Showing posts sorted by date for query Abdalla kassim hanga. Sort by relevance Show all posts
Showing posts sorted by date for query Abdalla kassim hanga. Sort by relevance Show all posts

Friday 5 June 2015



Tanbihi ya Tanbihi: Kumbukumbu, Kusahau, na Zanzibar Mpya

Na Harith Ghassany

Zanzibar 1950
  
Madhumuni ya maandishi haya mafupi si kumjibu Mzanzibari mwenzangu na kaka yangu Ahmed Rajab, mwandishi maarufu na mwenye kusifika barani Afrika. Nia yangu ni kuweka sawa baadhi ya dhana zake kwa manufaa ya Zanzibar ndani ya wakati huu tulionao.

Mwandishi maarufu wa riwaya, Milan Kundera, aliandika: “Mapambano ya binaadamu dhidi ya nguvu [za dola] ni mapambano baina ya kumbukumbu na kusahau.” Suala kuu la kwa kila Mzanzibari aliyeishi kabla au baada ya miaka 50 iliyopita ni, anakumbuka au anakumbushwa nini, anasahau au anasahaulishwa kitu gani, na kwa nini? Suala hilo ni la kwanza kabisa. Suala la chuki, kulipizana kisasi, au kusameheyana bila ya kusahau, ni masuala ya mtitiriko wa suala kuu.

Kwa hiyo, tunapolizungumzia suala la kumbukumbu na kusahau, la kwanza la kujiuliza na kulizingatia ni, tunakumbuka au kusahau kitu gani? Na hicho kinachokumbukwa ni kipi na jawabu yake inatokana na kundi au makundi yepi kati ya makundi matatu  aliyoyataja Rajab:
1.        La wahusika
2.         La walioshuhudiya
3.         La walioyasikiya

Rajab kajiweka kwenye kundi la pili na kuzidi kujiaminisha na aaminike, ameandika kuwa ana ushahidi wa maandishi wenye kuthibitisha yale anayoyakumbuka. Nimefurahi sana kulijuwa hilo kwa sababu tuna mfano mzuri sana wa kufananisha usahihi wa nguvu za historia ya maandishi ya wakati wa tukio na udhaifu wa “historia simulizi” za baadae.

Napenda kumuomba kaka yangu mpenzi atupatie japo kopi ya kumbukumbu za maandishi ya mkutano wake na marehemu Abdalla Kassim Hanga pamoja na Wazanzibari wenzake wawili, ili tupate kipimo cha kuyapima yale ambayo yeye ameyahifadhi kama ni shahidi wa maandishi.

Lakini turudi nyuma kidogo kwenye kumbukumbu na kusahau hata bila ya kujaribu kuyakumbuka au kuyasahau yaliyotokeya katika mkutano wa miaka 47 iliyopita.

Kitabu cha "Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru," (na si "Kwaheri Uhuru, Kwaheri Ukoloni," kama alivyoandika Ahmed Rajab kwenye sehemu ya pili ya makala yake ya “Tanbihi”), kina kurasa 496.  Kati ya hizo ni kurasa tatu tu, ukurasa 267-270, zenye kuuzungumziya mkutano wa London baina ya Wazanzibari watatu na Hanga. Lakini hizo kurasa tatu ni muhimu katika muktadha wa maudhui ya kukumbuka na kusahau kwa sababu, na Mungu awazidishie afya Ahmed Rajab na Bwana Salum Hamdan ambaye anaishi Maskati, Oman, watu wawili hao wenye kuhusika moja kwa moja na suala la changamoto za kuandika historia, Alhamdulillah, wote wawili wako hai na wana akili zao.  

Kwanza napenda kumkumbusha msomaji kuwa Bwana Salum Hamdan ni wa kundi la pili, la waliyoshuhudiya, kama anavyojinasibunalo Ahmed Rajab. Tafauti yao ni Ahmed Rajab ameweka kumbukumbu ya maandishi ambayo narudiya tena, tutamshukuru sana akitupatiya ili tujifunze namna ya kuzizidhibiti changamoto katika suala zima la kuisajili historia na athari zake mbaya na nzuri za baadae.

Mzee Salum Hamdan ni mzee wa hikma na busara. Nilipokwenda kuonana naye kwa mara nyengine ili nizisajili kumbukumbu zake, aliniambia nisubiri mpaka atakapozungumza na Ahmed Rajab kwa sababu kuna mambo ambayo huenda akawa ameyasahau au hayakumbuki vizuri. Na hapo ndipo msomaji wa kurasa 267-270 katika kitabu cha “Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru,” atakutana na maneno yafuatayo ya Salum Hamdan yenye kuonyesha kuwa alikuwa shahidi wa mkutano ambaye aliamua kuzungumza na Ahmed Rajab kabla ya kuzungumza na mwandishi (Harith):

 “Sasa tulivyokuwa London yeye [Ahmed Rajab] kataja watu watatu tu.” Ukursa 267.
“Nnavyokumbuka mimi Oscar akatwambia sikilizeni bwana.” Ukurasa 268.
 “Ndivo navokumbuka mie na ndivo anavokumbuka Ahmed [Rajab].” Ukurasa 268.

“Mimi skumbuki ile nilikwenda railway station. Kile mimi sijakumbuka. Kama ulivosema, mimi nyumba nilikuwa naijuwa, sina haja ya Kasembe kunpeleka. Lakini inaweza kuwa nimekwenda mimi na Kasembe kumpokea Ahmed Rajab. Yeye Ahmed kafikiri tu na mie ni mgeni. Hajajuwa kuwa mimi na Kambona tunajuwana na jirani, na nyumba yangu mie na yake si mbali.” Ukurasa 268. “Yeye Ahmed amekumbuka  mambo mimi sijayakumbuka.” Ukurasa 268.


Oscar Kambona
Inasikitisha kuwa mwandishi gwiji na mahiri kama Ahmed Rajab angalau kusema kuwa Salum Hamdan alizungumza na yeye kama mwenzake kuyathibitisha yale walioyashuhudia pamoja na Hanga kabla ya kumpa mkusanyaji (Harith) taarifa za mkutano wa London. Ahmed Rajab kashindwa kuwa mkweli na muwazi na badala yake kaamua kujaribu kunirushia ndoo ya tuhuma yenye uchafu wa “msimamo wa kisiasa,” “dhana Fulani,” “kupotosha historia,” “kutoa maelezo kinyume na matukio halisi yalivyotokea,” na kumumunya “wanaoendeleza chuki wakikataa kusamehe.” Hee!

Lumumba

Kama tayari nilikuwa nina dhana fulani, kwanini nilizitupilia mbali simulizi za kina marehemu Ali “Lumumba” na wengineo, na kumfuata Mohamed Said Tanga na kuonana na wazee wazito wa Dar es Salaam? Marehemu Mzee Hamza Aziz ambaye alikuwa Kamishna wa Polisi aliniuliza suala dogo lakini zito. Aliniambia, “Sikiliza kijana. Inataka kwanza ujiulize yale Mapinduzi ya Zanzibar yalipangwa huku kwetu Tanganyika au kule kwenu Zanzibar?” Hapo ndipo nilipoipata ile Wazungu wanayoiita “gestalt switch” au “paradigm shift.” 

Aliyeshika Kiuno Katika Mavazi ya Polisi ni Inspector General of Police (IGP) Hamza Aziz Akiangalia Usalama Uwanja
wa Mnazi Mmoja Mbele ya Kibarua Bar Nyerere Akihutubia Kumueleza Abdallah Kassim Hanga. Pembeni
ya Hamza Aziz Kashika Kiuno ni Paschal Shija na Chini Yake Aliyekaa ni Kassim Hanga na Mbele ya Hanga
Aliyekaa Mwenye Miwani Akitabasamu ni Mzee Omari Londo Mzee wa TANU
Hassan Nasoro Moyo akisoma kitabu Kwaheri Ukoloni Kwaheri Uhuru

Haikuwa dhana wala uhodari wangu. Na hiyo ilitokeya baada ya kupoteza kama miaka miwili Zanzibar kuyatafuta Mapinduzi mchana kwa vibatari na kandili ndani ya vichochoro vya Mji Mkongwe na N’gambo yake!

Dr. Harith Ghassany na Mohamed Said

Hayo yote bado sijayaona umuhimu wake kwa sababu kuna faida au somo gani katika kukumbuka au kusahau kama Oscar Kambona ndiye au siye aliewaita Wazanzibari kwake au kama alimtuma Kasembe? Muhimu Ahmed Rajab alifika kwa Oscar Kambona na angelitaka angeliamua kutohudhuria mkutano baada ya kutambua kumbe Kasembe hakuwaambia alikuwa amewachukuwa kwenda kwa kitimbakwiri na msaliti wa ukombozi wa Afrika - Oscar Kambona. Haingii akilini hata kidogo kuwa Ahmed Rajab abebwe tu na Kasembe kama pakacha la madoriani halafu ajikute anafunguliwa mlango na Kambona!

Ali Mzee Mwenyekiti wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar akiwa na kitabu ''Kwaherri Ukoloni Kwaheri Uhuru,''

Rostam Aziz akiwa na kitabu Kwaheri Ukoloni Kwaheri Uhuru
Narudia tena. Yote hayo si muhimu kwa sababu suala muhimu kwa kila Mzanzibari ni kukumbuka au kusahau namna Zanzibar ilivyotoweka na kupotea au kupotezwa kama ni nchi yenye mamlaka kamili kupitia tukio la tarehe 12 Januari, 1964, na yaliofuatiliya.  Suala si nani alikuwa akitawala, uhalali au uharamu wake. Suala ni kupotezwa nchi kwa kuvamiwa na baada ya muda mfupi kumezwa ndani ya muungano. Ni kama vile kumbaka mwanamke halafu ukaamua kufunga pingu za maisha naye kwa kufanya harusi!

Na ndio maana mazungumzo ya Hanga kwa mujibu wa Salum Hamdan niliyaweka katika mlango wa “Hayeshi Majuto Yao.” Bwana Salum Hamdan ambaye yuhai amemnukuu marehemu Hanga:

“…sisi Mungu atusamehe, tumefanya mambo mengi ambayo mabaya, tumedhulumu, tumechukuwa watoto na wake za watu, na Mwenye Enzi Mungu anisamehe na ninajuta kwa haya nlioyafanya.” Ukurasa 269.

Kinyume cha Salum Hamdan, Ahmed Rajab kayasahau maneno ya Hanga yaliyonukuliwa na Salum Hamdan lakini ameyakumbuka maneno aliyojisafisha nayo Hanga kwa kumtusi Kambona.

Salum Hamdan ameeleza, “Lakini inasikitisa kuwa tangu wakati ule yeye [Hanga] yupo pale London habari zishafika Cairo. Walioko Cairo maambassador wa pale wameshapeleka habari Tanzania kwa Mzee Nyerere. Ikawa serikali inavosikia wamekaa wakimgojea arejee tu. Yeye Hanga hajajuwa, wala sisi hatujajuwa.” Ukurasa 270.

Anaandika Rajab: “Kutoka Conakry, Hanga alirudi nyumbani, akipitia Cairo, ambako alikuwa mgeni rasmi wa Ahmed Diria Hassan, Balozi wa Tanzania nchini Misri. Aliporudi Dar es Salaam ndipo Hanga alipokamatwa kwa amri ya Rais Julius Nyerere na akapelekwa Zanzibar ambako aliuliwa kikatili.” Ahmed Rajab hajui au hakumbuki kuwa kumbe Hanga alikuwa ameshauliwa kutoka Cairo.

 Kitabu cha “Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru,” si kitabu kilichosimama juu ya midomo ya simulizi peke yake. Kila mlango wa kitabu cha “Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru,” una marejeo ambayo yanatokana na "primary" na "secondary" “sources.” Kwenye utafiti wa kihistoria, "primary" “sources” ni marajeo ya watu ambao walishiriki na waliyashuhudia yale ambayo wanayazungumzia. "Secondary" “sources” zinaweza zikawa ni vitabu ambayo vinategemea nini watu wengine wameandika na mwandishi mwenyewe si mwenye kuyashuhudia yale yalioandikwa au kusemwa. Simulizi za wazee si zangu mimi bali ni za wazee walioshiriki moja kwa moja au kwa karibu sana na tukio la Zanzibar la 1964. Na ikumbukwe pia, historia ya maandishi inatokana na historia ya simulizi. Yakumbuke ya Jibrili, Wahyi, na kukusanywa kwa Qur’an.

Kitabu cha “Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru,” kina milango ishirini na moja.

Sasa wacha twende mlango kwa mlango:
1. Kwenye "Mapitiyo kwa Jumla" kuna endnotes (mapitio) 24.
2. Mlango wa Kwanza una mapitio 25.
3. Mlango wa Pili una mapitio 42.
4. Mlango wa Tatu una mapitio 27.
5. Mlango wa Nne una mapitio 6.
6. Mlango wa Tano una mapitio 19.
7. Mlango wa Sita una mapitio 11.
8. Mlango wa Saba una mapitio 15.
9. Mlango wa Nane una mapitio 20.
10. Mlango wa Tisa una mapitio 14.
11. Mlango wa Kumi una mapitio 2.
12. Mlango wa Kumi na Moja una mapitio 16.
13. Mlango wa Kumi na Mbili una mapitio 18.
14. Mlango wa Kumi na Tatu una pitio 1.
15. Mlango wa Kumi na Nne una mapitio 18.
16. Mlango wa Kumi na Tano una mapitio 2.
17. Mlango wa Kumi na Sita una mapitio 6.
18. Mlango wa Kumi na Nane una mapitio 2.
19. Mlango wa Kumi na Tisa una mapitio 84.
20. Mlango wa Ishirini una mapitio 47.
21. Mlango wa Ishiri na Moja una mapitio 3.

Na ukiingia na ukazama ndani ya hayo mapitio ndipo utakapoweza kuunganisha na kuona wapi penye udhaifu wa sahau na wapi ambapo sahau imepikuliwa na maandishi ambayo hata mwenye sahau utamuona anajikuta hajui au hakumbuki kitu. Wakati kweli nguvu za kukumbuka na kusahau zina uwezo wa kutupiga chenga, jee, maandishi ambayo ni "primary sources" ambayo yako karibu sana ki wakati na tukio lenyewe, hayana uzito wowote kwa gwiji wa fani ya habari na uandishi mtamu kama ndugu yetu Ahmed Rajab? Au tuseme hakuwa na wakati na alizisoma zaidi simulizi za wazee na ndio maana akaona udhaifu katika "methodology" ya uandishi wa “Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru?” Au alizilenga kurasa tatu tu kati ya kurasa 496?

Kuridhika nako kuna miko yake. Mtu anaweza akakubali lakini asiridhike na jawabu wala ushahidi. La msingi, kama nimekosea au nimedanganywa, kama ni muwongo au nimezuwa; Alhamdulilllah, uhai na uwezo wa wengine kuja na maelezo mbadala na yenye kusimama na hoja zenye ushahidi, bado upo. Suala: kwanini hawakosowi pale wanapoona pametiwa chumvi au pamepotoshwa kwa kulitimiza lengo la mwandishi au la watu fulani? Tumeweke wapi Salum Hamdan? Katika kundi la waliyoshuhudiya au katika kundi walioyasikiya tu na kumkabidhi mwandishi wa makala hii?

Naanza kuamini na kuridhika kuwa kuna tatizo kubwa zaidi hata kuliko kukukmbuka au kusahau. Kitabu cha “Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru,”  kimewashitusha, kimewaporomosha na kuwashusha daraja baadhi ya watu katika majivuno na majigambo waliyokuwa wakijivunia siku zote za Uwao. Kilichowashtuwa zaidi kuwa kimepokewa na kukubalika na hata wale ambao hawakubaliani nacho wameamuwa kukaa kimya.

Kimewashangaza kuona kimefikia kua kigezo cha ushahidi wa kusadikika na kukubalika Bungeni, hiyo ilikuwa fimbo. Walitamani angekuwa kiongozi au viongozi fulani kuipata sifa hiyo. Ahmed Rajab anashaka juu ya nini hali anajuwa kuwa niliyoelezwa yanatokana na mashahidi wa matukio hayo na washiriki wengine bado wahai na hadi leo hakuna aliyeyapinga maelezo yao. Vipi yeye awe na shaka nayo! Yeye na walio kama yeye hawaji na ushahidi au kitu kipya. Ni ushahidi wa kukosoa na kupanga hoja kwa kutumia kipaji cha uandishi na mantiki za kupinduwa hoja.

Katika mapambano baina ya kukumbuka na kusahau, kinachotakikana khasa ni ukombozi wa kiroho kwanza, na wa kiakili baadae, wa kila Mzanzibari, anaeishi ndani au nje ya Zanzibar na vizazi vyao. Ni ukombozi wenye kukubali, tena kwa hoja zenye kusimama juu ya ushahidi juu ya yale ambayo yamekuwa yakiogopwa kuzungumzwa hata kwa siri tena kwa zaidi ya nusu karne. Kinachotakikana ni uongozi mpya wa kizazi kipya ambacho kiko tayari kuinusuru Zanzibar kutokana na maradhi ya ukaidi na kujipambiya sifa ili kujitawadhisha na utawala.

Zanzibar imezungukwa na bahari ya ushahidi wa kuvamiwa kutoka kila upande wa roho na mwili wake lakini bado ina baadhi ya magenerali ambao wameamua kuingia kwenye vita vya kuinusuru huku wakiwa hawana hakika baina ya kuuandama “umimi” au kuyaweka juu kabisa maslahi ya Zanzibar na maslahi ya Wazanzibari ambao wengi wao ni watu wema na wanyonge.

Kizazi kipya hakikubali tena kudanganywa na kuingiliwa na mchwa wa miaka 51 iliopita. Kizazi kipya ni aina ya mbao mpya ambayo mchwa hawezi kuila. Mchwa aliebakiya Zanzibar na nje ya Zanzibar ni yule ambaye ameshaila fimbo ya Nabii Suleiman.

Na hadithi ya Musa ndani ya nyumba ya Firauni haijamalizikia na tukio la kihistoria liliomo ndani ya vitabu vitukufu vya Qur’an na Bibilia. Wakati hauko tena mbali Firauni wa Zanzibar akatoa shahada huku anazama.

Hapo ndipo suala la kukumbuka na kusahau litakapokuwa na maana mpya kwa Zanzibar Mpya na vizazi vyake – Ameen.  

Monday 12 May 2014



Kushoto: Abdallah Kassim Hanga, Julius Nyerere na Rais Pompidou wa Ufaransa

Waliokaa Kushoto Kwenda Kulia: Abdallah Kassim Hanga na Abeid Amani Karume

Leo hii asubuhi katika Bunge la Bajeti Mheshimiwa Tundu Lissu kamtaja Kassim Hanga kuwa aliuliwa...

In Sha Allah tunatayarisha kitu kwa kumbukumbu ya Hanga na wenzake waliopoteza maisha baada ya kuipindua serikali ya Sheikh Mohamed Shamte...

Fuatilia ukurasa huu...

Haya hapa chini ni baadhi ya maneno aliyosema Mheshimiwa Lissu Bungeni kuhusu kuuliwa kwa Abdallah Kassim Hanga, Abdulaziz Twala,  Saleh Saadalla, Othman Shariff, Mdungi Ussi na Jaha Ubwa...


''Swali kuu ambalo sisi tuliozaliwa ndani ya Muungano tunataka lijibiwe kwa ukweli kabisa ni ‘waasisi’ hawa wengine wa Muungano, akina Abdallah Kassim Hanga, Abdulaziz Twala na Saleh Saadalla Akida kwa upande wa Zanzibar; na Oscar Kambona, Bhoke Munanka na Job Lusinde kwa upande wa Tanganyika walipotelea wapi na kwanini hawatajwi katika historia rasmi ya Muungano na waasisi wake? Kassim Hanga alikuwa Waziri Mkuu na baadaye Makamu wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar; wakati Twala alikuwa Waziri wa Fedha wa Serikali hiyo na Saleh Saadalla alikuwa mjumbe wa Baraza la Mapinduzi. Kwa upande wa Tanganyika, Oscar Kambona alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ulinzi wakati wa Mapinduzi ya Zanzibar na baadaye wakati wa kuzaliwa kwa Muungano; Bhoke Munanka alikuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais mwenye dhamana ya masuala ya usalama, na Job Lusinde alikuwa Waziri wa Serikali za Mitaa. Katika Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru!,  Ghassany ameonyesha jinsi ambavyo akina Hanga, Twala na Saadalla pamoja na viongozi wengine waandamizi katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kama vile Othman Shariff, Mdungi Ussi na Jaha Ubwa waliuawa na kuzikwa katika handaki moja katika sehemu inayoitwa Kama, nje kidogo ya mji wa Zanzibar. Sisi wa kizazi cha Muungano tunataka kujua ukweli juu ya makosa waliyoyafanya hawa waasisi wa Muungano hadi wakauawa na kuzikwa katika kaburi au handaki moja. Tunataka kujua ukweli kama walifanya makosa walishtakiwa katika mahakama gani iliyowahukumu adhabu ya kifo. Aidha, tunataka kuambiwa ukweli kwa nini mchango wao katika kuzaliwa kwa Muungano umefichwa kwa muda wote wa nusu karne ya Muungano huu.'' 


Job Lusinde kama anavyoonekana hivi sasa
Wakati Dk. Harith Ghassany anaandika kitabu chake, ''Kwaheri Ukoloni Kwaheri Uhuru,'' siku moja usiku kanipigia simu kutoka Washington. Wakati ule mimi naishi Tanga. Dk. Ghassany akaniuliza kuhusu Hanga nadhani katika mazungumzo yetu siku za nyuma nilipata kumweleza kuwa nikimjua Hanga katika utoto wangu. Baada ya kumpa kisa hiki sikumaliza akanikatisha na kunambia angependa anirekodi katika kinasa sauti ili atumie maelezo yangu kwenye kitabu. hapa chini ndiyo niliyosema kuhusu Hanga na ndivyo yalivyo katika kitabu:

''Mimi nikiishi na baba yangu mtaa wa Somali, namba 22. Klabu ya mwanzo maarufu ya Kilwa Jazz Band ilikuwa kwenye nyumba ya mama yake Abdu Kigunya. Mbele ya nyumba yao ikifika kama saa tisa, kumi, laasiri, wazee walikuwa wanaweka jamvi pale, wanacheza bao. Sasa hivi ukenda pamejengwa majumba ya maghorofa. Hanga akija pale mtaa wa Gogo, kona na Mtaa wa Mchikichi, nyumba ya kona barazani wazee wametandika majamvi wanacheza bao. Mimi nilimjuwa Hanga kwa sababu nikimuona kwenye magazeti. Na wakati ule mawaziri wakitembeya na yale magari meusi yakiitwa “Humber.” Sikumbuki kumuona Hanga kuja pale na gari. Basi ikapita, mapinduzi Unguja yakatokeya sisi wadogo, hatujui nini kinachotokea. Mwaka 67 nadhani, pale Mnazi Mmoja, Dar es Salaam, Anatoglou Hall, tukicheza mpira wa miguu pale. Mambo yalianza Mnazi Mmoja katika mkutano wa hadhara. Hanga katolewa jela Ukonga kaletwa pale kuadhiriwa na Nyerere. Sisi ni watoto, mambo yale na nyimbo zile lazima tujumuike. Hanga akaletwa pale. Namuona Hanga mimi kwa macho yangu ya kitoto na miwani yake ile. 



Abdallah Kassim Hanga na Julius Nyerere

Hanga alikuwa mwembamba na mrefu na alikuwa na ''thick hair.'' Alikuwa mtu mwenye kupendeza. Kaja pale na uso ulionyongonyeya. Lakini sisi hatujui kinachotendeka. Watoto wa Kiswahili miaka 14, 15, 16, ni wadogo. Hatujui kinatendeka nini. Lakini mimi najua kuwa yule pale Hanga namuona kuwa ni mfungwa. Hanga miwani iko puani uso umemparama kama jiwe la kiama, madevu yamemjaa. Anaadhiriwa! Jua la saa sita mchana linampiga vizuri. Kwa pale kukaa na kajiinamia nilijuwa kuwa mambo si mazuri. Nyerere pale anazungumza na wote wanasikiliza. Nyerere unajua. Nyerere alikuwa ni, ''orator.'' Na kuna kumuuwa mtu kiungwana. Nakumbuka incident moja Nyerere anamuonyesha kidole Hanga anasema “hili, hili, hili. Hana lolote. Hakuna lolote anaweza kufanya huyu. Afadhali huyu mwanzake [Babu].” Ukitizama kwenye Tanganyika Standard, wakati ule bado halikuchukuliwa na serikali, wakati ule, ''editor,'' ni yule Muingereza, Brandon Grimshaw. Utakuta full page. Mimi kwa jicho langu nimeona kwa sababu baba yangu mimi akinunua lile gazeti. Picha ya Hanga iko mbele na madevu na miwani yake ile. Si mimi tu, watu wengi wanakumbuka hiki kisa. Mimi baba yangu rafiki zake walikuwa Jaha Ubwa, Twala…Wakitembeleyana zamani wakati wa Easter…baba yangu alikuwa memba wa band ya Black Birds ya Bwana Ally Sykes. 



