Showing posts with label historia. Show all posts
Showing posts with label historia. Show all posts

Tuesday, 5 June 2018


Shajara ya Mwana Mzizima:
TAARABU NA UHURU WA TANGANYIKA
Na Alhaji Abdallah Tambaza

Abdallah Tambaza

Mwalimu Subeti Salum Subeti
(1903 - 1974)
mmoja katika wapiga fidla (violin) maarufu wa
Egyptian katika miaka ya 1940


KUPATIKANA kwa Uhuru wa Tanganyika mnamo mwaka 1961, kwa kiasi kikubwa kumechangiwa na uhodari, umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi na umahiri wa viongozi wa vyama vya siasa wakati huo; hasa chama cha TANU kilichoongozwa na hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Lakini, kwa upande mwengine, harakati za kudai uhuru zilinogeshwa (spiced) na uwepo wa vikundi mbalimbali vya burudani na sanaa vilivyokuwa vikihamasisha na kuwatia hamasa wananchi kila palipokuwa pakifanyika mikutano— hususan ile ya hadhara— kwa kutoa burudani mbalimbali zilizoleta shamrashamra, nderemo, vifijo na hoihoi.

Kwenye mikutano ile ya wazi hapa Dar es Salaam, kabla ya kuhutubiwa na wale viongozi waandamizi wa TANU—Sheikh Suleiman Takadir, Bibi Titi na Nyerere—kulitanguliwa na usomaji wa mashairi pamoja na tenzi zilizobeba ujumbe mzito kwa waliohudhuria.

Pia, nyimbo za kwaya zenye kusisimua zilizoimbwa kwa madaha na weledi mkubwa na bingwa wa kwaya siku hizo, hayati Mzee Makongoro; zilibeba ujumbe mzito: Uhuru! Uhuru! Uhuru na Umoja.

Kwa upande wa ngoma alikuwapo Mzee Morris Nyunyusa (alikuwa haoni kabisa), ambaye pia alikuwa akipata nafasi ya kupiga kwa ustadi mkubwa zile ngoma zake kumi kwa wakati mmoja. Mmoja wa nyimbo zake ni ule mashuhuri unaopigwa kwenye Radio Tanzania mpaka leo kuashiria kwamba ni wakati mwengine tena wa kusomewa taarifa ya habari.

Mzee Ramadhani Mwinamila wa Unyanyembe Tabora, pia alikuwa akihanikiza na kikundi chake cha ngoma ya kiasili ya Kinyamwezi kilichojulikana kama ‘’Hiyari ya Moyo,’’ huku akiwa amejiviringisha na joka kubwa ambalo hurandaranda nalo mgongoni akienda huku na kule kwa midundo ya kiasili ya Kinyamwezi ya ‘igembe nsabo’ na ‘mipanga lolo’.  

Mwamko ule; hamasa ile; na vuguvugu lile lililosababisha maelfu kwa maelfu ya Wananchi kufurika kwenye mikutano,  ulimtisha na kumshitua Gavana wa Kiingereza, Lord Twinning. Hakukuwa na namna nyingine bali TANU kuipenda tu!

Kutokana na watu wengi mno kupokea na kuelewa ujumbe, sasa ikawa ni lazima mikutano ile ifanyike viwanjani Jangwani, kwani Mnazi Mmoja pakawa hapatoshi tena kubeba mzigo ule mkubwa.

Nyerere wakati fulani, alipigwa marufuku kuhutubia mikutano ya hadhara, hali iliyosababisha harakati za ukombozi kudorora.

Wananchi wa Dar es Salaam, walisononeka sana kukatishwa kwa uhondo ule wa kumsikiliza kijana mdogo wa Kizanaki, msomi kutoka Butiama, akiwaliwaza na maneno yake mazuri yaliyojaa lafudhi ya Kikurya, lakini yaliyobeba ujumbe mzito wenye mazingatio na matumaini makubwa.

Mmoja wa watu walioathirika kwa kusitishwa na kutokuwapo kwa mikutano ile, ni mama yangu mlezi nyumbani kwetu, hayati Bi. Fatuma Kigwe, ambaye daima alikuwa akituchukua sisi tukiwa bado vijana wadogo siku hizo— iwe Mnazi Mmoja au Jangwani— kwenda kumsikiliza Nyerere na Titi na yale waliokuja nayo.

Mama, alikuwa na kipaji kikubwa sana cha kuigiza sauti za watu (personification). Sasa, jioni baada ya mikutano ile, wakati tumekusanyika kwenye mduara wa chakula cha usiku, alikuwa akitoa burudani upya kwa kumwigiza ‘Nyerere wa Butiama’ na namna alivyokuwa akizungumza mkutanoni.

“Nisikilizeni … ‘babe zangu’ na ‘mame zangu’, Mkoloni Mwingereza huyu anatapatapa tu, anatapatapa tu …ataondoka, ataondoka tu  …ataondoka atuachie nchi yetu, ndiyo…ndiyo, ni mtu mbaya sana …hana huruma huyu hata kidogo!” Mama alikuwa akimpatia kweli kweli Mwalimu, hasa pale alipokuwa akirudiarudia neno moja mara mbili. Hapo tulikuwa tukipata burudani upya kumsikiliza ‘Nyerere wa Butiama’ akikonga nyoyo za Watanganyika wenzake waliokuwa wamechoshwa na kutawaliwa.

Sasa, pamoja na mambo mengine mengi, mbinu mpya ikabuniwa ya kumpiku Gavana Twinning na amri yake ya kukataza mikutano: Watu wa kawaida tu, wakawa wanaandaa shughuli majumbani mwao; hasa zile za harusi, ambapo kwa zamani, kwa mila ya watu wa Mrima, ni kawaida Bwana na Bibi Harusi watolewe uwanjani kuonyeshwa kwa ndugu na jamaa huku muziki wa taarabu ukitumbuiza.

Sasa, ikawa inapotokea mtaani kuna harusi, viongozi wa chama wa eneo husika humwendea mwenye shughuli kumtaka kutumia shughuli yake kwa kumwalika Nyerere kuja kuwa mmoja wa wageni ili baadaye apate nafasi ya kuhutubia hafla ile. Halikuwa jambo gumu lile kutekelezeka, kwa sababu wakati huo Nyerere alikuwa ni raia wa kawaida tu, ambaye kuhudhuria kwake kwenye shughuli yoyote halikuwa  jambo lililowahusu watu wa usalama ama wakoloni wenyewe.

Mbinu ile, ikawa na mafanikio makubwa sana, kwani kila fursa ilipopatikana, ilizungumzwa siasa tupu na maendeleo ya harakati za chini kwa chini za kudai nchi yetu kutoka kwa Wazungu wale wababaishaji kutoka Ulaya Ingereza. Vinanda na nyimbo za hamasa za taarabu pia huchukua nafasi hiyo kuimba nyimbo za siasa tu, badala ya ‘kimasomaso mwanangu usimwone’. Kadi mpya ziliuzwa hapo pia.

Egyptian Musical Club, ni moja ya vikundi vikongwe vya muziki wa taarabu hapa nchini ambayo ilisheni waimbaji wazuri na wenye vipaji haswa, pamoja na wapigaji ala mahiri sana kwa ukanda huu wa Afrika Mashariki. Wao ndio waliofanya kazi hiyo kwa kiwango cha juu sana. Maskani ya bendi hiyo, kwa muda mrefu yalikuwa palepale New Street (sasa Lumumba) jijini Dar es Salaam, ikiwa ni mita chache tu—mkabala— na mahala lilipokuwepo jengo la Makao Makuu ya Chama cha TANU.

Muziki wa Taarabu asilia, asili yake ni mchanganyiko wa muziki wa Kiswahili na ule wa Afrika Kaskazini (kwenye nchi kama Egypt, Tunisia na Morocco) uliosheheni ala mbalimbali mithili ya Ochestra ya bendi za Muziki ya Kizungu ama kihindi inayohusisha zaidi vinanda na ala nyingine kama vile accordion, magitaa ya bass na rythim, udi, ghanoon, tumba na violin.


Mpiga violin
Vifaa vyengine ni saxophone, organ, tarumbeta, piano na marimba. Ukiacha mpigaji wa gitaa la bass na mwimbaji, wapigaji wengine wote huwa wamekaa kwenye viti vyao wakivurumisha vinanda kwa mpangilio na uongozaji wa kiongozi wa bendi (band master).

Egyptian Musical Club, ni bendi iliyoanzishwa miaka mingi nyuma mnamo karne ya 18 hivi, jijini Dar es Salaam ikiwa moja ya uendelezaji wa utamaduni wa Mswahili wa Mrima uliochanganyika na ujio wa walowezi wa Kiarabu kutoka nchi za Kaskazini mwa Afrika.

Mara zote nyimbo zake, pamoja na kubeba ujumbe, hutungwa kwa kuzingatia maadili na utamaduni wa Mswahili wa Mwambao na lugha yake adhimu ya Kiswahili ndiyo iliyotumika, ingawa mara chache nyimbo  hizo hupigwa kwa mahadhi ya Kihindi na Kiarabu. Ni aghlabu sana taarabu kuimbwa kwa Kingereza ingawa wasanii wajanja wa kileo wamefanikiwa kufanya hivyo.

Ukiacha bendi hii ya Egyptian, bendi nyengine zilizokuwepo wakati huo jijini Dar es Salaam ni Alwatan Musical Club na Bombay Musical Club (baadaye ikajiita Jamhuri pale uhuru ulipopatikana). Tofauti na sasa, muziki huu siku za nyuma ulikuwa ukipigwa kwa ajili ya kuburudisha watu na si kwa ajili ya kujipatia chochote kwa wasanii husika kama ambavyo sasa imezoeleka.

Kule Tanga nako kulikuwa na bendi kadhaa za muziki huu, ikiwamo Lucky Star ya mwimbaji maarufu hayati Bi Shakila, aliyejizolea sifa kemkem hapa nyumbani na Afrika Mashariki yote kwa sauti yake nyororo na maudhui yenye mafunzo. Habari zinasema mbinu hii iliyokuwa ikitumika hapa Dar es Salaam kutumia taarabu kisiasa ilifanikiwa pia kule Tanga na kwengineko.

Kule Zanzibar, ingawa hakukuwa na marufuku yoyote kukataza wanasiasa kufanya kazi za ukombozi, lakini pia nako taarabu ilitumika kwa kutunga nyimbo zenye maudhui ya kudai kujitawala wenyewe miongoni mwa jamii ya Waafrika.

Mara zote wakati wa Sikukuu za Pasaka, Wazanzibari wakati ule walishuhudia kumwona Nyerere akihutubia kwenye kukaribisha wageni wa ‘Sports’ kulikokuwa kukifanywa na vilabu vya mpira vya Sunderland (sasa Simba) na Yanga.

Wimbo kama, Abeid nenda, Oya! Oya!; Tunakutuma, Oya! Oya! Ulitungwa mahsusi na Bendi ya Culture ya Unguja kumhamasisha Abeid Karume katika safari yake ya kule kwenye Mkutano wa Lancaster House, mjini London uliojadili mustakabali wa Zanzibar mpya baada ya kujitawala.

Kwa muktadha huu basi, hapana budi kwa wale wasomi watakaokuja kuandika historia sahihi ya mapambano ya uhuru wa nchi yetu kutilia maanani jambo hili la kuwakumbuka wapigaji vinanda wale wa Bendi ya Egyptian Musical Club. Ni ukweli ulio wazi kabisa kwamba kwa kiasi kikubwa tu katika kipindi kile kigumu, kwa kushirikiana na wazalendo wa kawaida tu, waliweza kupeleka mbele harakati zile.

Mara chache hupata watu wakaitaja klabu ya Yanga ya Dar es Salaam kwamba ilikuwa na mchango mkubwa katika ukombozi wa taifa hili. Kwa kiasi fulani ni kweli maana wengi wa wanachama wake walikuwa ni watu weusi, hivyo wakawa pia na kadi za TANU, lakini vyovyote vile iwavyo, Yanga hawakuwa na mchango unaoikaribia au kuipiku bendi ya Egyptian Musical Club; kwani wao walipiga na kutumbuiza kwenye shughuli nyingi ambazo ‘Mheshimiwa’ Julius Nyerere alipata fursa ya kupenyeza maneno yake, wanawake wakapiga vigelegele na wanaume kushangilia kwa makofi kuchangamsha harusi na harakati za ukombozi kuzipa nguvu.

Bendi ya Egyptian ya miaka hiyo ya 1950 na 60s, ilikuwa na wazee kama Mzee Bom Ambaroni aliyeshirikiana na Mzee Salum Mboga na Mwalimu Subeti Salum katika upigaji wa ‘violin’. Maalim Abubakar Mzinga yeye ghanoon na kuimba nyimbo pia.

Shamas bin Abubakar, Hamis George,  Abbas Mzee, Saleh Mtumwa na Muhiddin Kingaru, hawa wao walikuwa waimbaji wa zile nyimbo maarufu zilizotokea kupendwa kwa muda mrefu za: ‘’Kharusi Jambo la Kheri;’’ ‘’Kila Mwenye Uwezo Asaidie Yatima;’’ na ‘’Umaridadi si Kufua Nguo, Bali Usafishe Wako Moyo.’’ Nuru bint Suud na Mtumwa Rajab wao walikuwa miongoni mwa waimbaji wanawake.

Bendi nyengine iliyoundwa baada ya uhuru kupatikana kwa msaada mkubwa wa mwanasiasa nguli kutoka hapa Mzizima hayati Kitwana Kondo, ilikuwa ni New Extra Musical Club. Ikiwa na makao yake pale Mtaa wa Mafia na Livingstone jijini Dar es Salaam, New Extra ilitumika sana katika kuhamasisha wananchi kutilia maanani suala la kilimo kwa kutunga wimbo maarufu wa ‘Shambani Mazao Bora Shambani’. Khamis Juma Mzinga ndiye aliyeuimba wimbo huo ambao mpaka leo unatumika na kupigwa na Radio Tanzania linapokuja suala la Kilimo Kwanza.

Ni bahati mbaya sana muziki huu wa Taarabu Asilia umetoweka katika medani ya muziki hapa kwetu Tanzania Bara, kule Zanzibar ndio kwanza ‘mkoko unaalika maua’, kwani huwaambi kitu katika kumuenzi na kumtukuza hayati Bi Kidude na Siti bint Saad aliyekufa miongo kadhaa nyuma kabla uhuru kupatikana.

Ni sehemu muhimu sana ya utamaduni wa Mtanzania ukiangalia kule nyuma tulikotoka. Ilikuwa ni muziki huu wa taarabu asilia, serikali ya awamu ya kwanza ya hayati Baba wa Taifa, iliyoutumia kwa kuwastarehesha wageni wote wakubwa wa siserikali walioitembelea nchi yetu siku za nyuma, kwenye dhifa za chakula cha usiku (state banquets), pale Ikulu na kwenye holi la Diamond Jubilee, Upanga.

Wageni wakubwa wa kukumbukwa  ambao walipigiwa taarabu ni pamoja na Rais Gamal Abdel Nasser wa Misri, Kwame Nkurumah wa Ghana, Kenneth Kaunda wa Zambia, Huophet Boigny wa Corte de Voire na Chou en Lai wa Jamhuri ya Watu wa China.

Wengine ni Rais Tubman wa Liberia, Modibo Keita wa Mali, Ahmed Sekou Toure wa Guinea, Houari Boumedienne wa Algeria na Sir Abubakar Tafawa Balewa wa Nigeria pamoja na wengine wengi.

Taarabu Asilia, ilikuwa kwenye programu zote za mikutano mikuu ya Chama cha TANU na baadaye CCM, kwa kuwaburudisha wajumbe baada ya mchoko wa mikutano.

Hivyo, kama ulivyopotea muziki wa dansi wa kina Mbaraka Mwinshehe, Juma Kilaza, Michael Enock – huu wa kina TX Moshi William na Muhiddin Gurumo nao unaelekea huko huko— taarabu asilia nayo imekwenda na maji mbele ya macho yetu! Ni msiba mkubwa.
Alamsiki!
Simu: 0715808864    

Monday, 28 May 2018


Shajara ya Mwana Mzizima:
Historia ya Viwanja vya Mnazi Mmoja Dar-es Salaam
Sehemu ya Pili
Na Alhaji Abdallah Tambaza

JUMA lililopita katika safu hii, tulielezea historia ndefu ya eneo la Mnazi Mmoja la hapa jijini Dar es Salaam na matukio au mambo makubwa ya kukumbukwa yaliyokuwa, ama yakifanyika hapo kila wakati; kwa vipindi maalumu, au pale linapotokea tukio muhimu linalohitaji mjumuiko mkubwa wa watu viwanjani.

Kwa muktadha huo basi, tulielezea ile mikutano mikubwa iliyofanyika hapo kabla ya kupatikana uhuru wetu na baada yake; ambayo ilihutubiwa kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja na hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na viongozi wenzake wa mwanzo wa TAA na TANU, aliokuwa nao katika mapambano ya kuikomboa nchi yetu hii adhimu ya Tanganyika kutoka kwa wakoloni Waingereza.

Tulipokea simu kadhaa za pongezi kutoka kwa wasomaji wetu ambao walitoa maombi maalumu ya kuendeleza simulizi za mahala pale kwa mara ya pili, kwani bado walikuwa hawajakatika kiu zao; sababu maeneo mengi ama tuliyaruka au kuyaacha kutokana na uhaba wa nafasi gazetini, ambayo haimpi mwandishi uwanda mpana kucheza nao.

Mwisho wa makala ile tulielezea kwa kifupi namna Mwalimu na wenzake serikalini walivyokusudia kuifanya Mnazi Mmoja iwe ndiyo katikati ya Jiji la Dar es Salaam (kwa maana ya City Center pale ulipopatikana uhuru), kwa kuzileta ofisi kuu na muhimu za Serikali kutoka kule mjini na kuzijenga upya kwenye eneo hilo.

Mpango ule ulishindikana kutekelezwa kutokana na wakazi wengi wa eneo lile kutoridhika kuhamishiwa maeneo mengine, pamoja na kuwapo kwa ushawishi na kampeni iliyofanywa na Mwalimu Nyerere mwenyewe.

Mwanahistoria maarufu na mchambuzi wa masuala ya kisiasa nchini, Sheikh Mohammed Said, alipozungumza nami hivi karibuni alinihadithia kwamba katika kutilia mkazo jambo lile, kuna watu ilibidi Mwalimu awaandikie barua yeye binafsi kutokana na kuwaheshimu na uzito wao katika jamii.
Mmoja kati ya hao ni Bi Mruguru bint Mussa wa Mtaa wa Kipata, Gerezani, ambaye ni mama wa wanasiasa mashuhuri wa harakati za kudai uhuru, akina Abbas, Ali na Abdulwahid Sykes. Mohammed anasema:

“…Nimehadithiwa na Balozi Abbas Sykes kwamba katika kadhia ile, Mwalimu alimwandikia mama yao barua binafsi kumtafadhalisha aridhie nyumba yake kuvunjwa na kupewa mbadala ili nchi ipige hatua kimaendeleo kwa kulijenga upya jiji letu… Bwana Abbas alisema: ‘unajua Nyerere akimuheshimu sana mama kwani alimchukulia kama ni mamake mzazi vile.’

“Bi Mluguru kutokana na mapenzi yake kwa Mwalimu, yeye alikubali kuvunjwa kwa nyumba yake.
Sasa tunapoliangalia eneo hilo leo, takriban miaka karibu 60 kupita, ingawa hakuna majumba ya kiserekali mahala hapo, lakini majengo yake si yale tena yalikuwapo kwenye miaka ile ya 1960s; kwani sasa nyumba zote karibu ni za ghorofa tupu zilizojengwa na wafanyabiashara; ama kwa kuzinunua za zamani au kwa kufanya ‘ubia’ na wenye mali.

Jirani na ile Hospitali ya Mnazi Mmoja, ambayo kwa sasa imeboreshwa kwa kuwa na wodi mpaka za wazazi kujifungulia, huduma za macho na meno, wakiwamo pia hata na Madaktari Bingwa (zamani ni Mabwana Mganga tu wa kufunga vidonda na kutoa dawa za kikohozi na mafua); kunapatikanwa jengo mashuhuri la Arnautoglo.

Likijulikana kama Holi la Arnautoglo, mahala hapo palikuwa sehemu muhimu sana iliyokuwa ikitumika kwa kufanyia mikutano ya ndani ya kila aina, ikiwamo ile ya siasa na ya kijamii, vikao muhimu na mambo ya namna hiyo.

Holi hilo pia lilitumika kwa shughuli za harusi, michezo ya kuigiza, michezo ya masumbwi (boxing), na miziki ya dansi kila wakati ikishirikisha bendi mashuhuri za wakati huo za Kilwa Jazz (Dar es Salaam), Moro Jazz (Morogoro), Kiko Kids (Tabora) na Dar Jazz (Dar es Salaam).

Vikundi vya Muziki wa Taarab asilia, ambayo hupigiwa watu wakiwa wamekaa kwenye viti; na si kuruka na kucheza na chupa ya bia mkononi, pia vilikuwa vikiutumia ukumbi huo kwa shughuli zake. Wakati huo vikundi mashuhuri kabisa vilikuwa ni Egyptian Musical Club, Alwatan Musical Club na ile ya Bombay Musical Club, iliyokuwa maeneo ya Kisutu karibu na Makaburi ya Kisutu kabla hakujavunjwa na kujengwa vile vyuo vya Biashara na kile cha Ufundi.

Kwa siku za Jumamosi na Jumapili, vijana wadogo wengi waliokuwa wakisoma shule za sekondari kwenye miaka ile ya mwanzo ya uhuru (1960s), ilikuwa ni zamu yao kuja kucheza ‘’Buggie’’ muziki wa Kizungu, hasa ule wa Kimarekani uliojulikana kama Soul, Jazz na Blues. Wakati huo bendi za vijana wadogo zikipiga nyimbo za kina James Brown, Ottis Redding, Aretha Franklin, Percy Sledge, Ray Charles na Babu BB King.

Mzee Mustafa Songamebele alivyo hivi sasa

Hali hii haikumfurahisha hata kidogo aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Dar es Salaam wakati huo, Mzee Mustapha Songambele. Haraka haraka, Mzee Songambele akatoa tamko kwa Vyombo vya Habari kwamba Serikali ya Tanganyika imepiga marufuku muziki wa Soul kupigwa kwenye kumbi za starehe na redioni. Tangazo lile lilishitua sana, kwani muziki na uja uzito ni vitu viwili tofauti; na kwamba ule muziki ilikuwa ni sehemu ya utamadauni (culture) wa Wamerekani. 

Bila shaka yeyote, kuitangazia Dunia kwamba Tanganyika imepiga marufuku nchini mwake kupigwa muziki wa Kimarekani, lilikuwa ni tukio baya kidiplomasia, hasa kwa nchi changa kama yetu wakati ule. Haikupita hata wiki moja, likatoka tangazo jengine kwamba ‘ni ruhsa’ sasa kupiga muziki ule nchini bila matatizo. Vijana wakashangilia kwelikweli, kwani ndio waliokuwa wapenzi wakubwa wa muziki huo kama ambavyo labda leo ukataze muziki wa kizazi kipya wa kina Diamond, Ali Kiba, Dully Sykes, sijui Q-Chief na labda Lady JD—utachokoza nyuki wakuume bure!   

Kwa wakati ule wa ukoloni, mtu mweusi hakuwa na sehemu nyingine ya kwenda kufanya starehe zaidi ya hapo Arnautoglo na Ukumbi wa Amana pale Ilala, wakati huo ukijulikana kama ‘Kwa Ramadhani Minshehe’. Huyu Ramadhani Minshehe ndiye aliyekuwa baba mzazi wa mwanasiasa mashuhuri na kada wa Chama Cha Mapinduzi hapa nchini hayati Ditopile Mzuzuri.

Katika wakati huo mgumu, Mzee Minshehe alikuwa ni mmoja wa wazalendo waliokuwa na uwezo mkubwa wa kifedha hapa jijini, kwani pamoja na jumba hilo, pia alimiliki mashamba na majumba mengi kule maeneo ya Ilala yaliyokuwa yakimwingizia kipato si haba.

Sehemu nyingine za burudani kwenye mahoteli yale kule mjini, mtu mweusi hakuruhusiwa kuingia humo na kuchanganyika na mabwana wakubwa. Iwe kwenye vilabu vya starehe au mahotelini, utakaribishwa na maandishi mazito milangoni yanayosomeka, tena kwa Kingereza, ‘Members Only’ au ‘Management Reserves the Right of Admission’. Hayo yalifanyika hapa; na huo ndio ukoloni maana yake.

Ni ubaguzi; ubaguzi mtupu kila mahala na kutuona mtu mweusi ni kinyaa! Sasa sijui wale ndugu zangu wanaojiita wao ni Liverpool; sisi Manchester, Arsenal, Chelsea… watasemaje Wazungu wale wakikasirika kunasibishwa na wewe pia kwenye club yao! Ingeeleweka kama pengine mtu angesema anapenda tu namna Manchester inavyocheza, lakini anadiriki kusema “sisi (Chelsea si wa kuchezea) tuna mtoto mpya huyo balaa, lazima tukufungeni tu!” Duh! Tafadhalini tupunguze hiyo. ‘Mazungu yale ni mabaguzi’ wala hayashituki kupendwa na sisi.

Jumba la Arnautoglo pia limekuwa ndio mahala kwa kina mama wakati huo wa zamani za kale kwenda kujifunza kazi za mikono kama ushonaji nguo, ufumaji vitambaa na kazi za nyumbani kama mapishi (wenyewe wakiita domestiki).

Masomo ya Watu Wazima pia yalikuwa yakitolewa hapo kwa wale walioikosa elimu hiyo utotoni, na hivyo ikawa mkombozi mkubwa kwa wale waliotaka kuondoka kwenye ujinga kwa kujua kusoma na kuandika. Kwa sasa, jengo la Arnautoglo limesheheni ofisi mbalimbali za Halmashauri ya Wilaya na Jiji la Dar es Salaam.

Jamiatul Islamiya ni madrassa kubwa yenye jengo la gorofa moja  iliyojengwa kwa nguvu za wakazi wa jijini hapa chini ya uongozi wa hayati Mzee Kliest Sykes. Taasisi hiyo kongwe ambayo haipo tena sasa, ilianzishwa baada ya Waafrika chini ya Mzee Sykes tena, kuanzisha African Association ili kuja kuziba mapengo makubwa yalikuwamo katika upatikanaji wa elimu miongoni mwa wazalendo wa Kiafrika.

Wakoloni waliwaachia Wamissionari jukumu kubwa la kutoa elimu na hivyo watu wengi wa dini ya Kiislamu wakawa na woga kwamba watoto wao wangebatizwa na kubadilishwa dini kirahisi.

Jamiatul Islamiya, iliyohamiya mjengoni hapo mwaka 1935, ilifanya kazi kubwa kusomesha vijana wa kike na wa kiume elimu zote mbili, kwa maana ya  Sekula na ya Kiislamu, ni mahala ambapo watoto wengi jijini walipitia kupata manufaa yake. Ilikuwa ni mahala hapo ambapo watu mashuhuri walisoma kama vile akina Abdulwahid Sykes na nduguze, baba mzazi wa mwandishi huyu hayat Mzee Mohammed Tambaza, Imam Mkuu wa Masjid Mwinyikheri Sheikh Ahmed Haidar Mwinyimvua na nduguze, hayati Mzee Zubeir Mtemvu na nduguze pamoja na wazee wengi ambao tayari wameshatangulia mbele ya haki.

Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika Muslim School

Jengo lile, ni kielelezo tosha kwamba watu wanapoungana na kuazimia kufanya lao basi Mungu hubariki jambo hilo na bila shaka mafanikio hupatikana. Linaweza likaonekana ni la kimasikini kwa dunia ya leo, lakini ukichukulia mazingira ya ukoloni na hali dhalili za watu wake wa Kiafrika haikuwa kazi ndogo kusimamisha mjengo pale.

“Wazazi wa Kiislamu waliombwa wachange fedha ili jengo la kudumu lijengwe … Aljamiatul Islamiya ilienda nyumba kwa nyumba ikikusanya michango kutoka kwa Waislamu …

“Kwa bahati nzuri mnamo mwaka 1936 Aga Khan alitembelea Tanganyika na akafahamishwa kuhusu ujenzi wa shule ile. Alitoa fedha na shule ikajengwa jirani kabisa na mahala ilipokuwa African Association kwenye Barabara ya New Street (sasa Lumumba).

“Hii ni moja ya shule za mwanzo kabisa kujengwa na Waislamu wa Tanganyika wakati huo wa …ni moja ya mifano hai ya kuonyesha juhudi za Waislamu wa Tanganyika katika kujiletea maendeleo wenyewe…,”anaandika Mohammed Said katika kitabu chake cha Maisha na Nyakati za Abdul Wahid Sykes, ukurasa 45.

Balozi Abbas Sykes, ni mmoja katika wale mashujaa wa mwanzo kabisa walioitoa TAA ilipo na kuifanya iwe TANU mwaka 1954, kwa kuipa meno kuja kupambana na Mwingereza kudai nchi yetu. Ndiye mtu aliyeshika wadhifa wa kuwa Mkuu wa Jimbo la Pwani (PC siku hizo) ikiwamo na mji wa Dar es Salaam na Mzizima yake, akichukua madaraka kutoka kwa PC (Provincial Commissioner) Mzungu.

Abbas Sykes katika miaka ya 1950/60

Wakati huo Balozi Sykes akiwa PC, alifanikiwa kumwoa mmoja wa wanawake warembo kabisa (celebrity) jijini na mtangazaji maarufu na mahiri wa redio; mwenye sauti nyororo na ya kuvutia wa Idhaa ya Kiingereza ya Sauti ya Tanganyika, Tahia Abdulwahaab.

Akiwa bado kijana mdogo na mbichi kama alivyo Mheshimiwa Makonda sasa hivi, utawala wake jimboni ulivuma kweli kweli Pwani nzima; kwani alikuwa mtu asiyetaka masikhara hata kidogo kwa raia na watendaji.

Spidi yake ilikuwa kali kwelikweli, na hivyo Kamishna Sykes hakudumu sana katika wadhifa ule, kwani alibadilishiwa kazi na kupelekwa kuwa balozi kwenye nchi kadhaa duniani.

Miongoni mwa nchi hizo alikopita kwenye safari yake ndefu, ni pamoja na Paris, Ufaransa, Montreal Canada, United Nations, New York na Khartoum, Sudan. Akiwa kule Ufaransa aliwakilisha nchi pia kwenye Shirika la UNESCO (Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi na Utamaduni), kama Mwakilishi Mkazi.

Balozi Sykes, amestaafu kazi miaka mingi na sasa amepumzika tu nyumbani kwake pale Sea View. Alamsiki! Tukutane juma lijalo InshaAllah.
Simu: 0715 808 864
atambaza@yahoo.com

Monday, 14 May 2018


Shajara ya Mwana Mzizima:
WAJUE WANA SAIGON CLUB WA MZIZIMA
Na Alhaji Abdallah Tambaza

Saigon Khitma  Jumapili 13 May 2018
Raia Mwema 14 - 15 May 2018

JUMA hili, shajara imeonelea ichepuke kidogo kutoka kwenye siasa na kuangalia mambo ya kijamii kidogo ili wasomaji wasichoshwe na historia ya siasa peke yake;   leo tutaangazia habari nyengine kutoka katika jamii tunamoishi.

Vijijini kule tunakotoka, ukitaja neno ‘klabu’ au klabuni, basi moja kwa moja hiyo inamaanisha kwamba umekusudia mahala ambapo watu – wanawake kwa wanaume—watakuwa wamejazana wakinywa ‘mapombe’ yale ya kienyeji yaliyovunda na kutoa harufu mbaya kabisa.

Mijini hali kadhalika, ukisema ‘nakwenda klabu’ maana yake ni kwamba unakusudia klabu cha usiku (Night Club), ili pia ukalewe na, au kukesha huko ukicheza muziki na mambo mengine ya anasa kama kucheza kamari na kuvinjari na warembo wa mjini hapo. Klabu pia inaweza kuwa kama vile klabu za mpira za Simba, Azam na Yanga ili kwenda kujumuika na wapenzi na marafiki mzungumzie masuala ya soka na michezo mengine kama tenisi na gofu (Gymkhana) na Leaders Club (Klabu ya Viongozi pale Barabara ya Ali Hassan Mwinyi), siasa na biashara—basi hakuna zaidi.

Jijini Dar es Salaam, hususan maeneo ya katikati ya Kariakoo, inapatikana klabu moja mashuhuri sana inayojulikana kama Saigon Club, yenye maskani yake pale Mtaa wa Narung’ombe na Livingstone. Ni klabu kongwe ambayo umaarufu wake umezagaa kila pembe, ambapo hakuna mwenyeji wa jiji hili, atasema haijui au hajawahi kuisikia. Saigon kabla ya kuhamia Mtaa wa Narung’ombe na Livingstone ilikuwa Mtaa wa Sikukuu na Narung’ombe.

Madhumuni ya klabu hiyo—‘raison d’etre’— ni tofauti kabisa na vilabu vingine vyote tulivyovizoea katika maisha ya kawaida. Hapo hapachezwi mpira (ingawa wanachama wake labda kwa kiasi fulani ni wapenzi wa mpira), wala mchezo wa aina yoyote ile kama karata, drafti na dhumna. Hii siyo kusema kuwa Saigon haikuwa klabu ya mpira. Saigon ilianza kama klub ya mpira ya watoto wadogo wa shule za msingi na wakakua nayo hadi ukubwani na walipokuwa sasa hawawezi tena kucheza mpira Saigon ikabaki kama barza, mahali wanakutana kwa mazungumzo.

Klabu hii ya kupigiwa mfano au yenye mfano wa kuigwa, ni mahala ambapo watu huenda jioni na kuzungumza mambo mbali mbali ya kijamii na namna ya kuyatafutia ufumbuzi wa haraka kwa mustakabali wa jiji la Dar es Salaam na watu wake.

Orodha ya wanachama wake imekusanya watu kutoka katika kada mbalimbali wakiwamo kwanza hao wanamichezo, wapenzi wa michezo, masheikh, maimamu, walimu wa skuli na madrassa; pamoja na wanasiasa waandamizi wakiwamo mpaka marais, mawaziri, wabunge na madiwani.

Wamo pia wanajeshi la Ulinzi, Polisi, Usalama wa Taifa, Madaktari na wafanyabiashara wakubwa na wadogo wa mjini Dar es Salaam wa jinsia zote.

Klabu ya Saigon ina madhumuni tofauti na vilabu vyengine na mambo yanayofanyika pale ni aghlabu kuyakuta kwenye vilabu vya kawaida tulivyovielezea hapo awali.

Kwanza, uanachama wake hauangalii umri, jinsia, dini, kabila, itikadi ya vyama vya siasa, cheo, na mambo kama hayo. Utanzania wako ndiyo kigezo kikuu cha kuwa mwanachama ingawa klabu ni ya watu wa Dar es Salaam.

Katika kalenda yake ya mwaka, Klabu ya Saigon huadhimisha mambo makubwa  matatu hivi.



Kwanza, ni kuandaa shughuli kubwa siku chache kabla ya kuingia mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa kuwaalika watu mashuhuri kuja kujumuika na jamii ya kawaida kuja kuwaombea dua wanachama wa klabu hiyo waliotangulia mbele ya haki, pamoja na wakazi wa jiji hili ambao maisha na matendo yao walipokuwa hai, yaliacha athari na kumbukumbu kwa watu wa jiji hili.

Kushoto Brigadier General Mstaafu Simba Waziri, Mwinyi Mangara
na Boi Risasi katika futari ya mwaka wa 2010
Hao ni pamoja na wasanii wa fani mbalimbali; mashekhe na walimu wakubwa; wazee mashuhuri pamoja na viongozi waliopata kushika nyadhifa mbalimbali jijini Dar es Salaam na kugusa nyoyo za watu.
 
Katikati Abdallah Tambaza mwandishi wa makala hii na kulia
Mussa Shagow na kushoto ni Mwinyikhamis Mwinyimadi

Shughuli hiyo ya khitma, husababisha kufungwa kwa matumizi ya kawaida, barabara yote ya Narung’ombe kuanzia Sikukuu mpaka ile ya Livingstone. Idadi ya wahudhuriaji huwa zaidi ya watu elfu 4000 mpaka 5000. Vyakula vya aina mbalimbali hupikwa kwa wingi sana siku hiyo na vinywaji baridi na matunda hutolewa kwa wageni.

Sherehe hii, ambayo huwa si ya kukosa kuhudhuria kwa wenyeji, hufana sana maana huwa imepangiliwa kwa ustadi mkubwa kuanzia madua na visomo mbalimbali, pamoja na wazungumzaji wa kutoa nasaha zenye mazingatio kwa waalikwa.

Kila mwaka huwa inaushinda mwaka uliotangulia kwa ubora. Huwa ni hadhara ya aina yake iliyojaa vicheko, utani na vitimbi mbalimbali vya Usimba na Uyanga kwa watu kupigana vijembe vya upendo.

Pili, ni kuandaa futari maalumu katika siku moja ya Ramadhani na kufuturisha watu wa jiji hili bila ubaguzi, hata kama mtu hukufunga au si Mwislamu huwa anakaribishwa kujumuika. Kitendo hicho, si tu kinajenga udugu miongoni mwa wanachama, bali hutoa fursa kwa watu mbalimbali kukutana na kula pamoja futari hiyo katika hali ya furaha na upendo.

Daima kwenye futari hizo za kimrima, waandaaji huhakikisha vile vitu vyote vizuri vinakuwamo sahanini, siniani na vyanoni—iwe ndizi mzuzu na mihogo kwa papa; tambi, kaiamati na maandazi; mikate ya kusukuma na ya kumimina; bajia, sambusa na kachori pia huwamo. Uji wa pilipili manga na ‘chai za zatari’ huhanikiza kwa harufu nzuri mahala hapo. Waandaji huweka pia makombe (mabakuli makubwa) ya michuzi ya kuku, maini na mbuzi pia. Vitu huwa vimekamilika kisawasawa vyenye kutamanisha machoni na mdomoni!    

Wazalendo hawa wa Saigon huwa hawaishii hapo, bali pia huandaa sherehe ya usiku mmoja ya kasida za Mtume Muhammad, kwa ajili ya mahujaji wa jijini ambao walibahatika kwenda kufanya Ibada ya Hija na kurejea salama. Hii nayo hupendeza kwelikweli, maana hutoa fursa kwa mahujaji, wakiwa kwenye kanzu zao nzuri zenye kumeremeta, kuja kuelezea waliyoyaona na kuyadiriki walipokuwa kule kwenye miji mitukufu ya Makkah na Madina katika Hijja na Umra kwa kuwaburudisha kwa kasida zinazoimbwa na kughaniwa kwa sauti nyororo.

Hii huwa ni nafasi nzuri kwa wasiobahatika kuwenda Hijja ya kuombewa dua na watu wale watukufu siku za mwanzo kabisa, kwani imesemwa kwamba dua za mahujaji kabla ya siku 40 kwisha huwa mustajaba (hukubaliwa na anayeombwa).

Saigon Sports Club, hapo mwanzoni iliundwa na vijana wadogo wa skuli za Mchikichini na Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, mwaka 1966, ikiwa kama klabu ya mtaani kwa madhumuni ya kucheza mpira na watoto wenzao wa mitaa mingine.

Kwa mujibu wa Alhaji Mussa Mohammed Shaggow, mwanachama mwandamizi, waanzilishi wachache wa mwanzo wa klabu hii wakati huo ikijulikana kama Everton ni pamoja na Mussa Shaggow mwenyewe, Harudiki Kabunju, Yaakub Mbamba, Atika Kombo, Abdu Shiba, Dachi na Salum Khalil akiwa Golikipa wa mwanzo klabuni.


Kulia Atika Kombo, Harudiki Kabunju na Sunday Kayuni
wakijikinga mvua katika khiyma ya mwaka wa 2017

Kushoto Abdu Shiba na Mohamed Said

Timu nyingine za watoto wa mitaani siku hizo hapa Kariakoo, ni pamoja na iliyokuwa jirani yao, Cuba Rovers, New Take Time, New Port (mwandishi huyu alikuwa mwanachama), Dundee, Young Kenya na Young Boys. Zote hizo ziliundwa na vijana wadogo wa umri wa wastani wa miaka 14 wa maeneo ya Kariakoo, ili kutoa ushindani wa kimpira.

