TANU Ilivyovunja Ngome
ya Kanisa Katoliki Jimbo la Kusini, 1955
Sehemu ya Nne
DC
mkoloni alikataa kutoa kibali kwa TANU kufanya mkutano wa hadhara. Akiwa
amekasirika sana, Shabaan Msangi aliitisha mkutano wa dharura wa tawi
uliohudhuriwa na Nyerere na Tambwe. Baada ya mkutano huo Tambwe alikwenda
kumwona DC. Ruhusa ilitolewa, na adhuhuri hiyo siku ya Jumapili, katika kiwanja
ambacho Wazungu walikuwa wakicheza gofu, ambako mwaka mmoja uliopita Gavana
Edward Francis Twining alitoa hotuba iliyowavunja moyo Waafrika, Nyerere
alihutubia mkutano wa hadhara. Kamwe haijapata kutokea kabla ya siku ile katika
historia nzima ya Jimbo la Kusini, watu wengi kiasi hicho kujumuika mahali
pamoja. Wazungu na Wahindi pamoja na askari, watu wakiwa wamekaa na wengine
wamesimama katika ya jua kali walikuja
kumsikiliza Nyerere akihutubia. Ili kuhakikisha amani na usalama pale mkutanoni
serikali iliweka askari waliouzunguka uwanja mzima wa mkutano. Nyerere
aliwafikishia watu ule ujumbe wa TANU wa kuwa, kutawaliwa ni fedheha, na
Waafrika wa Tanganyika lazima wadai uhuru wao. Uingereza ilikuwa ikiitawala
Tanganyika chini ya udhamini kwa niaba ya Umoja wa Mataifa, na wakati ukiwa
muafaka inabidi Uingereza ikabidhi nchi kwa wananchi wenyewe. TANU ilikuwa
imewasili Jimbo la Kusini.
Tangu
mwaka 1954 tetesi za chama cha siasa kilichoanzishwa Dar es Salaam kupigania
uhuru zilikuwa zimepenya na kufika Mikindani, mji mdogo kusini mwa Lindi. Huko
Mikindani kama ilivyokuwa mjini Lindi, harakati za utaifa zilianzia kwa wakazi
wa mjini, Wamakonde wengi wao wakiwa Waislam. Kinyume na imani ya watu wengi
kuwa Wamakonde ni wapagani, Wamakonde pekee waliokuwa si Waislam walikuwa wale
waliokuja kutoka Msumbiji, koloni la Wareno. Hawa ni Wamakonde waliovuka mto
Ruvuma kuingia Tanganyika kutafuta kazi katika mashamba ya mkonge kama manamba.
Uislamu ulikuwa umeimarika Kilwa na sehemu nyingine za pwani kwa zaidi ya miaka
elfu moja. Wamakonde wasio Waislam wanaweza kutambulika kwa chale
walizochanja katika nyuso zao na ndonya
kwa wanawake wao. Wamakonde wa Tanganyika kutoka Lindi, Mikindani na Mtwara
katika mwambao wa ukanda wa pwani wa kusini ni kabila la Waislam wengi.
Wamakonde Wakristo wanatoka katika maeneo yanayozunguka Masasi ambayo hadi sasa
ni eneo la Wamishonari. Wamishonari wa UMCA waliingia Masasi, nchi inayokaliwa
na Wamakua na Wamakonde katika mwaka 1876.
Mikindani
haikuwa kama Lindi. Lindi ilikuwa kituo cha biashara na utawala wa kikoloni
katika Jimbo la Kusini. Lindi ilikuwa na uwanja wa gofu, sinema na kilabu
mahususi kwa Wazungu ambayo hakuna Mwafrika au Mhindi aliyekanyaga hapo bila
sababu ya maana. Lindi ilikuwa na barabara za lami na mitaa yake iliwashwa taa
usiku kuondoa giza. Kadhalika mji ulikuwa na idadi ya kutosha ya Waafrika
waliokuwa katika utumishi wa serikali. Wakati huo Lindi ilikuwa manispaa iliyokuwa
ikikua na yenye shughuli nyingi. Ikilinganishwa na Lindi Mikindani ilikuwa
kijiji kikubwa cha uvuvi kisichokuwa na mambo ya mjini na wakazi wake bado
walitumia taa za kandili. Si watu wengi waliokuwa wakihamia Mikindani kutoka
sehemu nyingine kuja kutafuta kazi. Uhamiaji wa watu kutoka sehemu
nyingine kuja mjini Mikindani ulikuwa
katika kiwango cha chini sana. Watu pekee waliokuja Mikindani walikuwa
Wamakonde kutoka Newala na Masasi ndani ya Tanganyika na wale kutoka upande wa
pili wa mpaka toka Msumbiji. Hawa walikuja kufanya kazi katika mashamba ya
mkonge yaliyokuwa yakimilikiwa na ukoo wa Karimjee. Hawa Wamakonde wahamiaji
walikuwa wakidharauliwa na wenyeji na kwa ajili hii Wamakonde wakiwa hawana
dini walijitenga na wenyeji. Hakukuwa na maingiliano baina ya Wamakonde kutoka
koloni la Wareno la Msumbiji na Wamakonde Waislam wa Tanganyika. Wakiwa mbali
na nyumbani ambako maisha chiini ya Wareno yalikuwa magumu sana hawa
Wamakonde waliangukia chini ya ulezi wa Kanisa.
Ili
kuepuka mgongano na Waislam wamishonari walikuwa wamejenga kanisa kubwa sana
juu ya kilele cha mlima maili chache toka Mikindani sehemu moja ikijulikana
kama Mchuchu. Karibu na kanisa walikuwa
wamejenga shule ambayo Alfred Omari alikuwa akifundisha. Baba yake Alfred
alikuwa Mmakua Muislam lakini mwanae alibatizwa kwa ajili ya kupata elimu.
Inasemekana Mwafrika wa kwanza kusoma shule ya misheni kule kusini alikuwa
Charles Suleiman. Huyu alikuwa kijana wa Kiislamu aliyebatizwa na wamishonari.
Alikuja kuwa Mwafrika wa kwanza kufuzu ualimu katika miaka ya mwishoni ya 1800.
Mbali
na changamoto hii kwa Uislamu kutoka kwa wamishonari, Mikindani ilibakia kuwa
chemchemu ya elimu ya Kiislamu. Mikindani ilijivunia mchanganyiko wa wanachuoni
wenye sifa kubwa ndani na nje ya Tanganyika. Elimu ya dini ya Kiislamu
ilifundishwa Mikindani na Sheikh
Suleiman bin Said na mdogo wake Ali, Wagunya kutoka Mombasa; Kenya; Sheikh
Saleh Maondoa kutoka visiwa vya Comoro; Sheikh Hassan bin Hassan Mchendange,
Mmakonde kutoka Mikindani; Sheikh Ahmed Mohamed Ghazal, Mwarabu kutoka Mombasa;
Sheikh Abdallah wa Mwalimu; Mohamed bin Abdallah na Sheikh Fumai bin Silim,
Mmakonde wa Mikindani. Kutokana na hawa usufi uliota mizizi na tariqa za
Kadiria na Shadhly zilidumu katika sehemu zote za Waislam huko kusini. Kadiri
miaka ilivyopita wenyeji wa sehemu zile za kusini, Wamakonde, nao wakaipata
elimu hii ya Kiislam kutoka kwa wageni na mabadiliko haya yalikuja kukutana na
kuibuka kwa harakati za kudai uhuru mara baada ya vita kuu ya pili.
Wanachuoni
wa Kiislamu mjini Mikindani hawakuwa wakipendeza machoni mwa Waingereza kama
vile walivyokuwa hawapendezi kwa Wajerumani. Mbali na chuki dhidi ya utawala wa
kikoloni kufuatia Vita Vya Maji Maji, Waislam walikuwa na chuki zao binafsi
dhidi ya Waingereza kutokana na amri waliyotoa ya kumfukuza mwanachuoni
mashuhuri wa Kiislamu, Sheikh Abdallah wa Mwalimu. Sheikh Abdallah aligombana
na Waingereza juu ya jambo la akida na uadilifu. Sheikh Abdallah alikuwa liwali akihukumu kwa mujibu wa sharia
za Kiislam pale Mikindani. Katika wadhifa huu, afisa wa kikoloni aliamuamuru
kutekeleza wajibu ambao Sheikh Abdallah aliuchukulia kuwa ulimvunjia hadhi
yake, heshima na itibari kwa Uislamu. Sheikh Abdallah, kutokana na ugomvi huu,
alihamishiwa Kondoa Irangi, sehemu yenye Waislam watupu katika Tanganyika,
jimbo la kati. Sheikh Abdallah aliishi Kondo Irangi katika miaka yake ya mwisho
na kufariki huko. Waislam mjini Mikindani hawakuweza kuwasamehe Waingereza wala
kusahau ule udhalimu dhidi ya Sheikh Abdallah. Mwanae, Sheikh Mohamed bin
Abdallah wa Mwalimu aliitwa kutoka Lindi kuja kuongoza Tariqa ya Kadiria mjini
Mikindani baada ya kifo cha baba yake. Mohamed bin Abdallah, alisoma elimu ya
Kiislamu mjini Kondoa. Mjini Lindi alianzisha zawiyya, akahuisha Tariqa ya
Kadiria na akawa na madras yake mwenyewe. Alipofariki Sheikh Suleiman bin Said
na mdogo wake, Mikindani, nyumbani kwa Sheikh Abdallah wa Mwalimu kukawa hakuma
khalifa wa kuongoza tariqa. Hatua ya Sheikh Mohamed kuja Mikindani ilisadifiana
na kuibuka kwa TANU. Sheikh Mohamed akiwa khalifa wa Kadiria na murid wake
ndiyo walikuwa watu wa kwanza kujiunga na TANU pale Mikindani.
1 comment:
Tunaelezwa na wazee pale UHURU ulipopatikana katika Mikutano ya hadhara khasa DaresSalaam waliokuwa wakihudhuria kwa wingi walikuwa ni Waislamu. Nyeyere akitamka mambo ambayo yakiwagusa Waislamu wakisema, Pasuaaaaaaaaa! Siku Nyerere akasema "Ikija kuchanika asilie mtu, " Taib, iliwachanikia Waislamu kuanza kupigwa pande na mwisho kutumiliwa Waislamu wenzao kuiua EAMWS.
Mie lakini nitaitumia Pasuuuuuuuu, kwa kwetu hapa Visiwani, anapoelezea kitu mtu, kikakuna na ikiwa sehemu ya kurusha madongo, hunena, Pasuaaaa.
Ben Riajl
Post a Comment