Thursday, 2 June 2016

UCHAGUZI WA ZANZIBAR: MASHEIKH WA PEMBA WAVUNJA UKIMYA - SALMA SAID



Ujumbe wa ofisi ya Mufti Zanzibar umefanya ziara na kukutana na baadhi ya Masheikh Kisiwani Pemba kwa lengo la kutaka kuzungumzia haki ya sasa inayoendelea kisiwani humo ambapo baadhi ya wananchi hususiana kuuziana bidhaa na kukataa kuzikana kufuatia stafahamu iliyotokana na uchaguzi mkuu wa Octoba 25 ambapo inasemekana kilichofanyika ni dhulma ya wazi wa kupora ushindi wa Chama Cha CUF na kuwapa Chama cha CCM.
Ujumbe huo umefika Pemba na kuwataka Masheikh watumie taaluma yao ya dini kuwataka wananchi waondokane na hali ya kutengana na kuishi kama zamani. Haya soma kilichojiri katika kikao hicho ambacho Mufti wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kaabi alikuwa miongoni mwao:
Katika maelezo yake Sheikh Saleh Kaabi na ujumbe wake aliokwenda nao wakiwataka Masheikh hao kuilimisha jamii kuishi vyema kwa upendo na mashirikiano kwa kutumia hadithi na aya za Quran Tukufu huku Masheikh wakielezwa kwamba wana umuhimu katika jamii.
Lakini Masheikh hao wamekuja juu na kusema kwamba hapawezekani kuwa na amani na upendo pasi na haki na uadilifu kutendeka.
Mmoja wa masheikh ambao walipata nafasi ya kuchangia alisema na kuhoji kua tunawezaje kuyafikia mafanikio wakati hatujapita katika njia ya mafanikio? Huku akisistiza kuwa Uislam hauangaliwi vipande vipande bali unapaswa kutizamwa kwa ukamilifu wake ambapo alisema kuwa hatuwezi kuangalia mwisho wa tatizo tu bali pia tunatakiwa kuangaia na chanzo cha tatizo.
Sheikh huyo alimkabili Sheikh Kaabi kwa kumpa fumbo la Kiswahiki kwamba asitegemee kukoroga kinyesi halafu akategemea kusikia harufu mzuri puani mwake.
Sheikh mwengine naye alipata nafasi ya kuongea alisema kuwa Dk Shein kafanya dhulma kubwa na mikono yake inanuka damu na yeye mwenyewe anajua na kumtaka Mufti huyo wa Zanzibar Sheikh Saleh Kaabi amwambie Dk Shein arejeshe haki ya wananchi aliowadhulum ndipo amani na upendo utarudi visiwani humo.
Shekh Saleh pia alinasihiwa na kuambiwa kua aya na hadithi alizowatolea masheikh hao aende akawatolee na viongozi wa serikali kama vile Dk Shein, Balozi Seif na Maalim Seif Sharif Hamad huenda labda na wao kama binaadam wakafaham na wakaamua kutenda haki.
Huku Sheikh mmoja naye alihoji ni kwa nini mambo haya waambiwe wao wasiende kuambiwa hao waliosababisha matatizo haya ambao ni wenye mamlaka ya nchi na vyombo vyake?
Alisema daima viongozi wa dini umuhimu wao siku zote hujulikana kipindi cha shida tu na matatizo lakini kukiwa hakuna vitu hivyo na nchi imetulia hawaitwi hata kupewa asante ingawa juhudi za kuituliza nchi kwa kiasi kikubwa hufanya na viongozi wa dini.
Katika suala la Mazombi na kamatakamata na utesaji pia baadhi ya Masheikh katika kikao hicho wamelizungumzia ambapo aliulizwa Sheikh Saleh Kaabi jee wananchi watafanyaje ikiwa mtu ambaye hana bunduki na uwezo wowote anateswa na kupigwa na kudhalilishwa na Jeshi la Polisi na Mazombi bila ya kosa?
Je ni haram kwao wao kuchukia tu wakati hatua za kuyakataa hayo zipo tatu kwa mujibu ya mafundisho ya Bwana Mtume?
Pia aliulizwa tunawezaje kuwa na mapenzi ya kushirikiana na watu ambao waliwaweka mashekhe wetu ndani na kujisifia katika majukwaa ya kisiasa huku mashekhe hao na familia zao zikiendelea kupata tabu kwa mwaka wa tatu sasa?
Hapo hapo mmoja wa Mashekhe hao akamwambia Sheikh Saleh kuwa kutokana na alivo anaamin kua kama angeamua kusimama usiku na kuwaombea dua tu masheikh wale basi Masheikh wale wangepata nusra ya Mwenyeenzi Mungu lakini inaonekana hata hilo limeonekana limemshinda.
Aliendelea sheikh huyo kwa kusema kua watu waliomba dua nyingi ili kuinusuru Zanzibar na mambo mbali mbali lakini kuna viongozi wa kisiasa na serikali wakawa wanapita na kusema kua vi Alamtara vyenu havitowasaidia chochote (Astaghafurullah) sasa je mtu kama huyu ambaye anadharau na kuidhalilisha hadi Quran (maneno ya Allah) nae tushirikiane nae?
Hakika Sheikh Saleh ambaye ni Mufti wa Zanzibar juzi alipata wakati mgumu sana ambapo hali kama hii aliwahi kukutana nayo wakati ule alipokwenda Pemba na kukutana na wanafunzi wake na kumueleza jukumu lake alilonalo serikalini ambapo Masheikh wa Jumuiya ya Uamsho wakiteseka magerezani huku yeye akiwa amesalia madarakani.
Masheikh hao wamesema hakuna nusura wala dua itakayoombwa ambayo itainusuru Zanzibar zaidi ya waliotenda dhambi hiyo ya dhulma ni kurejesha amana kwa waliowadhulumu ambao ni wananchi wa Unguja na Pemba.
Sheikh Saleh Kaabi aliinama chini mbele ya wanafunzi wake na kulia sana kwa uchungu baada ya kuelezwa atajibu nini mbele ya Allah hali ya kuwa Masheikh wanadhalilishwa magerezani na kuthubutu kusimama mbele ya mahakama na kuangusha vilio vya mateso na udhalilishaji wanaofanyiwa haki ya kuwa yeye bado yupo serikalini, hali hiyo ilimfanya achukue uamuzi wa kutaka kujiuzulu lakini wenye mamlaka walikataa uamuzi huo na hivyo bado anaendelea na wadhifa huo wa kuwa nduo kiongozi mkuu wa kidini serikalini.
Haizidi kwa mwenye kudhulumu ila khasara.



No comments: