Friday, 20 May 2016

TUWACHE MIFARAKANO NA MAREHEMU SHEIKH ALI MUHSIN BARWANI


Utangulizi


Waumini wakiwa nje ya msikiti palipofanyika mauaji

Yaliyotokea Mwanza jana katika sala ya Isha ni kitendo ambacho hakijapatapo kutokea Afrika ya Mashariki nzima. Waislam waliokuwa wakiswali sala ya Isha walivamiwa katika sijda na watu walioficha nyuso zao wakapigwa mapanga. Watu watatu wameuawa hapo hapo ndani ya msikiti. Tumepokea mikono mingi ya taazia katika ukumbi huu kuanzia jana hadi hii leo. Mmoja katika ndugu zetu katuletea taazia ya aina yake. Kafungamanisha katika mkono wake wa pole na makala hii ambayo Sheikh Ali Muhsin Barwani aliandika kama indhar kwa umma wetu huu kuhusu khatari za farka.

Nami naziweka hapa nasaa za marehemu Sheikh Ali Muhsin:

“Na mwenye kumuuwa Muumini kwa kukusudia, basi malipo yake ni Jahannamu humo atadumu, na Mwnyezi Mungu amemlaani, na amemuandalia adhabu kubwa.” 

(Annisaai: 93).

Ole wao walioingia kuwauwa ndugu zao Waislamu kwa makusudi na bila ya kosa lolote.

Watu kuzidi kuelimika na kuchanganyika kwa kila yao, wanafahamu ya kwamba kwa hakika hakuna chenye kutafautisha hivyo baina ya Sunni na Ibadhi. Ilivyo katika Usuul-l-Fiqh, Ibadhi inafundisha na kufuata zilezile zilizomo katika kitabu cha Imam Shaafii, Arrisala. Mufti wa Oman, Sheikh Ahmed bin Muhammad Al Khalili; ameeleza ya kwamba hakuna moja lenye kufuatwa na Ibadhi ambalo halifuatwi na moja kati ya madhehebu manne ya Sunni. Oman na pia Zanzibar Sunni na Ibadhi wanasali msikiti mmoja, wanaowana na wanashirikiana kwa kila lao bila ya kuhisi taabu na bila ya ubaguzi wowote ule. Unaweza kuingia msikitini na ukamfuata Imam katika Salaa na kumaliza na bila ya kujuwa ni wa Madhehebu gani. Sio sivyo ukisema ya kwamba Ibadhi sawa na Sunni, ni Ahli Sunnah, kwa sababu Hadithi za Mtume wetu mpenzi s.a.w. ndio marejeo ya pekee baada ya Qur’ani Tukufu kwa Waumini wote. Hili neno Sunni halikuwa likitumika isipokuwa mnamo karne ya saba baada ya Hijra, hivi ni muda mrefu kupita baada ya Maimamu wote wanne wa Sunni kufariki, yaani Imam Hanafi, Imam Malik, Imam Shafii na Imam Hambal. Wote hawa wakati wa uhai wao, na pia Maimamu wa Kiibadhi, Jabir bin Zayd, na Abdulla bin Ibadh, walikuwa wakijuulikana kwa jina la Imam Muslimiina (Imam wa Waislamu). Hivi hivi ndivyo hali ilivyokuwa kwa Maimam wakubwa wa Kishia, Imam Muhammad Al BaqirJaafer Assadiq, na Zayd bin Ali. Waislamu wote walikuwa wakiwaendea Maimamu wote hawa kwa uwongozi wao na kusoma kwao.

Ni hakika ya kwamba utaratibu wa mtu kujifungia katika fikra zake na upungufu wa ilimu ulisababisha kuwepo vizingiti kuzuia watu kufahamu yaliomo katika madhehebu mbalimbali, haya ndivyo yalivyokuwa Zanzibar na Oman pia. Hali hii ilikuwa zaidi sehemu za ndani sana huko Oman kuliko ilivyokuwa visiwani Zanzibar. Mwenyezi Mungu Mtukufu amjazi kheri kwa kazi yake ya faida sana alioifanya mwanazuoni maarufu wa Kiibadhi wa Algeria, Sheikh Muhammad bin Yusuf Al It’feish, kwa yale maelezo yake katika Qur’ani katika kitabu chake Sharh Nnil, kitabu cha Fiqh, kwa kazi zake adhimu hizi mengi yaliokuwa yakisababisha mfarakano baina ya madhehebu yaliweza kubainishwa hakika yake na kuondolewa. Kazi hii hivi leo inaendelezwa na Mufti wa Oman, Sheikh Ahmed bin Muhammad Al-Khalili. Khatua kubwa na ya kishujaa aliichukuwa Sultan Qaboos pale alipotowa amri yake ya kusaliwa Salaa ya Ijumaa Oman. Kwa karne, Ibadhi wa Oman na hata waliokuweko katika Afrika Mashariki walikataa kusali Salaa ya Ijumaa kwa kuwa ati ni aibu kwao. Wakifanya hivi kutekeleza fikra za baadhi ya wanazuoni wao ambao walishindwa kutambuwa maamrisho ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kama yalivyo ndani ya Qur’ani Tukufu. Hakuna Salaa iliotajwa kwa uwazi kabisa katika Qur’ani kuliko Salaa ya Ijumaa. Sura nzima imepewa jina la “Surat Al-Jum’a”:

 “Enyi mlio amini! Ikiadhiniwa Sala siku ya Ijumaa, nendeni upesi kwenye dhikri ya Mwenyezi Mungu, na wacheni biashara. Hayo ni bora kwenu, lau kama mnajua”.  
(Al-Juma’: 9)

Kwa hii amri yake Sultan Qaboos ya kuwataka Ibadhi wasali Sala ya Ijumaa iling’oa kisingizio kilichokuwa hakikuwa na msingi na kuwaweka Maabidhi sawa na ndugu zao wa madhehebi yote katika kutekeleza maamrisho ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, khasa hii Sala ya Ijumaa. Hivi leo Ibadhi hajioni kuwa ni tafauti na mwenziwe yeyote yule au haoni kuwa sivyo kusali na asiekuwa Ibadhi mwenziwe. Ibadhi hivi leo wameweza kufuta kabisa zile tuhuma ambazo hazikuwa na ukweli wowote ule kuwa ati Ibadhi inatokana na Khawaarij. Alhamdulillah, leo sio tu ya kwamba wanasali pamoja Sala ya Ijumaa bali Sala zote tano katika wiki nzima wanasali pamoja bila ya tafauti yoyote ile. Kwa upande wao, Masunni na wao wanazidi kutambuwa ya kwamba hakuna tafauti yoyote ile ya kimsingi baina ya Ibadhi na Sunni. Kwa hakika hata hizo tafauti ziliopo baina ya Sunni na Shia, sio tafuti katika mambo ya misingi ya dini. Nyingi ya tafauti hizi asili yake ni mambo ya kisiasa na taarikh ya kale, leo hayana tena pahala katika Waumini. Wenye busara miongoni mwa wanazuoni wa madhehebu mbalimbali wanasisitiza ya kwamba umefika wakati Waumini tujivue hizi pingu za mfarakano katika dini yetu zilizo sabibishwa na mambo ya kisiasa na taarikh ya kale ambayo hayana msingi wowote ule. Wanazuoni maarufu wenye busara na maarifa wameandika kukhusu juhudi za kuondoa mfarakano wa madhehebu katika Uislamu, tafadhali tusome kitabu cha Dr. Mustafa Shak’a:  Islamu Bilaa Madhaahib” (Uislamu Bila ya Madhehebu), vilevile tusome kitabu cha Dr. Moosa Al I’sawy:  “Ash-shiia wa Ttas-hih”kitabu cha Sheikh ShaltoutAl-Islam A’qidatah wa Sharia’h” (Uislamu A’qida na Sharia). Katika Qur’ani mumejaa Aya zenye kuhimiza umoja wa Waumini na kukataza mfarakano wa aina yoyote ile, khasa wa madhehebu. Ametueleza Mwenyezi Mungu Mtukufu:

  “Hakika walio igawa Dini yao na wakawa makundi makundi, huna ukhusiano nao wowote. Bila ya shaka shauri yao iko kwa Mwenyezi Mungu; kisha atawaambia yale waliokuwa wakiyatenda.”                                            
(Al-Ana’am: 159)

Kisha akatueleza Mwenyezi Mungu Mtukufu uovu wa wale wenye kuigawa dini makundi makundi na vile kuwa kila kikundi hufurahia yale yalio yao:

Muwe wenye kutubia kwake, na mcheni Yeye, na shikeni Sala, na wala msiwe katika washirikina. Katika wale ambao kwamba wameigawanya dini yao, na wakawa makundi makundi, kila kikundi kinafurahia kilicho nacho.”         
(Ar-ruum: 31-32)

Ikiwa kuna Bid’a iliyotoka nje kabisa na maarisho ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, basi ni vile kuzusha mfarakano; hata ikiwa mfarakano huo umekuja kwa kile kisingizio cha kupigana na Bid’a. Kwa hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu anatakaza mfarakano katika dini - wacha baina ya madhehebu, kama vile dini ya Kibudi, Ukiristo na Uislamu, zote hizi kwa vile asili yake ni kitu kimoja. Ametueleza Mola wetu Mlezi:

Amekuamrisheni Dini ile ile aliyo muusia Nuhu na tuliyo kufunulia wewe, na tuliyo wausia Ibrahim na Musa na Isa, kwamba shikeni Dini wala msifarikiane kwayo...” (Ash-shura: 13).

Inasikitisha kuona ya kwamba mpaka hii leo wako baadhi ya watu wenye fikra potofu ambao wanavuka mipaka katika kushindana na kugombana kwa ajili ya kuthibitisha tafauti za kimadhehebu na kuzifanya kama kwamba ni zenye muhimu katika dini, hufanya hivyo hata kufika kutumia Qur’an na Hadithi za Mtume (SAW). kwa kutaka kuthibitishia mawazo yao. Hivyo ndivyo walivyokuwa Wafarisayo (wanafik wa Kiyahudi) miongoni mwa Mayahudi, Sayyidna Isa a.s. moja kwa moja alikataza vitendo vyao hivyo. Kwa hakika wenye kufanya hivyo ilivyo khasa ni kwamba bila ya wao kutambuwa wanaleta uharibifu katika Uislamu kwa jumla na kwa hayo madhehebu wanayo jinasibisha nayo. Wenye ilimu na maarifa miongoni mwetu ni busara kutowaachilia watu wenye fikra potofu kama hao kuvunja juhudi zinazofanywa katika kujenga na kuimarisha mafahamiano mema baina ya binadamu, ikiwa ni katika dini au baina ya madhehebu.

Kuweko misikiti ya zamani sana, kama ile ilioko Kilwa Kisiwani katika Tanganyika, Ndagoni PembaKizimkazi na Tumbatu Zanzibar, na Gedi katika Kenya, ni ushahidi wa kutosha kuthibitisha ya kwamba Uislamu umefika katika Afrika Mashariki kwa karne na karne nyuma. Sisi tulikwisha kuwa Waislamu hata kabla ya mtindo wa kujigawa Waislamu vikundi vikundi na kuingizwa kwa madhehebu katika dini. Waislamu badala ya kujinasibisha kuwa ni Waislamu na kufuata Uislamu kama ulivyokuja, wameona ni ndivyo kuwania na kujinasibisha na madhehebu. Kwa karne nyuma watu wa Afrika Mashariki walisalimika na hii balaa ya mfarakano wa madhehebu ambao umekuwa kwa muda sasa unabomowa umoja wa Waislamu katika sehemu nyingi za ulimwengu.

Yalikuweko katika Zanzibar madhehebu mbalimbali, hakukuweko mivutano au mashindano ya kimadhehebu. Japokuwa sehemu kubwa ya wakaazi wa sehemu hizi walikuwa “Sunni”, na kwa muda wa miaka mia mbili waliokuwa wakihukumu ni Ibadhi. Wakihukumu kutoka Zanzibar na kwa nufudhu kubwa ilioenea Afrika Mashariki na ya Kati, na wakiwemo sehemu ndogo kabisa ya wakaazi wa Kishia, wengi wenye asili ya Kiasia. Juuyayote haya, hapakuwepo ubaguzi wowote wala mvutano wowote baina yao kwa sababu ya hivi kuwa wa madhehebu mbalimbali.

Katika Afrika Mashariki mingi ya misikiti imejengwa na Ibadhi, ambao pia walijenga vyuo na kuwasaidia kimaisha wengi wa walimu wa vyuo hivyo. Yote haya wakitenda kwa ajili ya manufaa ya watu wote, wengi wao wakiwa ni Sunni. Haikupata kutokea kuwa madhehebu yoyote yale kutaka kumgeuza Muislamu yeyote yule kutoka madhehebu na kuingia madhehebu mengine.  Haikutendwa hivyo kwa nguvu, au kwa kulaghai kama vile kwa kuwarubuni kwa vyeo, au vijizawadi, au kwa kuwapa fursa za safari za nje.

Mmoja wa wazee wangu ndie alieanzisha mji na bandari ya Lindi, alianzisha mji na bandari hii kwa kufyeka pori na kukata mikoko. Wakaazi wa sehemu hizi, Wamakonde walioonesha imani yao ya kuwa Waislamu, yeye mzee wangu ambae alikuwa ni Ibadhi alikwenda kumleta Sheikh Omar Stambuli kutoka Malindi Kenya ili aje awafundishe Wamakonde Uislamu na Sharia zake. Sheikh Omar alikuwa ni mwanazuoni wa Kisunni. Haikumpitikia mzee wangu huyo kuwa ni muhimu amlete mwanazuoni wa Kiibadhi kwa wajibu huu. Kama angelitaka kufanya hivyo, basi angeliweza kupata mwanazuoni huyo kutoka Zanzibar au hata kutoka Oman na kueneza Uibadhi. Lililokuwa muhimu kwake sio madhehebu yake, bali ni dini yake. Uislamu unapinga mfarakano wa kimadhehebu. Kwa kuzidi Mwenyezi Mungu Mtukufu kutukataza mfarakano na kutuhimiza juu ya dharura ya kushikana sote pamoja na kuepusha mfarakano, ametwambia Mola wetu Mlezi, Subhaanahu wa Ta'aala:

Na shikamaneni kwa Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yenu: vile mlivyo kuwa nyinyi kwa nyinyi maadui naye akaziunganisha nyoyo zenu; kwa neema yake mkawa ndugu. Na mlikuwa ukingoni mwa shimo la Moto, naye akakuokoeni nalo. Namna hivi Mwenyezi Mungu anakubainishieni Ishara zake ili mpate kuongoka.”      
(Al ‘Imraan: 103).

Na akaendelea Mwenyezi Mungu Mtukufu kutueleza katika Sura hii hii juu ya haja na dharura ya watu kuwa wamoja na kuepukana na mfarakano na waweko miongoni mwetu wenye kuamrisha kutenda mema na kukataza kutenda uwovu:

 “Na uwe kutokana na nyinyi umma unao lingania kheri na unao amrisha mema na unakataza maovu. Na hao ndio walio fanikiwa. Wala msiwe kama wale walio farikiana na kukhitalifiana baada ya kuwafikia hoja zilizo wazi. Na hao ndio watakao kuwa na adhabu kubwa”.                  
(Al ‘Imraan: 104-105).

“Kulingania kheri”, maana yake ni kulingania binadamu wawe wamoja, sio kufariqiana vikundi vikundi na madhehebu madhehebu; sio kufariqiana baina ya ndugu - Waumini. Kulingania kheri sio kutukanana, wala sio kutuhumiana wenyewe kwa wenyewe. Kulingania kheri muhimu na kukuu kwenye kuhitajika ni kwamba sote tuwe kitu kimoja bila ya mfarakano wa aina yoyote ule. “Kukatazana maovu”, ni kukatazana kila lile ambalo ni ovu kwa binadamu, na ambalo linaondoa mafahamiano mema baina ya viumbe. Kama tunavyoona hapo juu, adhabu kubwa itawafikia wale wenye kufariqiana na kukhitalifiana baada ya kuwa ushawafikia uwongofu na maamrisho ya Mwenyezi Mungu Mtukufu ya kutakiwa wawe wamoja. Adhabu ya Mwenyezi Mungu Mtukufu huanza kuwafika viumbe vyake tangu hapa ulimwenguni. Ni wajibu wetu tujihisabu kabla ya kuhisabiwa, hivi ili tuweze kujuwa makosa yetu ili tupate kujisahihisha, na kutenda mema. Wema hufuta uwovu:

Mambo mazuri na mabaya hayawi sawa. Ondosha (ubaya unaofanyiwa) kwa mema; tahamaki yule ambaye baina yako na baina yake kuna uadui atakuwa kama ni jamaa (yako) mwenye kukufia uchungu. Lakini (jambo hili) hawatapewa ila wale wanaosubiri, wala hawatapewa ila wenye hadhi kubwa (kwa Mwenyezi Mungu).        (Fusilat: 34 –35).

Uislamu sio dini mpya, Uislamu ni mchanganyiko wa dini zote alizoziteremsha Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa viumbe vyake; mchanganyiko wa dini zote ili viumbe vyote wawe ni kitu kimoja. Uislamu unakataza hata kuwatukania makafiri waungu wao, ili kuepusha na wao kwa ujinga wao kumtukana Mwenyezi Mungu Mtukufu:

Wala msiwatukane hao wanao waomba badala ya Mwenyezi Mungu, wasije na wao wakamtukana Mwenyezi Mungu kwa jeuri bila ya kujua. Namna hivyo tumewapambia kila umma vitendo vyao. Kisha marejeo yao yatakuwa kwa Mola wao Mlezi, naye atawaambia waliyo kuwa wakiyatenda”.                   
(Al An-‘aam: 108).

Leo imefika kuwa baadhi ya Waislamu wanawatukana Maimamu wa wenziwao, bali wamefika hata kuwatukana baadhi ya Masahaba wa Mtume wetu mpenzi s.a.w. Huu sio Uislamu. Tafadhali isome Qur’ani kama vile imeteremshwa kwako weye khaasa. Isome Qur’ani na izingatie vyema maana yake. Tuisome Qur’ani na tujitahidi kuifuata na kutekeleza maarisho yake na kujiepusha na yale tunayokatazwa kama tunavyoweza. Ni ndivyo kuongozwa waliokosea Njia, lakini sio kwa kutukanana. Kuongozana ni kwa njia ya upole, maarifa, busara na kustahamiliana, ametwambia Mola wetu Mlezi:

 “Waite waelekee kwenye Njia ya Mola wako Mlezi kwa hikima na mawaidha mema, na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora....”. 
(Annahal: 125).

Hao waliofarikiana na kugawana vikundi vikundi, hao ndio sisi tulivyo hii leo. Natija yake imekuwa tumejidhuru wenyewe na kujifanya kuwa ni dhaaifu baada ya kuwa tumeletewa Uwongofu. Uislamu haujaja kwetu jana. Tangu ulipoteremshwa sisi tulikuwa Waislamu. Juuyahivyo imekuwa leo sisi ndio wenye kufarikiana na kuzozana juu ya mambo ambayo sio ya kimsingi wala yenye faida yoyote katika dini yetu. Mambo ambayo yameletwa kwetu na watu ambao ni hii leo tu ndio wamekuwa Waislamu. Wametuletea sababu hizi za kufariqiana kwa maslaha yao wao wenyewe binafsi au kwa maslaha ya fikra zao dhaifu za kikabila au kimadhehebu. Kwa ajili ya kutekeleza na kuendeleza maslaha yao hayo ndio wanasababisha mfarakano baina yetu. Wao wanachotaka ni wafuasi na wahami wa fikra na vitendo vyao miongoni mwetu sisi. Wao hawataki kueneza Dini ya Mwenyezi Mungu Mtukufu Lillahi Ta’ala. Ni wajibu wetu tutahadhari na Siku itakapofika na Mwenyezi Mungu Mtukufu kutuuliza: “Je! Mlikufuru baada ya kuamini kwenu?” Mlikhitalifiana baada ya kukufikieni Uwongofu kutoka Kwangu?

Inatupasa tutahadhari na wale ambao - japokuwa ni wachache - wanataka kutubabaisha fikra zetu kwa njia hii au nyengine na kuleta mfarakano baina ya Waislamu wa Afrika Mashariki. Mwenyezi Mungu Mtukufu atujaalie tuwe wenye kushikamana kwa Kamba Yake ili tupate kumqabili Siku ya Hisabu na hali yakuwa nyuso zetu ni zenye kung’ara kwa Rehema Zake – Aamyn!

Sisi ambao tulikuwa wenye kupigiwa mfano kwa jinsi tulivyo shikamana na kuwa wamoja. Wamoja kwa kila njia na maana, leo na sisi tume jitumbukiza katika hii balaa ya mfarakano. Leo tumekuwa huyu anamtukana huyu kwa kisingizio cha “Bid’a” na yule anamtukana yule na kufika kumwita ni kafiri. Huu sio Uislamu, wala sivyo ulivyofundisha Uislamu. Kukhitilafiana rai Maimamu katika mambo ya Fiqh isiwe ndio sababu ya sisi kuleta mfarakano baina yetu na kufika kuwacha tabia yetu ya ustahamilivu na kuchukuliana. Kukhitilafiana rai katika mambo madogo madogo (ambayo sio ya misingi) hakutaacha kuwepo. Kwa hikika hivyo ni rehema kwa Waumini, madhali hatutoki katika misingi ya Dini yetu. Khitilafu katika Fiqhi au katika kuifahamu taarikh kusiwe ndio sababu ya bughdha na kujenga mfarakano, mvutano na adawa baina yetu.

Hebu natuizingatie hali ya Zanzibar ilivyokuwa kabla ya nchi yetu kuvamiwa na kumezwa na kufisidiwa kila kitu. Mfalme alikuwa ni Ibadhi. Sehemu kubwa ya Umma walikuwa ni Sunni. Sehemu ndogo walikuwa ni Shia. Juuyahivyo, katika kalenda ya Serikali kuliwekwa siku mbili kuwa ni siku za kufungwa kazi serikalini, mwezi 21 Ramadhani, siku aliouliwa Imam Ali r.a. na mwezi kumi Muharam, siku aliouliwa Imam Hussein r.a. Nchi ngapi ambazo zinafanya hivi kwa kuhishimu wananchi wao ambao ni sehemu ndogo kabisa ya wananchi. Hatuoni hayo kufanyika hata katika zile nchi ambazo Shia ni nusu ya wananchi wa nchi hizo.

Watu wa Afrika Mashariki wamepata faida kubwa kutokana na ukarimu wa aila ya Karimjee Jivanjee, Bwana ambae ametujengea hospitali, nyumba za wazee waliokuwa hawana njia za kujisaidia, mwahala mwa kujumlikia na klabu mbalimbali. Aila ya Karimjee inatokana na Mabohora ambao ni Shia. Ukarimu wao umewafaa kila mtu, sio basi Waislamu. Kwani kuna Mabohora wangapi katika Afrika Mashariki hata iwe ukarimu wao huo wanakusudiwa wao tu? Hata huko Zanzibar Mabohora ni wachache kabisa.

Siwa Hajee, ni Shia wa Kismailia, wao ndio wafuasi wa Aga Khan, yeye ndie aliejenga hospitali ya mwanzo Zanzibar na akajenga nyengine huko Dar es Salaam. Ismaili mwengine, Tharia Topan, yeye aliwacha Wakfu ambao ndio ukaasisiwa Madrasa katika Msikiti Barza, wa Sunni; na misikiti mingine mingi ilijengwa kutoka na mali yake alioiwacha kwa makusudio hayo. Kwa bahati yeye Bwana Tharia Topan alikuwa ni waziri wa Sayyid Barghash. Watu wasiofadhila wamefika hata kufuta majina ya hao mabwana waliofanya kheri hizo juu ya majengo walioyajenga, kama vile jina la Karimjee kwenye hospital ya Mnazimoja. Hospitali aliwajengea wananchi wa Zanzibar, badala yake wavamizi wakaiita hospitali hio kwa jina la V. I. Lenin, mtu ambae sisi hatuna makhusiano nae hata chembe. Kuzidisha msumari wa moto juu ya kidonda kwa bwana karimu huyu, Sir Tayabali Karimjee, wavamizi wakamnyang’anya nyumba yake ambayo ndiyo aliokuwa akiishi yeye na aila yake na ndiyo aliokusudia aishi humo katika utuuzimani mwake na kumalizia uhai wake. Kwa kufikishwa katika idhlaali ya hali hii, yaani kunyang’anywa nyumba yake na kuachwa hana pakukaa, ilimlazimu aihame nchi yake - Zanzibar - na kwenda kuishi ugenini, Pakistani na kufia huko. Yeye Bwana Tayabali alikuwa ni mzaliwa wa tano wa Kizanzibari. Hivi ndivyo sisi tunavyowalipa wale wanaotutendea kheri. Na hivi ndivyo tulivyo mpaka hii leo. Huu ndio uungwana wetu. Mwenyezi Mungu Mtukufu ametwambia ya kwamba tukimshukuru atatuzidishi neema zake, na tukimkufuru basi adhabu yake ni kali:

 “Na alipo tangaza Mola wenu Mlezi: Mkishukuru nitakuzidishieni; na mkikufuru, basi adhabu yangu ni kali.
(Ibrahim: 7).

Asieweza kumshukuru binadamu mwenziwe basi huyo hamshukuru hata Mwenyezi Mungu Mtukufu.




No comments: