![]() |
| Prof. Ibrahim Noor |
| Zanzibar 1950s |
Kubadilisha
masomo ya taarikh iliyopotoshwa sana si kazi nyepesi kwani kuna
wachache wenye nguvu ambao wanaing'ang'ania na kuilinda kwa nguvu zao, na za
wakoloni wa leo wakiwa nyuma yao, kuwalinda kwa mirututu ya bunduki na risasi
za moto ambazo wako tayari kuzitumia wakati wowote kuwauwa Wazanzibari. Si
umeona aina ya vifaa vilivyoteremshwa visiwani wakati wa "uchaguzi"!
Na si umeona vile walivyouendesha huo "uchaguzi" uliokataliwa na
wengi!
Jambo
moja ukishalitia katika bongo za vijana wakati wangali watoto wadogo na
kuendelea nalo mpaka kumaliza masomo yao, huwa ni shida kubwa sana
kulirakibisha; nalo ni kufundisha chuki, hata chuki hizo zikiwa hazina msingi
wala ukweli ndani yake. Si unaona vile tunavyopata taabu kuwailimisha
waliojazwa chuki hizo tokea utotoni mwao! Bila ya hizo siasa na masomo ya chuki
yenye ukweli finyu na uwongo mwingi akina fulani hawatakuwa tena na madaraka na
nyadhifa za juu, na hapa ndipo penye matatizo yote. Kwani wako tayari kuiuza
nchi na uhuru wa wananchi wao kulinda matumbo yao. Potelea mbali raia wafe na
njaa...
Juzi
nilikuwa nazungumza na mhishimiwa mmoja na akaniambia: "tafadhali njoo
utembee kwenu, siku nyingi hujaja. Nakuhakikishia hakuna lolote litalokukuta.
Utakuja uondoke salama." Mimi nikamjibu: "Hakuna lolote linalonistua
katika huu umri wangu. Kwani, nini kubwa watakaloweza kunitenda? Hakuna kubwa
kama kuuwawa. Na hili pia halinistui. Kwani nikidhulumiwa roho yangu,
watakaonidhulumu si watajitwika wao madhambi yangu wakifanya hilo?
Linalonifanya nisitake kuzuru kwetu ni kuwa kila nikija nilikozaliwa huwa naondoka
na majonzi mapevu sana kuona vile hali za watu zilivyodidimia vibaya sana.
Ukiangalia unagundua kuwa mtu na aila yake kupata mlo mmoja wa kisawasawa kwa
siku ni shida pevu sana. Ukiangalia hali ya masomo unatokwa na machozi.
Ukiangalia hali ya matibabu unataka kulia. Kwa ufupi, kama wewe una hisia na
watu wako na ni mtu mwenye huruma, haya onayoyaona hayaachi kukutia katika
dhiki kubwa sana ya moyo.
Zanzibar
kumetendwa dhambi kubwa sana zilizokemewa na Mola Subhana waTaala, za kuuwa
watu kama nguruwe mwitu bila ya haqi, kuraruwa wanawake, kuwafunga na
kuwaadhibu raia bila ya sababu, kudhulumu haqi za raia na kumetendwa na
madhambi mengi mengineyo, na ikisha kumkejeli Mwenyezi Mungu kila mwaka kwa
kuyasherehekea maovu yote hayo, na zaidi, kuviita vitendo viovu vyote
hivyo: "Matukufu"! Nandika haya huku nalengwa na machozi
nikifikiria vipi wanaosema kuwa wao ni Waislamu na wengine Wakristo
wanavyojiandikia na kujipalilia wenyewe Moto, si wa Qiyama tu, bali tunaoneshwa
tungali papa hapa Duniani malipo ya kumkejeli Mwenyezi Mungu kwa kusema na
kutenda ya dhulma. Nani katika sisi wenye umri wa miaka sabini na zaidi
tulifikiria kuwa hali ya Wazanzibari itafikishwa hivi ilivyo? Na bado
inaendelea kudidimia. Kwa fikra zangu, hakuna njia ya kutokana na janga hili
ila umma kutubia tawban nasuha na kumuomba Mwenyezi Mungu atuswamehe.
Atuteremshie Rehma Zake. Vinginevyo ni kuwafurahisha wachache ambao hata na wao
hawana raha ya Dunia na huko Akhera watajijua wenyewe.
Siachi
kukutakieni nyote kila la kheri
Alichoandika Salim Msoma:
http://www.mohammedsaid.com/2016/05/zanzibar-agony-of-its-history-by-salim.html
No comments:
Post a Comment