Monday, 5 May 2014

KIFO CHA SHEIKH ILUNGA HASSAN KAPUNGU NI MSIBA KWA VIJANA

Sheikh Ilunga Hassan Kapungu 1988

Nyuma  Wapili Bakari Saleh Mwisho Kulia Ilunga  Hassan Kapungu
Mstari wa Mbele Watatu Kutoka Kushoto Mwandishi
Hawa ni Baadhi ya Vijana wa Kiislam Waliohudhuria Semina Dodoma
Chuo Cha Biashara 1988

Sheikh Ilunga Hassan Kapungu kaingia katika historia ya Dar es Salaam katika kifo chake. Bahari ya watu waliojazana Msikiti wa Kichangani kuja kuswalia jeneza lake na kisha kulifata nyuma jeneza hilo hadi Makaburi ya Mwinyimkuu, Magomeni Mapipa haijapatapo kuonekana. Sheikh Ilunga ni ''mgeni'' katika mji wa Dar es Salaam kwa maana ya kuwa hakuzaliwa Dar es Salaam wala hakuwahi kuishi Dar es Salaam wala hakuweza kujinasibu kwa lolote au chochote katika mji wa Dar es Salaam. Alikuwa akija na kuondoka zamani akirejea kwao Tabora na baadae baada ya kuhamia Mwanza, akija Dar es Salaam na kurejea Mwanza. Iweje leo mji mzima wa Dar es Salaam usimame na utoke kuja kumzika Sheikh Ilunga Hassan Kapungu? Hakika hili ni swali linalotaka majibu ya kuridhisha. Jibu ni dogo na rahisi sana. Hivi ndivyo Waislam wanavyofanya dunia nzima kila wanapofiwa na kipenzi chao. Labda linaweza kuja swali jingine, ''kipenzi?'' Sheikh Ilunga kawaje kuwa kipenzi cha Waislam? Naam Sheikh Ilunga Hassan Kapungu juu ya udogo wake wa umri alikuwa kipenzi cha Waislam na si Waislam wa Dar es Salaam peke yao. Sheikh Ilunga alikuwa kipenzi cha Waislam wa Tanzania nzima. Kibla cha kila msikiti wa Waislam katika Tanzania kilikuwa kinamkaribisha kama si kuwaidhi basi angalau asimame awasalimie nduguze Waislam. Sheikh Ilunga alipendwa na umma hakuwa katika lile kundi la mesheikh wanaoogopa kuswali katika baadhi ya misikiti au hata kupita nje yake. Sheikh Ilunga hakuwa katika lile kundi la masheikh wenyeji katika futari za serikali na''misikiti ya wakubwa'' lakini wageni katika misikiti ya ndugu zao Waislam, Manzese au Tandale. Kubwa Sheikh Ilunga hakukosa usingizi wala kujiona duni kwa kukosa kualikwa futari Ikulu au kualikwa katika dhifa za kitaifa akapigwa picha kavaa kanzu za kupendeza kakaa na waheshimiwa na kutokea katika runinga na magazeti siku ya pili ukurasa wa mbele. Sheikh Ilunga Hassan Kapungu hakushughuliswa na hayo. Yeye alishughulishwa na kuliweka juu jina la Allah Subhana Wataala. Hili ndilo lililokuwa likimshughulisha mpaka siku Allah alipomuhitimisha.

Ilunga katika Madras yake Mwanza

Sheikh Ilunga kaweka historia katika historia ya mazishi makubwa Dar es Salaam, historia inayokwenda nyuma kiasi miaka takriban 100 ukianzia mazishi ya Sheikh Mwinyikheri Akida sheikh aliyeasisi Msikiti wa Mwinyikheri Akida Kisutu, unakuja kwa Sheikh Idrissa bin Saad Khalifa wa Tariqa Askariyya, kisha Sheikh Kaluta Amri Abeid, halafu Abdulwahid Sykes, kisha Sheikh Kassim bin Juma, halafu Sheikh Abbas Kilima. unakwenda kwa Prof. Kighoma Ali Malima unaishia kwenye maziko ya Mzee Kitwana Dau baba yake Dk. Ramadhani Dau. Iweje Ilunga kijana mdogo mno aungane na majina ya watu maarufu kama hawa na kupata maziko makubwa kiasi kile? Kitu kilichompandisha daraja Ilunga katika umma wa Waislam Tanzania ni kuwa Ilunga alikuwa mtumishi wa Waislam. Wakimtuma Ilunga kila kazi na akiifanya kwa moyo mkunjufu, kuanzia kujenga madras na shule hadi kuwasomeshea watoto wao. Juu ya haya yote kilele cha Sheikh Ilunga katika kuutumikia Uislam ni ile siku aliposimama Ukumbi wa Diamond kuitahadharisha serikali kuwa kuna ''Mfumokrsisto'' nchini unaotawala na kudhulumu haki za Waislam. Hii ilikuwa mwaka 2012. Nilikuwa mmojawapo wa Waislam waliokuwa pale ukumbini kushuhudia kitendo kile cha kihistoria. Kwa nini nakiita kitendo cha kihistoria? Nakiita kitendo cha kihistoria kwa kuwa kwa takriban miaka 40 Waislam walikuwa wanasemea pembeni harakati zikienda chini kwa chini vijana wakiwatayarisha Waislam wajue kuwa ipo dhulma.

Sheikh Hussein Malik alikuwa akisema, ''Wafahamisheni Waislam wajue kuwa ipo dhulma kisha wadaie haki zao. Ikiwa utawadaia haki zao ikiwa hawajui dhulma ipo, wao ndiyo watakuwa wa kwanza kukupigeni vita kwani kama mtu hajui anadhulumiwa basi hiyo dhulma haipo.'' Sheikh Ilunga alikuwa katika kundi la vijana waliokuwa wakihangaika kuitafuta haki ya Waislam. Siku ile pale Ukumbi wa Diamond wakati ulikuwa umefika na kwa niaba ya Waislam Sheikh Ilunga akasimama kuitahadharisha serikali kuhusu kuiachia dini moja ikahodhi fursa zote za nchi kwa hila. Hotuba ya Sheikh Ilunga ilirushwa na Radio Imaan na TV yake mubashara, yaani ''live.'' Kote Radio Imaan ilikosikika Waislam walimsikia Sheikh Ilunga akieleza nini Waislam walifanya katika Tanganyika wakati wa kupigania uhuru kuuondoa dhulma na kuleta haki kwa kila mwananchi na vipi Waislam walisalitiwa baada ya uhuru kupatikana. Vyombo vyote vya habari ukitoa vile vya Kiislam viligoma kabisa kutangaza kongamano hili la Waislam. Ikawa kama vile hapajapatapo kutokea kitu chochote. Waislam hawakukata tamaa kuanzia siku ile Sheikh Ilunga alitembea nchi nzima na kufanya mikutano ya hadhara kuitahadharisha kwanza serikali kuhusu Mfumokristo na pili Waislam wa Tanzania khasa wale waliokuwa gizani ili wajue nini kilikuwa kinawatafuna.

Msikiti umejaa hadi nje



Prof. Ibrahim Lipumba Akiswali Nje ya Msikiti kwa Kukosa Nafasi Ndani
Gari ya Maalim Seif Ikitoka Msikiti wa Kichangani
Kuelekea Makaburi ya Mwinyimkuu

Jeneza la Sheikh Ilunga Likitolewa Msikitini

Nilimfahamu vipi Sheikh Ilunga Hassan Kapungu? Nilianza kuzisikia sifa zake katika miaka ya 1980 kabla sijauona uso wake. Wakati ule Sheikh Ilunga alikuwa kijana mdogo sana na mdogo kwangu kwa miaka kadhaa. Wakati naingia kusoma Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam Ilunga alikuwa maarufu pale chuoni msikiti wa Muslim Students Association of the University of Dar es Salaam (MSAUD) kiasi unaweza ukadhani kuwa na yeye ni mwanafunzi. Ilikuwa Ilunga na wenzake akina Mohamed Kassim Lulengelule ndiyo walioleta ''Nyaraka za Waikela'' na kuzihifadhi katika maktaba ya MSAUD. Hizi nyaraka zilikuwa zimefichwa Tabora kwa karibu miaka 20. Katika nyaraka hizi kulikuwa na kisa kizima cha kile kilichokuja kujulikana kama ''Mgogoro wa East African Muslim Welfare Society (EAMWS),'' Ndani ya jalada zilimohifadhiwa nyaraka zililofikishwa MSAUD kulikuwa na kumbukumbu za mikutano ya EAMWS, taarifa ya Kamati ya Upatanishi iliyokuwa inajaribu kupatanisha kati ya kundi la Adam Nasibu na wenzake waliokuwa wanampiga vita Mufti Sheikh Hassan bin Amir, Patron wa  EAMWS Aga Khan na Katibu wa jumuia hiyo Tanzania, Aziz Khaki pamoja na rais wa jumuia hiyo Tewa Said Tewa; kulikuwa na ''cuttings'' ya magazeti ya ''Uhuru,'' ''Nationalists'' na ''Tanganyika Standard,'' magazeti makubwa ya zama zile yaliyokuwa yakifuatilia kwa karibu sana mgogoro ule. Ndani ya jalada lile kulikuwa na taharir ya ''The Nationalist,'' ambalo Mhariri Mkuu wake alikuwa Benjamin William Mkapa na pia kulikuwa na tahariri ya ''Tanganyika Standard,'' ambalo Mhariri Mkuu alikuwa Brendan Grimshaw. Tofauti ya tahariri hizi ni kuwa wakati tahariri ya Mkapa ilikuwa ikishambulia uongozi wa EAMWS tahariri ya Grimshaw ilikuwa ikiomba sulhu ipatikane. Nyaraka hizi za Mzee Bilal Rehani Waikela zilikuwa hazina kubwa. Kutokana na nyaraka hizi ndipo ukweli wa nini na nani alikuwa nyuma ya kuvunjwa EAMWS na kuundwa kwa BAKWATA ukafahamika. Lakini kubwa zaidi waliokabidhiwa Nyaraka za Waikela walizileta zikiwa na maelezo ili maelezo yale yaende na kile kitakachosomwa ndani ya jalada. Ilikuwa wazi kuwa hapakuwa na mgogoro katika EAMWS. Kilichofanya Nyerere aipige marufuku EAMWS na kumfukuza Sheikh Hassan bin Amir Tanganyika kumrudisha Zanzibar ni kuwa Kanisa Katoliki halikupenda Waislam wajenge Chuo Kikuu na tayari jiwe la msingi lilikwishawekwa na yeye mwenyewe Nyerere. Katika maelezo yake Mzee Waikela aliweka na majina ya Waislam wanafik walioipiga vita EAMWS.

Hii Picha Ilipigwa Siku ya Julius Nyerere Alipoweka Jiwe la Msingi
Chuo Kikuu Cha Waislam, Chang'ombe 1968 Nyerere 

Anapeana Mkono na Mufti Sheikh Hassan bin Amir Katikati yao
ni Tewa Said Tewa Rais wa EAMWS Tawi la Tanganyika


Ilunga alikuwa kijana wa Mzee Waikela. Katika hali ya unyonge sana walikuwa wakiendesha shule ya Nujum katika juhudi za Waislam kujitoa katika dhulma ya elimu. Mzee Waikela alimsomesha vyema Ilunga kuhusu fitna na chuki ya Nyerere kwa Uislam na Waislam na mbinu zinazotumika kuudhalilisha Uislam. Bilali Rehani Waikela alikuwa mmoja wa waasisi wa TANU Western Province mwaka wa 1955 na ni yeye na wazee wake akina Abdallah na Maulidi Kivuruga na wazalendo wengine ndiyo waliomleta Nyerere Nyerere na Bi. Titi Mohamed kuja kuitia nguvu TANU Tabora. Ilunga akasomeshwa na Mzee Waikela historia ya kweli ya uhuru wa Tanganyika na akaijua na yeye maisha yake yote akaisomesha kwa wanafunzi wake. Mzee Waikela vilevile alikuwa Katibu wa EAMWS Western Province. Mzee Waikela alikuwa mfano na kigezo kikubwa kwa Ilunga katika maisha yake ya kuwatumikia Waislam na kwa upande wake Ilunga alikuwa mwanafunzi hodari na aliteka ilm nyingi kwa huyu mwalimu wake.

Nyaraka za Waikela hizi nilizikuta Maktaba ya MSAUD na nilisoma jalada lile tena na tena. Wakati nazisoma nyaraka zile nilijihisi kama Edward Crankshaw siku alipofikishiwa mswada wa kitabu cha Nikita Kruschev ''Kruschev Remembers,'' mswada uliovushwa kwa siri kutoka Urusi hadi Amerika kutafuta ''publisher.''  Kwangu mimi ilikuwa kweli nasoma yaliyokuwa ndani ya jalada lakini hapo hapo akili yangu inakataa kuamini kuwa kweli hii ndiyo kweli yenyewe.  Nikaweka azma ya In Sha Allah kwenda Tabora kuonana na na Ilunga na Mzee Waikela. Hivi ndivyo nilivyokutana na Sheikh Ilunga kwa mara ya kwanza mwaka 1987 na yeye na shemeji yake Salum Ali Mkangwa wakanipeleka kwa Mzee Waikela. Msomaji zingatia kuwa haya yote ambayo Ilunga aliyokuwa akisomeshwa na Mzee Waikela kuhusu hujuma dhidi ya Uislam ilikuwa kabla hata John Sivalon hajaandika kile kitabu chake maarufu, Kanisa Katoliki na Siasa ya Tanzania Bara 1953 Hadi 1985 (Ndanda, 1992). Kitabu hiki ni maarufu kwa Waislam hakihitaji maelezo.

Bilali Rehani Waikela
Sheikh Hamid Jongo


Turudi nyuma kidogo. Baada ya kuonana na Ilunga Tabora mwaka 1987 tukajakuonana tena mwaka 1988 katika semina ya vijana wa Kiislam ''Unity of Muslim Umma'' iliyowakusanya vijana wa Tanzania Bara na Visiwani iliyofanyika Dodoma. Mmoja katika wahadhir katika semina ile alikuwa Sheikh Hamid Jongo ndiyo kwanza anatokea masomoni Saudi Arabia. Alikuwapo pia Sheikh Mangocho (sasa ni Sheikh wa BAKWATA Mtwara).Wakati ule sote tulikuwa bado vijana na sote tukipambana na BAKWATA. Katika semina hii alikuwapo marehemu Mussa Mdidi, Waziri Nyelo, Salum Abdallah Amour, Faiz Iddi Faiz Mafongo, Abdulkadir Faya, Ahmed Olotu, Said Kambi, Ahmed Omar Mnyanga, Sheikh Hassan Mnjeja, Sheikh Hussein Abdallah wa Tanga, Sheikh Ali Kilima katika wachache ninaowakumbuka. Nakumbuka mada aliyotoa Sheikh Ali Kilima ambayo ilijaa changamoto kwa vijana wasomi wa Kiislam wa enzi zile. Mada yake ilikuwa inauliza: ''Mlango wa Kujitahidi Umefungwa?'' Sikushangaa miaka mingi baadae kujamuona Sheikh Ali Kilima sasa si kijana tena bali ni mtu mzima akijishughulisha na tafasiri na uchapaji wa vitabu vya Kiislam. Dalili zilikuwapo toka siku za mwanzo. Semina hii kwetu sote ilikuwa kama semina ya kuuaga ujana kwani wengi wetu  tulikuwa tukielekea katika utu uzima na wengi kati yetu wametangulia mbele ya haki.

 Kushoto Kwenda Kulia: Salum Abdallah Amour (Zanzibar),
Sheikh Hussein Abdallah (Tanga) na Sheikh Ali Kilima (Dar es Salaam)

Mchungaji Mtikila



Kipindi hiki kilikuwa kigumu sana kwa Waislam khasa kwa kuwa rais aliyekuwa madarakani alikuwa Muislam, Ali Hassan Mwinyi. Kubwa zaidi ni kuwa Nyerere aliwaacha Waislam katika hali mbaya sana ya unyonge kwa kuitumia BAKWATA. Vijana wa Kiislam kupitia WARSHA walikuwa na mtandao wa aina yake wakifuatilia kila jambo na kujitahidi kuuhami Uislam. Sheikh Ilunga hakuwa mchezea pembeni, alikuwa katikati ya harakati hizi zote. Semina hii ilipokuja ilitukutanisha wengi tukajuana kwa sura na majina. Uelewa wa Ilunga katika harakati hizi ulijitokeza wazi katika semina ile. Baada ya sala ya Alfajir katika semina ile Ilunga alikimbilia uwanja wa mpira wa kikapu kupiga ''shots'' katika kikapu. Ndipo nilipokujakujua kuwa Ilunga alikuwa mchezaji bingwa wa mchezo huu. Nilistaajabu sana kuona jinsi alivyokuwa mwepesi kuruka na kukimbia achilia mbali kuwa na umbo kubwa. Baadhi yetu katika kundi hili halikufika mwisho wa safari. Walishuka njiani na kupanda treni nyingine iliyokuwa inaelekea upande mwingine na ndiyo maana leo wamekuwa masheikh na ''makadhi'' wa BAKWATA.



Sheikh Gwiji Akifanya Mahojiano ya TV na Mwandishi Nyumbani Kwake
Zanzibar Mwaka  2012 Akimweleza Mitihani Waliyopitia Katika Kadhia ya
 Sophia Kawawa  Baada ya Kuhukumiwa Kifungo Cha Miezi 18
Vijana wa Kizanzibari Waliohukumiwa Kwenda Jela Kwa Kuihami Qur'an
Wakisindikizwa Baada ya Kuhukumiwa Kifungo Waliingia Jela kwa Furaha
ya Kupata Sunna ya Nabii Yusuf na Kusadikisha Yale Allah Aliyoahidi

Miaka ya 1990 Sheikh Ilunga alikuwa amehamia Mwanza akitokea Tabora. Hii ilikuwa baraka kubwa kwa Mwanza kwani mara tu alipofika alianza kuendesha darsa katika misikiti na kutoa mihadhara. Alianza kufundisha somo la Maarifa ya Kiislam katika shule mbalimbali na akaweka darsa la kudumu Msikiti wa Sheikh Alamin Maftah mbali na kuendesha darsa duara kadhaa. Hapo ndipo yeye na wenzake wakaamua kujenga shule - Nyasaka Islamic Secondary. Haikupita muda hali ya Mwanza ikabadilika darsa za Sheikh Ilunga zilizaa matunda vijana walijitathmini upya na taratibu umoja wa Kiislam ukaimarika na hii iliingia hadi BAKWATA. Viongozi waliochaguliwa kuongoza BAKWATA walikuwa kweli viongozi na viongozi hawa wakawa sasa wanafanya kazi ya Allah. BAKWATA ya Mwanza ikawa tofauti na BAKWATA nyingine nchini. Kuna siku Ilunga alinifahamisha kuwa BAKWATA ya Mwanza inamtumikia Allah, Waislam wasiwe na hofu yoyote. Alinifahamisha kuwa msimamo waliouweka ni kutiana nguvu katika yale ambayo wanakubaliana, mathalan elimu kwa vijana. Haukupita muda mrefu Mwanza ukawa mji wa kupigiwa mfano katika juhudi za maendeleo ya Waislam na Ilunga alikuwa katikati ya juhudi hizi. Ilikuwa katika kipindi hiki siku moja usiku wa manane Ilunga akavamiwa nyumbani kwake na ''majambazi.'' Haya ''majambazi,'' yalikuwa matatu. Mmoja alibaki nje akilinda doria na wawili walivunja mlango na kumwingilia ndani na mapanga. Ilunga nilivyokwishaeleza alikuwa mtu wa miraba minne. Alikabiliana nao na nyasi zilisagika hata hivyo Ilunga aliumizwa vibaya sana. Wakati yale majambazi yanakimbia kutoka ndani Ilunga alimsikia mmoja akimuuliza mwenzake, ''Vipi umemmaliza?'' Jibu likatoka, ''Utasikia kesho.'' Nilipokuja kukutana na Ilunga nilimuuliza ni nani waliotaka kumuua. Ilunga alinifahamisha. Akasema ''Wale niliopigananao wote wawili walikuwa wam evaa buti zilizofanana na buti hizo nazijua zinapovaliwa lakini sina ushahidi zaidi ila Allah ndiye mjuzi.''

Sheikh Ponda

Mauaji ya Waislam Msikiti wa Mwembechai mwaka 1998 lilikuwa jambo kubwa katika historia ya Uislam. Katika kuadhimisha mwaka mmoja tangu mauaji yale Waislam walimualika Sheikh Ilunga aje azungumze Msikiti wa Mtambani. Kipindi hiki Sheikh Ponda alikuwa amejificha baada ya kupata taarifa kuwa anataka kukamatwa. Waislam walikuwa na ghadhabu na serikali ya Mkapa. Hali ilikuwa ya wasiwasi sana. Dar es Salaam ilikuwa haijamsikia Ilunga. Siku ile ndipo walipokiona kipaji chake cha kuzungumza. Hadhira ile ilikuwa kama vile imemwagiwa maji baridi. Sauti iliyosikika ikiunguruma katika vipaza sauti vyenye nguvu kubwa vya Mtambani ilikuwa sauti ya Ilunga ikipokewa hapa na pale za vibwagizo vya ''Takbir Allahu Akbar.'' Kamera zilizokuwa mbele ya kibla kuchukua tukio lile zilikuwa hazihesabiki. Video za Sheikh Ilunga zikasambazwa nchi nzima na athari yake ilikuwa kubwa sana. Wale Waislam walikuwa hawajui kinachotendeka nchini walianza kujua ukweli wa mambo. Kilio cha Waislam kuhusu dhulma kikawa sasa kinatambaa nchi nzima. Serikali nayo kwa upande wake ilizidi kuwaandama masheikh na viongozi wa Waislam na hii ikapelekea kuzinduliwa Azimio la Tungi. Hakuna aliyeshangaa siku viongozi wa Waislam walipokusanyika Msikti wa Tungi na kutoa ''Azimio la Tungi,'' ambako kwa mara ya kwanza neno ''Mfumokristo'' lilitumika. Msomaji wa Azimio la Tungi alikuwa Sheikh Ilunga Hassan Kapungu. Azimio la Tungi lilikuwa Azimio la vita. Vyombo vyote vya habari havikuweza kuandika Azimio la Tungi limesema nini. Maneno yaliyokuwa ndani ya Azimio lile yalikuwa maneno mazito yenye ukakasi uliokusudiwa. Ilikuwa baada ya Azimio la Tungi ndipo Waislam baada ya matayarisho ya kutosha wakasimama Ukumbi wa Diamond kuieleza serikali kuwa inaendeshwa na Mfumokristo. Yaliyobaki ni historia. Unahitaji kuandika kitabu kizima kumweleza Ilunga. Ilunga alikuwa jasiri  mtu asiye na uoga wa kumuogopa yeyote yule. Sheikh Ilunga amesomesha vijana wengi sana katika maisha yake na bila ya yeye mwenyewe kusema kwa dhahiri. Ukiangalia maisha yake na kama ulibahatika kuhudhuria darsa zale utajua kuwa Sheikh Ilunga alikuwa anawalenga vijana na kwa hakika niliwaona vijana wake wengi katika maziko yake.

Kwa kuhitimisha turejee nyuma zaidi na kuangalia wapi historia hii imetoka hadi kufikia Sheikh Ilunga. Hebu tujiulize vipi mahali kama Tabora juu ya hali ilivyokuwa ngumu imeweza kumtoa mtu kama Sheikh Ilunga? Kupata jibu inakubidi uwatazame wale waliomlea Ilunga. Uitazame silsila ya Ilunga kuanzia kwa mzee na mwalimu wake, Mzee Waikela, kisha umtazame na yeye mwenyewe Mzee Waikela na wale aliokuwanao katika kuutumikia Uislam katika miaka ya 1950 wakati wa ukoloni. Huwezi kumtaja Sheikh Ilunga katika kuupigania Uislam ukaacha kutamtaja Mzee Waikela. Huwezi kumtaja Mzee Waikela usimtaje Sheikh Hassan bin Amir. Sheikh Ilunga kaingia katika mnyororo ya silsila ya watu hawa. Hao watakaokuja baadae wataisoma historia hii na silsila hii na kila wakiwarehemu waja hawa wema Sheikh Ilunga atatajwa pia kwa wema pamoja nao. Nani hii leo katika sisi asiyetaka kunasibishwa na historia iliyoachwa na watu hawa? Historia inayoanza miaka ya 1940 na Sheikh Hassan bin Amir akizunguka Tanganyika nzima hadi Congo, Malawi., Rwanda na Burundi kueneza Uislam. Inapokelewa na Mzee Waikela katika miaka ya 1950 wakati wa kudai uhuru akiwa mmoja wa vijana wa Sheikh Hassan bin Amir na mkono wa kulia wa sheikh. Harakati hizi zinakuja kupokelewa na kijana wa baada ya uhuru, Ilunga Hassan Kapungu katika miaka ya 1970 mwishoni. Hakika historia hii ni ya kuandikwa kwa wino wa dhahabu. Sheikh Ilunga kama wale waliomtangulia walivyofanya, wale waliomfanyia Allah na Mtume wake SAW uadui yeye hakuwafanya marafiki zake. Hadi umauti unamfika Sheikh Ilunga alikuwa anakabiliwa na kesi ya ''uchochezi'' na video zake zinatafutwa na vyombo vya dola. ''Uchochezi '' uliokusudiwa na hao waliomfikisha mahakamani ni kwa Sheikh Ilunga kuidai haki ya Waislam iliyoporwa. Hakika Waislam tumepoteza jemadari.


Wanne Kutoka Kushoto Aliyevaa Kofia ni Sheikh
Chambuso
Baada ya maziko nilimuona mmoja wa vijana wake Sheikh Chambuso Rajab Ramadhani kutoka Tanga na wenzake wamelibeba jeneza lililombeba mwalimu wao wanalirudisha msikitini wakiwa katika majonzi mazito.

Allah amsamehe ndugu yetu Sheikh Ilunga Hassan Kapungu makosa yake na amjazie pale palipopungua na amtie katika Pepo ya Firdaus.
Amin.

Sheikh Eng. Ali Kilima kanikumbusha mambo.

Anasema tulimuomba Mzee Hassan Nassoro Moyo wakati ule Mkuu wa Mkoa Dodoma aje atufungulie semina yetu kama Mgeni wa Heshima na akakubali akatuomba tumtayarishie hotuba ya ufunguzi. Marehemu Mussa Mdidi akaiandika ile hotuba akapelekewa. Dakika za mwisho kabisa akatuletea taarifa kuwa hatoweza kuja kama Mgeni Rasmi kutufungulia semina. Tukawa tumepwelewa. Katika mjadala nani tumwendee atufanyie kazi hiyo jina mojawapo lililotajwa lilikuwa la Sheikh Ahmed Zuberi. Jina lake lilipingwa kwa kuwa wengi walisema Sheikh Zuberi ni kijana kama sie ingekuwa bora na itapendeza ikiwa tutampata sheikh mtu mzima wa makamo hapo ndipo alipoendewa marehemu Sheikh Khamisi Khalfani. Nasaa alizokujatupa zilitutia moyo sana. Jingine alonikumbusha Sheikh Ali Kilima ni kuwa yeye alipopendekeza jina la Ilunga ndiye atuongoze katika mazoezi ya viungo asubuhi palipitika kicheko. Sababu ya kicheko kile ni kuwa wengi waliangalia ule mwili mkubwa wa Ilunga wakadhani hatoweza. Tulipofika kwenye uwanja wa mazoezi kicheko cha mwisho kilikuwa chake Ilunga.

Ali Kilima na Mwandishi



9 comments:

Unknown said...

Waislamu popote pale tulipo tunamlilia Shekh wetu Ilunga. Alikua msomi na mwalimu hodari kabisa wa historia ya Waislamu wa Tanzania na vitimbi vya mfumokristo tokea zama za Mjarmani na Mngereza na Nyerere na wafuasi wake. Shekh Ilunga katufungua macho. Mwenyezi Mungu amlaze pahala pema.

Mohamed Said Historia, Siasa na Maendeleo Tanzania said...

Inna lillahi wainna ilaihi raj'uun! Waislamu wa Tanzania tumefikwa na msiba mkubwa. Tumeondokewa na Jemedari wa Kikosi cha Mstari wa Mbele. Twataraji "2 I/C" atashika nafasi haraka in sha Allah.
Mwenyezi Mungu Amlaze pahala pema Sheikh wetu, Amin.

Unknown said...

Inna lillahi wainna ilaihi rajiuun.
MwenyeziMungu amlaze mujahedeen wetu na Kimpenzi chetu na Mwalimu wangu Ustaadh Lipunga ibn Kapungu katika pepo yake ilio njema kabisa.
Aamin

Unknown said...

Alikua mchochezi hatari wa kidini kwa kuchochea udini na uvunjifu wa sheria. Kiongozi wa dini kama yeye ni hatari kwa amani. Alifunza waislaam kukejeli na kudharau wakristo kitu ambacho ni kinyume na katiba ya nchi inayotoa uhuru wa kuabudu kwa kila raia.

Unknown said...

Inna lillah

Unknown said...

HAKUNA DINI INAYOONGOZA KWA KUNYANYASA DINI INGINE KAMA ISLAM! IKITAWALA MAHALI UJUE DINI ZINGINE HAZINA HAKI! WAKATI WA MWEZI MTUKUFU UTALAZIMISHWA KUFUNGA HATA KAMA HAUTAKI! LAKINI IKITOKEA MAHALI WAO WAMEZIDIWA KWA IDADI JIANDAE KWA MABOMU NA TINDIKALI! HAKIKA SISI WANAFUNZI WA YESU MTU YEYOTE ANAYEHALALISHA MAUAJI YA WANADAMU WENGINE YU ANA DHAMBI SANA LAKINI KWA WAISLAM NI SHUJAA!!

Mohamed Said Historia, Siasa na Maendeleo Tanzania said...

Bwana Mtangoo,
Qur'an inasema hakuna kulazimishana katika dini. Ikiwa kuna mtu anamlazimisha mtu mwingine kufunga hayo ni makosa. Hayo mabomu ya tindikali si katika Uislam na uuaji wa aina yoyote bila sababu ya kisheria si katika Uislam, Bahati mbaya sana kuna propaganda nyingi sana dhidi ya Uislam. Nakusihi jitahidi kuusoma Uislam utagundua ukweli ya mafunzo yake uongo mwingi unaotungwa dhidi yake. Uislam unamtambua Yesu kama mmoja wa mitume wa Allah na mama yake Yesu, Bi. Mariam ana sura nzima katika Qur'an. Yesu mwenyewe kaandikwa kwa sifa zote katika Qur'an. Kwa kuanzia hebu itafute Qur'an na anza kwa kuisoma Surat Mariam.

asrams said...

INALILAH WAINAILAYHI RAJIUN, KWELI KILA MWANADAMU NI HISTORIA, LEO TUMEISOMA HISTORIA NZURI YA SHEIKH ILUNGA, MWENYEZIMUNGU AMPANULIE KABURI LAKE NA AMLIPE MALIPO MAKUBWA, AMIN

kaaput said...

Samahani ndugu yangu, Shekhe alifunua watanzania macho kwamba serikali ambayo yatakikana iwe kando na dini inatumia mfumo udini ndani yake. Hivyo basi ni kosa sababu dini si moja kwa watanzania, dini nyengine pia zina haki. Huu si uchochezi bali ni tahadhari sababu watanzania wa dini inayo tumiwa na serikali watafurahia matunda ilihali watanzania wa dini nyenginezo watadhulumika na dhuluma kama hiyo itaelekezewa dini ambayo inakubali kuwa mfumo katika serikali. Shekhe anaposema hilo si uchochezi bali ni kuuelelezea unafiki na hatari ambayo yaweza leta mtafaruku mkubwa kwa watanzania, mfano mmoja ni wewe kuona shekhe alifunza waislamu kukejeli wakristo ili hali ni ukristo ndio umejipelekea kukejeliwa kwa sababu ya kujihusisha ndani ya serikali ambayo yatakikana isiwe na udini ndani yake, Kosa la nani ???