| Zitto Zuberi Kabwe |
''Ndugu Wananchi mnajua
mara baada ya uchaguzi mkuu wa Zanzibar kufutwa chama chetu kiliweka msimamo wa
wazi kwamba kinatambua ushindi wa Maalim Seif Sharif Hamad kama Rais
aliyechaguliwa na Wazanzibari na anayepaswa kula kiapo na kuunda Serikali ya
Umoja wa Kitaifa.
Tuliandika pia masuala
10 muhimu kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuyafanyia kazi, na moja
ya jambo tulilomtaka Rais Magufuli Kulifanyia kazi ni suala la demokrasia ya
Zanzibar. Rais hakusikia wito wetu na aliruhusu ufutwaji usio halali, kisiasa
wala kisheria wa uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa Oktoba 25, 2015.
Tunarudia kusisitiza
kuwa Chama chetu cha ACT Wazalendo hakiutambui uchaguzi wa marudio wa Zanzibar
uliofanyika mwezi Machi mwaka 2016 pamoja na matokeo yake yote. Kwa maana hiyo
hatutambui Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, Baraza la Mawaziri la Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar, na Pia Rais wa Zanzibar.
Wananchi, Hivi karibuni
kumekuwa na kuongezeka kwa sintofahamu huko Zanzibar kufuatia Mgombea Urais
aliyeshinda na kunyanganywa ushindi wake kwenda kwa wananchi kuzungumza nao.
Hali hii imepelekea jeshi la polisi kumhoji Maalim Seif na siku mbili baadaye
Dkt. Shein kutamka kuwa hamwogopi Maalim Seif kwa sababu "Hana vifaru na
mizinga".
Tunalaani kauli hii ya
Dkt. Shein ya kutisha kwa vifaru na mizinga. Kamwe huwezi kuzima haki za
Wananchi kwa vifaru na mizinga. Dkt Shein akumbuke kuwa Sultan alikuwa na
jeshi, vifaru na mizinga na ulinzi wa Dola kubwa kama Uingereza lakini
aliangushwa na wananchi wa Zanzibar mwaka 1964.
Dkt Shein akumbuke kuwa
nchi kadhaa duniani zilikuwa na madikteta wenye vifaru na mizinga lakini
waliondoka. Dkt Shein afute kauli yake hii na kuacha vitisho badala yake aanze
mchakato wa kupata maridhiano ya jamii ya Zanzibar. Hatutaki kurithi damu,
tunataka kurithi nchi yenye amani, haki na demokrasia.
Wananchi, sisi ACT
Wazalendo, tunajua hali mbaya ya kisiasa iliyopo Zanzibar na mkwamo uliopo hivi
sasa Kisiasa, Kijamii na Kiuchumi. Hata hivyo ni lazima tupate jawabu kupitia
sanduku la kura. Tunapendekeza kuwa Vyama vikuu vya siasa Zanzibar vikubali
‘kufa kidogo’ yaani ‘to die a little’, kwa vyote kukubali kuwa Chaguzi zote
Mbili, wa Mwaka 2015 na ule wa mwaka 2016 zilikuwa batili, zifutwe na Uchaguzi
Mkuu mpya uitishwe.
Uchaguzi huo utanguliwe
na Serikali ya Mpito itakayohusisha vyama vyote vya siasa na baadhi ya
wanajamii wanaoheshimika na Wazanzibari wote ili kujenga kuaminiana. Tunadhani
hii itatupa nusra kwa Zanzibar. Tunawaomba Wazanzibari watumie mwezi mtukufu wa
Ramadhani kutafakari maoni haya na wote kwa pamoja baada ya Ramadhani kuja na
jawabu ya hali ya kisiasa. Tunatamani Zanzibari irudi kwenye hali ya kawaida na
ishamiri. Zanzibar ikiingia kwenye mtafuruku Tanzania nzima itakuwa kwenye
mtafaruku. Ni dhahiri kuwa Rais Magufuli ameshindwa kutoa uongozi kwenye suala
hili na hivyo ni wajibu wa Wazanzibari wenyewe kukaa na kupata mwafaka wa
kijamii na kusonga mbele.''
Zitto Ruyagwa Kabwe
Dar es Salaam
Juni 5, 2016
No comments:
Post a Comment