Friday, 21 February 2014

Dossa ‘’The Bank’’ Aziz: Tajiri Aliyefilisika Kwa Kupigania Uhuru wa Tanganyika: Sehemu ya Kwanza



Dossa ‘’The Bank’’ Aziz:
Tajiri Aliyefilisika Kwa Kupigania Uhuru wa Tanganyika

Waasisi wa TANU, 1954

Kushoto Kwenda Kulia: Dossa Aziz, Abdulwahid Sykes
Kushoto Kwenda Kulia: John Rupia, Julius Nyerere



Dossa Aziz alipewa jina la ''Benki'' wakati wa harakati za kudai uhuru wa Tanganyika kwa sababu jambo lililokwama kwa ukosefu wa fedha lilitanzuka mara tu Dossa akifika. Waliomfahamu na kuishinae wanasema Dossa alikuwa mtu karimu sana... Jambo la kusikitisha sana ni kuwa katika maziko yake pale kaburini CCM hawakuwa wanajua waseme nini kuhusu Dossa kwa kuwa hawakuwa wanaijua historia ya kudai uhuru wa Tanganyika na aliyekuwa anaijua Nyerere hakuwepo mazikoni...

Utajiri wa Dossa ulitokana na nini?

Baba yake Dossa, Aziz Ali alipofariki mwaka 1951 alimwachia Dossa biashara ya ujenzi na malori saba ya kubeba mchanga na kokoto...

Mwaka wa 1951 wakati Dossa na wenzake wapo katika juhudi za kuipa uhai mpya TAA Dossa aliandikiwa barua na V.M. Nazerali aliyekuwa mjumbe wa Baraza la Kutunga Sheria akimuomba Dossa aunge mkono juhudi zake na za Ivor Byaldon na Brig. Scupham za kutaka kuunda chama cha siasa kitachowashirikisha watu wa rangi zote. Bayldon na Brig. Scupham walikuwa kama alivyokuwa Nazerali, wajumbe wa Baraza la Kutunga Sheria. 

Wanasiasa wengine walioombwa kuunga mkono juhudi hizi walikuwa Chifu Kidaha Makwaia, Liwali Yustino Mponda wa Newala, Dr. Joseph Mutahangarwa, Chifu Abdieli Shangali wa Machame, Chifu Thomas Marealle wa Marangu, Chifu Adam Sapi Mkwawa, Chifu Harun Msabila Lugusha, Dr. William Mwanjisi, Abdulkarim Karimjee, Dr. Vedas Kyaruzi, Liwali Juma Mwindadi, H.K.Viran, Stephen Mhando, Ally Sykes na Abdulwahid Sykes. Dossa na wenzake waliikataa ghilba hii kwa kuwa lengo lao lilikuwa ni kuanzisha chama cha siasa cha Waafrika wa Tanganyika kwa minajili ya kudai uhuru. 

Mwalimu Nyerere alipofika Dar es Salaam kwa mara ya kwanza mwaka wa 1952 kama mwalimu wa shule ya St. Francis' College, Pugu hakuna mtu aliyekuwa anamjua au kupata kusikia habari zake katika ulingo wa siasa. Kassela Bantu ambaye alikuwa akijuana na Nyerere kwa siku nyingi alimchukua Nyerere kwa Abdulwahid Sykes kumtambulisha. Wakati ule Abdulwahid alikuwa Rais wa TAA. Nyerere mara moja akajiunga na baraza la siasa lililokuwa likifanyika Mtaa wa Mbaruku nyumbani kwa Dossa. Ikawa kila Jumapili Nyerere anakuja kutoka Pugu kuja kumtembelea Dossa. Ilikuwa katika baraza hii ndipo Nyerere alipokutana na wanasiasa wengi wa wakati ule kama Ramadhani Mashado Plantan aliyekuwa anamiliki gazeti lililokuwa likijulikana kama Zuhra, John Rupia, Dunstan Omari, Zuberi Mtemvu na wanasiasa wengine. Fikra za Nyerere za kudai uhuru zilisikika kwa mara ya kwanza kupitia kalamu ya Mashado Plantan na gazeti lake la Zuhra lililokuwa likitoka kila siku ya Ijumaa. Fikra za Nyerere ziliingiza msisimko mpya katika baraza lile na haukuchukua muda mwaka 1953 uongozi wa ndani ukampendekeza agombee urais wa TAA.

Dossa anasema ingawa wao kwa kuwa karibu na Nyerere walikuwa wamekiona kipaji chake cha uongozi, wanachama wengi hawakumkubali mara moja na ndiyo maana katika uchaguzi wa TAA uliofanyika Arnautouglo Hall tarehe 17 Aprili, 1953 kati ya Abdulwahid aliyekuwa Rais na Nyerere aliyekuwa anagombea dhidi yake, Nyerere alishinda uchaguzi ule kwa taabu sana. Haukupita muda chama kikaanza kuzorota na mwisho kikafa. Dossa anakumbuka kuwa yeye alikuwa anawapitia viongozi kwenda kwenye mkutano. Akipiga honi ili mtu atoke waende mkutanoni kiongozi alimtuma mkewe atoke nje na aseme kuwa hakuwepo nyumbani. 

Dossa anasema ilikuwa baada ya kushauriana na Abdulwahid, Makamu Rais wa TAA ndipo lilipokuja wazo kuwa ni lazima wapate nguvu ya wazee wa Dar es Salaam ili kukifufua chama.Hivi ndivyo TAA katika miaka ya mwisho ya uhai wake ilipokuja kupata kuungwa mkono na wazee wa Dar es Salaam na kupelekea kuundwa kwa Baraza la Wazee wa TANU mwaka 1955 chini ya mwenyekiti wake Sheikh Suleiman Takadir. Nyerere amepata kusema kuwa alikuwa Dossa ndiye aliyemfahamisha aache kuvaa kaptula kwa kuwa sasa atakuwa akitoka mbele ya watu wazima na hiyo si adabu nzuri. 

Dossa alikuwa kati ya wale wazalendo watano, Abdulwahid Sykes, Ally Sykes, John Rupia na Julius Nyerere waliokutana ndani ya ofisi ya TAA new Street (sasa Lumumba Street) katika miezi ya mwisho ya 1953 na kwa pamoja wakapitisha azimio la siri la kuibadili TAA kuwa chama cha wazi cha siasa na kukipa chama hicho jukumu la kuiongoza Tanganyika katika kudai uhuru wake. Hili ndilo lililokuwa azimio la kwanza la busara katika historia ya Tanganyika. Azimio la pili la busara ni lile la Tabora la mwaka 1958. 

Tarehe 7 Julai, 1954 wazalendo hawa wafuatao wakakutana Dar es Salaam kubadili Katiba ya TAA ili kuanzisha chama cha TANU: Dossa Aziz, Abdulwahid na Ally Sykes, Tewa Said Tewa, Patrick Kunambi, Kasella Bantu, John Rupia, Julius Nyerere, C.O. Millinga,Germano Pacha, Joseph Kimalando, Japhet Kirilo; Abubakar Ilanga, L.M.Bugohe, Saadan Abdu Kandoro, S.M. Kitwana na L.M. Makaranga. Dossa Aziz kadi yake ya TANU ni namba 4 iliyotolewa na kusainiwa na Ally Sykes. Haukupita muda mrefu TANU ikampeleka Nyerere Umoja wa Mataifa. Tarehe 17 Februari, 1955 Nyerere aliondoka Dar es Salaam na kwenda New York kuhutubia Baraza la Udhamini la Umoja wa Mataifa na ndani ya mkoba wake hakuwa na hotuba nyingine ila yale mapendekezo aliyopewa Gavana Edward Twinning mwaka wa 1950 na uongozi wa TAA. Nyerere aliporudi nchini alikuta umati mkubwa wa wananchi unamsubiri uwanja wa ndege. Haikuwezekana kwake kutoka nje ya uwanja jinsi umati wa watu ulivyojazana kumlaki.. Walinzi wa kikoloni walimruhusu Dossa aingize gari yake hadi chini ya mlango wa ndege. Nyerere akashuka na kupokelewa na swahiba wake Dossa na akaingia ndani ya gari la Dossa. 

Siku ya pili ulifanyika mkutano mkubwa Mnazi Mmoja ambao gazeti la Zuhra lilikadiria kuwa zaidi ya watu 25,000 walihudhuria. Baada ya mapokezi na mkutano mkubwa, ukafanyika mkutano Mtaa wa Kipata na Sikukuu nyumbani kwa Clement Mohamed Mtamila mkutano ambao ulihudhuriwa na Titi Mohamed, Iddi Faiz Mwafongo, Tatu bint Mzee, Asha Ngoma, Mzee Haidari Mwinyimvua na Nyerere. Katika mkutano huo Nyerere aliwaambia wajumbe kuwa Father Walsh amemuambia ama achague siasa au aendelee kufundisha. Mkutano ukamshauri aache kufundisha ili awe Rais wa chama"Full time" ili kufanikisha wazo hili, Dossa Aziz alijitolea kumlipa mshahara hadi ushindi utakapopatikana. 

Ahadi hii aliitimiza. Hizi ndizo zilikuwa harakati za Dossa Aziz. Mzee Dossa akijibu hoja iliyokuwa ikipandikizwa kubadili historia ya kudai uhuru kuwa ati TAA kilikuwa chama cha starehe, Dossa alisema kuwa mtafiti yeyote anaesema kuwa TAA kilikuwa chama cha starehe na aende kwa Nyerere amuulize ikiwa mwaka 1953 alipojiiunga na chama alijiunga kwa minajili ya kujistarehesha au kwa ajili ya siasa. Mzee Dossa alieleza kuwa suala la kupotoshwa kwa historia ya Tanganyiika lilianza kujitokeza mara tu TANU ilipoanza kupata nguvu na viongozi wapya kuingia katika chama hasa baada ya Uchaguzi wa Kura Tatu mwaka 1958 na akasema kuwa hashangai kuwa leo kuna watu wanabeza juhudi zao na kudai kuwa siasa ilikuja na Nyerere kutoka Butiama.


Nyerere Akihutubia Mkutano wa Hadhara Viwanja Vya Jangwani

Habari za Chifu David Kidaha Makwaia zinapatikana hapo chini:
http://www.mohammedsaid.com/2013/12/chief-david-kidaha-makwaia-1922-2007.html

No comments: