Sunday, 22 May 2016

“MAMBO YA ZANZIBAR HAYANIHUSU” SAID IBRAHIM


Mwanzoni mwa miaka ya 1970, mgogoro wa Burundi ulipopamba moto na wakimbizi kutoka nchi hiyo wakitapakanyika kukimbilia nchi zinazoizunguka hiyo, Tanzania ndiyo ilikuwa nchi lengwa ya kwanza na wakimbizi hao.

Kwa historia ya nchi zote za Maziwa Makuu wakati huo - Kongo, Burundi, Rwanda na Uganda, zote zilikuwa katika hali ya sintofahamu. Kongo ilikuwa katika mzozo wa miaka mingi na sehemu kubwa ya nchi hiyo ikitawaliwa na waasi. Rwanda nako, chuki baina ya Wahutu wachache na Watutsi wengi, hakukuwa na utengamano. Uganda ndiyo ilikuwa ipo chini ya utawala wa nduli Idd Amin Dada baada ya kumpindua Rais Milton Obote mwa 1971.

Nchini Burundi, watu wa makabila ya Watwa, Wahutu na Watutsi, waliishi pamoja kwa amani kwa miaka ipatayo 500 hivi, ambamo kwa miaka 200, nchi hiyo ilikuwa ya ki-falme. Baada ya  kuingizwa kwa fitna za wakoloni wa Kijerumani za “wagawe ili uwatawale” mwanzoni mwa karne ya 20, Burundi ilitwaliwa na Ujerumani na kuingizwa na kuwa sehemu ya Tangayika. Baada ya Ujerumani kushindwa katika Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, Burundi pamoja na Ruanda zilitwaliwa na Ubelgiji na kuwa nchi moja ya Ruanda-Urundi.

Wakati machafuko yalipopamba moto nchini Burundi mwaka 1972, wakimbizi waliokuwa wakiingia Tanzania, miongoni mwao wakitiririka damu kutokana na majeraha ya risasi na mateso waliofanyiwa na majeshi na wapinzani wa nchi yao, Rais wetu wa wakati ule, Mwalim Julius Kambarage Nyerere aliamua kuufunga mpaka wa Tanzania na Burundi ili wakimbizi hao wasiingie. Baada ya kelele nyingi kutoka jumuiya za kimataifa ikiwemo Umoja wa Mataifa na wafadhili wetu, Mwalim alisema kwamba “MAMBO YANAYOENDELEA NCHINI BURUNDI HAYAIHUSU TANZANIA”. Aliposutwa na jumuiya hizo na kuulizwa kwamba” itakuwaje mambo hayo hayaihusu nchi yako wakati kuna damu inatiririka kuvuka mpaka wa nchi hizo mbili”, ndipo hatimaye Mwalim aliufungua mpaka wa Tanzania na Burundi, hivyo basi kuwa mwanzo wa wakimbizi wengi kutoka nchi hizo kukimbilia Tanzania; na mpaka hivi sasa, baadhi yao wamepewa uraia wa nchi yetu.

Nimeanza na utangulizi huo baada ya kutafakari kauli ya Mh. Bwana John Pombe Magufuli aliyoitoa wakati akihutubia Watanzania kupitia “Wazee wa Dar es Salaam (CCM)” mwezi Januari mwaka huu ambapo alitoa kauli kwamba hawezi kuingilia mambo ya Zanzibar kwa sababu HAYAMUHUSU KWA KUWA TUME ZA UCHAGUZI ZA VISIWANI NA BARA ZIKO HURU!!! (????) Ni kauli ya ajabu kupata kutolewa na kiongozi wa nchi ambaye watu wa Zanzibar, si tu kwamba walimpigia kura katika Uchafuzi Mkuu wa Ocktoba 25, 2015 lakini pia kodi zao – hata ziwe kidogo namna gani – zinachangia kuendesha serikali ya Muungano. Kana kwamba hiyo haitoshi, vijana wao waliopo katika vikosi vya ulinzi na usalama wanawajibika kwake yeye Bw. Magufuli. Endapo vijana hao wanavunja sheria na haki za binaadamu tena mchana kweupe – kwa kuwapiga, kuwatesa, kuwadhulumu mali zao na mengine mengi ambayo hayawezi kuandikwa na hawachukuliwa hatua yeyote na wawakilishi wa Rais wa Muungano wetu huu waliopo visiwani, ni nani wa kuulizwa?

Hivi, kama watawala wa Zanzibar hivi sasa wangeamua kujitoa katika muungano - na wana haki hiyo kama alivyopata kusema mzee wangu Hayati Abeid Amani Karume huko nyuma kwamba “ukihisi koti linakubana, si unalivua tu”, - Bw. Magufuli angeutangazia umma wa Watanzania na dunia nzima kwamba mambo yanayoendelea Zanzibar “hayanihusu?”

Historia inatukumbusha kwamba hakuna dola yeyote hapa duniani – kuanzia ile ya Firauni, Hitler, Mussolin, serikali za kikatili za Chile, China ya kabla ya Mao, Misri, Zaire ya Mobutu, Jamhuri ya Afrika ya Kati ya Bokassa na hata majirani zetu Uganda  ya Idd Amin Dada, ambazo ziliwafanyia ukatili wa kutisha raia wao na zikadumu! Hawa viongozi wetu hawana budi kutambua kwamba mambo wanayowafanyia raia wa pande zote mbili za muungano yana mwisho. Na mwisho siku zote hauwi mzuri na kama ilivyo kanuni ya ubaguzi kwamba haimuachi mtu anayefanya vitendo hivyo, basi na hii ni vivyo hivyo; na kama hawatolipa wao, basi watoto, wajukuu au hata vilembwe vyao vitakuja lipa tu,  kwa dhambi hizi zinazofanywa hivi sasa na wazee wao. Ni aibu na ajabu kwa watu wanaojiita ma-alhaj, masheikh, mapadri, wachungaji, maprofesa, madaktari na kadhalika kuendesha mambo ya kinyama aina hii.

Sababu ya CCM kushindwa katika uchaguzi wa 2015 zinajulikana na kila mmoja wa viongozi na wanachama wa chama chetu. Kwa kuwa Wazanzibari – tofauti na Watanganyika - hawana tabia ya kupapasa macho na kumung’unya maneno, sababu hizo zilikuwa zikisemwa hadharani peupe na viongozi na wanachama, kwamba madhali chama kimempitisha mgombea fulani kwa ngazi ya juu ya uongozi wa muungano kwa sababu aliwanyima Wazanzibari haki ya kujiamulia mustakabali wao wenyewe kwenye mchakato wa Bunge la Katiba, basi hawatakipigia kura chama chetu! Miongoni mwa waliokipigia kura chama cha CUF ni viongozi na wanachama wa CCM ambao walisema waziwazi kwamba wamechoshwa na jinsi mambo ya kuikandamiza Zanzibar yanavyoendeshwa, huku wakubwa wao wamekaa kiiiimya tu, ili mradi wananufaika.

Badala ya kukaa chini kuzungumza jinsi ya kuweka mambo hayo sawa, mtu aliyesababisha upuuzi huu wote na ambaye katika nchi yeyote duniani inayozingatia utawala bora na wa sheria, angestahili kuswekwa ndani, ameachwa na anadiriki kuitisha “uchaguzi wa marudio”. Kauli za viongozi mbalimbali walizozitoa kukemea hatua hizo za ajabu ajabu, zote zimepuuzwa na waliomo madarakani kwa hofu ya kupoteza ulwa wao huku maelfu ya wananchi wakidhalilishwa na kunyimwa haki yao ya kidemokrasia! Ni vema basi serikali kwa kushirikiana na CCM wakapeleka muswada wa kuirudisha nchi hii kwenye utawala wa chama kimoja cha siasa katika kikao kijacho cha bunge kwani ni dhahiri kwamba CCM hakitaki demokrasi ya vyama vingi. Vituko vinavyofanya kwenye uchaguzi wa meya wa jiji la Dar es Salaam unaonesha azma hiyo. Wakati viongozi na wanachama wa vyama vya upinzani wanaamshwa usiku wa manane katika hoteli walizofikia huko Mwanza na kukatiwa mpaka tiketi za ndege kusafirishwa hadi Dar es Salaam, kuja kumkabili Pilato, jeshi letu la polisi linageuza shingo upande wa pili kuwafikisha mahakamani watu walioghushi (jina) hati ya mahakama ya kusimamisha uchaguzi wa meya wa jiji letu.

Ndugu yangu Balozi Mstaafu Bw. Hassan Kibelloh – sijui yuko wapi bwana huyu baada ya kustaafu - alikuwa na msemo wake mmoja kwamba “popote penye watu wenye akili timamu na busara, mambo huwa hayaharibiki.” Suala la hali ya Zanzibar haliwezi kuachiwa liendelee tu eti kwa kuwa ni la “kihistoria”. Ingelikuwa vizuri basi kama pia tungeacha biashara ya utumwa – ambayo hasa ilifanywa na wazungu, wakiwemo wa Ulaya na Marekani na Waafrika na Waarabu kutumika kama mawakala tu, iendelee. Historia ya visiwa vyote dunia nzima inafanana. Hakuna mtu hata mmoja ambaye anaweza kudai kwamba yeye ndiye Mzanzibari halisi! Hakuna. Kuendana na historia ya visiwa hivyo, basi Washiraz kutoka Uajemi/Persia ya enzi hizo na Waarabu kutoka Omani, wana haki zaidi ya kudai uenyeji Zanzibar na Pemba kuliko Wamanyema, Wanyamwezi, Wasukuma, Watende, Wajaluo, Wahaya, Waganda, Wanyakyusa, Wanyasa, Wamakonde, Wahyao, Wagogo, Wakwere, Wasambaaa, Wanguu na Wadigo/Wasegeju kutoka Tanganyika, Kenya na Uganda; ambao kwenda kwao huko ilikuwa ni kutokana na ama kuchukuliwa kama watumwa au wapagazi wa wafanyabiashara au wainjilisti wa Kiarabu na Kizungu. Jambo la kustaajabisha ni kule kufumbia macho na mdomo kunakofanywa na uongozi wa CCM  na serikali kwa kukaa kimya kwa kitendo cha aibu kubwa cha ubaguzi wa “machotara” na “magozigozi” kilichofanywa na makada wa CCM katika sherehe za maadhimisho ya miaka 52 ya mapinduzi ya Zanzibar. Ule ulikuwa ni uhalifu.

Kituko cha ajabu - Bw. Benjamin Mkapa - mtu mwenye damu ya wananchi wa Pemba mikononi mwake kwa kusababisha mauaji na mateso makubwa kwa Wapemba baada ya uchafuzi wa 2000 na pia kupata kusema kwamba hakuna mtu wala chama chenye haki miliki ya kuongoza nchi hii, ameteuliwa kwenda kuwa msuluhishi nchini Burundi. Mwingine naye anakwenda kuwa msuluhishi huko Algeria! Ni kwamba kama wangefanya kazi ya kutafuta suluhu huko Zanzibar wasingepata mshiko kama huo watakoupata huko nje, au vipi?

Ili kuepusha maafa ni vizuri viongozi wetu wakachukua uamuzi mgumu na wa busara kwa kutafuta suluhu huko Zanzibar na kuufutilia mbali huo uchaguzi wa marudio, vinginevyo tutabaki kulalama na kujuta kwamba KITENDO MWANA, MAJUTO  MJUKUU.


No comments: