Utangulizi
Chokochoko imeanzishwa na mtu
mmoja anaitwa Pasco JF anasema wazee wangu wameenziwa kama wapigania uhuru wa
Tanganyika na akatoa mfano wa bango lililowekwa nje ya nyumba ya Mzee Mwinjuma
Mwinyikambi Mwananyamala. Bango hili limeandikwa kuwa hapo kwenye nyumba ya
Mzee Mwinjuma ndipo ilipoasisiwa TANU. Hakika hili bango lipo na nalijua vyema
kwani hata Mzee Mwinjuma na mkewe Bi. Fatuma ni katika wazee wangu kwa hiyo nikiwafahamu.
Ukweli ni kuwa sikuzote nikishangazwa na bango hili kuwa iweje liwekwe bango la
kusema kuwa TANU ilianzishwa nyumbani kwa Mzee Mwinjuma na lisiwekwe nyumbani
kwa Abdulwahid Sykes Mtaa wa Aggrey na Sikukukuu? Ushahidi wa kihistoria na kwa
ufahamu wa watu wa Dar es Salaam walioishi katika miaka ya 1950 wanaijua vyema
historia ya Abdul Sykes na TANU akiwa na mdogo wake Ally na Julius Nyerere na
wazalendo wengine.
| Kushoto: Mwinjuma Mwinyikambi, Max Mbwana, Julius Nyerere na Mshume Kiyate |
Umesema kweli TANU imeanzishwa mahali pengi.
Lakini chanzo cha matawi hayo yote ni nyumbani kwa Abdul Sykes
Mtaa wa Aggrey na Sikukuku.
Fatilia historia ya TANU hapa chini:
Lofawamali,
Unajua kisa cha mtaa ule kuitwa Aggrey?
Mwaka wa 1924 Dr. Kwegyr Aggrey alikuja Dar es Salaam kusaidia
serikali ya kikoloni katika suala la elimu kwa Waafrika wa Tanganyika.
Huyu bwana alikataliwa kulala Africa Hotel ikabidi atafutiwe malazi
Government House.
Dr. Aggrey alikutana na watu maarufu wa Dar es Salaam na mmoja
wao alikuwa Kleist Sykes.
Alimuuliza kama Waafrika wa Tanganyika wana chama chochote cha
kushughulikia mambo yao na jibu likawa hapana.
Dr. Aggrey akawashauri waunde African Association.
Wazo hili Kleist alilipenda na alilifanyia kazi na ilipofika mwaka wa 1929
wakaunda African Association Kleist akiwa katibu na rais Cecil Matola.
Kutokana na ujio wa Dr. Aggrey ndiyo mtaa ule ukapewa jina lake na
ikasadifu kuwa Kleist Sykes alikuwa akiishi mtaa ule kuanzia mwaka wa
1942.
Nyumba hii ndiyo alikuja kuishi mwanae Abdul Sykes na hapo pakaja
kuwa kituo kikubwa cha harakati za kuunda TANU na kudai uhuru.
Mikutano mingi ya wanaharakati ilikuwa ikifanyika pale katika miaka ya
mwanzoni 1950 na Nyerere ndipo alipopelekwa na Joseph Kasella
Bantu kwenda kujulishwa kwa Katibu wa TAA na Kaimu Rais Abdul
Sykes mwaka wa 1952.
Nyerere alipoacha kazi mwaka wa 1955 alikuja kukaa nyumba hii na
Abdul Sykes.
Alipotoka hapa ndipo Mwalimu Nyerere akahamia Magomeni Majumba
Sita nyumba aliyotafuta Mzee John Rupia.
Nyumba hii ya Mtaa wa Aggrey (sasa Max Mbwana) imevunjwa.
Nyumba hii kwa sasa haipo tena badala yake Bwana Ally Sykes kajenga
gorofa.
Baba yangu Salum Abdallah amenihadithia kuwa siku ya kwanza kumtia
Nyerere machoni ilikuwa nyumba hii kwa rafiki yake Abdul Sykes.
Unaweza kusoma historia ya Dr. Aggrey hapo chini:
James Emman Kwegyir Aggrey - Wikipedia, the free encyclopedia
Pasco,
Sasa ingekuwa kibao cha kuonyesha TANU ilipoundwa hakuna mahali awla
zaidi kuliko nyumbani kwa Abdul Sykes kwa sababu wanasiasa wote wa
wakati ule kuanzia Hamza Mwapachu, Chief Kidaha Makwaia, Julius
Nyerere wote hao kwa nyakati tofauti wameruka kizingiti cha mlango wa
nyumba ya Abdul kuja kuzungumza hali ya baadae ya Tanganyika.
TANU haikuundwa nyumbani kwa Mzee Mwinjuma Mwinyikambi.
Hakuna ushahidi wowote katika hili.
Kama ulivyosema, huo ni uongo.
Ikitokea fursa In Shaallah nitakujuza kuhusu mswada wa kitabu cha historia
ya TANU ulioandikwa na Abdul Sykes na Dr. Wilbert Klerruu mwanzoni
mwa miaka ya 1960 mara tu baada ya Tanganyika kupata uhuru wake.
Kwa leo staladhi na haya nilokueleza.
No comments:
Post a Comment