Wednesday, 4 May 2016

HISTORIA YA UHURU WA ZANZIBAR MUINGEREZA AONDOKE KWA AMANI AU KWA SILAHA - SALIM MSOMA


Sheikh Ibrahim,
Pamoja na kwamba hukumtaja aliekuletea maelezo ya hapo juu napenda kukuhakikishia kuwa mimi kama mtafiti wa historia ya karibuni (recent past) ya siasa za Zbar, nilifanikiwa kuwasaili Wazanzibari wawili ambao bado wahai na ambao walikuwemo kwenye kikundi kilichopelekwa Misri na ZNP mwaka 1960.
Wamenieleza kuwa mpango wa kumuondoa mfalme ulikuwa moja ya dhamira ya mafunzo yao chaguo lilikuwa aidha aondoke kwa amani kwa mazungumzo (abdication) au kwa mapambano. Jambo la kutiliwa maanani hapa ni mkutano wa Kuta la Tembo ambao ulihutubiwa na Al-Marhum Ahmed Seif Kharusi (Kishkiro).Yeye alitumwa na viongozi wenzake wa Hizbu kukutana na waliorejea kutoka Misri na kuwapa taarifa kuwa "ule mpango wa kuuondoa ufalme umebatilishwa."
Unajuwa ndugu yangu Sheikh Ibrahim baadhi ya walioshiriki mafunzo hayo wamejikuta mwishoni wakikimbilia nchini Oman na kupata ukimbizi na hatimae uraia huko.Sasa kisaikolojia wanapata taabu ndani ya nafsi na nyoyo zao kujikuta wamepokewa na kusitiriwa na ukoo uleule ambao wao waliwahi kuuchukia na kudhamiria kuutokomeza!
Kwa hiyo sishangai wanapokataa au kukana kuwepo kwa mpango kama ule miaka ile. Na hisia kama hizo zanawajia watu wengi kwenye mazingira tafauti ya kisiasa.Ni hisia za kujuta na kusikitika pale unapobaini kuwa wale uliokusudia kuwatendea vibaya kumbe ndio watakaokuokoa maishani baadae! ALLAHU AKBAR! Nakumbuka hadithi alotupa Al-Marhum Sheikh Aboud Maalim jinsi alivyopokelewa alipokwenda Uarabuni baada ya Mapinduzi 1964 kwa mara ya kwanza akiwa Waziri.
Alikutana na Mzanzibari ambae Sheikh Aboud alikumbuka alimfanyia mabaya wakati wa ukhasama wa kisiasa huko nyuma.Yule Mzanzibari alionyesha ukarimu na bashasha kubwa kwa Sheikh Aboud hadi ikamsababisha atokwe na machozi.Alilia kwasabu alikuta yule aliemtendea uovu ndie aliempokea na akajisikia yuko nyumbani.Ninachotaka kusema ni kwamba sisi wasomi watafiti tuendelee na utafiti. 
Nduguyo Salim.

 
Maandamano: Maalim Aboud Jumbe, Maalim Aboud Maalim na Abdulrahman Babu


No comments: