BAKWATA
Sehemu ya Tano
Mkutano wa Taifa wa
Waislam, 1968
Hadi
kufikia juma la kwanza la mwezi wa Desemba, mikoa mitatu kati ya kumi na saba
ilikuwa tayari imeshajitenga kutoka EAMWS. Kile kikundi cha Adam Nasibu
kikaunda kamati kwa ushirikiano na Kamati ya Maulidi ya Dar es Salaam, Adam
Nasib akiwa katibu na Sheikh Abdallah Chaurembo mwenyekiti. Kamati hii
ikaitisha mkutano Ukumbi wa Arnatouglo tarehe 3 Desemba, 1968 kujadilia
ëmgogoroí. Aliyetumiwa kutoa tangazo lile alikuwa katibu wa Kamati ya Maulidi
na Swala ya Iddi, Y. Osman. Kundi la Adam Nasib lilikuwa na mchanganyiko wa
watu waliokuwa wanaungwa mkono na serikali Adam Nasib akiwa kiongozi,
halikadhalika kulikuwa na Waislam waliokuwa na nafasi katika TANU kama Sheikh
Abdallah Chaurembo na Juma Sued kiongozi wa TANU kutoka Bukoba. Ilikuwa wazi
kuwa serikali ilikuwa inamtayarisha Sheikh Abdallah Chaurembo kuchukua nafasi
ya mwalimu wake na mtu aliyemfikisha pale alipo, Sheikh Hassan bin Amir. Ikawa
sasa lazima Sheikh Hassan bin Amir aondolewe na kupelekwa Zanzibar ili lile
kundi la serikali chini ya Adam Nasibu liweze kuchukua uongozi wa Waislam bila
ya kipingamizi chochote.
Wakati
wa vurugu hizi Kamati Kuu ya TANU ilikuwa inafanya kikao chake Tanga. Sheikh
Kassim Juma, Adam Nasibu, Omari Muhaji,
Sheikh Abdallah Chaurembo na Saleh Masasi
walipanda ndege hadi Tanga kwenda kushauriana na Kamati Kuu ya TANU
jinsi ya kumaliza mgogoro wa Waislam.
Ujumbe huu ulikwenda Tanga kuonana na Nyerere huku ukiwa na orodha ya
Waislam ambao kile kikundi cha Adam Nasibu walikuwa wanataka serikali wakamatwe
na kutiwa kizuizini ili msuguano upate kumalizika. Dossa Aziz aliona Nyerere
akipewa karatasi wakati kikao kikiendelea lakini hakufahamu ujumbe uliokuwamo
ndani ya karatasi ile hadi hapo baadae. Alikuja kutambua habari za karatasi ile
baada ya majuma mawili kupita wakati alipofatwa na jamaa yake mmoja na kumuomba
aingilie kati ili rafiki yake (Ahmed Rashad Ali) aliyetiwa kizuizini na Nyerere aachiwe kutoka
Jela ya Ukonga. Nyerere alipofahamishwa habari zile na Dossa, alisema kuwa yeye
hakufahamu kuwa rafiki yake Dossa alikuwa katika orodha ile ambayo kwa umuhimu
wa jambo lile ilibidi aletewe Tanga wakati wa mkutano wa Kamati Kuu. Kwa kejeli
Nyerere akamwambia Dossa kuwa yeye huwa hachukuwi tabu ya kusoma majina ya watu
anaowaweka kizuizini kwa kuwa anawaamini wale wanaofanya kazi ya kumletea
majina yale.
Inspekta
Jenerali wa Polisi, Hamza Aziz, mdogo wake Dossa alipopokea amri kutoka kwa
rais kupitia Waziri wa Mambo ya Ndani kuwa amkamate Sheikh Hassan bin Amir, hakuweza
kuamini masikio yake. Alitaka afahamishwe sababu za kutaka kukamatwa Mufti, kiongozi wa juu kabisa katika safu ya uongozi wa Waislam katika Tanzania.
Alipoambiwa kuwa sababu ni kuwa anaihujumu serikali, Hamza Aziz alimwambia
Waziri wa Mambo ya Ndani kuwa huenda kuna makosa katika amri ile. Alimfahamisha
waziri kuwa yeye binafsi alikuwa anamfahamu mzee yule toka yeye Hamza alipokuwa
mtoto mdogo. Akimfahamu Sheikh Hassan bin Amir kama mwalimu na mtu aliyeshiriki
katika ukombozi wa Tanganyika. Msimamo
wake heshima na hadhi yake mbele ya Waislam ipo juu kabisa. Inspekta Jenerali
wa Polisi alimwambia waziri kuwa haitawezekana kwake yeye kutii amri ile kwa
sababu yeye haamini kuwa tuhuma zile dhidi ya Mufti Sheikh Hassan bin Amir ni
za kweli. Nyerere alifahamishwa na Waziri wa Mambo ya Ndani kuwa Inspekta
Generali wa Polisi, Hamza Aziz amekataa kutii amri yake ya kumkamata Mufti.
Nyerere alitoa amri kwa Usalama wa Taifa kumkamata Sheikh Hassan bin Amir. Hii
ilikuwa ni kinyume na utaratibu kwa kuwa Usalama wa Taifa hawana mamlaka ya
kukamata watu.
Usiku
wa manane siku hiyo hiyo Sheikh Hassan bin Amir alikamatwa na makachero wa
Usalama wa Taifa akapelekwa uwanja wa ndege na kurudishwa Zanzibar. Inaelekea kulikuwa na mpango uliokuwa
umetayarishwa kabla ya serikali ya Mapinduzi Zanzibar kumpokea Sheikh Hassan
bin Amir. Inasemekana mara kadhaa Karume alipata kumueleza Sheikh Hassan bin
Amir kuwa Nyerere alikuwa hamtaki nchini kwake na akawa anamshauri arudi
nyumbani Zanzibar. Sheikh Hassan alikataa ushauri ule hadi alipokamatwa na
kurudishwa kwa nguvu. Karume alimpa Sheikh Hassan bin Amir hadhi zote
alizostahili kama ulamaa na akamruhusu kuendesha madras. Lakini Zanzibar
ilikuwa imebadilika. Mapinduzi ya mwaka 1964 yalikuwa yameingiza katika
Zanzibar fikra potofu zilizokuwa zinapinga Uislam. Karume mwenyewe alikuwa
ametoa amri ya kuchoma vitabu vyote vya dini. Nakala za Qurían Tukufu
zilichomwa moto pamoja na taka za mji. Muslim Academy chuo kilichokuwa
kikisomesha masomo ya dini kilifungwa. Mashine za kuchapa kwa lugha ya Kiarabu
zikatupwa kutoka Government Press.
Maulama wengi na wanafunzi wa Sheikh Hassan bin Amir walikuwa wamekimbia
Zanzibar kwenda kuishi uhamishoni. Zanzibar haikuwa tena kitovu cha elimu na
maarifa ya Kiislam. Sheikh Hassan bin Amir akawa sasa mfungwa katika nchi yake
mwenyewe kwa kuwa hakuwa na ruhusa ya kuondoka visiwani hapo na kurejea
Tanzania Bara. Mara baada ya kukamatwa kwa Sheikh Hassan bin Amir, Adam Nasibu
akatangaza kufanyika kwa mkutano ambao ulikuja kujulikana kama Mkutano wa Waislam
wa Taifa. Mkutano ambao ilitangazwa utafanyika Iringa kuanzia tarehe 12-15
Desemba, 1968. Agenda kuu ya mkutano ule ilikuwa kujadili katiba kwa ajili ya
jumuiya mpya ya Waislam.
Baada
ya kukamatwa kwa Sheikh Hassan Bin Amir Tewa Said Tewa gazeti moja la
Kiingereza lilimfuata ili afanye mazungumzo nalo. Tewa alimfahamisha mwandishi
kuwa kulikuwa na hofu juu ya maendeleo yanayofanywa na Waislam na mikutano
mikubwa ya Waislam iliyokuwa ikifanyika nchi nzima. Waislam waliokuwa na vyeo
katika serikali walikataa kabisa
kuisaidia Tume ya Kikwima kwa njia yeyote wakidai kuwa kufanya hivyo ni
sawasawa na kuchanganya dini na siasa. Waislam hawa walikaa pembeni kama
watazamaji huku Nyerere kwa taratibu akivunja uongozi wa EAMWS na kutayarisha watu wake kuwaongoza Waislam.
Kundi la Adam Nasibu lilikataa kukutana na Tume ya Kwikima. Maulamaa wa Kiislam
ambao walikuwa na hadhi na uwezo wa kuleta sulhu katika sakata ile hawakuweza
kufanya hivyo kwa kuwa walikuwa wanajua fika kuwa aliyekuwa akivunja EAMWS
hakuwa Adam Nasibu, yeye na wenzake walikuwa wakitumiwa tu. Kundi la Adam
Nasibu lilikuwa halitaki chochote ila EAMWS ivunjwe na badala yake iundwe
jumuiya itakayokuwa chini ya kivuli cha serikali. Vilevile kukawa na uvumi kuwa Muislam yeyote
ambae atakaejejihusisha na shughuli za EAMWS atawekwa kizuizini na serekali.
Tume ya Kikwima haukuweza kupuuza vitisho hivyo kwa sababu serekali ilishawahi
kuwaweka vizuizini masheikh.
Tume
ya Kwikima ilikuwa inafahamu lile kundi la Adam Nasibu halikuwa na nguvu wala
uwezo wa kuivunja EAMWS. Kufuatia kutangazwa kwa mkutano wa Iringa wa kundi la
Adam Nasibu, Tume ya Kwikima ilitoa taarifa yake tarehe 11 Desemba ñ siku moja
kabla ya mkutano wa Iringa kuanza.
Taarifa ambayo ilitolewa kwa Waislam wote, iliitisha mkutano mkuu wa
EAMWS ambao ulikuwa ufanyike mwezi Februari mwaka unaofuata kujadili na kutoa
uamuzi wa mwisho kuhusu mgogoro.
Tarehe ya mkutano ilibadilishwa
hapo baadae na kuwa Januari kutokana na umuhimu wa mgogoro uliokuwa
ukikabili EAMWS. Gazeti la TANU baada ya kusoma taarifa ya Kwikima iliamua
kutoa maoni yake kuhusu taarifa ile kwa kusema kuwa haikuwa sawa. Huu ulikuwa
mpango uliosukwa mapema kuonyesha kuwa uongozi wa EAMWS ulikuwa na ubadhirifu.
Juma lile lile Aga Khan ambae ndiye aliyekuwa akishambuliwa na kundi la Adam
Nasibu, baada ya kutambua kuwa EAMWS isingeweza kamwe kuokolewa, akiwa Paris,
Ufaransa alijiuzulu nafasi yake kama patron wa EAMWS.
No comments:
Post a Comment