| Kushoto: John Limo, Mbwana Abushiri, Hemed Seif na Saleh Zimbwe wote wachezaji wa timu ya taifa kutoka Tanga African Sports na Coastal Union |
Katika miaka ya mwisho wa 70 na miaka ya 80 nilikuwa Mlezi
(Patron) wa African Sports Club, Tanga. Nikiwa kiongozi nilijitahidi sana
kuijenga timu ya mpira ya Sports na tulipata matokeo mazuri na ya kujivunia.
Wanakimanomano waliogopwa na timu maarufu kama Yanga na Simba, mbali na watani
wetu -Coastal Union. Ukweli ni kwamba timu za Sports na Coastal Union si tu
ziliunda kikosi kikubwa cha timu ya Taifa Stars kwa miaka mingi, lakini pia
zilichangamsha jiji la Tanga na kuvutia vijana wengi chipukizi na mahiri wa
kucheza mpira wa miguu kutoka pande zote za Tanzania. Hivyo ni
jambo la kusikitisha sana hii leo kuona timu tatu za mpira toka Tanga
zikishushwa daraja kwa mpigo. Msemo wa miaka ya karibuni, 'Tanga kunani' ni
muhimu katika kuchunguza hali inayojitokeza katika fani ya mpira wa miguu kwetu
Tanga.
| Wachezaji wa mpira wa zamani wa Tanga pamoja na viongozi wa mpira. Katika picha yuko Hemed Seif, Ahmed Kea, Belesi Kakere, Omar Zimbwe Mohamed Majura, Yahya Dondo na wengine wengi |
Hivi karibuni niliandika makala katika gazeti la Guardian
nikilalama kuhusu kufifia kwa jiji la Tanga. Hakika ufikapo mjini Tanga huwezi
kutoshikwa na huzuni kwanini Taifa letu au niseme Serikali yetu iuachie mji huu
wa kihistoria ufikie hatua ya vijana kuukimbia. Upole wa
wenyeji na ushwari wa Tanga hautoshelezi kimaendeleo. Sishangazwi na hata
kuzuka hivi karibuni kwa umjahidina na hata ugaidi katika maeneo ya Jiji la
Tanga. Ni matokeo ya vijana kukosa mwelekeo katika mazingira magumu ya ukosefu
wa ajira. Katika miaka ya mwishoni mwa 60 na miaka yote ya 70 hadi katikati ya
miaka ya 80 Tanga ilikuwa ni eneo lenye makampuni mengi ya Umma na binafsi,
tena maarufu nchini. Na Bandari ya Tanga pamoja na reli vilichangia kutoa ajir
anyingi kwa vijana .
Timu za
mpira za African Sports, Coastal Union na Bandari ziliweza kuwa na wachezaji
mpira wa miguu wenye ajira katika makampuni haya. Na hawa vijana walipewa
nafasi ya kuimarisha na kukuza vipaji vyao kupitia misaada mingi kutoka kwenye
makampuni na mashirika bila kujali kutokuwepo kazini mara kwa mara. Ilikuwa nia aina kubwa ya 'corporate social responsibility'
kwa vyombo hivi.Leo Tanga
haina tena mashirika ya umma. Makampuni binafi ya nguo na mafuta ya kupikia
yamefunga kutokana na kipindi kigumu kilichopitiwa baada ya Serikali kufungua
milango kiholela ya bidhaa kutoka nje kati ya mwaka 1986 na 1995. Ubinafsishaji
uliyofuatia haukuzalia matunda yoyote kwa Tanga. Kiwanda cha Sementi
alhamdullillahi ni mkombozi kikifuatiwa na Tanga Fresh cha Maziwa na Pembe
kinachotengeneza unga. Hamisi Kindoroko naye kasaidia kujenga hoteli ya kisasa
-Tanga Beach Resort. Athi River Mining wanakamilisha kiwanda kipya cha sementi.
Labda Tanga itaibuka tena katika miaka mitano ijayo ukifikiria pia bomba la
mafuta toka Uganda kuishia Tanga bandarini. Tusubiri kuibuka tena kwa African
Sports na Coastal Union ambazo ni timu za watu. Mgambo ni timu ya Jeshi.
Nashangaa kushuka kwake daraja!
Lakini
kwa miaka mingi Tanga imekuwa ni kama mtoto yatima katika mageuzi ya uchumi.
Uyatima huu pia umekumba fani ya mpira wa miguu. Mnauliza, 'Tanga kunani'? Jibu
mnalo. Si jibu kutoka kwa wana Tanga peke yao. Taifa zima na Serikali wanalo
jibu. Kamahatua madhubuti hazitachukuliwa kwa haraka, basi Mwenyezi Mungu
atunusuru na janga ninalohisi linajengeka taratibu na mbalo sote tunaweza
tukalijutia.
| Kushoto: Salim Kajembe (African Sports) na Hemed Seif (Coastal Union) Wote walicheza timu ya taifa. Wote ni marehemu. |
No comments:
Post a Comment