Tarehe
27 Aprili, 1985 Julius Kambarage Nyerere, sasa akijulikana kama ''Baba wa Taifa,'' katika sherehe kubwa katika viwanja vya Ikulu, alitoa jumla ya medali 3979 kwa
Watanzania waliochangia katika maendeleo ya taifa. Kati ya wale ambao walipewa
medali hizo alikuwa Sheikh Abdallah Chaurembo. Wazalendo waliotajwa ndani ya
kitabu hiki ambao walipigania uhuru wa Tanganyika, hakuna hata mmoja wao
aliyekuwa katika orodha ile ya heshima. Baada ya siku chache kupita, Nyerere
kama mtu aliyegutuka alimualika Dossa Aziz Ikulu. Dossa Aziz, wakati wa kudai
uhuru wa Tanganyika alikuwa mtu maarufu, mwenye nafasi, na kujiweza sana. Sasa
Dossa baada ya miaka kupita hakuwa akifahamika tena na ule umaarufu na utajiri
wake ulikuwa umetoweka. Alikuwa akiishi maisha ya kawaida kijijini Mlandizi,
maili chache nje ya Dar es Salaam. Katika sherehe ya faragha Nyerere
alimtunukia medali Dossa Aziz, rafiki yake wa zamani.
Fuatilia historia ya Dossa Aziz
Tunatengeneza...
Dossa ‘’The Bank’’ Aziz: Tajiri Aliyefilisika Kwa Kupigania Uhuru wa Tanganyika: Sehemu ya Pili
Urafiki kati ya Dossa na Nyerere ulishamiri kwa
kipindi chote cha kudai uhuru na kuja kufifia mara tu uhuru ulipopatikana mwaka
1961. Sababu kubwa ya kukatika kwa urafiki wao ni kuwa kuanzia mwaka 1962 kwa
mara ya kwanza nchi ilianza kukumbwa na migogoro ya dini kati ya serikali na
Waislamu ambao walihisi kuwa Nyerere alikuwa akifanya njama za kuuhujumu
Uislamu kinyume na maadili na ahadi ya TANU. Mwaka wa 1963 Halmashauri Kuu ya
TANU ilivunja Baraza la Wazee wa TANU kwa kile kilichodaiwa kuchanganya dini na
siasa. Nyerere taratibu aliwahama marafiki zake na wahimili wake wa siku za
awali na akaanza kujenga nguvu mpya kutoka kwa wasio Waislamu kwa hofu ya kuwa
akiwa karibu na waasisi wa TANU ambao wengi wao walikuwa Waislamu
kungehatarisha nguvu zake na nguvu za Kanisa Katoliki. Kuanzia kipindi hiki
Nyerere akawa mbali na Dossa na rafiki zake Dossa.
Mwandishi wa makala hii alipomtembea Dossa Aziz
nyumbani kwake Aprili, 1987 ilikuwa asubuhi kiasi cha saa nne na alimkuta Mzee
Dossa amekaa barazani kwake akiwa amefungulia radio yake akisikiliza BBC. Mara
alipotambulishwa kwake alimpokea kwa ukarimu mkubwa. Ukarimu ulikuwa ndani ya
damu ya Dossa.
Mbele ya baraza yake yalikuwepo mabaki ya Landrover
ambayo Dossa alimfahamisha mwandishi kuwa gari ile aliitumia na Nyerere katika
safari za kutembelea majimbo ya Tanganyika kwa niaba ya TANU wakati wa kudai
uhuru. Mzee Dossa akionyesha kidole mabaki ya gari yake alisema, "Gari hii
imetembea sehemu nyingi sana nikimpeleka Nyerere sehemu tofauti za Tanganyika
na katika siku za mwanzo mimi mwenyewe ndiye nilikuwa nikiiendesha gari hii
hadi pale tulipomwajiri Said Kamtawa kama dereva wa TANU." Hata kwa wakati
ule Mzee Dossa alionyesha dalili zote za kupigwa na maisha. Katika picha ya
pamoja ya waasisi wa TANU kuna watu wawili tu ambao wanaonekana wamevaa suti na
tai, hao ni Abdulwahid Sykes na Dossa Aziz. Ishara tosha ya hadhi zao.
Waliobaki wote wamejivalia mavazi yao ya kawaida. Nyerere akiwa amevaa kaptula
na soksi ndefu zilizogota magotini, mavazi maarufu wakati ule kwa wasomi. Picha
hii imebeba maneno elfu moja. Dossa aliyeonekana pale kibarazani Mlandizi si
yule aliyekuwa kwenye picha ya waasisi wa TANU. Dossa mtanashati, mtoto wa Mwafrika
tajiri, Aziz Ali, Waziri Dossa Aziz aliyetoa mali kuipa TANU ili Nyerere
aitumie katika shughuli za kuikomboa nchi alikuwa amechoka akionyesha dalili
zote za kusahauliwa na nchi aliyoipigania ijitawale.
Tarehe 27 Aprili, 1985, Julius Kambarage Nyerere,
sasa akijulikana kwa jina jipya la ''Baba wa Taifa,'' katika viwanja vya Ikulu
alitoa jumla ya medali 3,979 kwa Watanzania walioiletea nchi hii maendeleo. Si
Dossa wala yeyote aliyetajwa katika kumbukumbu hii ya marehemu Dossa Aziz
alikuwa katika hao waliopata heshima hiyo. Lakini baadae kama mtu aliyegutushwa
Baba wa Taifa alimkaribisha Dossa Ikulu na kumpa medali katika sherehe fupi.
Kwa muda mrefu sasa kumekuwa na hofu kubwa sana ya
wale walioshika madaraka ya kuendesha serikali wakiogopa wananchi kuhusisha
uasisi wa TANU na nguvu za siasa za Waislamu walioishi miaka ile. Matokeo yake
ni kufutika kwa hisotoria ya wazalendo wengi waliojitolea maisha yao kuupigania
uhuru wa Tanganyika. Dossa Aziz ni kati ya wazalendo ambao historia imedhulumu
haki zao za kutambulika kama mashujaa wa uhuru wa Tanganyika. Kwa kipindi cha
zaidi ya miaka thelathini si CCM wala si rafiki yake mpenzi Julius Nyerere
alikuwa anafahamu Dossa anaishi vipi na ana hali gani. Rafiki zake wachache
waliokuwa wakimtembelea nyumbani kwake pale Mlandizi walihuzunishwa na hali
yake. Dossa mtu aliyekuwa na mali katika miaka ya 1950 alikuwa akiishi katika
hali ya ufukara. Hali hii ya ufukara ilitaka kumkosesha kuhudhuria Mkutano Mkuu
wa CCM mwaka1987 pale Kizota ambapo waasisi wote wa TANU walialikwa. Sababu
kubwa ilikuwa ni ukosefu wa nguo na viatu vya kuvaa katika hadhara kama hiyo.
Ilikuwa mmoja wa marafiki zake wa zamani Abbas Sykes ndiye
aliyemnunulia nguo na viatu vya kumwezesha kwenda Dodoma. Rafiki zake
walipomshauri aende kwa Nyerere ampatie msaada Dossa alijibu kuwa yeye hawezi
kulifanya hilo kwa kuwa Nyerere anajua kuwa yeye alitumia fedha zake nyingi
katika harakati za kudai uhuru na kama yeye Nyerere leo kamsahau yeye hana
sababu ya kumfuata. Jibu la Dossa lilikuwa jibu la muungwana, mtu asiyekubali
kujidhalilisha.
Kauli hii ya Dossa na msimamo
wake huu thabiti ulithibitishwa na Mwalimu Nyerere mwenyewe siku ya Jumapili
tarehe 19 Aprili 1998 katika khitma ya marehemu nyumbani kwa Dossa pale Mlandizi
wakati Nyerere aliposimama kusema machache katika hadhara ile kuhusu uhusiano
wake na Dossa na mchango mkubwa wa marehemu Dossa Aziz katika kuleta uhuru wa
Tanganyika. Nyerere alisema kuwa hata siku moja Dossa hakupata kumuomba kazi au
kuonyesha dalili za kutaka ukubwa. Mwalimu Nyerere aliposema maneno haya
alibubujikwa na machozi na waliokuwepo nao walilia kwa huzuni.Subira
aliyokuwanayo Dossa ndiyo sababu kubwa iliyomfanya astahamili dhiki kwa miaka
yake ya mwisho ya uhai wake na afe masikini katika hospitali ya Tumbi, Kibaha
badala ya St. Thomas Hospital, London, Dossa hakuwa wa kwanza kukutwa na haya.
Haya yalimkuta Mzee Mshume Kiyate, Sheikh Mohamed Ramia na wengine wengi. Baada
ya kuleta uhuru wazalendo hao wakageuzwa ganda la muwa. Hakuna unachoweza
kufanya na ganda la muwa ulilolifyonza ila kulitema tu na kama utaweza
kuelekeza mdomo wako kwenye jalala na kutembea humo hivyo ni bora zaidi kwani
hata kulitema ganda hilo kwenye mkono wako wa kushoto kisha kulitupa jalalani
ni kulipa hadhi ganda hilo. Habari za Dosa Aziz zinahitaji utafiti wa kina wa
msomi makini. Hii ni changa moto kwa wana historia, wana historia wa Tanzania
ya leo. Ni katika kuijua historia ya uhuru wa nchi hii ndipo wenye madaraka
hivi sasa wanaweza kujua kwa nini hii leo wajukuu wa akina Dossa wameiona
dhulma na wanapambana na polisi na askari wa kuzuia fujo kwa mawe kisha
wanachoma moto ofisi za CCM ambacho asili yake ni mababu zao.
Dossa Aziz na Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam
Ilikuwa
kawaida ya Dossa baada ya mikutano ya TANU pale Mnazi Mmoja kumchukua Nyerere
na gari lake kumrudisha Pugu. Njia ya zamani kwenda Pugu ilikuwa inapita hapo
kilipo Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam. Sasa ilikuwa kiza kimeingia na walitaka
kutoka nje ya gari kuangalia mandhari ya Dar es Salaam maana kutokea pale mji
ulikuwa unapendeza sana kwa taa zilizokuwa zikiwaka barabarani. Nyerere
alimwambia Dossa, “Dossa tukipata uhuru wetu hapa lazima tujenge chuo kikuu.”
Hili wazo lilifanyiwa kazi na wananchi wakahamasishwa kuchangia ujenzi wa Chuo
hicho. Fedha zilichangwa na Chuo kikajengwa pale New Street kwenye kiwanja cha
John Rupia alichokitoa kuwapa TANU. Hapo
ndipo kilipoanza Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam. (Chuo hiki sasa ni Chuo Cha Watu
Wazima). Abdallah Salum alikuwa mmoja wa wachangiaji wa chuo hicho na mwanae
Salum Matimbwa hadi leo amehifadhi stakabadhi ya malipo ya sh. 50.00 stakabadhi
ambayo ina sahihi ya Bhoke Munanka. Wazee hawa walikuwa wazalendo wa kweli kabisa. Baada ya uhuru kupatikana mwaka wa 1961 na
zilipokuwa zikianzishwa harakati za ushirika Abdallah Salum Matimbwa alitoa
lori lake Commer Fargo DSY 435 kama mtaji kuingiza katika Coast Region
Transport Company (CORETCO). Pamojanae katika kuanzisha CORETCO walikuwa wazee
wengine kama Sharia Bofu na nduguye Ibrahim Bofu, Salum Kambi, Juma Mzee na
wengineo.
No comments:
Post a Comment