siku
zilivyoenda, Sheikh alipanuka na akawa na ofisi kubwa pale Government Road,
Nairobi na akanunua jumba la kifahari maeneo ya Kileleshwa, nje kidogo (suburb)
ya Nairobi. Kileleshwa ni kama vile
Beverly Hills, Laguna Beach ama Bel Air kule Los Angeles, California, ambako
huishi watu maarufu na wenye uwezo mkubwa. Kamwe huwezi kupafananisha na Masaki,
sijui Mbezi Beach ama Oysterbay ya hapa kwetu.
Abdallah Mohamed na Mohamed Said, Nairobi 1972 |
Siku moja,
katika miaka ya 1970s, nikiwa mfanyakazi pale Nairobi kwenye Jumuiya ya Afrika
Mashariki ya zamani, kulifanyika maonyesho makubwa ya All Africa Trade Fair
katika viwanja vya Ngong. Maonyesho hayo,
kidogo yanafanana na maonyesho ya Sabasaba hapa kwetu. Rafiki yangu, Alhaj Mohamed
Said (mwanahistoria maarufu nchini) na mimi, tulitembelea maonyesho yale na
tukafika hadi kwenye banda la Sheikh Yahya.Tulimkuta Sheikh akitoa maelezo
namna anavyotabiria watu kuhusu maisha yao kufuatana na michoro ilivyo kwenye
viganja vyao vya mikono. Ghafla akapaza sauti kuniita mimi nipande pale
jukwaani, “… ehe! Njoo hapa we Mswahili, njoo…” Niliingiwa na woga sana,
nikajifanya sikusikia, maana sikujua nini anataka kunifanya mnajimu yule.
Alipong’ang’ania sana ikabidi niende. Alichukua mkono wangu akaunyanyua juu na
kuanza kuelezea nini maana ya ile michoro iliyo kiganjani mwangu. “….Hii
inaonyesha wewe eh! utasafiri nchi za mbali na kufika katika makontinenti mengi
duniani na utazuru sehemu takatifu…haya nenda zako,”alisema.
![]() |
Abdallah Tambaza Akiwa Mwanafunzi Chuo Kikuu Cha California, Los Angeles Marekani |
Niliondoka
zangu na kuyaacha nyuma ‘matabiri’ yale ya Sheikh Yahya. Wakati huo sikuwa
najua nchi au mji wowote zaidi ya Nairobi na Dar es Salaam kwetu nilikozaliwa. Miji
kama vile Tanga na Morogoro kwangu ilikuwa ni miji ya mbali tu. Lakini miaka
kadhaa baadaye, nilikuja kugundua tayari nimeshatembelea sehemu nyingi duniani
na hivyo kujiuliza, ‘ala kumbe utabiri ule umetimia!’ Kwa schorlaship kutoka
ICAO, yaani Shirika la Umoja wa Mataifa la Usafiri wa Anga, mwaka 1984
nilipelekwa katika Chuo cha Usalama wa Anga (L’ENAC) kule Toulouse, Ufaransa.
Nilipokuwa huko, nilipata fursa iliyoniwezesha kufika kwenye kituo kikubwa cha
setelilaiti duniani kilichojulika kama SARSAT- CORPAS (Search and Rescue
Satelite).
Nilipanda pia
ule mnara wa kihistoria jijini Paris, unaoitwa ‘le Tourefel’ na pia kuyashuhudia
maonyesho makubwa ya ‘madege’ duniani ya Le Burget Air Show. Kama hiyo
haitoshi, mwaka 1988 mwandishi alipata nafasi ya kujiunga na Chuo Kikuu cha
California pale Los Angeles, na hivyo kufika sehemu nyingi maarufu kule
California ikiwamo Hollywood, Beverly Hills, Las Vegas pamoja na Disney Land. Nilikuwapo
pia pale Rose Bowl Stadium, Pasedina kushuhudia fainali za kihistoria za Kombe
la Dunia baina ya Brazil na Italy na kumwona Robberto Baggio akipaisha juu
penati. Nilitembelea pia nchi za Mexico,
Belgium Uingereza, Spain, Sweden na Germany.
Lakini utabiri wa Sheikh Yahya sikuanza kuuhisi, hadi pale nilipojiona nimesimama viwanja vya Arafat pale Mecca kwa Ibada ya Hijja. Sikuamini macho yangu kwamba na mimi ni miongoni mwa umati ule uliokuwapo pale, mahali ambapo baba yetu Adam ndipo alipoungana tena na mama Hawa tukazaliwa sisi binadamu.
Sheikh Yahya hakuwa mnajimu wa Afrika Mashariki peke yake. Alikuwa na ofisi London, Lusaka na kule Mbabane Swaziland, ambako mmoja wa wateja wake alikuwa ni Mfalme Sobhuza aliyekuja kumpa uraia wa heshima wa nchi hiyo mnamo mwaka 1990. Hii inaelezwa na Hassan Yahya Hussein aliyekuwa kaambatana na babake nchini humo kikazi. Katika kuishi kwake Kenya, Sheikh Yahya aliishi kifahari sana hata ikasababisha baadhi ya wabunge wa nchi ile kumwonea ngowa. Walianzisha mjadala bungeni wa kutaka Sheikh Yahya afukuzwe nchini kwao:

Lakini utabiri wa Sheikh Yahya sikuanza kuuhisi, hadi pale nilipojiona nimesimama viwanja vya Arafat pale Mecca kwa Ibada ya Hijja. Sikuamini macho yangu kwamba na mimi ni miongoni mwa umati ule uliokuwapo pale, mahali ambapo baba yetu Adam ndipo alipoungana tena na mama Hawa tukazaliwa sisi binadamu.
![]() |
Abdallah Tambaza Akiwa Rose Bowl Stadium, Pasedina Akisubiri Kuingia Kushushudia Fainali za World Cup 1994 |
Sheikh Yahya hakuwa mnajimu wa Afrika Mashariki peke yake. Alikuwa na ofisi London, Lusaka na kule Mbabane Swaziland, ambako mmoja wa wateja wake alikuwa ni Mfalme Sobhuza aliyekuja kumpa uraia wa heshima wa nchi hiyo mnamo mwaka 1990. Hii inaelezwa na Hassan Yahya Hussein aliyekuwa kaambatana na babake nchini humo kikazi. Katika kuishi kwake Kenya, Sheikh Yahya aliishi kifahari sana hata ikasababisha baadhi ya wabunge wa nchi ile kumwonea ngowa. Walianzisha mjadala bungeni wa kutaka Sheikh Yahya afukuzwe nchini kwao:
“…Hii mutu kutoka pande ya Tandhania anatengeneza pesa mingi sana
na kunyonya watu ya Kenya si akwende kwao…” walisikika wabunge wa Kenya
wakilalamika.
![]() |
Hii ni Kileleshwa Nairobi Alikokuwa Akiishi Sheikh Yahya Hussein |
Sheikh Yahya
yalimfika hayo kutokana na maisha ya anasa aliyokuwa akiishi, ikiwamo kuendesha
magari mapya mapya ya kifahari na namna alivyokuwa akiweka mwilini mwake
‘designer suits’ (Pierre Cardin, Yves Saint Laurent, na mguuni akiwa na kiatu cha Kitaliano Bruno
Magli) zilizokuwa zikimkaa kwelikweli. Sheikh Yahya alikuwa mtu mkarimu na
mwenye huruma pia. Kila asubuhi pale nyumbani kwake Magomeni, alikuwa akikutana
na kuwasaidia watu wasiojiweza misaada mbalimbali ya kujikimu kimaisha. Daima
dumu, wakati akiwa jijini Dar es Salaam, Sheikh Yahya alikuwa akifika katika
hoteli maarufu ya Shibam pale Magomeni au Seiyun Hotel iliyoko Kariakoo, ili
kusalimiana na watu. Akiwa hapo mara zote huwa analipia watu wote vyakula
walivyokula, “…eh! eh! Waache wende zao, wache wende tu… tutalipa, tutalipa
sisi, hapana’ shaka,” Sheikh alikuwa akisema, kumwambia mwenye hoteli.
Hivyo, wakati
huu ambapo tunakumbuka na kuenzi maisha na nyakati za mtu huyu mashuhuri ambaye
ametangulia mbele za haki na kutuachia haiba nyingi sana, nashindwa kuelewa
ilikuwaje kiongozi wa serikali akatoa amri na tingatinga watu wakalivunjevuje
kaburi lake ati kazikwa eneo la ‘serikali’— ni ujahili na majahili tu wanaoweza
kufanya ushenzi ule!
Tuseme tu: Allahuma
ghufirlahu; waarhamu; wamaskanahu filjannah! Eh! Molla, msamehe madhambi yake;
umrehemu na peponi iwe ndio maskani yake—Ameen.
No comments:
Post a Comment