BAKWATA
Sehemu ya Sita
Wakati
Tume ya Waislam inasubiri mawazo ya Waislam sasa kundi la Adam Nasibu
wakijionesha wazi kuwa serikali na TANU ilikuwa nyuma yao, lilikutana kwa ajili
ya kile walichokiita Mkutano wa Waislam wa Taifa ulioanza tarehe 13 Desemba,
1968. Serikali ikifanya kazi nyuma ya pazia ilijitahidi sana kuhakikisha kuwa
mkutano ule unafanikiwa. Serikali ndiyo iliyotoa fedha za kufanyia mkutano ule,
ukatoa vyombo vyake vya habari kwa ajili ya kuutangaza vizuri na ukatoa ulinzi
kwa wajumbe wote.
Wajumbe
waliohudhuria mkutano ule walikuwa kama mia mbili. Mkutano huu ulihudhuriwa na
Waislam waliokuwa na vyeo katika serikali na TANU, Waislam waliokuwa wakuu wa
wilaya na mikoa na Waislam wenyeviti wa TANU. Waislam wote wenye majina
walialikwa, pamoja na Waislam waliokuwa katika halmashauri kuu ya TANU na
baadhi ya wajumbe wa mkutano walitoka Zanzibar. Ulikuwa mkutano wa wanasiasa
Waislam ambao ukitoa majina yao walikuwa hawana chochote katika harakati za
Uislam isipokuwa majina yao. Lakini uzito wa mkutano huu ulitokana hasa na kuwa
ulikuwa mkutano ambao ulitawaliwa na Waislam waliokuwa hawapendezi mbele ya macho
ya umma wa Kiislam. Ni ukweli usioweza kupingika kuwa kama mkutano ule
ungelikuwa hasa umetayarishwa kwa ajili ya kumtumikia Allah, ni wazi
ungehudhuriwa na Waislam wa kweli na wenye historia ya unyenyekevu na mapenzi
kwa dini yao. Waislam wa sifa hizi hawakuwepo katika mkutano ule ukimtoa Sheikh
Mohamed Ramia wa Bagamoyo na wengine wachache ambao kwa kutotambua mambo
waliitika mwito. Mkutano ulifunguliwa na Karume na kufungwa na Kawawa. Katika
hotuba yake ya ufunguzi Karume alisema maneno haya:
Dini haiwezi kuwa nje ya siasa kwa sababu siasa
ndiyo damu inayoipa jamii uhai wake. Wakati wa ukoloni wananchi na daini zao
zilikuwa chini ya utawala wa wageni. Hivi sasa watu wamevua mabaki ya ukoloni
pamoja na kutawaliwa kwa misingi ya dini. Kuanzaia sasa uongozi wa dini lazima
ukwe chini ya wananchi wenyewe bila ya kuongozwa na kiongozi kutoka nje.
Mkutano
wa Iringa ulipitisha katiba ya jumuiya mpya ya Waislam, katiba ambayo ilikuwa
sawasawa na katiba ya TANU. Hivi ndivyo BAKWATA ilivyoundwa. BAKWATA ikamchagua
Saleh Masasi, Muislam tajiri na ambae alikuwa kama mwenyekiti wa mkutano ule
kuwa Mwenyekiti wa Taifa na Adam Nasibu akawa Katibu Msaidizi. Nafasi zote za
juu katika BAKWATA kama ilivyotegemewa zilichukuliwa na kundi la Adam Nasibu,
kundi ambalo toka mwanzo lilikuwa likidai kuvunjwa kwa EAMWS. Uongozi wa
BAKWATA uliomba serikali itambue jumuiya hiyo mara moja na ipige marufuku EAMWS
kama jumuiya isiyo halali na mali zake zizuiwe. BAKWATA ilitoa maazimio kadha
lakini azimio namba nne ndilo hasa linafaa kuelezwa. Azimio hilo liliomba
serikali, TANU na ASP kuwatazama na kufanya uchunguzi wa kina kwa viongozi wote
wa EAMWS, hasa Rais, Makamo wa Rais, Katibu wao na baadhi ya viongozi wa mikoa
na wilaya ambao wana chuki na hii jumuiya mpya. Uongozi wa BAKWATA katika
ushindi wao hawakutaka salama na mawaelewano na Waislam wenzao katika EAMWS
wala kuwaonea huruma kama Uislam unavyofundisha, bali ulitaka chama na serikali
uwaandame, hasa wale waliokuwa viongozi.
Baada
ya kuundwa BAKWATA, ili kuondoa wasiwasi na kuwarudishia imani Waislam, Katibu
wa Tume ya Waislam, Mussa Kwikima alitoa taarifa iliyosema:
Hakuna anaeweza kutishia kuwepo kwa EAMWS
isipokuwa wanachama wake, sheria na serikali, lakini si watu binafsi hata ikiwa
mikoa yote kumi na saba ikijitoa haitamaananisha kuwa jumiya imekufa kwa kuwa
kuwepo kwake hakutokani na kuwepo kwa mikoa hiyo kama wanachama isipokuwa
kuwepo kwa wanachama wake, Waislam.
Wakati
ilipotoka taarifa hii BAKWATA ilikuwa bado haijaandikishwa rasmi na Msajili wa
Vyama. Kisheria ilikuwa haiwezekani kwa kundi la Adam Nasibu kuunda jumiya mpya
iliyokuwa na malengo sawa na jumuiya ambayo tayari ishaandikishwa. Kwa muda wa
siku tatu BAKWATA na EAMWS zikawepo kwa wakati mmoja. Ilionekana kama kwamba
EAMWS itashinda vitimbi vya serikali na vya kundi la Adam Nasibu.
Tarehe
19 Desemba, 1968 serikali kama vile imegutushwa na taarifa ya Kwikima, iliipa
BAKWATA Cerificate of Exemption na kuifungia EAMWS. Waziri wa Mambo ya Ndani Said Ali Maswanya
kwa niaba ya serikali alitoa taarifa fupi:
Waziri wa Mambo ya Ndani kwa kuamriwa na Rais
anatangaza kuwa tawi la Tanzania la East African Muslim Welfare Society na
Baraza la Tanzania la la East African Muslim Welfare Society ni jumuiya
zisizotambulika kisheria chini ya kifungu 6 (i) cha Sheria ya Vyama.
Kwa
tangazo hilo la Rais wa Tanzania, Julus Nyerere, Waislam walinyimwa nafasi ya
kukutana na kuzungumza kuhusu tatizo ambalo kwa kweli liliwahisu Waislam peke
yao. Kwa ajili hii basi Waislam walinyimwa nafasi ya kujadili na kulitolea
uamuzi tatizo hilo.
Viongozi
wa EAMWS waliitwa mbele ya Kabidhi Wasii ambae ndiye alikuwa amekabidhiwa na
serikali jukumu la kusimamia shughuli za kufunga rasmi shughuli za EAMWS.
Viongozi walifahamishwa kuwa chini ya sheria ya vyama mali zote za EAMWS
zitauzwa na madeni yatalipwa kutokana na fedha hizo na fedha zitakazobaki
watapewa wanachama. Serikali ilikuwa haiwezi kufanya kama sheria ilivyokuwa
imeelekeza. Ilikuwa jambo zito sana kwa serikali ya Nyerere kuonekana
anasimamia kuuzwa kwa mali za Waislam. Viongozi wa EAMWS walipoitwa kwa Kabidhi
Wasii mara ya pili walifahamishwa kuwa serikali imebadilisha mawazo yake
kutekeleza amri kama sheria inavyosema kwa ajili hiyo basi imefanya mabadiliko
ya sheria ya vyama ambayo yanaiwezesha sasa kutoa mali ya EAMWS na kukabidhi
BAKWATA. Hivi ndivyo mali za EAMWS zilivyochukuliwa na kupewa BAKWATA bila ya
ridhaa ya Waislam wenyewe. Hivi ndivyo shule zote zilizojengwa na EAMWS pamoja
na mradi wa Chuo Kikuu cha Kiislam kilipoanguka katika mikono ya kundi la Adam
Nasibu. BAKWATA haikuwa na uwezo wa kuendesha mipango yoyote na taratibu shule
na miradi yote ya elimu ikafifia na mwishowe kufa kabisa. Hivi ndivyo
halikadhalika moto wa Waislam uliowashwa kwa kupatikana kwa uhuru waliopigania
hadi ukapatikana ulivyokufa. Moto huu ulikuja ukawaka tena, lakini hiki ni kisa
kingine. Insha Allah Mwenyezi Mungu akipenda tutakuja kukieleza.
Huu
ndiyo ukawa mwisho wa kile kilichokuwa kikijulikana kama mgogoro wa Waislam
ulivyomalizika. Mgogoro ambao ulianza pale mwalimu wa shule ya msingi
asiyefahamika na yeyote alipofanya maandamano katika mitaa ya Bukoba akimuunga
mkono Julius Nyerere na Azimio lake la Arusha na ukaishia kwa mwalimu huyu
akiwa na nafasi juu katika jumuiya ya Kiislam ambayo ilikuwa ikichukiza machoni
mwa Waislam. Mwalimu huyu ambae sasa amekuwa Makamu Katibu Mkuu wa BAKWATA
alianza kazi yake kwa kuwashutua Waislam. Katika mkutano wa waandishi wa habari
Adam Nasibu aliiomba TANU na ASP kujikinga na watu wanaohujumu umoja wa nchi
kupitia dini. Akaendelea na kusema kuwa BAKWATA ni sawa na Baraza la Kikristo
la Tanzania. Kwa kuwa Waislam walinyimwa
fursa ya kujadili ìmgogoroí hivi sasa kilichobaki na dhana tu, kuwa nini
kingelitokea endapo wangeliruhusiwa kufanya mkutano ule ulioitishwa na EAMWS.
Waislam wa Bukoba ambao ilitaarifiwa kuwa walifanya maandamano kuunga mkono
Azimio la Arusha hawakutayarisha maandamano ya kuunga mkono BAKWATA. Dar es
Salaam na katika miji mingi ya Tanzania, neno BAKWATA halina tofauti na tusi.
Kumuita Muislam kuwa yeye ni mwanachama wa BAKWATA ni sawa na kumuita Mkristo
mfuasi wa Yuda Iscariot, aliyemsaliti Yesu kwa vipande thelathini vya fedha.
Mjumbe
mmoja wa Tume ya Waislam inastahili kuelezwa habari zake ni Mussa Kwikima. Mussa
Kwikima mwaka 1968 alikuwa ameteuliwa kuwa jaji na Rais Nyerere. Yeye ndiye
hasa alikuwa nguvu kuu katika tume ya Waislam. Wakati alipojitolea kuisaidia
tume katika kupambana na kundi la Adam Nasibu, Waikela alimuonya kuhusu hatari
ambayo itamkabili yeye mwenyewe binafsi na kazi yake. Kwikima alijibu kuwa
umoja wa Waislam ni muhimu kuliko maslahi yake binafsi. Ilipoundwa BAKWATA na
hapo kuwa ndiyo mwisho wa ''mgogoro,'' Kwikima alihamishwa kutoka Dar es Salaam
na kupelekwa Mwanza kama Hakimu Mkazai na Rais Nyerere akamvua madaraka ya
ujaji wake.
No comments:
Post a Comment