Monday, 6 June 2016

KARIBU RAMADHANI - KHALFAN KITANI


Photo

Karibu ewe Ramadhani
Mwezi ulo mtukufu
Karibu wetu mgeni
Kwa moyo mkunjufu 
Karibu kwa imani
Na wingi wa insafu
Ewe wetu mgeni
Karibu Pasi na hofu

Sote tulo waumini 
Kwa hamu twakutaraji
Mgeni uliye thamini
Mwezi ulopewa taji 
Nyingi zetu imani
Kwa furaha na vifiji 
Tukiomba ufike lini 
Uje mgeni kutufaraji

Mgeni wetu adhimu 
Mwenye zako sharafu 
Wewe kwetu muhimu 
Mwezi ulojaa utukufu  
Na sisi sote Waislamu 
Tumejipanga kwa safu 
Kila kitu tena umetimu 
Kwa wako umaarufu

Njoo ukaribie mgeni 
Kwa hamu twakungojea 
Sote tulioko mijini 
Na mashamba hata pia
Hakika twakutamani
Kwa neema kutuletea 
Twajua yako thamani 
Furaha nyoyoni imetujaa

Ni nyingi zako neema 
Na baraka ziso mithilia 
Qur'an twazidi kuisoma 
Na Misikiti kung'ara pia  
Mashetani nao wakoma 
Kwa waumini kusogea 
Waislamu nao kwa hima 
Tarawehe kuzisimamia

Ni nguzo ilio faradhi
Dini yetu imetuletea 
Saumu ni yake hadhi 
Mwezi mtukufu ukiingia
Ni mja mwenye maradhi 
Na msafiri asamehewa 
Twaomba zako radhi 
Funga zetu tutakabalia

Sala na zake salamu 
Zimfikie wetu Nabiya
Mtume wetu Hashimu 
Dini ya haki kutuleteya
Na wote walo muhimu 
Kamba yake kuizuwia 
Sote tulio Waislamu  
Dua zetu twakuombea


No comments: