Sunday, 5 June 2016

KUTOKA JF: UHURU UMELETWA NA NYERERE PEKE YAKE WAISLAM WALIPIGA DUFU




Mshume Kiyate na Julius Nyerere 1964


Pasco,
Hayo hayo uliyoandika ungeweza kuyaandika kwa adabu bila kejeli.
Hakika Mwinjuma Mwinyikambi kapewa mtaa lakini hujui kisa chake.

Mwinjuma Mwinyikambi nyumbani kwake limewekwa bango kuwa
hapa ndipo palipoanzishwa TANU.

Hii si kweli na kama ulivyoandika huu ni uongo.

Lakini zipo sababu za kutaka historia ionyeshe hivyo na waliofanya
hivyo walifanya kwa lengo maalumu na ndiyo sababu wakakoleza
kwa kumpa barabara.

Max Mbwana kapewa mtaa pamoja na Mshume Kiyate wakati wa
Kitwana Kondo alipokuwa Meya.

Sina hakika kama kibao cha jina kimewekwa.

Uhakika niliokuwanao ni kuwa kibao cha Mshume Kiyate hadi leo
hakijawekwa zaidi ya miaka 20 sasa.

Wazee wetu hawakupatapo hata siku moja hata kwa mbali kufikiria
kushusha hadhi ya Mwalimu Nyerere na ndiyo maana hata ilipoandikwa
historia ya TANU mwaka 1981 na wao mchango wao haukuonyeshwa
ikawa Nyerere ndiye aliyeanzisha TANU wao walibaki kimya hadi wanaingia
kaburini.

Wangetaka wangeuliza mbona sisi tulianza mambo haya na Abdul Sykes
1950 na Abdul ndiye aliyemleta Nyerere kwetu na kutujulisha na tukijua
mipango ya kuunda TANU?

Lakini sisi ni waungwana tunajua heshima ya fadhila na utu.
Kwetu kusimanga ni mwiko mkubwa sana.

Kiyate MshumeAbdul Sykes, John Rupia, Dossa Aziz, Sheikh
Hassan bin Amir
 kuwataja wachache hawakuchangia juhudi za kudai
uhuru kwa kupiga dufu.

Ikiwa hujui michango ya wazalendo hawa yote nimeyaeleza katika itabu
cha maisha ya Abdul Sykes.

Kitafute kitabu usome.

Kinapatikana Ibn Hazm Media Centre Bookshop Msikiti wa Manyema
na Mtoro.

Mwisho nataka nikueleze kuwa safari ya Nyerere UNO ilianza kupangwa
mwakawa 1950 na mtu aliyesaidia sana alikuwa Earle Seaton kwa ushauri
wa kisheria na Seaton alikuwa rafiki ya Abdul Sykes na ndiye aliyemleta
katika siasa za TANU.

Lakini waliosimamia safari lilikuwa Baraza la Wazee wa TANU chini ya uenyekiti
wa Sheikh Suleiman Takadir na mkusanyaji fedha za safari alikuwa Idd
Faiz Mafongo.


Kushoto: Idd Faiz Mafongo, Sheikh Mohamed Ramia, Mwalimu
Julius Nyerere, Saadan Abdu Kandoro na Haruna Taratibi 1956

Huyu ndiye alikuwa mweka hazina wa Al Jamiatul Islamiyya Fi Tanganyika na
TANU.

Yako mengi lakini kwa sasa tosheka na maelezo haya.

Nahitimisha kwa kukueleza kuwa huo Mtaa wa Ally Sykes kajipa mwenyewe
na kauita Ally Sykes Close.

Mtaa huo hakutunukiwa na haupo katika ramani ya jiji.

No comments: