BAKWATA
Katika
hali ya kawaida, uongozi wa EAMWS pale makao makuu Dar es Salaam
ungelikasirishwa kidogo na kitendo cha Adam Nasibu cha ushabiki wa siasa.
Lakini uongozi wa EAMWS haukumuonya kiongozi wake wa Bukoba kuhusu jambo lile
ambalo dhahiri halikuwa la kupendeza katika jumuiya. Bila shaka uongozi wa
EAMWS ulichelea kuwa kwa kufanya hivyo wangelionekana si uzalendo, hasa
ukiichukulia jinsi wananchi walivyohamasika na Azimio la Arusha. Hata hivyo
Waislam siku zote ndiyo waliokuwa mbele katika kuongoza siasa. Makao Makuu
walibaki kimya kama vile hakuna kilichotokea. Funika kombe mwana haramu apite.
Tofauti
na mwaka wa 1963 wakati Nyerere alipojaribu kufanya mapinduzi dhidi ya uongozi
wa EAMWS, mwaka wa 1967 hali ya mambo yalikuwa yamebadilika sana yakimwendea
Nyerere vyema. Serikali ilikuwa imedhibiti vyombo vyote vya habari ukiondoa
gazeti la The Tanganyika Standard ambalo bado lilikuwa chini ya Lonrho. Nyerere
alikuwa amemuweka Martin Kiama kama mkurugenzi wa radio ya taifa, na Benjamin
Mkapa kama mhariri wa magazeti mawili ya
TANU, The Nationalist na Uhuru. Adam Nasibu aliandikwa katika magazeti na
habari zake kutangazwa katika radio kwa ajili ya kitendo chake, hasa kuhusu
yale maneno aliyosema kuwa ujamaa ni sawa na mafundisho ya Qurían. Katika hali
ya mambo kama yalivyokuwa wakati ule hasa jinsi uhasama ilivyokuwapo baina ya
serikali na Waislam, baadhi ya Waislam walimuona Adam Nasibu kama kibaraka
anaetafuta umaarufu wa bure kwa kujipendekeza kwa TANU, Nyerere na serikali
yake. Juu ya haya yote kile kitendo cha katibu wa Bukoba wa EAMWS kitakuja
kuwaathiri vibaya jumuiya hiyo na uongozi wake wote pamoja na Mufti Sheikh
Hassan Bin Amir.
Kwa
wengine Adam Nasibu alionekana kama mzalendo na Muislam mwenye ëuoni wa mbalií.
Kwa ajili hii basi serikali ikamuoana kama kiongozi wa baadae ambayo ingeweza
kumtegemea wakati wa shida. Uongozi wa EAMWS makao makuu ukaonekana haupo
pamoja na wananchi, wala haujali shida zao na uko mbali sana na sera za
serikali. Lakini kwa hakika EAMWS kama taasisi ya dini isingeliweza kujitokeza
na kuunga mkono Azimio la Arusha kwa kuwa hayo yalikuwa mambo ya siasa. Kwa
kufanya hivyo ingelikuwa inakwenda kinyume na msimamo wake wa kutojiingiza
katika siasa. Kwa zaidi ya robo karne toka iasisiwe EAMWS ilikuwa imejiweka
mbali sana na mambo ya siasa ikishughulika na masuala ya Uislam tu. Hata hivyo
kuwa nje ya Azimio la Arusha kukaonekana kama kitendo cha kukosa uzalendo na
kutoa picha kuwa jumuiya hiyo ilikuwa haijali maendeleo na ustawi wa watu wa
Tanzania. Mambo yakawa yamevurugika zaidi kwa kuwa rais wa EAMWS, Tewa Said na
makamo wake Bibi Titi Mohamed walikuwa katika baraza la mawaziri la Nyerere na
wakapoteza nyadhifa zao za ubunge katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1965. Kwa ajili hii basi serikali ikawa inaeneza
propaganda kuwa kwa kuwa Tewa na Bibi
Titi walikuwa katika uongozi wa juu wa EAMWS, walikuwa wanatumia nafasi zao
kujijengea himaya mpya kutoka kwa Waislam dhidi ya Nyerere. Viongozi hawa ikawa
lazima washughulikiwe na kuangamizwa. Mtu wa kufanya kazi hii hakuwa mwingine
ila Adam Nasibu katibu wa EAMWS Bukoba, mwalimu wa shule ya msingi ambae elimu
yake wala haikuwa kubwa. Adam Nasibu alikuwa tayari keshafanikiwa kufanya
mapinduzi dhidi ya rais wa EAMWS, Tewa Said Tewa. Kutokana na vitendo vyake
alikuwa ameidhihirishia serikali kuwa yeye angeweza kuwa mtumishi bora kwa dola
kuliko ule uongozi wa EAMWS uliokuwa pale makao makuu Dar es Salaam ambao
ulikuwa ukionekana umechoka.
Wakazi
wa Dar es Salaam kila mwaka walikuwa wakifanya maulidi katika viwanja vya Mnazi
Mmoja kuadhimisha kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW). Huu ndiyo toka asili
ulikuwa uwanja ambao TANU ilifanya mikutano yake yote wakati wa kupigani uhuru.
Mwezi Juni 1968 maulidi mbili katika usiku mmoja zilisomwa kuadhimisha kuzaliwa
kwa Mtume (SAW). Maulidi moja ilisomwa
Mnazi Mmoja na nyingine Ilala. Chanzo cha haya yote ni kuwepo kwa kutoelewana
kati ya viongozi wa Waislam waliokuwa wanajiona kuwa ni ëwazalendoí wafuasi wa
TANU na wale na wale viongozi wa EAMWS ambao kambi nyingine ilikuwa ikiwaona
kama wapinzani wa TANU. Yale maulidi yaliyosomwa Ilala yalihudhuriwa na
viongozi wa EAMWS na yalipata watu wengi na yakafana sana ukilinganisha na yale
maulidi ya Mnazi Mmoja, ya wafuasi wa TANU. Uongozi wa TANU ulitishika na hali hii
iliyokuwa ikijitokeza kwa maana ilikuwa inaonyesha kuwa chama kilikuwa
kinapoteza wafuasi ambao walikuwa wakijiunga na kambi ya Tewa na Titi iliyokuwa
ikisemekana ipo dhidi ya Nyerere.

No comments:
Post a Comment