Sasa kadri miaka ilivyokuwa inakwenda mbele na vijana wale kuondoka kutoka utoto na kwenda ukubwani, wakabadilisha madhumuni ya klabu yao na kuwa haya sasa ili kudumisha udugu wao pamoja na kuwapokea wanachama wapya wakiwamo wanawake na wazee pia.

Kwa sasa, Saigon mpya yenye malengo mapya na maono mapya, inaongozwa na Mahmoud Mbarak kama Mwenyekiti, akisaidiwa na Juma Abeid ‘Spencer’. Boi Juma ni Katibu wa Klabu akisaidiwa na Mohammed Msitu na Alhaji Mussa Shaggow Mweka Hazina akisaidiana na Abdul Risasi. Kwenye orodha ya wajumbe yumo Muharram Mkamba, Mohammed Tall, R. Sultan na wanawake Hamida Simba na Awena Kitama.

Iddi Simba, mwanasiasa mkongwe na aliyewahi kugombea urais wa nchi hii, kupitia CCM ndiye mlezi wa Saigon ambaye kila mara amekuwa mstari wa mbele kuitetea na kuihami pale inapotaka kutetereka au kwenda kombo, kwani klabu hii ni kioo cha uzalendo uliotutuka kwa kufanya mambo makubwa ambayo wengi wamejaribu kuyaiga lakini wameshindwa vibaya.

Dr. Gharib Bilal akitoa nasaha katika Khitma ya Saigon
Kushoto Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi na mwisho kulia Idd Simba

Wamo pia katika wanachama na wapenzi wakubwa wa Klabu ya Saigon, Rais mstaafu wa Awamu ya Nne Jakaya Mrisho Kikwete na Makamu wake Dk. Mohammed Gharib Bilal. Wengine ni Mwanasiasa mashuhuri wa nchi hii hayati Ali Sykes na nduguye Balozi Abbas Sykes pamoja na watoto wao Kleist Sykes (sasa marehemu), Abraham na Ayoub Sykes. Yumo pia Mussa Azzan Zungu, Mbunge wa Ilala, na marehemu Balozi Abdul Cisco Mtiro na ACP Kamanda Mohammed Chico (sasa marehemu).


Kulia Ally Sykes, Sheikh Issa ''Smart Boy'' Ausi, mwisho
kushoto Juma ''Spencer'' Abeid

Kulia marehemu Balozi Cisco Mtiro, Mrehemu Sheikh Hussein, Sheikh
Shomari na Abraham Sykes katika Khitma ya Saigon
   
Mheshimiwa Mussa Zungu katikati akifuturu

Madhumuni mapya ya uwepo wa Klabu hiyo, pamoja na hayo niliyaeleza hapo juu ni pamoja na kusaidiana kwa shida; kufa na kuzikana. Saigon pia imekuwa kimbilio kubwa la wanasiasa wakubwa na wadogo wanaowania nafasi za uongozi katika ngazi mbali mbali hapa nchini ili kupata kuungwa (endorsement).

Hivyo basi kutokana na kuwa na wanachama wa rika na kada mbalimbali inakuwa rahisi kwa mgombea kukubalika jijini kama watu wa Saigon watamridhia na ‘kumpigia debe’ tiketi yake. Hiyo imethibitika mara nyingi na hivyo kuwa na ulazima wa kujitambulisha mapema kwa wana Saigon pale mgombea anapotangaza nia. Cha ajabu ni kwamba, hiyo si kwa wanasiasa peke yao bali hata wale wanaogombea kwenye vilabu vya mpira vya Simba na Yanga na kwenye ofisi za TFF za Taifa—Saigon wana mkono mrefu na nguvu kote huko. Fitna za siasa na mpira wanajua kuzicheza.

Lakini basi pamoja na mafanikio yote hayo mazuri, klabu ya Saigon imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo zimesababisha kuwepo na makundi mawili hasimu yasiyoiva pamoja. Jitihada mbalimbali zimefanywa kuwarudisha pamoja kwa faida ya watu wa Dar es Salaam, mpaka leo hazijazaa matunda. Hivyo ni jukumu letu kuzidi kumwomba Allah (SWT) aipeperushe fitna hii kwa mbali na amani nzuri irejee pale Saigon ili Dar es Salaam yetu iendelee kustawi. Wahenga walisema; ‘wengi huitwa wale na mmoja huitwa yule!’

Hiyo ndiyo Saigon Club, yenye kuunganisha watu kwa namna ya kipekee ambayo haijapata kufanywa, kuwepo au kutokea mfano wake hapa Tanzania katika huu umri wa miaka 60 wa kujitawala.

Jana tarehe 13 May 2018 Saigon walifanya khitma ambayo juu ya kuwa ilinyesha mvua kubwa wengi walihudhuria.
Alamsiki!
Simu: 0715808864
atambaza@yahoo.com

Wednesday, 9 May 2018

  
UBAGUZI WA RANGI ULIVYOMKUMBA DR. AGGREY UKIWEMO WA NEW AFRICA HOTEL ENZI ZA UKOLONI

Na Kamili Mussa


Dr. James Emmanuel Kwegyir Aggrey ni jina ambalo takriban 98% ya Watanzania hawalijui wala hawajawahi kulisikia.

Dr. Aggrey, mghana aliyetokea Achimota Ghana, ingawa kwa sasa ni marehemu, ni mwafrika ambaye bado anayeheshimika sana ulimwenguni licha ya kufariki miaka karibu 100 iliyopita.

Dr. Aggrey ameacha historia kubwa barani Afrika ikiwemo Tanzania. Katika maisha yake alikumbana na kila aina ya ubaguzi toka kwa wazungu.

Hapa Tanzania pia, ubaguzi wa rangi haukumuacha salama kwani alikumbana nao katika hoteli maarufu ya New Africa Hotel.

Hoteli hiyo ya New Africa Hotel iliyopo maeneo ya posta jijini Dar es Salaam, ilijengwa na Wajerumani baada ya kukabidhiwa Tanganyika kufuatia Berlin Conference 1884-85.

Enzi za ukoloni wa Mjerumani na Mwingereza, ilikuwa ni marufuku kwa Mwafrika kukanyaga hotelini hapo labda tu kwa kibali maalum au kama ni mfanyakazi wa hoteli hiyo.

Dr. Aggrey alikuja Tanganyika mwaka 1924 kama Mjumbe wa Phelps-Stokes Fund Commission kuja kuangalia jinsi ya kuwaendeleza Waafrika kielimu. Dr. Aggrey alikuwa Mwafrika pekee kwenye Commission hiyo. Commission iliundwa kutokana na Ms. Carolyne Phelps Stokes, ambaye alifariki mwaka 1909 na kuacha kitita cha fedha, ($ 1,000,000) na usia uliosema- "I bequeath the same to My trustees to be used for the education of Negros, both in Africa and the United States, North American Indian and needy and deserving white students".

Ni kutokana na wosia huu ndipo ilipoundwa Commission hiyo ambayo ilizuru mataifa kumi ya Afrika. Commission hiyo ilizuru Tanganyika na Zanzibar toka Machi 1924 hadi April 1924.

Baada ya Commission hiyo kuwasili jijini Dar es Salaam, wajumbe waliamua kufikia New Africa Hotel, moja ya hotel chache kubwa na ya kuheshimika nchini wakati huo.

Katika hali ya kusikitisha, Dr. Aggrey, akiwa Mwafrika pekee katika Commission hiyo, alikataliwa kupewa chumba katika hotel hiyo ya kutokana na Uafrika wake!

Hili jambo lilimuhuzunisha sana lakini hakukata tamaa na akaendelea na harakati zake za kuwasaidia waafrika wenzake kwa kadri alivyoweza.  Baada ya kukataliwa chumba, ilimbidi Dr. Aggrey akajitaftie chumba kwenye hoteli nyingine.

Dr. Aggrey, akiwa Dar es Salaam, ndiye aliyemshauri Kleist Sykes kuunda chama kwa maana ndiyo inhekuwa rahisi kupigania haki zao kwa pamoja. Kleist alikuwa kijana msomi mwenye kuzungumza Kijerumani na Kiingereza fasaha. Ilimchukua Kleist miaka mitano kuunda chama kiitwacho African Association (AA) hapo mwaka 1929 kwa minajiri ya kuwapigania Waafrika. African Association baadae ilibadilishwa na kuwa Tanganyika African Association (TAA) mwaka 1948. AA ndiyo iliyokuwa chimbuko la TANU iliyoanzishwa tarehe 7.7.1954.

Kutokana na wazo hilo muhimu kwa historia ya nchini yetu, wahenga watakumbuka kuwa iliamuliwa Dr. Aggrey apewe mtaa jijini Dar es Salaam kama kumbukumbu. Ndipo mtaa huo uliopo maeneo ya Kitumbini kuelekea Kariakoo, jijini Dar es Salaam ukapewa jina la Mtaa wa Aggrey.

Dr. Aggrey alikuwa ni mwalimu mwenye utaalamu wa hali ya juu aliyetambuliwa na kuheshimika duniani kote.

Mwaka 1895 akiwa Mwalimu wa shule ya Wesleyan Memorial School, alifanya mtihani, pamoja na waalimu wengine 119 nchi nzima ya Ghana, uliotungwa Uingereza. DR. AGGREY aliibuka Mwanafunzi Bora na ndiye pekee aliyepata Second Class na kutunukiwa cheti maalum.

Cheti hicho alichotunukiwa na Malkia wa Uingereza kiliandikwa-: "This Certificate of Distinction qualifies you, without further examination, to teach in any similar school in any British colony, the world over". Dr. Aggrey alikuwa Mwafrika wa kwanza kutunukiwa tuzo hiyo.

Commission hiyo, baada ya kutoka Tanganyika ilikwenda Belgian Congo. Huko, baada ya shughuli ya siku nzima za siku ya kwanza, Gavana (mzungu) akaialika Commission kwaajili ya Dinner, Ikulu. Gavana alipomuona Dr. Aggrey akiwa na wajumbe wengine ambao walikuwa ni wazungu aliamuru asiingie ndani hivyo akabaki mlangoni akiliwa mbu na kupigwa baridi hadi wenzake walipomaliza dinner!

Figisu hizi hazilumkatisha tamaa Dr. Aggrey na badala yake zilimpa nguvu zaidi kwani alielewa kuwa jukumu lake ni kuwasaidia Waafrika kielimu. Baada ya hapo Commission ilikwenda Angola ambako masaibu ya ubaguzi wa rangi yaliendelea dhidi yake ambapo kuna siku alichelewa kutoa mhadhara baada ya kusukumizwa nje ya treni kwavile tu ni mweusi!

Commission hiyo baada ya hapo ikaenda Afrika ya Kusini ambako Dr. Aggrey alitoa moja kati ya hotuba bora kabisa kuwahi kutolewa na Mwafrika ambapo, kwa ufupi, alisema: 

"By Education, I don't simply mean learning. I mean the training of the mind, in morals and in a hand that helps to make one socially efficient. Not simply the three R's, but the three H's ie the Head, the Hand and the Heart. No race or people can rise half slave, half free. The surest way to keep a people down is to educate the men and neglect the women. If you educate a man you simply educate an individual but if you educate a woman you educate a family."

"I am proud of my colour and whoever is not proud of his colour is not fit to live. Keep your temper and smile. That is what Jesus meant when he told men to turn the other cheek."

"I have no time for revenge that is not African. Some white people ought to be transformed to Negros just for a few days, so as to feel what we feel and suffer what we suffer. I prefer to be a Spokesman of my entire country: Africa, My Africa".

"My fellow Africans, I dont care what you know; show me what you can do. Many of you who get educated dont work, but take to drink. You see white people drink so you think you can drink too. You imitate the weakness of the white people, but not their greatness. You won't imitate a whiteman working hard".

"If you play only the white notes on a piano, you get only sharps; if only the black keys, you get flats. But if you play the two together you get harmony and beautiful music".

Baada ya kutoa muhadhara huo White settlers walichanganyikiwa kwa uwezo mkubwa wa Dr. Aggrey na na kiongozi wao akatamka-: Damn his colour, he is a saint!

Dr. Aggrey alikuwa ni mjuzi wa mambo mengi lakini hobby yake kubwa ilikuwa ni kusoma vitabu vya kila aina na alipenda kusema-: I want to know everything". Alikuwa akijisomea hadi usiku wa manani. Aliposinzia, alikuwaakichukua taulo akalichovya kwenye maji na kujifunga kichwani na kuweka miguu yake kwenye karai la maji ya baridi ili aendelee kusoma vitabu vyake! Kwa hakika, alipenda sana kusoma vitabu.

Dr. Aggrey alikuwa akiongea Queen's English na alipozuru US kwa mara ya kwanza, wamarekani hawakuamini kama Mwafrika angekuweza kuongea kwa lafudhi ile na kupelekea Waziri HEC Byrant aseme:

"He is dark as dark, but very few in America can use English as he can".

Dr. Aggrey alifariki dunia nchini US tarehe 30 Julai 1927 kutokana na ugonjwa wa Meningatis na kuzikwa North Carolina, US.



Kwa heshima ya Dr. Agrey, mwaka 2017 nchini Ghana, picha yake iliwekwa kwenye fedha ya nchi hiyo (5 Cedi Bill).

Huyo ndie Dr. James Emmanuel Kwegyir Aggrey mwenye mchango mkubwa katika historia ya taifa letu.