Thursday, 13 February 2014

TANU Ilivyovunja Ngome ya Kanisa Katoliki Jimbo la Kusini, 1955 Sehemu ya Kwanza

TANU Ilivyovunja Ngome ya Kanisa Katoliki Jimbo la Kusini, 1955
Sehemu ya Kwanza


Waasisi wa TANU, New Street, Dar es Salaam 7 Julai, 1954

TAA mjini Lindi ilikuwa chini ya uongozi wa Suleiman Masudi Mnonji aliyekuwa Rais na Katibu wake alikuwa Mohamed Waziri. Mnonji alikuwa fundi cherahani na Waziri alikuwa mchoraji wa ramani za nyumba. TAA ilichelewa kuanza mjini Lindi. TAA ilianzishwa Lindi mwaka 1953 wakati uongozi wa TAA mjini Dar es Salaam si tu ulikuwa unaigeuza TAA kuwa chama cha siasa bali ulikuwa ukifanya mipango kumpeleka mjumbe wake Umoja wa Mataifa kudai uhuru. Masudi Mnonji alikuwa na uzoefu wa kutosha katika siasa. Baada ya Vita Kuu ya Pili alikuwa amejaribu kuanzisha vyama vya wafanyakazi katika mashamba mbalimbali ya mkonge kusini mwa Tanganyika. Vilevile aliwakusanya wapishi na madobi mjini Lindi waanzishe umoja wao. Ilikuwa kupitia juhudi zake binafsi TAA ijapokuwa ilichelewa, ilikuja kuanzishwa mjini Lindi na Mnonji alijitolea nyumba yake katika mtaa wa Makonde kama ofisi ya chama. Mnonji kwa kutambua umuhimu wa kuwa na uongozi ulioelimika vizuri, alimleta Nangwanda Lawi Sijaona kutoka Nachingwea aje aishauri TAA jinsi ya kufanya mambo kwa utaalamu.

Wakati huo mjini Lindi kulikuwa na chama cha wafanyakazi bandarini Dockworkersí Union chini ya uongozi wa Mussa Athumani Lukundu, chama ambacho kwa kiasi chake kilianzisha vuguvugu la siasa za vyama vya wafanyakazi. Ingawa vyama hivi viwili, yaani TAA na Dockworkersí Union vilikuwepo katika mji mmoja, siasa za hiki chama cha pili cha wafanyakazi bandarini hazikupitia TAA kama ilivyokuwa mjini Dar es Salaam. Hii kidogo ilidhoofisha mwamamko wa siasa kwa wananchi. Jimbo la Kusini lilikuwa katika usingizi mzito wakati sehemu nyingine Tanganyika zilikuwa zikipiga hatua kwenda mbele zikiandaa vita dhidi ya utawala wa kikoloni. Chanzo cha usingizi huu mzito huko kusini ulikuwa na asili yake katika historia ya Tanganyika.

Vita vya Maji Maji vilipoanza kusini ya Tanganyika mwaka 1905 kwa nia ya kuwafukuza Wajerumani kutoka Tanganyika, zile sehemu zenye Wakristo wengi zilikataa kujiunga na vita na badala yake wakajiunga na majeshi ya Wajerumani na kupigana bega kwa bega dhidi ya wazalendo. Hii ilitokana na sababu ya kuwa uasi dhidi ya dhulma wa Wajerumani ulianza katika maeneo yenye Waislam wengi na vita vikachukua sura ya vita vya Kiislamu dhidi ya Wazungu ambao dini yao ni Ukristo. Kwa kuwa wamishonari walikuwa washirika wa wakoloni, walichukuliwa kama maadui na hivyo ikawa vituo vyao vinashambuliwa na wapiganaji wa Maji Maji. Kutokana mashambulizi haya, Wakristo walivichukua Vita Vya Maji Maji kama vita dhidi ya Ukristo. Harakati za Maji Maji zilishindwa na Wajerumani walifanya fisadi kubwa dhidi ya wananchi na viongozi wao. Jambo hili liliacha kovu kubwa katika fikra za wananchi na kwa upande wa Wakristo ambao walinusurika na ghadhabu ya Wajerumani, wengi wao wakajiweka mbali na aina yoyote ya kupinga ukoloni.

Selemani Mamba Shujaa wa Vita vya Maji Maji Aliyenyongwa
na Wajerumani. Selemani Mamba alikuwa Kiongozi wa Wamwera.
Viongozi Wengine Walionyongwa walikuwa Kinjikitile Ngwale Kiongozi
wa Wamatumbi, Abdallah Chiami Kiongozi wa Wangindo, Mataka Ambuje
Kiongozi wa Wayao na Songea Rauf Mbano Kiongozi wa Wangoni 
Kufuatia historia hii Waafrika waliokuwa kusini ya Tanganyika sasa wakiwa chini ya utawala wa Waingereza na kuwa chini ya himaya ya wamishonari walipumbazwa kiasi kiasi kwamba waliogopa siasa. Baada ya Waafrika kushindwa vita kwa silaha kali za Wazungu sasa Kanisa likaona ndani ya fadhaa ile fursa yao kutawala sehemu hiyo kwa kutoa vishawishi kama vile shule na hospitali. Kwa hiyo Wamishionari na Waingereza walionekana kama mabwana wema wenye kuwajali raia zao kinyume na serikali katili  na ya kidhalimu ya Wajerumani. Vuguvugu la siasa kama ilivyokuwa Vita vya Maji Maji, lilianza katika maeneo ya Waislam kufuatia mfumo ule ule kama ilivyokuwa katika upinzani wa ukoloni wa Wajerumani. Wakristo katika Jimbo la Kusini waliiona TANU kama walivyoviona Vita Vya Maji Maji, kama harakati nyingine za Waislam zilizowa zinakuja tena kwa mara ya pili kuvuruga amani na utulivu. TANU ilipoanza ikawa inavuma kuwa safari hii Waislam walikuwa wamemua kuanzisha vita dhidi ya Waingereza kama walivyoanzisha vita na Wajerumani.

TANU ilipoanzishwa mjini Dar es Salaam na hisia za utaifa  zilipokuwa zikipanda pole pole katika fikra za wananchi katika sehemu nyingi za Tanganyika, Jimbo la Kusini lilikuwa bado usingizini likiishi  katika zama za kale. Mnonji na Waziri, kwa sababu ya utu uzima wao, daraja yao katika jamii na hasa kutokana na kuhusika kwao katika siasa za pale mjini, walikuwa na nguvu kubwa katika TAA. Wakati TANU imeshachukua nafasi ya TAA, uongozi wa TAA Lindi haukutaka kufungua tawi la TANU. Mtu wa kwanza kuutanabaisha uongozi wa TAA mjini Lindi juu ya mageuzi yaliyokuwa yakitokea Tanganyika na kuanzishwa kwa chama kipya cha siasa mjini Dar es Salaam alikuwa Abdallah Juma Makopa, kijana kutoka Tanga akifanya kazi ya ukarani Posta ya Lindi. Makopa aliwaendea Mnonji na Waziri na kuwajulisha kuhusu kuanzishwa kwa TANUmjini Dar es Salaam na aliwashauri waanzishe TANU pale Lindi. Jambo hilo lilipingwa moja kwa moja na Mnonji, Waziri, Said Nassoro, Abdallah Mhuji na wanachama wengine wa TAA.

Chama cha Waafrika ambacho kilianzishwa siku nyingi mjini Lindi na kwa hakika ndicho kilikuwa chama cha pekee kushughulikia maslahi ya Waafrika sehemu za kusini kilikuwa African Welfrare Association ambacho mlezi wake alikuwa John Nevi, Mjaluo kutoka Kenya na katibu wake alikuwa Casian Njunde, Mngoni wa Songea. Makopa aliposhindwa kukishawishi kile kikundi cha wazee wa TAA aliwaendea Yusufu Chembera na Rashid Salum Mpunga. Chembera alikuwa na umri wa miaka thelathini na nne na Mpunga alikuwa kijana wa miaka ishirini na saba. Chambera alikuwa amesoma hadi shule ya msingi na Mpunga alikuwa amemaliza madras. Chembera alikuwa akifanya kazi katika kantini ya Lindi Welfare Centre, wakati Mpunga alikuwa dereva wa lori aliyeajiriwa na mfanyabishara wa Kihindi. Makopa aliwashauri Chembera na Mpunga juu ya uwezekano wa kuwahamasisha wananchi wawaunge mkono ili tawi la TANU lifunguliwe pale mjini. Aliwaambia alitaka sana kufanya hivyo yeye mwenyewe lakini asingeweza kwa sababu yeye alikuwa mtumishi wa serikali na hakuwa akifahamika sana mjini. Uongozi kama wao ndiyo ungeweza kuaminiwa na wananchi na usingetiliwa mashaka. Makopa, Chembera na Mpunga walikubaliana kuwa kabla ya kuanza kufanya kampeni waziwazi kwa ajili ya TANU, lazima wawaandikishe wanachama wachache kama waasisi wa chama. Mpunga na Chembera walimwandikisha kijana mmoja akiitwa Abdallah Faraj na katika muda mfupi waliweza kuwapata takriban wanachama 15  walioridhia kujiandikisha kama wanachama waasisi wa TANU.

Mwandishi Akiwasilisha Mada, ''Tanzania Nchi Isiyokuwa na Mashujaa,''
Nyuma Yake ni Picha Inayomuonyesha Dossa Aziz, Nyerere, Abdulwahid Sykes na Nangwanda  Lawi Sijaona

No comments: