| Kushoto Kwenda Kulia: Idd Faiz Mafongo, Sheikh Mohamed Ramia, Juliusa Nyerere, Saadan Abdu kandoro na Haruna Taratibu |
Huwezi
kuhadithia safari Nyerere Umoja wa Mataifa bila ya kueleza mchango wa Idd Faiz Mafongo katika kufanikisha safari ile. Kwa hakika na na katika mambo ya
kuhuzunisha sana kuwa wazalendo kama hawa leo hawatambuliwi wala juhudi
hazionekani kufanyika kuhifadhi historia zao. Kumbukumbu zinaonyesha kwamba Idd
Faiz Mafongo alihudhuria mkutano wa kwanza kabisa wa uzinduzi wa TANU uliofanyika
katika Ukumbi wa Arnautoglu. Waliohudhiria mkutano huu hawatimii watu ishirini.
Haifahamiki kwa hakika hasa ni lini Idd Faiz alijiunga na TANU kwa sababu kadi
yake ya kwanza ya uanachama ilipotea na akapewa kadi nyingine iliyokuwa na
namba 915 iliyotolewa tarehe 28 Agosti, 1954. Watoto wake kwa kuthamini mchango
wa baba yao katika kupigania uhuru wa Tangayika wamehifadhi nyaraka zake
mojawapo ni hii kadi yake ya TANU. Kwa kukisia tu kutokana na kadi ambayo Idd
Faiz mwenyewe aliitoa kwa kaka yake Idd Tosiri ambayo ilikuwa kadi namba 25 na
yenye saini yake kama afisa aliyetoa kadi hiyo, inaweza kuchukuliwa kwa uhakika
kuwa Idd Faiz alikuwa miongoni mwa wale watu wa mwanzo kabisa kuingia TANU.
Idd
Faiz na nduguye Idd Tosiri, muasisi wa Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika,
walikuwa Wakusu, moja ya makabila ya Kimanyema, kwa upande wa baba yao; na
Wabwali kwa upande wa mama yao. Wote wawili walikuwa katika Batetera Union
(Congo Association), chama kilichokuwa kikiwaunganisha Wamanyema wa Tanganyika.
Mzee bin Sudi alikuwa rais muasisi wa chama hicho na baada ya kifo chake Sheikh
Hussein Juma alichaguliwa kushika nafasi hiyo. Idd Faizi alikuwa mweka hazina
wa Al Jamiatul Islamiyya na vilevile mweka hazina wa TANU. Idd Faiz aliifanyia
kampeni TANU kuanzia siku ilipoanzishwa, akifuatana na Nyerere katika safari za
mwanzo kabisa za kukitangaza chama, akihutubia mikutano jukwaa moja na
Nyerere. Ilikuwa ni Idd Faiz na kaka
yake Idd Tosiri ndiyo waliompeleka na kumtambulisha Nyerere kwa binamu yao
Sheikh Mohamed Ramia wa Bagamoyo aliyekuwa khalifa wa Tarika ya Kadiria.
Ilikuwa ni baada ya utambulisho huu kwa Sheikh Ramia ndipo urafiki ukajengeka
kati ya Sheikh Ramia na Nyerere na TANU ikakubalika Bagamoyo.
Baraza
la Wazee TANU chini ya uenyekti wa Sheikh Suleiman Takadir ilichukua mafanikio
ya safari ya Nyerere Umoja wa Mataifa kuwa jukumu lao binafsi. Sehemu ya kwanza
ya maandalizi ilitakiwa ifanyike kwa siri sana. Uongozi wa TANU ulikambidhi Idd
Faiz kazi ya kuandaa, kukusanya na kusimamia mfuko wa safari ya rais wa TANU
kwenda Umoja wa Mataifa, New York. Safari ilikuwa ifanyike mwezi wa Februari, 1955.
Wanahistoria wazalendo na hata yeye mwenyewe Nyerere alikuwa akitoa picha kama
vile ile safari yeye aliipanga. Ukweli ni kuwa fikra ya kwenda Umoja wa Mataifa
ilikuwapo tola 1950 kabla hata Nyerere hajajulikana. TANU ilihitaji takriban shilingi
elfu kumi na mbili kumwezesha Nyerere kusafiri kwenda Umoja wa Mataifa, New
York. Kamati ya Abdu Kandoro, Japhet Kirilo na Abbas Sykes iliyokuwa
ikijishughulisha na mgogoro wa ardhi ya Wameru mwaka 1953 ilikuwa imekusanya
kiasi cha fedha kutoka majimboni kilitumika katika safari ya Ally na Phombeah
kwenda kwenye Pan African Congress mjini Lusaka. Kiasi cha fedha kilichobaki hakikutosha
kumpeleka Rais wa TANU, Nyerere Amerika. Ilibidi fedha za ziada zitafutwe
kutoka kwa wananchi ili kumwezesha Nyerere kufanya safari hiyo.
John
Rupia alichangia zaidi ya theluthi moja ya fedha zilizotakikana. Wanachama
wengine walichangia kwa uwezo wao wote lakini TANU katika siku zile ikiwa bado
changa ilikuwa maskini, kiasi hicho kilikuwa bado kiko nje ya uwezo wake. Ikitambua ule upungufu wa fedha za safari ya
Nyerere, Idd Faiz aliombwa na uongozi wa Al Jamiatul Islamiyya kutoa fedha
katika mfuko wa Al Jamiatul Islamiyya na kuzitia katika hazina ya TANU
kukiwezesha chama kumpeleka Nyerere Umoja wa Mataifa. Hata pamoja na fedha zile
kutoka Al Jamiatul Islamiyya hizo hazikuweza kukidhi haja. Al Jamiatul
Islamiyya haikuwa na jingine isipokuwa kumuomba Idd Faiz asafiri kwenda Tanga kutafuta
michango zaidi. Mwalimu Kihere alikusanya fedha na ikawa anasubiriwa mtu
akazichukue kuzipeleka makao makuu. TANU ilipata habari kwamba yeyote ambaye atakwenda
Tanga kuchukua fedha hizo kwa ajili ya safari ya Nyerere atakamatwa na
makachero wa serikali. Kabla ya kuondoka, Oscar Kambona, Katibu Mkuu wa TANU,
na John Rupia, Makamo wa Rais wa TANU, walikwenda kuonana na Idd Faiz nyumbani
kwake Ilala kumuaga, kumtakia safari njema na kumpa maelezo kwa ufupi. Safari
ya kwenda Tanga haikuwa na tatizo lolote, lakini katika wakati wa kurudi basi
ambalo Idd Faiz alikuwamo lilisimamishwa njiani Turiani na makachero. Idd Faiz
alikamatwa, akavuliwa nguo na kupekuliwa, lakini hakukutwa na fedha.
Hili
lilimshangaza na kumchanganya yule afisa aliyemkamata kwa sababu walikuwa na
taarifa kwamba Idd Faiz alikuwa amechukua fedha kutoka kwa Mwalimu Kihere kule
Tanga. Idd Faiz aliwekwa chini ya ulinzi na kupelekwa Dar es Salaam kwa usaili
zaidi wakati wote akiwa analindwa na askari wenye silaha. Wkati wote Idd Faiz
yeye alikataa akisema hajui chochote kuhusu fedha za TANU kutoka Tanga. Ilibidi
wamuachie huru kwa kuwa hakukuwa na ushahidi wowote wa kumtia hatiani. Wakati
Idd Faiz yuko mikononi mwa polisi fedha za safari ya Nyerere tayari zilikuwa zmeifika makao makuu
ya TANU Dar es Salaam, salama salimini. Idd Faiz hakuwa amezishika yeye zile
fedha. Zile fedha alikuwa amepewa msichana mdogo aliyekuwa abiria ndani ya basi
lile alimokuwa Idd Faiz.
Mnamo tarehe 17 Februari, 1955 Nyerere aliondoka kwenda New York kuhutubia Baraza la Udhamini la Umoja wa Mataifa. Nyerere aliiweka wazi nia ya TANU kuwa alikuwa ametumwa na wananchi wa Tanganyika kuwasilisha ujumbe ufuatao kuwa “Kuona kanuni ya uchaguzi ikianzishwa na Waafrika kujiwakilisha katika taasisi zote za umma... Hii tunaamini, ni kwa mujibu wa masharti ya Makubaliano ya Udhamini na Ibara ya 76 ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa.” Mbele ya Umoja wa Mataifa, TANU haikuwa ikidhihirisha tamko lolote jipya, yale yote yaliyowasilishwa pale yalikuwa ni maoni ya kamati ndogo ya siasa ya TAA yaliyowakilishwa kwa Constitutional Development Committee ya Gavana Edward Twining mwaka wa 1950. Mapendekezo ya TAA ambayo Gavana Twining aliyapuuza. Badala yake aliendelea na mipango yake ya kuwa na wawakilishi wa rangi zote katika Baraza la Kutunga Sheria. Wakoloni hawakukubali kushindwa kirahis serikali ilituma ujumbe wake Umoja wa Mataifa kuipinga TANU uliowakilishwa na I. C. Chopra, Mwasia; Sir Charles Phillips, Mzungu na Liwali Yustino Mponda, mjumbe wa Baraza la Kutunga Sheria kutoka Newala. Inastaajabisha sana leo kusikia wanasiasa wakizikebehi juhudi za akina Abdulwahid Sykes kuwa ati walikuwa wakiendesha chama cha starehe. Sawa TAA na tujaalie kilikuwa chama cha starehe, nayo Jamiatul Ilsamiyya fi Tanganyika nayo kilikuwa chama cha starehe?
Nyerere
alirudi kutoka New York Jumamosi, tarehe 19 Machi, 1955 na alipokelewa uwanja
wa ndege na halaiki ya watu. Dossa Aziz anakumbuka kuwa aliruhusiwa pale uwanja
wa ndege kuingiza gari yake hadi ndani ya uwanja chini ya ndege hadi chini ya
ngazi ili kumrahisishia Nyerere kuingia ndani ya gari na kuepuka msongamano wa
watu. Dossa Aziz anasema kama isingekuwa kwa msaada huo Nyerere angesongwa sana
na watu na ingekuwa kazi kubwa kumtoa pale. Watu walikuwa kila mahali
wakisukumana na kusongamana wakijaribu angalau kumtia Nyerere machoni. Watu
walikuwa wakiimba na kucheza mganda, ngoma ya Kizaramo, wakiimba “Baba Kabwela
Yuno.” Maana yake “Baba karudi kutoka UNO.” Jambo la kushangaza ni kwamba
hakuna mtu aliyewahi kuusikia wimbo huu kabla ya siku ile na hakuna ajuaye lini
ulitungwa. Ile gari ya Dossa Aziz aliyopanda Nyerere ilisukumwa kutoka uwanja
wa ndege hadi nyumbani kwa Nyerere, Magomeni Majumba Sita, kiasi cha kama
kilomita ishirini. Siku iliyofuata ilikuwa Jumapili. TANU ilifanya mkutano wa
hadhara Mnazi Mmoja ambao ulihudhuriwa na umati ambao kamwe haukupata kuonekana
Dar es Salaam.
Inakisiwa
zaidi ya watu 40,000 walikuja kutoka kila upande wa mji kumsikiliza Nyerere.
Hakuna mtu aliyekuwa na raha ya kuandika kuhusu mkutano ule na safari ya
kihistoria ya Nyerere kwenda Umoja wa Mataifa kuliko Mashado Plantan katika
gazeti lake Zuhra. Mtambo wa gazeti wa Mashado uliokuwa Mtaa wa Ndanda, Mission
Quarters ulichapisha nakala za ziada za gazeti hilo na toleo lote liliuzika. Mikutano
ya TANU ya siku za mwanzo ilikuwa ikifanyika kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja
mbele ya Princess Hotel. Kwenye jukwaa lililojengwa kwa miti walikuwa wakikaa
wale viongozi wa mstari wa mbele ndani ya TANU - Nyerere rais wa TANU, Sheikh
Suleiman Takadir, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa TANU, Bibi Titi Mohamed,
John Rupia na Clement Mtamila. Sahani ya santuri ilikuwa ikipigwa katika
gramafoni kupitia kipaaza sauti kuvutia watu kuja mkutanoni. Mwimbo uliokuwa
ukipigwa ulikuwa wa Frank Humplink. Frank alikuwa kijana wa Kichagga kutoka
Moshi. Baba yake alikuwa Mzungu.
Hamplink alikuwa mwimbaji na mpiga gitaa maarufu sana wakati ule akipiga muziki
wake na dada zake wawili Maria na Regina Humplink. Wimbo uliopendwa sana na
TANU na ndiyo uliokuwa ukipigwa katika mikutano yake yote na uliosisimua
wananchi ulikuwa na mashairi yafuatayo:
Uganda
nayo iende,
Tanganyika
ikichangamka,
Kenya
na Nyasa zitaumana.
| Frank Humplink |
Mwimbo
huu ulikuwa na ujumbe wa kisiasa kwa Waafrika wa Tanganyika. Ujumbe katika
wimbo huo ulikuwa kuwa, Tanganyika itakapoamka, kutakuwa vilevile na mapambano
nchini Uganda, Kenya na Nyasaland. Wimbo huu ulikuwa ukivuma toka kwenye vipaza
sauti mfululizo kabla ya mkutano huku watu wakikusanyika viwanjani. Haikupita
muda mrefu serikali ya kikoloni ilipata maana halisi ya wimbo huo. Mara moja
mwimbo huo ukapigwa marufuku na serikali hauruhusiwi tena kupigwa Sauti ya Dar
es Salaam. Serikali ya kikoloni iliamuru kwamba mashairi ya wimbo huo yalikuwa yakiwashawishi
watu kuasi. Lakini kabla ya wimbo huo kupigwa marufuku ulipendwa sana na
ulikuwa ukiombwa na wasikilizaji na kupigwa katika Sauti ya Dar es Salaam.
Baada ya amri ya serikali kutoka kituo hicho kiliacha kabisa kupiga wimbo
huo. Huenda huu ulikuwa wimbo wa kwanza
kupigwa marufuku katika lllivcrxsz;’zxf-f-asmi wa TANU. Inaelekea uzalendo na
shauku ya uhuru ndiyo vitu vilivyomtia hamasa Humplink hata akatunga na kuuimba
wimbo huo.
Miaka
mingi baadae mwandishi wa makala haya akizungumza na Mzee Humplink nyumbani
kwake Lishoto alisema kuwa hakusalimika, alikamatwa Moshi na kuwekwa ndani hadi
alipotolewa kwa msaada wa Chifu Thomas Marealle aliyewaambia wakoloni kuwa
Frank alikuwa kijana akipiga muziki tu wala hakuwa na lolote nje ya hilo.
Askari wa kikoloni wakaingia nyumba hadi nyumba wakiisaka ile santuri ya Frank
na ilipopatikana ilivunjwa hapo hapo. Katika mikutano ya TANU katika zile siku
za mwanzo, kabla Nyerere au Bibi Titi kuhutubia umma, Sheikh Suleiman Takadir
alikuwa akisimama na kuomba dua kisha kumtambulisha Nyerere kwa wananchi.
| Chief Thomas Itosi Marealle |
Baada ya hapo atasimama Bibi Titi kuhutubia na mwisho atapanda Nyerere. Bibi Titi alikuwa akijulikana kwa maneno yake makali wakati Nyerere alikuwa bingwa wa fikra tulivu na utoaji wa ujumbe mzito. Sheikh Suleiman Takadir mwenyewe, vilevile alikuwa msemaji mzuri sana. Ilikuwa kwa sababu hii na umri wake mkubwa ndiyo alipewa heshima na wazee wa mji ya kuzungumza kwanza kabla ya yoyote hajasema. Katikati ya hotuba na mwanzo na mwisho wa mkutano vijana wa Bantu Group kama akina Hamis Bakas, Juma Mlevi, Rajab Sisson na wenzake walikuwa wakichangamsha kwa vibweka vyao vya kila aina huku wakiungwa mkono na nyimbo za lelemama za akina Bi. Hawa bint Maftah, Tatu bint Mzee, akina bint Chanzi. Hawa Bantu Group ndiyo walikuwa wakitoa ulinzi kwa Nyerere wakiwa wamevaa majani na huku wameshika pinde, vishoka na silaha nyingine za kijadi. Bantu Group walichangamsha sana mikutano ya TANU.
| Mwandishi na Mzee Frank Humplink Nyumbani Kwake Lushoto |
Hotuba
aliyotoa Nyerere siku ile pale Mnazi Mmoja kama taarifa yake ya safari ya Umoja
wa Mataifa ilikuwa ya kusisimua. Hapa ndipo hasa ndiyo mwanzo wa historia mpya
ya Tanganyika. Kabla ya hapo Waafrika wa Tanganyika hawakupata kuonyesha shauku
na matumaini katika mustakbali wao kwa kiwango kile. Katika viwanja vya Mnazi
Mmoja Nyerere aliwaeleza halaiki ya watu wenye furaha na waliokuwa
wakimsikiliza kwa makini kuwa miongoni mwa mataifa kumi na mbili yanayounda
Baraza la Udhamini saba kati yao yalitoa idhini kuwa muda wa utawala wa ndani
wa Tanganyika utakapowadia, Waafrika wa Tanganyika lazima wapewe nchi yao.
Katika hotuba yake Nyerere alitilia mkazo sera ya TANU kuhusu mahusiano mema
baina ya Waafrika na watu wa mataifa mengine na aliwaonya wanachama wa TANU
ambao walikuwa wameanza kuwabagua watu wa rangi tofauti kuwaambia kuwa hivyo
haikuwa sawa. Alisisitiza juu ya umoja miongoni mwa wananachi na hatimaye
aliwadhihaki wasikilizaji kwa kuwauliza ikiwa wangesubiri kwa miaka ishirini na
tano kuwa huru. Halaiki hiyo ya watu kwa pamoja ilipiga kelele, “Hapana.”
Wananachi kwa pamoja walijibu kwa sauti kubwa wakisema walitaka uhuru kesho au
kesho kutwa.
![]() |
| Kushoto Kwenda Kulia: Sheikh Suleiman Takadir, Mbuta Milando, John Rupia na Julius Nyerere Wamezungukwa na Bantu Group |
Nyerere
ambaye alikuwa akiogopa kuchukua uongozi wa TANU tangu 1953 alikuwa amefarajika
sana na mshikamano huu ulioonyeshwa na wananchi. Sasa ilikuwa dhahiri kwake
kwamba rafiki yake Abdulwahid, Ally, Dossa Aziz, Rupia na uongozi mzima wa TANU
pamoja na lile Baraza la Wazee wa TANU lilikuwa limemsafishia njia kuongoza
harakati kwa niaba yao. Lakini Padri Walsh na Wamishionari katika shule ya
Mtakatifu Francis, Pugu, walitazama harakati hizi kwa mtazamo mwingine kabisa.
Wamishionari hawakuweza tena kumvumilia Nyerere kuwa mmoja wa walimu katika
shule yao. Hatima ile ile iliyowasibu wazalendo wengine kabla yake sasa
ilimkabili Nyerere. Aliambiwa ama abakie mtumishi mtiifu wa Kanisa au ajiuzulu;
Kanisa halikuweza kukaa kimya na kumuangalia Nyerere akiwatumikia mabwana
wawili. Nyerere alilipeleka tatizo hili kwa Clement Mtamila, Mwenyekiti wa
Kamati Kuu ya TANU. Mtamila aliitisha mkutano wa kamati kuu nyumbani kwake mtaa
wa Kipata na TANU ilijadili tatizo hilo. Tarehe 23 Machi, 1955 Nyerere
alijiuzulu ualimu.
![]() |
| Nyerere Akihutubia Mkutano Viwanja Vya Jangwani |


No comments:
Post a Comment