TANU Ilivyovunja Ngome
ya Kanisa Katoliki Jimbo la Kusini, 1955
Sehemu ya Sita
Siku
iliyofuatia mkutano wa hadhara ulifanyika mjini Mikindani mahali palipojulikana
kama Jangwani, karibu na ufuko wa Bahari ya Hindi. Mkutano huu uliohudhuriwa na
watu wengi na uliendelea bila mushkeli wowote ukitoa kitendo kidogo
kilichofanywa na mwalimu mmoja wa shule, Abdulrahman Muhibu aliyekuwa amelewa.
Muhibu alikuwa ametoka kunywa pombe na alipita karibu na uwanja wa mkutano
ambapo Nyerere alikuwa akihutubia. Katika hali yake ya ulevi alimpigia kelele
Nyerere akamwita muongo. Huenda Muhibu alikuwa akifahamu vyema ujumbe wa Nyerere,
na akiwa vile alivyokuwa, mtumishi wa serikali na mlevi, aliona wazo la mwalimu
wa shule Mwafrika kama yeye kuwaongoza watu hadi uhuru upatikane ni jambo
lisilowezekana. Kwa haraka Muhibu alikamatwa na watu na ilikuwa karibu wamtie
adabu ndipo Nyerere alipoingilia na hivyo kumnusuru.
Jioni
hiyo baada ya mkutano Nyerere na ujumbe wake waliondoka kwenda Newala, kwenye
ngome ya Yustino Mponda. Mponda alikuwa mmoja wa wale wajumbe wa Baraza la
Kutunga Sheria waliosafirishwa na Gavana hadi Umoja wa Mataifa, New York,
kumpinga Nyerere. Sasa TANU ilikuwa ikichukua mkokoto wake wa kampeni hadi
ndani ya ardhi ya Mponda ambayo yeye alikuwa liwali na mjumbe wa Baraza la
Kutunga Sheria. Nyerere alipomaliza ziara yake ya Jimbo la Kusini, fikra za
Wakristo zilibadilika. Wakristo hawakuamini tena kuwa TANU ilikuwa harakati za
Waislam sawasawa na Vita Vya Maji Maji. Nyerere, Tambwe na Diwani walipokuwa
wanashika njia kurudi Dar es Salaam, matawi ya TANU yalikuwa yamefunguliwa
Masasi, Ndanda na Newala ambazo zilikuwa sehemu za Ukristo na ngome ya
Ukatoliki katika Tanganyika.
Nyerere
aliporudi Lindi mwaka 1959, TANU ilikuwa ina nguvu sana na ilikuwa imekumba
kila mtu. Wale watumishi wa serikali wengi wao wakiwa Wakristo, walio kuwa
wakiibeza TANU mwaka 1955 kwa sababu ilikuwa
ikiongozwa na Waislam ëwasiokuwa na elimu,í ukweli ulikuwa umewadhihirikia na
sasa walikuwa wakionyesha heshima kwa chama. Hawakuwa na khiyari na ilibidi
waonyeshe heshima kwa sababu bwana mwenyewe, yaani serikali ya kikoloni,
ilikuwa na heshima kwa TANU. Serikali ilikuwa imetambua kuwa dhamiri ya watu ya
kukataa kutawaliwa haiwezi tena kupuuzwa. Nyerere alikuwa amelihutubia Baraza
la Udhamini la Umoja wa Mataifa mara mbili, mara ya pili ikiwa mwaka 1957.
Ujumbe wa TANU ulikuwa wazi, watu wa Tanganyika walikuwa tayari kujitawala.
Kila siku zilivyopita ndivyo TANU ilivyopata nguvu. Rashidi Salum Mpunga,
dereva wa lori, aliweza kumshawishi na akafanikiwa kumuingiza TANU mmoja wa
masheikh wenye kuheshimiwa sana mjini Lindi na mshairi maarufu, Sheikh Mohamed
bin Yusuf Badi. Sheikh Badi alipoingia TANU kwa ajili ya heshima yake na
kukubalika na watu, idadi kubwa ya Waislam walimfuata na kukata kadi za TANU.
Nyerere alipokuja Lindi kujadili tatizo la kura tatu na uongozi wa Jimbo la
Kusini, Sheikh Yusufu Badi alimpokea Nyerere na madras yake, wanafunzi
wakimwimbia Nyerere kasda na kumpigia dufu. Kuanzia hapo sasa kila mtu
alijiunga na TANU. Si Mponda wala Kanisa lilikuwa na uwezo wa kupambana na TANU
kwa wakati ule. Polepole lakini na kwa kwa uhakika, TANU ilingia ndani ya
maeneo ya Kikristo huko Songea, Masasi, Tunduru na Newala, nyumbani kwa Yustino
Mponda.
Lakini
matukio mawili ya kumbukumbu kubwa yalikuwa katika safari ya pili ya Nyerere
alipozuru tena Jimbo la Kusini. Kumbukumbu ya kwanza ilikuwa tawaswil
aliyosomewa Nyerere na Sheikh Yusuf Badi mwenyewe pamoja na Waislam
aliowachagua yeye sheikh mwenyewe maalum kwa hafla hiyo, pamoja na
waliochaguliwa na masheikh wengine. Kumbukumbu ya pili ni ile karamu iliyoandaliwa kwa heshima ya Nyerere na Mussa
Athumani Lukundu, kiongozi wa Dockworkersí Union. Hii ilikuwa heshima kubwa
aliyoonyeshwa Nyerere, ilikuwa kilele cha upendo na heshima kwa Muislamu yoyote
anaweza kumfanyia asiyekuwa Muislamu.
Siku
ya ukumbusho mkubwa sana mjini Lindi ilikuwa siku ya uhuru, tarehe 9 Desemba,
1961. Sheikh Badi, bingwa wa mashairi, aliombwa na TANU kuandika hotuba ya
uhuru itakayotolewa na Yusuf Chembera mbele ya DC akiwa kama mwakilishi wa
utawala wa Kiingereza uliokuwa ukingíoka. Hotuba hiyo ya Sheikh Badi na
iliandikwa kwa Kiarabu na Chembera. Akiwa mtoto mdogo Chembera alipelekwa kwa
Sheikh Yusuf Badi na baba yake kwenda kusoma elimu ya dini na aliendelea kuwapo
hapo chuoni kwa Sheikh Badi hadi alipohitimu. Sheikh Badi hakuona kama ipo hotuba
yoyote iliyoandikwa na mwanadamu iliyostahiki hafla kama ile ya siku ya
kujikomboa kutoka minyororo ya ukoloni. Sheikh Badi alimsomea mwanafunzi wake
Chembera, dua ya kunut ambayo husomwa na Waislam katika kila sala ya alfajir.
Usiku wa manane wa tarehe 9 Desemba, 1961 ulikuwa usiku adhim sana kwa wote
wawili, mwalimu na mwanafunzi wake, pale watu walipokusanyika katika ule uwanja
wa gofu na kumsikiliza Chembera akisoma kunut kupokea uhuru wa Tanganyika.
Lakini mara tu baada ya uhuru Wakristo walianza kuuchimba ule waliouona kuwa
uongozi wa Waislam katika TANU kwa kisingizio kuwa uongozi ule haukuwa na
elimu. Suleiman Masudi Mnonji alikamatwa na kutiwa kizuizini kwa amri ya
Nyerere chini ya Preventive Detention Act ya mwaka 1962 kwa kile kilichoitwa ''kuchanganya
dini na siasa'' na Waislam wengine waanzilishi wa harakati za kudai uhuru
walitupwa nje ya uongozi.
Mwisho
No comments:
Post a Comment