Showing posts with label uchunguzi. Show all posts
Showing posts with label uchunguzi. Show all posts

Thursday 23 February 2017




*Hii Story ni Uzushi. Mzee yuko salama nyumbani kwake na jioni hii ataungana na Jumuiya ya Mabalozi pamoja na wadau wengine katika kusherehekea Siku ya Taifa ya Kuwait iliyoandaliwa na Balozi wa nchi hiyo hapa Dar es Salaam*


Tunamuomba Mwenyezi Mungu amjaalie afya na siha njema na umri mrefu- Amiin 

_Dkt Abdullah H. MAKAME_ Katibu wa Rais Msaafu Mzee Ali Hassan Mwinyi.


Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi akiwa katika dhifa ya Siku ya Kuwait leo

Thursday 26 January 2017




Utangulizi
Kalamu ya Mh. Ally Saleh haiandiki bali inazungumza. Siku zote ninapomsoma Alberto siishi kushangazwa na uwezo wa fikra zake na jinsi anavyojua kuchagua maneno ya kutumia kumfanya msomaji asiwe anasoma bali awe anasikiliza. Ndugu msomaji msikilize Mh. Ally Saleh akieleza mauaji yaliyoitia nchi yetu katika orodha ya dunia ya wananchi ambao waliuliwa kwa dhulma kuanzia Amristar India, Sharpaville na Soweto Afrika Kusini na Zanzibar.
MS
Mh. Ally Saleh
Mbunge wa Malindi

KUMBUKUMBU YA MAUAJI YA 26 - 27 JANUARI 2001 
NA ALLY SALEH
Wakati naanza kutaka kuandika kumbukumbu hizi mwili umenisimka mara kadhaa maana katika akili yangu tukio lile halitafutka. Si kwa kuwa niliona chochote kile kwa macho yangu, la hasha, lakini nimeona zaidi kwa akili yangu.
Kwa sababu ya maumble yangu kila inapofika kuripoti matukio makubwa kama hili la Januari 26 na 27 au kuzingirwa kwa Mtendeni, au kuzama kwa MV Spice Islander, mfumo wangu wa utendaji huwa zaidi kukaa mbali na kukusanya taarifa na kuzituma, na kutoka mara moja kwa mahojiano ya kimkakati.
Sikuwa naamini kuwa serikali ingechukua hatua za kuua wananchi wake waliosema na kuweka dhamira kwa sababu ya kuandamana kwa suala la haki. Suala hilo wengi wetu tutalisimamia hadi mwisho wa uhai wetu, na baadhi yetu maandishi yetu yataendelea kupaza sauti zetu hata tukiwa katika makaburi yetu na mifupa yetu imeshakuwa mchanga nalo ni kuwa: CUF iliibiwa uchaguzi mwaka 2000 kama ilivyoibiwa 1995.
Na pia tutasimamia ukweli kuwa CUF pia wameibiwa uchaguzi 2005, 2010 na wazi kabisa 2015 na ndio maana kumbukumbu ya mauaji ya Janurari 26 - 27 itaendelea kuwepo kwa sababu dhulma dhidi ya umma, CUF na Maalim Seif itaendelea.
Utawambiaje kwa mfano wananchi wa South Africa wapuuze au waisahau kumbukumbu ya Sharpvile ambao watoto wasio na hatia waliuuwa huko na baadae Soweto? Hivi itafutika vipi jambo kama hilo? Utakuwaje binaadamu ukilifuta hilo? Na wengine wengi katika mataifa yao wanayo mambo kama hayo.
Asubuhi ya Januari 26 haikuwa siku ya kawaida maana tuliamka na ukimya mkubwa sana kama ishara kuwa mauaji makubwa yatafanywa kwa sababu ya kulinda madaraka ya mtu aliyepata ushindi usio halali na kupewa nguvu na Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
Nikiwa nyumbani asubuhi na mapema nilisikia risasi ya kwanza ikilia kwa kutokea upande wa Darajani mimi nikiwa Hurumzi. Watoto wangu Abdul-razak Shau na Dorid Alberto wakaamua kutoka kiwenda kushiriki maandamano angalau kwa maneno yao wakarushe mawe na mimi sikuwazuia.
Siku hiyo mbali na kuishia barabarani askari waliojihami kwa silaha za kila aina waliingia mpaka vichochoroni ambako milango yetu mingi ilitishiwa kuvunjwa.
Basi jinsi nilivyokuwa nimejipanga nilikuwa nikipata ripoti kila baada ya dakika tano,na kwa kuwa mbali na BBC nilikuwa naandikia pia Reuters, basi kila nikipata ripoti mpya nilifanya, ‘’filing,’’ ama ya kuhojiwa upya au ya kuandika new piece.
Niliandika au nilihojiwa mara nyengine huku nalia. Baada kama nilivyosema sikushuhudia kitu lakini ripoti nilizopata zllikuwa, ‘’so graphic,’’ hata kwa kuhadithiwa utaweza kuona kila kitu. Waliopigwa njiani, waliopigwa msituni, walioingiliwa nakunajisiwa majumbani, waliokimbia wakiacha watoto au kuwafungia.
Hata hivi leo hasa Pemba, watu waliokuwa watu wazima au watoto wana hadithi za maumivu makubwa ya kuona, kuhisi, kusikia na yaliowakuta wenyewe
Mara baada ya tukio hllo nilihojiwa na mashirika kadhaa ya haki za binaadamu na watafiti lakini niliitwa kutoa mhadhara Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambako nililia mara kadhaa huku nikielezea yaliojiri siku mbili ambapo, “mvua ya risasi ilinyesha.”
Na bado nikaendelea kupata maumivu ya kisaikolojia wakati kupitia mfuko mmoja wa Kimarekani ulipotupa fedha mimi na Salma Said kupitia Zanzibar Journalists Association kwenda kuwashawishi wanawake wa Pemba wajitokeze kutoa ushuhuda wao juu yaliotokea kwenye Tume ya Uchunguzi ya Hashim Mbita.
Na ubabe wangu wote ambao najidai ninao wallahi siwezi kurudia tulioambiwa na wahanga hao, itosehe tu nikikwambieni kuwa “it was horrible experience.”
Wanawake hao walikwenda kwenye tume hiyo kama walivyokwenda wengine wengi wa Unguja na Pemba. Cha kusikitisha hakuna chochote Tume ilichokiona kwa maana ya nani wakuwajibishwa na kwa hivyo Serikali haikutoa onyo, karipio, haikushtaki mtu yeyote kuanzia askari mkubwa wala mdogo na kabisa kuhusu wanasiasa ambao ndio waliofanya maamuzi ya kuzima maandamano hayo.
Kwa maana kuwa hata baada ya watu 31 kufariki kwa hesabu ya serikali, watu kwa makundi kujeruhiwa na wengine wakipata vilema na watu 4,000 kukimbilia ukimbizi Shimoni, Kenya na Somalia hakuna alieguswa hadi hii leo, kama kwamba hawakufa binaadamu, hapakujeruhiwa mtu.
Hii ndio kumbukumbu yangu ya Januari 26 na 27, 2001 na ndio maana mara nyingi hupenda kuisema ili wengine wajue jambo hili kubwa lilopita katika nchi yetu kwa sababu ya uamuzi wa uhuru wa kuchagua.
Na miaka kadhaa mbele bado uhuru wa kuchagua haupo na ndio maana CUF hawaoni sababu ya kutoendelea kutafuta mamlaka kupitia kisanduku cha kura na wanashika ule msemo kuwa kama yaliowafika hayo kwa kutaka sauti ya kura basi sasa, “They have got nothing to lose but their chains” yaani hawana tena cha kupoteza zaidi ya minyororo yao.
Na ndio sababu kwamba CUF ina wanachama imara, waadilifu na wasioyumba kwa sababu wanabakia na jukumu la kusimamia matakwa ya waliojitoa muhanga, mbali ya wengi kwa maelfu tulioshitakiwa kwa maelfu, tunaopigwa majumbani na kwenye baraza zetu hata leo.
Eti kuna watu hujitia upofu wa kusema, "kila kitu wao , kila siku wao," kama kwamba hawajui yote yaliowafka watu bila ya kosa zaidi tu kuwa mwanachama au shabiki wa CUF.
Kama kupandwa mbegu ya CUF kudai haki yao ya kutawala kupitia kisanduku cha kura basi ilipandwa Januari 26 - 27 na dalili za kufika dhamira hiyo zimeanza kujitokeza Oktoba 25, 2015 na kutujenga imani wengi kuwa sasa siku zinahesabika.

Wednesday 14 December 2016


Dondoo Fupi Kuhusu Mali za Waislamu Zilizodhulumiwa mwaka 1968 Ilipoundwa Bakwata

1.       Kulikuwa na jumuiya ya Waislamu wakati wa ukoloni wa Muingereza ikiitwa East African Muslim Welfare Society (EAMWS). Jumuiya hii  ilifanya kazi za kuwaletea maendeleo Waislamu wa Tanganyika na kusimamia mali zao zilizokuwa ndani ya  jumuiya hiyo.

2.     Baada ya uhuru kupatikana mwaka wa 1961wakajitokeza Waislamu wachache katika jumuiya hiyo ya EAMWS kwa kurubuniwa na Wakaanza kuleta chokochoko dhidi ya katiba na mfumo wake. Hata hivyo, Waislamu wengi  wanachama wa jumuiya hiyo walikataa madai yale ya wachache.

3.      Hatimae mwaka 1968 wale wachache wakaamua kuunda jumuiya yao iitwayo Bakwata kwa msaada wa kuungwa mkono na serikali. Lakini Waislamu walio wengi nchini hawakuitaka Bakwata. Waliipenda EAMWS.

4.  Mwaka huohuo katika kipindi cha kuundwa Bakwata,  serikali ikaivunja jumuiya ya EAMWS, Waislamu wanachama wa EAMWS waliipinga hatua hiyo ya serikali wakiungwa mkono na Waislamu walio wengi nchini.

5.      Serikali haikuishia hapo. Ikachukua mali za Waislamu zilizokuwa zikimilikiwa na  zikisimamiwa na EAMWS na kuzikabidhi Bakwata.  Waislamu wanachama wa EAMWS wakiungwa mkono na Waislamu wengi nchini walikipinga kitendo hicho cha serikali na kuendelea kuikataa na kuitenga Bakwata. Pamoja na mali za EAMWS, mali za jumuiya nyinginezo nazo zikachukuliwa na serikali na kukabidhiwa Bakwata. Jumuiya hizo ni pamoja na Al Jamiiyyatul Islamia fii Tanganyika, ambapo Bakwata hadi waliweka makao yao makuu katika majengo ya jumuiya hiyo huru iliyoanzishwa kabla ya EAMWS.

6.  Sasa tunatangaziwa kuwa kumeundwa Tume ya Mufti wa Bakwata kurudisha mali za Waislamu zilizopewa Bakwata na serikali mwaka wa 1968. Swali kubwa ni kuwa Je, Tume ya Mufti wa Bakwata hii itazirudisha mali za Waislamu wa EAMWS na za Aljamiiyyatul Islamia fii Tanganyika pamoja na zile za jumuiya nyinginezo kadhaa ikiwemo Arusha Muslim Union?

7.   Imetangazwa kuwa Tume hii ni ya Mufti na si Tume ya Bakwata. Lakini hapohapo  tunaambiwa kuwa Mufti kaunda Tume hii kwa mujibu wa mamlaka aliyonayo chini ya katiba ya Bakwata.

8.    Hebu na tujaalie kuwa mtangazaji amejichanganya katika kutangaza hayo ya kumtofautisha Mufti na Bakwata.  Ni vema basi tukaambiwa, Mufti huyu asiye Bakwata alichaguliwa na jumuiya au taasisi ipi, katiba ya jumuiya au taasisi hiyo ni ipi, huyu Mufti hivi sasa anatumikia nafasi yake kwa kulipwa ujira wake na jumuiya au taasisi gani?

9.      Kwa kuwa tangazo limeonesha kuwa mali hizi chini ya Bakwata zimekumbwa na matatizo kadhaa yakiwemo ya kutojulikana zilipo, kufujwa, kukabidhiwa au kutumika chini ya mikataba isiyoeleweka, je, uchunguzi unaweza kuwa huru endapo itaonekana kuwa Mufti na hata baadhi ya wajumbe ni Bakwata?  Je, mali hizi endapo zitapatikana zinaweza kuwa salama endapo zitaendelea kuwa mikononi mwa Bakwata au kitengo chake? 

10.  Mwisho, kwa kuzingatia haki na uadilifu chini ya misingi ya sharia za Uislamu zitokanazo na Allah, kama baada ya Tume kumaliza kazi au hata pasipokuwepo kwa Tume, je, ni halali kwa Mufti au Bakwata kushiriki katika kuhodhi na kuzitumia mali zisizo zao, mali ambazo zilizoporwa kwa uonevu? Mali za dhulma zilizoporwa kwa kutumia mabavu, toka jumuiya zilizokuwa na wanachama wake na malengo waliojiwekea wenyewe, ambayo si ya Kibakwata na Mufti wake?



Al Jamiatul Islamiyya Muslim School



Chuo cha Maalim Mzinga kilichoanzishwa mwaka wa 1935


Moja ya shule walizojenga Waislam baada ya nakama ya mwaka wa 1968

Tuesday 22 November 2016




 



Gamba la Nyoka,
Nafurahi sana kila nikikusoma jinsi unavyoandika kwa utulivu na kuweka
wazi ukweli ambao serikali inatakiwa kuuangalia.

Tatizo kubwa ni kuwa serikali haitaki kuileta hii hali katika agenda yake
ikajadiliwa na ufumbuzi kupatikana.

Haitaki kwa kuwa wanujua ukweli na wahusika wakuu wa tatizo hili toka
uhuru mwaka 1961.

Hii ndiyo sababu hata historia ya kweli ya kupigani uhuru wa Tanganyika
inawatisha na wanafanya juhudi zote kuifukiafukia isijuliknakwa dhahiri
yake.

Ngoja nikupa mkasa niliokutananao Ujerumani, Zentrum Moderner Orient
(ZMO), Berlin mwaka wa 2011.

Hii taasisi sawa na London School of Oriental and African Studies (SOAS).

Hawa jamaa walinialike nikafanye mhadhara na kuandika mada ambayo
nitaawacha hapo kwao.

Ratiba yao ni kuwa unaanza na muhadhara wa wazi kisha unakaa na
kuandika chochote na zaidi kuhusu nchi yako.

Mada yangu niliyochagua ilikuwa: ''Christian Hegemony and the Rise of
Muslim Militancy in Tanzania.''

Hadhira yangu ilikuwa kimya kwa muda na imejiinamia.

Baada ya ule muhadhara wakati wa chakula cha mchana akanijia mtafiti
mmoja kutoka University of Humburg akaniambia, ''Sheikh Mohamed
umewasononesha sana leo wenyeji wako.''

Mimi nikashtuka nikamuuliza, ''Kipi kilichowasononesha?''

Akanambia kuwa, ''Wahadhiri wote kutoka Tanzania wakija hapa
wanatoa picha ya nchi ambayo kiongozi wake alikuwa kiongozi muadilifu
aliyetoa haki sawa kwa raia wake wote bila ubaguzi sasa wewe leo umekuja
na historia hapa ni ngeni kabisa haipatapo kusikika hapa.''

Nikamwambia kuwa, ''Hiyo ndiyo hatari ya propaganda na elimu kuhodhiwa
na kundi moja katika jamii.

Mimi nimekuja na kitu kipya kwa kuwa mimi ni Muislam natoka katika
kundi lililopigania uhuru wa Tanganyika ambalo ndilp kundi leo hii sasa
limedhulumika.''

Hao waliokuja kuhadhiri hapa kabla yangu hawawezi kusema kweli kwani
ukweli hauko katika maslahi yao.

Hii ndiyo hali ya nchi yetu na kibri cha kujiona mabwana kinaonekana
wazi kwa wachangiaji wengi wakitukashifu na kutuhimiza kupeleka watoto
shule kwani tuko nyuma kwa kuwa hatupendi wala hatuthamini elimu.

Kuwa Wizara ya Elimu ni moja ya ngome za dhulma hili hawalisemi na
wala hawataki lije kwenye agenda ili lijadiliwe.

Wala hawasema kuwa Kanisa linapewa Bilioni 91 kila mwaka na serikali
ili lijiwekwe vizuri.

Wao watatoa kasoro za shule za Kiislam shule ambazo ni za kimasikini
si kwa kutaka kwetu ila kwa kuwa Waislam ni masikini.

Wao wakitaka sisi tuamini ati shule zao nzuri kwa juhudi zao si kwa kuwa
zinapokea mabilioni ya walipa kodi wa Tanzania Waislam wakiwa nap pia
walipaji wa kodi hizo.

Mkurugenzi wa ZMO Kai Kresse na mwandishi
Mohamed Said: Christian Hegemony and the Rise of Muslim Militancy in Tanzania Mainland

Thursday, July 7th, 2011, 4 pm, ZMO
MWAMKO WA WAISLAM DHIDI YA MFUMO KRISTO KATIKA TANZANIA – Islamic Resistance against Christian Hegemony in Tanzania

Baraza with Mohamed Said (Independent Scholar, Tanzania)

Mohamed Said gave a talk on the relationships between Muslims and Christians in Tanzania. He is the author of “The Life and Times of Abdulwahid Sykes (1924-1968). The Untold Story of Muslim Struggle Against British Colonialism in Tanganyika”and was a guest at the ZMO in July 2011. He is currently working in a book project called “Islamic Movements and Christian Hegemony in Tanzania”. The observation of discrimination against Muslims in their own country led him to stress their historic entanglements in the struggle for independence.

Friday 18 November 2016








Britanicca,
Unauliza kuhusu uhusiano wa Vatican na nafasi ya Urais katika Tanzania.

Nakuwekea jibu hapo chini ni ''document,'' ya utafiti ya maneno 19,000+
kwa hiyo litahitaji muda mtu kusoma:

Mohamed Said: MWL. JULIUS K. NYERERE, KANISA KATOLIKI NA UISLAM: DOLA NA TATIZO LA UDINI TANZANIA

Hapo chini nakuwekea, ''excerpts,'' kwa kusoma mswada mzima fungua hapo juu:
MWL. JULIUS K. NYERERE, KANISA KATOLIKI NA UISLAM: DOLA NA TATIZO LA UDINI TANZANIA

Utangulizi

Baada ya kifo cha Julus Kambarage Nyerere tarehe 14 Oktoba 1999 mengi yamesemwa na kuandikwa kuhusu msimamo wake na uadilifu kuhusu Uislam Tanzania. Nia ya kitabu hiki ni kueleza jinsi Mwalimu Nyerere katika kipindi chake cha uongozi alivyoshughulikia suala la Uislam na Waislam wa Tanzania. Hii ni historia ya uhusiano wa Mwalimu Nyerere na Waislam kwa kipindi cha takriban robo karne toka pale aliposhika madaraka ya nchi mwaka 1961 hadi alipoachia madaraka mwaka 1985. Ni mategemeo ya mwandishi kuwa kitabu hiki kidogo kitaweka wazi yale ambayo hayafahamiki kwa wengi.

Theluthi mbili ya Waislam wote wa Afrika ya Mashariki wanaishi Tanzania [2] ambayo ndiyo nchi yenye watu wengi kuliko zote katika Afrika ya Mashariki, yaani Kenya, Uganda na Tanzania. Hii ni pamoja na Zanzibar – nchi ya Kiislam yenye Waislam takriban asilimia tisini na tisa na kuna wakati ilikuwa ndiyo kitovu cha maarifa ya Kiislam katika Afrika ya Mashariki na Kati. Kutokana na sensa ya mwaka 1957, kwa kila Waislam watatu walikuwepo Wakristo wawili. Kwa wakati ule hii ilionyesha kuwa Tanganyika ilikuwa na Waislam wengi katika nchi zote Kusini ya Ikweta. Lakini katika sensa ya kwanza mwaka 1967 baada ya uhuru jumla ya Wakristo Tanzania Bara ilikuwa asilimia thelathini na mbili na Waislam asilimia thelathini na Wapagani asilimia thelathini na saba. Sensa hii inaonyesha kuwa Wapagani ndiyo walio wengi Tanzania. Sensa hii ya mwaka 1967 haikueleza kwa nini katika kipindi cha miaka kumi kwa ghafla Waislam wamepungua nchini au kwa nini ghafla Wapagani wameongozeka katika nchi ya waumini. Hii ndiyo ilikuwa sensa ya mwisho iliyokuwa ikionyesha mgawanyo wa dini. Inaaminika kuwa matokeo ya sensa hii yalifanyiwa mabadiliko kwa ajili ya sababu za kisiasa pale ilipobainika kuwa Waislam Tanzania walikuwa wengi kupita Wakristo. Upo ushahidi kuwa mwaka 1970, ilipobainika kuwa Waislam ni wengi Tanzania serikali iliiamrisha Idara ya Takwimu kuchoma moto matokeo yote ya sensa ya mwaka 1970.[3]

Bahati mbaya mgao wa madaraka katika siasa Tanzania umewatupa nje Waislam, ingawa inafahamika kuwa usalama na utulivu wa nchi yeyote unategemea mizani hii kuwa sawa. Vyanzo tofauti vya takwimu vinatoa takwimu tofauti zinazopingana kuhusu hesabu ya Waislam na Wakristo katika Tanzania. Hii inatokana na ukweli kuwa somo hili ni nyeti. Katika nchi za Kiafrika ambazo zina wafuasi wengi wa dini hizi mbili, kwa mfano Tanzania na Nigeria,[4]uchunguzi wa kuwa ni dini gani ina wafuasi wengi kupita mwenzake ni chanzo cha mgongano na mzozo. Tatizo hili lipo Tanzania. D.B. Barret [5] anasema kuwa Waislam Tanzania ni wachache wakilinganishwa na Wakristo. Takwimu zake zinaeleza kuwa Waislam ni 26%, Wakristo 45% na Wapagani ni 28%. Takwimu za Tanzania National Demographic Survey za mwaka wa 1973 zinaonyesha kuwa Waislam ni wengi kidogo kupita Wakristo wakiwa 40%, Wakristo 38.9% na Wapagani 21.1%. Lakini takwimu za Africa South of the Sahara,[6] zinaonyesha Waislam ni wengi Tanzania kwa 60%. Takwimu hizi zimebaki hivyo bila ya mabadiliko toka mwaka 1982. Kwa kuwa utafiti wa Waislam wenyewe katika suala hili ni mdogo sana au haupo kabisa, suala la wingi wa Waislam katika Tanzania halijafanyiwa utafiti na Waislam wenyewe.[7]

Mkristo akawa ananufaika na mfumo wa kikoloni. Waislam wakawa wanataabika kwa kuwa dini yao ilikuwa inapingana na dini ya mtawala. Mwafrika Mkristo akawa mnyeyekevu kwa serikali wakati wa ukoloni na baada ya kupatikana kwa uhuru akaja kushika madaraka ya serikali. Waislam wakatengwa na kuteswa katika ukoloni kwa kubaguliwa na kunyimwa elimu hivyo kuwaondolea fursa ya maendeleo. Kuwepo kwa Waislam kama raia na ili kuinusuru dini yao ilibidi Waislam wasimame kuutokomeza ukoloni. Baada ya uhuru Kanisa likabaki na msimamo wake wa enzi ya ukoloni wa kutii na kujipendekeza kwa serikali mpya iliyokuwa madarakani. Ushirika huu kati ya Kanisa na serikali, uliojengwa na tabia ya Kanisa ya kukubaliana na mfumo wowote wa serikali ulililelewa vyema na umeisaidia sana Kanisa. Kanisa likaweza kujijengea mazingira mazuri ya kufanya shughuli zake bila ya kipingamizi wala wasiwasi. Kutokana na uhusiano huu maalum Kanisa likajifanyia msingi imara wenye nguvu kutokana wa Wakristo waliowasomesha katika shule zao. Kanisa likatumia nafasi na uhusiano huu kwanza na serikali ya kikoloni kisha na serikali ya wananchi kujijengea himaya ambayo wafuasi wake wakaja kushika nafasi zote muhimu katika uongozi wa juu wa serikali, bunge na mahakama katika Tanzania. Katika miaka yake mia moja tu Kanisa likaweza kupata safu yake ya viongozi ambao wanadhibiti kila sekta katika jamii ya Watanzania.

Kanisa Katoliki ambalo ndilo lenye nguvu zaidi, lilikuwa tayari limeshajikita Tanganyika. White Fathers walikuwa wapo Tabora, Karema, Kigoma, Mbeya, Mwanza na Bukoba; Holy Ghost Fathers walikuwa Morogoro na Kilimanjaro; Benedictine Fathers walikwepo Peramiho na Ndanda; Capuchin Fathers walikuwepo Dar es Salaam; Consolata Fathers walikuwepo Iringa na Meru; Passionist Fathers walikuwa Dodoma; Pallotine Fathers walikuwa Mbulu; Maryknoll Fathers walikuwapo Musoma; na Rosmillian Fathers walikuwa Iringa. [8]

Haiwezekani kuielewa ahadi ya Nyerere katika haki na usawa kwa raia wote kama alivyoahidi wakati wa kudai uhuru, hadi usome hotuba yake aliyoitoa tarehe 10 Desemba, 1962 katika Bunge wakati Tanganyika inakua jamuhuri. Hotuba ya Nyerere ilijikita kwenye matatizo ya upogo kati ya Waislam na Wakristo. Nyerere alifanya hivi labda akijua kuwa ingawa yeye alikuwa Rais Mkatoliki lakini waliomuweka madarakani kuitawala Tanganyika walikuwa Waislam. Nyerere alikuwa na haya ya kusema:

''Hakuna njia nyepesi ya kuondoa tafauti baina ya raia wetu Waafrika na wasio Waafrika; hakuna njia nyepesi ya kuondoa tofauti za elimu kati ya Wakristo na Waislam, au baina ya wachache wenye elimu na wengi wa watu wetu wasio kuwa na elimu; hakuna njia nyepesi ambayo Wamasai na Wagogo wanaweza wakalingana na Wahaya na Wachagga na Wanyakyusa.''[24]

Hii ilikuwa kauli ya serikali ya kudhihirisha nia yake njema. Kauli hii ilikuwa ya kuwapa matumaini na kuwahakikishia Waislam na wale wote walioathirika na dhulma ya wakoloni, kuwa serikali ilikuwa inatambua shida zao na itachukua hatua zifaazo kurekebisha hali hiyo. Wakati Nyerere anatoa kauli hii ya kutia moyo, serikali iliyokuwa imejaa viongozi wa Kikristo na taasisi za Kikristo zilikuwa imejaa hofu wakiogopa harakati za Waislam za kujiletea maendeleo zilizokuwa zinatapakaa nchi nzima kwa kasi. Walifahamu fika nguvu na umoja wa Waislam ukitumiwa vyema hapana shaka Waislam watakuja juu. Kwa viongozi wa Kikristo waliokuwa wameshika madaraka ya serikali hii ilimaananisha kugawana madaraka sawa na Waislam, kwao wao harakati hizi mpya ziliashiria kuanguka kwa himaya yao katika madaraka kama viongozi.

Sura ya Tatu

Kusalitiwa kwa Maadili

Tarehe 5 Novemba, 1985 kabla hajastaafu urais, Nyerere aliwahutubia wazee wa Dar es Salaam. Hotuba hii ilijaa simanzi, Nyerere akikumbuka jinsi Waislam walivyompokea Dar es Salaam kwa mapenzi makubwa ingawa yeye alikuwa Mkristo. Wazee hawa wengi wao walikuwa wanachama wa zamani wa TANU waliomuunga mkono Nyerere wakati wa kudai uhuru. Nyerere aliusifia mchango wa Waislam katika kipindi kile kigumu cha kudai uhuru. Nyerere alisema kuwa upogo katika elimu uliorithiwa na serikali yake kutoka kwa Waingereza baina ya Waislam na Wakristo yeye ameuondosha katika kipindi cha utawala wake:

''Waislam wametupa nafasi kupitia sera yetu ya elimu, kurekebisha upogo. Sasa nipo katika hali ya kufarahisha kwa kuwa wakati mwingine sielewi kama Mbunge mpya, Waziri, au Katibu Mkuu katika wizara zetu za serikali, ni Muislam au Mkristo au hana dini labda pale jina lake la kwanza linapotoa utambulisho. Na hata hivyo hiyo siyo njia ya kuaminika kutoa utambulisho wa dini kwa kuwa tuna Wakristo wenye majina ya Kiislam, na Waislam wenye majina ya Kikristo. Kuvumiliana huku nyie ndiyo sababu; nilichofanya mimi ni kuzungumzia maadili haya kwa niaba yenu.''[79]

Hotuba hii ilikuwa ya ulaghai. Ukweli ni kuwa miongo mitatu baada ya uhuru Waislam hawajanufaika chochote wako katika hali ile ile aliyowaacha wakoloni au mbaya zaidi. Sivalon amefichua kuwa Kanisa limeweza kujenga himaya yake ambayo inahodhi asilimia sabini na tano za viti katika Bunge la Tanzania. Kati ya viti hivyo asilimia sabini vipo mikononi mwa Wakatoliki na vilivyobaki vimegawika kati ya Waislam na Wakristo wa madhehebu nyingine.[80]Baada ya kupatikana uhuru, Kanisa lilipohisi wasiwasi, limeweza kwa urahisi kabisa kuwazuia na kuwadhibiti Waislam. Serikali imeweza kutumia nguvu iliyokuwanayo katika kudhibiti siasa kuzuia harakati za Waislam kudai fursa sawa na Wakristo katika kugawana madaraka katika serikali. Kanisa limehakikisha kuwa kupinduliwa kwa ukoloni si kizingiti kwa Ukristo, ingawa ingetegemewa kuwa Kanisa lingedhirika kwa kuanguka kwa ukoloni. Katika miaka yake zaidi ya mia moja, Kanisa lilikuwa limestarehe kama muokozi wa nafsi na watu wenyewe. Kanisa lilikuwa salama na halikupambana na msukosuko wowote kutoka kwa serikali kwa kuwa lilikuwa Kanisa ndilo lilishika hatamu ya serikali.

Hivi sasa Waislam wanamshutumu Mwalimu Nyerere na uongozi wa Kanisa kwa kusaliti dhamana aliyokabidhiwa na Waislam ambao ndiyo waliopigania uhuru wa Tanganyika. Waislam wa Tanzania hivi sasa ni kama wanazaliwa upya. Kila kukicha wanatafakari hali yao na jinsi historia yao ilivyokuwa ya kishujaa na ya kupendeza kwa namna walivyopambana na wakoloni, kuanzia vita vya Maji Maji mwaka 1905 hadi kuanzishwa kwa African Associatioin mwaka 1929 na TANU mwaka 1954; hadi uhuru ukapatikana mwaka 1961. Waislam wanaamini kuwa baadhi ya majibu ya matatizo yanayowakabili hivi sasa yapo kwenye hii historia yao ya kudai uhuru.

[1] A.A. Ahmed, ‘Lamu’s Sacred Meadows’, Fountain, April-June, 1995 Vol. 2 No. 10, p.30.
[2] August H. Nimtz Jr, Islam and Politics in East Africa, University of Minneapolis, 1980, p.11.
[3] See Family Mirror, Second Issue, November 1994, uk. 6.
[4] Ali A. Mazrui, ‘African Islam and Competitive Religion: Between Revivalism and Expansion’, in Third World Quarterly Vol. 10. No. 2 April 1988, uk. 499-518.
[5] D.B. Barret, Frontier Situations for Evangilisation in Africa, Nairobi, 1976. 
[6] Africa South of the Sahara, Europa Publication, London, No. 20, 1991, uk. 1027.
[7] Utafiti wa kuaminika kidogo ni ule uliofanywa na Dar es Salaam University Muslim Trustee (DUMT), Angalia ‘The Position of Muslims and Islam in Tanzania’, katika Al Haq International, (Karachi) September/October 1992.
[8] Angalia Kiongozi No. 6 June 1950. Kwa maelezo zaidi kuhusu kueneza kwa wamisionari Afrika ya Mashariki, angalia M. Langley & T. Kiggins: A Serving People, Oxford University Press, Nairobi, 1974, uk. 19.
[9] Mengi kuhusu kuingia kwa wamishionari wa mwanzo mwandishi ameandika kwa msaada wa Dr. Hamza Njozi wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam.
[10] C.D. Kittler, The White Fathers, London 1959, uk. 22-23 vilevile  R. Clarke (ed) Cardinal Lavigerie and Slavery in Africa uk. 302.
[11] Angalia  ‘Proceedings of CMS 1880-8’, uk. .22-23.
[12] Angalia I.N. Kimambo,  na A.J.A. Temu, History of Tanzania, EAPH, Nairobi, 1969 uk. 126.
[13] Katika kuuhisha vita dhidi ya Uislam serikali ya Tanzania mwaka wa 1993 ilitiliana sahihi mkataba na makanisa, mkataba uliokuja kujulikana kama Memorandum of Understanding makubaliano ambayo yalikuwa serikali kuidhinisha elimu, huduma za jamii na afya ziendeshwe na Christian Council of Tanzania (CCT) and Tanzania Episcopal Conference (TEC) kwa kushirikiana na serikali. Mkataba huu ulitayarishwa kwa siri  na Dr. Costa Mahalu, wa Kitivo cha Sheria Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam na ukatiwa sahihi na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Edward Lowassa. Mkataba huu ulitiwa sahihi bila ya kuwashirikisha  au kuwafahamisha Waislam. Ili makubaliano haya  yaweze  kutekelezeka, serikali ilibidi ifanye marekebisho kifungu 30 cha  Education Act No. 25, 1978.

[14] H.B Hansen, Mission, Church and State in Colonial Setting: Uganda 1890-1925, London 1984, uk. 26, vilevile angalia Ali M. Kirunda, “Uganda Muslims and their problems,” The Monitor June 4-June 8, 1993.
[15] Abel Ishuwi, Education and Social Change, (1980).

[16] Angalia P. Gerold Rupper, OSB, Pugu Hadi Peramiho: Miaka 100 ya Wamisionari Wabenediktini Katika Tanzania, Benedictine Publications, Ndanda-Peramiho, 1980, uk. 31-42.
[17] Angalia Yusuf Halimoja, Historia ya Masasi, East African Literature Bureau, Nairobi, uk. 163-175. Kwa kupata habari zaidi jinsi Wakristo walivyopigana upande wa Wajerumani katika Vita ya Maji Maji ili kulinda Ukristo dhidi ya kile kilichoonekana kuwa ni jihad, angalia Nimitz, op.cit. uk.12-13. 
[18] C.H. Becker, ‘Material for the Understanding Islam in German East Africa’, Tanzania Notes and Records, No. 68, 1968, p. 58.
[19] Al Jamiatul  Islamiyya ‘A’ iliundwa mwaka 1940 kutokana na mgogoro ulioanzishwa na Liwali wa Dar es Salaam wakati ule, Ahmed Saleh akishirikiana na Waingereza.
[20] Congress ilikuwa imegubikwa na matatizo ya ugomvi kati ya viongozi wake. Angalia Reporter (Nairobi), March – June, 1963. AMNUT ilikuwa katika siku zake za mwisho lakini ilikuwepo tamaa kuwa huenda kikapata nguvu mpya. Kassanga Tumbo aliyekuwa katibu wa TRAU ambae Nyerere alimteua balozi Uingereza, alikuwa amejiuzulu ubalozi akarudi Tanganyika na kuanzisha chama cha upinzani, Tanganyika Democratic Party. (TDP). Kulikuwa na mazungumzo ya kuunganisha TDP na AMNUT. Nyerere alifahamu kuwa endapo Waislam watamuunga mkono Tumbo utawala wake ungekuwa mashakani.Inasemekana kuwa nafasi ilie ya ubalozi Uingereza awali Nyerere alimpa Hamza Mwapachu. Mwapachu aliikataa kwa kuwa alihisi hiyo ilikuwa njama ya Nyerere kumeweka mbali na siasa nchini. Ilikuwa matumaini ya Mwapachu kuwa Nyerere angelimpa uwaziri ili achangie pamoja nae katika kuijenga nchi.
[21] Tanganyika Standard, 2 May, 1961. 
[22] Kilichofuata baada ya kupatikana uhuru ilikuwa ni kukamatwa, kuwekwa kizuizini na kuhamishwa kwa masheikh na Waislam wengine waliodhaniwa kuwa wanapinga utawala wa Nyerere. Mashuhuri miongoni mwao walikuwa: Abdillah Schneider Plantan, Sheikh Abdulkarim Abdulwahid, Maalim Popo Saleh, Suleiman Masudi Mnonji, Ali Migeyo, Mufti Sheikh Hassan bin Amir, Sharff Hussein Badawiy, Shariff Mwinyibaba, Shariff Adnan, Bilali Rehani Waikela, Sheikh Jumanne Bias, Maalim Matar, Abdalah Mwamba, Sheikh Hashim Haji Abdallah, Sheikh Nurdin Hussein, Salum Abdallah Popo, Sheikh Mzee Ali Comoriam, Sheikh Al Amin Maftah, Rajab Kiguu cha Mbuzi na wengine wengi.
[23] Tanganyika Standard, 15 April, 1961. Kwa hoja kama hiyo angalia vilevile John Hatch, Two African Statesmen, London, 1976, uk.128.
[24] Press Release B/1629/62 10th December, 1962.
[25] Tanganyika Standard, 12 th March, 1963.  
[26] K. Mayanja Kiwanuka, op. cit. uk. 57-58.
[27] Report ya East African Muslim Welfare Society, January/February 1961. 

[28] Kwa maelezo kamili ya mgogoro wa Waislam wa mwaka 1968, angalia M. Said, ‘Islam and Politics in Tanzania’, op. cit. Vilevile angalia ‘Kwikima Report’ katika The Standard, 12 th December, 1968, na katika The Nationalist, 24 th October, 1968.
[29] Mwaka wa 1963 hawa wafuatao ndiyo walikuwa viongozi wa EAMWS: Tewa Said Tewa, Aziz Khaki, Bibi Titi Mohamed, Saleh Masasi, Abdallah Jambia, Khamis Kyeyamba na Bilali Rehani Waikela.
[30] Kwa kiasi cha siku mbili Nyerere alikuwa hafahamiki yuko wapi. Wanajeshi walikuwa wakiwasiliana na Oscar Kambona kujaribu kutatua mgogoro uliokuwepo. Dossa Aziz ndiye aliyemtorosha Nyerere kutoka Ikulu akapita nae lango kuu Nyerere akiwa amejificha katika gari la taka chini ya takataka. Dossa akiwa na bunduki yake alienda na Nyerere hadi Kigamboni kwenye nyumba iliyokuwa ufukweni pwani ambayo ilikuwa ikitumiwa na Gavana kama mahali pa kupumzika. Baadae Rashid Kawawa aliyekuwa makamo wa rais alikwenda pale na wakawa pamoja na Kambona ambae alikuwa kiungo kati ya serikali na wanajeshi walioasi. Nyerere mwenyewe hajakieleza kisa hiki kwa yoyote. Baada ya kujitokeza waandishi wa habari walimuuliza alikuwa wapi wakati wote wa uasi wa wanajeshi. Nyerere kwa ukweli kabisa alijibu, ‘Nilikuwa Dar es Salaam’.
[31] Katika utawala wa Rais Ali Hassan Mwinyi na baada ya kupita miaka zaidi ya thelathini, amri ya kufukuzwa Sharif Hussein ilibatilishwa na akarudi Tanzania. Kwa kauli yake mwenyewe Shariff Hussein alimfahamisha mwandishi kuwa yeye wakati wa uhuru alikuwa akishiriki katika dua nyingi za kumuombea Nyerere mafanikio. Shariff Hussein akasema lakini malipo yake kutoka kwa Nyerere ilikuwa ni kumfukuza nchini. 
[32] Viongozi wa EAMWS walitishwa na makachero wa serikali watupe nyaraka na kumbukumbu zote za EAMWS au sivyo serikali itawachukulia hatua. Viongozi wengi walitishika na kuchoma moto majalada yao. Waikela alihifadhi nyaraka na majalada yake yote hadi yakamfikia mwandishi baada ya  zaidi ya miaka ishirini baada ya kufungiwa jumuiya hiyo. Regional Commissioner wa Jimbo la Magharibi wakati ule alikuwa Rashid Heri Baghdelleh yeye alikwenda kuonana na wafungwa wa siasa katika jela ya Uyui akiwa na salamu kutoka kwa Rais Nyerere kuwa wafungwa wa siasa waombe msamaha na yeye atawaacha huru. Waikela alikataa kuomba msamaha na hoja aliyotoa ilikuwa yeye hajatenda kosa lolote kwa hiyo haoni haja ya kuomba msamaha. Baada ya kutoka kizuizini mwaka 1965, Waikela alikuta ofisi ya EAMWS Tabora imefungwa na Waislam wanatishwa na serikali wasiifungue. Waikela aliwashawishi Waislam wakusanye sahihi zao na wamplekee kuomba ofisi ifunguliwe. Hili lilifanyika na ofisi ile ikafunguliwa upya chini ya Waikela na ikaendelea kutoa huduma kwa Waislam kwa miaka mitatu hadi serikali ilipoivunja EAMWS mwaka wa 1968. Hivi sasa Waikela ni mtu mzima na bado anajishughulisha na kuendeleza harakati za kueneza Uislam.
[33] Tabligh ilikuwa imepata mafanikio makubwa kiasi kuwa katika mkutano wa EAMWS wa mwaka 1966 Tewa Said Tewa aliomba kuwa taarifa maalum itolewe katika mkutano ujao kuonyesha takwimu za Wakristo waliorudi katika Uislam.
[34] Tewa Said Tewa, ‘A Probe…’
[35] Tewa op.cit.
[36] Habari katika sura hii zinatokana na mahojiano kati ya mwandishi na Tewa Said Tewa, Bilali Rehani Waikela na Ali bin Abbas mmoja wa wanafunzi wa Sheikh Hassan bin Amir. Habari nyingine zinatoka kwenye mswada wa Tewa ambao haujachapishwa, ‘A Probe in the History of Islam in Tanzania’. Tewa aliandika habari hizi kuhusu harakati za Waislam kujiletea maendeleo chini ya EAMWS miaka kumi na nne baada ya aliekuwa rais wa Tanzania Julius Nyerere kuivunja.
[37] Tewa Said, ibid.
[38] Angalia Kiwanuka, op. cit. uk. 75.
[39] Ibid.
[40] Benjamin Mkapa alishinda uchaguzi na kuwa rais wa tatu   wa Jamuhuri ya Tanzania mwaka 1995.
[41] Nyerere alizidi kutishika pale mara baada ya maulidi yale yaliyofanikiwa, mwezi Julai, 1968 Tewa akifuatana na masheikh wawili, Athumani Manzi na Sheikh Minshehe Mgumba akafanya safari ya kutembelea Dodoma, Kongwa, Mpwapwa, Kondoa, Tabora na Kigoma. Huko kote Waislam walikuwa wakijitokezakwa wingi kumpokea kiongozi wao. Tabora ulifanyika mkutano mkubwa uliohutubiwa na Sheikh Jumanne Biasi na Rehani Bilali Waikela. Kigoma Tewa alifanyiwa mapokezi makubwa akasindikizwa na magari hadi Ujiji msafara ukiongozwa na Sheikh Khalfani Kiumbe. Katika ziara hizi Tewa alikuwa akifungua shule zilizokuwa zimejengwa na EAMWS. Ilikuwa Kigoma ndipo Tewa Said Tewa alipoonyeshwa barua kutoka kwa Adam iliyoambatanishwa na miniti za mkutano kati ya Sheikh Abdallah Chaurembo na Sheikh Ramadhani Chaurembo akiuandikia uongozi wa EAMWS Kigoma akiwaomba Waislam wajitoe kutoka EAMWS kwa sababu ilisoma maulidi Ilala. Aliporudi Dar es Salaam Tewa aliufahamisha uongozi wa makao makuu kuhusu barua ile. 
[42]  Taarifa ya Kamati ya Utendaji EAMWS Mkoa wa Tanga 23rd Oktoba, 1968, Ripoti ya Sheikh A.J. Jambia. 
[43] Kiwanuka, op.cit., uk. 2.

[44] Angalia Ripoti ya Kwikima katika The Standard, 12th Desemba, 1968. Vilevile The Nationalist, 24 Oktoba, 1968.  
[45] Angalia Ripoti ya Kwikima.
[46] Tewa, ‘A Probe…’
[47] Ujenzi wa Chuo Kikuu ulikuwa umeanza na jiwe la msingi lilikuwa limewekwa na Julius Nyerere rais wa Jamuhuri ya Tanzania.
[48] Tume ya Uchunguzi ya Waislam ilikuwa na wajumbe wafuatao: Mussa Kwikima (Dar es Salaam), Rajab Ukwaju (Mara), Dr. Hussein Lweno (Dar es Salaam), Mussa Nabahani (Lindi), Bilali Rehani Waikela (Tabora), Abdul Karim (Tanga) na Khamis Khalfani (Dodoma).
[49] Tewa ibid.
[50] Barua ya Mwenyekiti Halmashauri ya Uchunguzi Mogogoro ya Waislam kwa Waziri wa Habari na Utangazaji, 21 Novemba, 1968.
[51] The Nationalist, nukuu kutoka kwa Kiwanuka, uk.81.
[52] Maelezo kutoka mwanakamati wa Halmashauri Kuu ya TANU ambae ameomba jina lake listiriwe.
[53] Mwezi Novemba 1967 Tewa Said Tewa alikuwa amefanya ziara ya Mwanza na Bukoba iliyokuwa na mafanikio makubwa kwa kuwa alifanya majadiliano na viongozi wa Waislam wa huko kama Sheikh Amin Abdallah wa Mwanza, Sheikh Ali Migeyo na Sheikh Suedi Kagasheki wa Bukoba.
[54] Kiwanuka, uk.2-3.
[55] Ibid., p.81
[56] The Standard, 9th November 1968 nukuu kutoka Kiwanuka p. 81. Vilevile angalia The Standard, 20 November 1968. 
[57] Sheikh Hassan bin Amir alianza kukosana na serekali mara tu baada ya uhuru pale Kanisa Katoliki ilipotoa vitu vya kukumbuka uhuru vilivyokuwa vimenakshiwa na picha za Kikristo. Sheikh Hassan bim Amir alikereka na hili na hasa pale George Kahama, Waziri wa Mambo ya Ndani, alipokwenda Italia kuweka uhusiano baina ya Tanganyika na Vatikano. Kuanzia hapo, Sheikh Hassan bin Amir, kupitia Daawat Islamiyya na kwa kupitia wanafunzi  wake waliokuwa wameenea nchi nzima alianza kuandika khutba za Ijumaa na kuzisambaza katika misikiti ya nchi nzima na khutba hizo zikawa zinasomwa katika sala ya Ijumaa. Ujumbe wake kwa Waislam ulikuwa Waislam watumie fursa iliyoletwa na uhuru kwa kujielimisha ili wagawane madaraka sawa na Wakristo katika kuiendesha nchi. Sheikh Hassan bin Amir akaanzisha mfuko wa elimu ambao Waislam walitakiwa kuchanga fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule. Kwa ajili ya kuingia kwake kati pale Nyerere alipotaka kuivunja EAMWS, Sheikh Hassan bin Amir akaonekana ni kikwazo kwa Ukristo kuukalia juu Uislam.
[58] Sheikh Kassim Juma aliitumikia serikali kwa karibu miaka ishirini hadi mwaka 1992 ghafla akaanza kuishitumu serikali na kumtaja Nyerere kama mtu aliyepanga njama za kuuhujumu Uislam. Sheikh Kassim alikamatwa mara mbili na kuwekwa ndani kwa kosa la ‘kuwachonganisha Waislam dhidi ya serikali’. Alipotolewa afya yake ikawa mbaya na akafa mwaka 1993. Historia fupi ya Sheikh Kassim ipo katika Al Haq Newline,(Pakistan) No.1 Muharram/Safar, 1415-A.H. ‘Sheikh Kassim bin Juma bin Khamis 1940-1994’ 
[59] Baada ya kundi la Adam Nasibu kutoka Tanga masheikh wakaanza kukamatwa na kuwekwa kizuizini na ni wakati huo Saleh Masasi alitangaza kujitoa kwa Iringa.
[60] Miaka mingi baadae Rashid Kawawa alisema kuwa anajuta kuunga mkono kukamatwa kwa Mufti wa Tanganyika na Zanzibar, Sheikh Hassan bin Amir akaelekeza lawama kwa wale waliomshauri kufanya hivyo.
[61] Ali Muhsin, op.cit. uk 87.
[62] Nyaraka za Tewa hazikuonyesha ni gazeti lipi lakini kwa kuwa wakati ule Tanzania magazeti ya Kiingereza yalikuwa mawili, The Nationalist gazeti la TANU na The Standard lililokuwa likimilikiwa na Lonrho, ni wazi gazeti lileThe Standard.
[63] Angalia Kwikima Report.
[64] Pamoja na mambo mengine Taarifa ya Tume ya Kwikima ilipendekeza mabadiliko katika katiba ya EAMWS, kuondolewa kwa nafasi ya Patron, kuasisiwa kwa jumuiya mpya ya Kiislam itakayokuwa haina ubaguzi wa rangi na taarifa ilisisitiza jumuiya mpya kutochanganya dini na siasa.
[65] Ibid.
[66] The Nationalist,15 December, 1968.
[67] Baraza,(Nairobi), 12 Desemba, 1968.
[68] Rashid Kayugwa Afisa wa Usalama Taifa, Dar es Salaam ndiye aliyepewa kazi ya kudumisha mawasiliano kati ya kundi la Adam Nasibu serekali. Kayugwa ndiye aliyekuwa akielekeza kundi la Adam Nasibu mbinu za propaganda na nini kifanyike na kwa wakati gani ili kuvunja umoja wa Waislam. Kayugwa alikuwa amepata mafunzo yake ya ukachero Israel, Checkoslovakia na Marekani. Katika kuhakikisha mafanikio ya mkutqano wa Iringa, Kayugwa ambae ni mzaliwa wa Iringa alipendekeza mkutano wa Waislam wa Taifa ufanyike Iringa kwa kuhofu vurugu na upinzani kutoka kwa Waislam wa Dar es Salaam. Baada ya kusoma kitabu cha Padri John Sivalon kilichoeleza kuwa Kanisa baada ya uhuru liliendesha hujuma dhidi ya Uislam na Waislam kwa kupitia serikali, ndipo ilipomdhihirikia ukweli na kuona kuwa alipokuwa akitumiwa kuhujumu EAMWS hakuwa akitumikia serikali kama alivyokuwa anadhani bali alikuwa akilitumikia Kanisa, kama kuomba maghufira kwa Mwenyezi Mungu, aliamua kueleza mchango wake katika kuwahujumu Waislam na Uislam ili iwe fundisho na onyo kwa Waislam watakao kuwa katika utumishi wa vyombo kama hivyo siku za usoni. Kabla ya kufa kwake alieleza masikitiko yake kwa kukandamizwa kwa Waislam na akatoa mfano wake mwenyewe wa kutopandishwa cheo katika Usalama wa Taifa kwa sababu tu yeye alikuwa Muislam. 
[69] Tewa ibid.
[70] Angalia Kiwanuka, uk.85. Vilevile Proceedings of the Iringa Conference 12th – 15th December,1968 katika Maktaba ya Chama cha Mapinduzi, Dodoma. Vilevile The Standard, 18th December, 1968. 
[71] The Standard,18th December, 1968.
[72] The Standard, 20th December 1968.
[73] Ibid.
[74] Tewa, ibid. Vilevile angalia The Standard, 20th December 1968.
[75] Kiwanuka, uk. 86. Habari nyingine kuhusu Mussa Kwikima zimepatikana katika mazungumzo na yeye mwenyewe Kwikima pamoja na maelezo kutoka kwa Bilali Rehani Waikela. Katika mabadiliko makubwa na bishara Mussa Kwikima ndiye alisimama mahakamani kumtetea Sheikh Kassim Juma wakati aliposhtakiwa kwa ‘kuwachonganisha Waislam na serekali’. Sheikh Kassim Juma alikuwa akimpiga vita Kwikima wakati akiwa katibu wa Tume ya Waislam chini ya EAMWS, Kwikima alipokuwa akitafuta sulhu baina ya pande mbili. 
[76] Pamoja na watu hawa watatu wengine waliokuwa katika mpango ule walikuwa: Omari Muhaji, Juma Jambia, Juma Swedi
[77] Baada ya miaka mingi ya Waislam kuisusia BAKWATA ikafika mahali ikawa inashindwa hata kufanya mikutamo ya uchaguzi wa viongozi kwa mujibu wakatiba yake. Kwa hali kama hiyo ilikuwa kwa Msajili wa Vyama kuivunja. Serikali ilipooona imekabiliwa na hali hiyo ikachukua jukumu la kutayarisha mkutano ili kuihuisha BAKWATA. Tarehe 28 Aprili 1993 Waziri wa Mambo ya Ndani na Makamo Waziri Mkuu Augustine Mrema aliitisha mkutano kati ya Waislam na Wakristo katika Ukumbi wa Diamond Jubilee Hall, Dar es Salaam. Mkutano ulikuwa hauna agenda. Kanisa lilipeleka ujumbe wa hali ya juu kabisa. Waislam hawakutokea isipokuwa BAKWATA. Katika mkutano ule Mrema alieleza kuwa uchaguzi katika BAKWATA umechelewa sana kwa kukosa faedha.Kanisa paleplale lilijitolea fedha kuipa BAKWATA ili ifanye uchaguzi wake. Halikadhalika Mrema alisaidia kukusanya fedha kutoka kwa wafanyabiashara kwa ajili ya uchaguzi wa BAKWATA. Mkutano ulifanyika Dodoma tarehe 10th -12th Mei. Badala ya kufanya uchaguzi BAKWATA ilirekebisha katiba yake ili iweze kumpa ruhusa Sheikh Mkuu wa BAKWATA haki ya kufukuza na kumweka katika uongozi au kumtoa mtu yeyote bila ya kipingamizi. 

[78] Angalia Bergen, uk. 238.
[79] Daily News, 6th November 1985.
[80] Sivalon, op.cit. uk.49.
[81] Ali Hassan Mwinyi, Rais wa Jamuhuri ya Tanzania mwaka 1985-1995.
[82] Warsha ndiyo jumuiya ya kwanza katika historia ya Tanzania baada ya uhuru kuanza kuwaanda Waislam na kupambana na dhulma zilizokuwa zikifanyiwa Waislam. Kwa kipindi chote cha uhai wake serikali ilikataa kukipa usajili. Hii ilikuwa heri kwao kwa kuwa kiliendesha kampeni zake chini kwa chini, kampeni ambazo zilileta mafanikio makubwa hasa katika kuwaelimisha Waislam kuhusu mbinu za adui. Warsha iliweza kufikia hatua ikachukua uongozi wa BAKWATA. Warsha haikudumu katika uongozi kwa muda mrefu. Serikali ikimtumia Adam Nasibu kwa mara ya pili iliweza kuwapiga marufuku vijana hawa wasishugulike na uongozi wowote katika jumuiya yoyote ya Kiislam. Hata hivyo athaari za Warsha zingalipo hadi sasa. Vongozi wengi wa jumuiya za Kiislam hivi sasa wamepata uamsho na mafunzo yao ya awali ya uongozi katika Warsha. Mwaka wa 1981 Warsha walifanya utafiti ambao ulikuwa haujawahi kufanyika kabla, Warsha walifanya utafiti katika elimu ya Waislam Tanzania. Utafiti ulionyesha Waislam walikuwa wana nafasi chache katika vyuo vya elimu ya juu. Taarifa ya utafiti huu ilisambazwa kwa Waislam wote wa Tanzania.
[83] Angalia Kiongozi, Julai 15-31, 1993.
[84] Hali ya Waislam katika Tanzania ni ya kusikitisha inapokuja suala la kueneza habari au propaganda. Vyombo vyote vya habari, vya serikali na vilivyo chini ya wamiliki binafsi vyote vipo katika mikono ya Wakristo. Vyombo hivi vinatumika vyema katika kupiga vita Waislam.
[85] Nje ya vyombo hivyo vya serikali, Profesa Malima alikuwa na jeshi kubwa ka Waislam waliokuwa nyuma yake, wengi wao wakiwa vijana. Wakiwa hawana vyombo vya habari wanavyovimiliki, Waislam walichapa makaratasi na kuyatawanya nchi nzima yakimuunga mkono Profesa Malima huku yakieleza udhalimu wa serikali, mengine yamkitaja Julius Nyerere na Kanisa Katoliki kama washiriki katika kuwadhulumu Waislam. Kwa ajili hii Profesa Malima alipendeza machoni mwa Waislam. Profesa Malima akawa anaalikwa katika kila hafla muhimu ya Waislam. Katika hafla zile Profesa Malima aliwahutubia Waislam kuhusu madhila wanayoyapata.

[86] Aboud Jumbe, The Partner-Ship, Amana Publishers, Dar es Salaam, 1995, uk. 125-138.
[87] Jan P van Bergen, Religion and Development in Tanzania, (Madras, 1981) passim.
[88] Kitabu hiki hivi sasa hakipatikani na kulikuwa na uvumi kuwa Usalama wa Taifa walikuwa wakikitafuta ili kikusanywe na kuteketezwa kwa kuwa kilikuwa kinahatarasha umoja na mshikamano wa wananchi na kwa ajili hiyo amani ya nchi. 
[89] John C. Sivalon, Kanisa Katoliki na Siasa ya Tanzania Bara 1953 Hadi 1985, (Ndanda,1992)
[90] Ibid. uk. 37.
[91] K. Mayanja Kiwanuka, The Politics of Islam in Bukoba District (1973), B.A. Thesis, University of Dar es Salaam.
[92] Mohamed Said, ‘Islam and Politics in Tanzania’ (1989) makala hii ilichapishwa tena kwa jina hilo hilo katika Al Haq International (Karachi) Vol. 1 No. 3 August-December 1993.
[93] ‘Kwikima Report’ imo ndani ya The Standard, 12th December, 1968, vilevile The Nationalist, 15th December, 1968. Angalia vilevile Bergen, uk. 238.
[94] Angalia, USAID/Tanzania ‘Tanzania Flash Points Study’, April, 1999.