Siku Nyerere Alipomuadhiri Hanga Viwanja Vya Mnazi Mmoja
Mbele ya Kibarua Bar Nyuma ya  Ukumbi  wa Arnatouglo
Hanga Alitolewa Jela Ukonga Kuletwa Pale Makhsusi kwa Shughuli Hiyo
Baada ya Siku Hii Hanga Hakuoenekana Tena

Nadhani kule ndo walikofanya urafiki na hawa jamaa wa Zanzibar. Picha yangu mimi ya Mzanzibari, wakija kule nyumbani, unamuamkia na suala lilikuwa “wewe umeshahitimu wewe.” Na ile ''sophistication'' za wake zao wakija nao pale, yale mavazi, mabuibui, uturi ule, vile vyakula wakiandaa nyumbani pale. Hi ndo picha yangu ya Mzanzibari. Palikuwa na picha pale ukutani ya marahemu father wangu na kina Jaha Ubwa. Ile picha ikapotea pale ukutani. Ikawa haionekani tena. Lakini palikuwa mzee akizungumza habari za akina Twala alikuwa akinong’ona. Nahisi mzee alikuwa ana khofu. Ile ni dalili ya woga. Kitu kibaya kimetendeka. Lakini lazima aulize. Vipi mkewe. Watoto vipi? Lakini hawezi kusema kwa sauti. Siku nilipokuja kukutana na Ali Nabwa aliponielezeya habari za Zanzibar, nikamwambia mimi baba yangu alikuwa ana masikilizano na akina Twala na yeye akaanza ku open up sasa. Nikasema duu! Alipotoka jela Ali Nabwa alikuja pale mtaa wa Narungombe na Skukuu. Pale palikuwa na baraza maarufu sana ya Saigon Football Club. Nabwa alikuwa anakuja pale. Tukitoka tukikaa pembeni tukizungumza chamber. Nilijua baadaye sana kuwa kumbe alikuwa ametoka jela. Pale ndo nilipoanza kuwaona Wazanzibari kwa sura nyingine sasa. Kumbe zile bashasha zinadanganya?


Saigon Club Katika Miaka ya 1970
Kutoka Kushoto Kwenda Kulia: Ahmed Abdallah (marehemu), Mwandishi na
Boi Juma Risasi Hapa Ndipo Mwandishi Alipokuwa Akikutana na Ali Nabwa
Katika Miaka ya 1970 kwa Mazungumzo
Kuwa Hanga ndiye aliyekuwa kinara wa Mapinduzi ya Zanzibar hili si jambo lenye utata tena. Ikiwa hivyo ndivyo Hanga hatoweza kuutua mzigo wa roho zilizopotea katika mapinduzi hayo. Ikiwa Hanga atalaumiwa kwa vifo vya maelfu ya Wazanzibari nani alaumiwe kwa mauti yaliomfika Hanga tena kwa kuuliwa kishenzi kwani hapana neno zaidi ya hilo linaloweza kutosheleza kuelezea jinsi Hanga alivyouliwa. Kichekesho kikubwa ni kuwa wale waliopoteza roho na kutangulia mbele ya haki yao yalikuwa yamekwisha. Lakini kwa wale wajane na mayatima waliobakia nyuma na kuhangaika, kifo cha Hanga na wenzake katika wale waliofanikisha mapinduzi kuuliwa kwao kulikuwa miujiza ya aina yake, uchawi usioelezeka nani fundi wake. Ilikuwa vigumu kueleza. Ingeeleweka vyema endapo kisasi cha kuitoa roho ya Hanga kingetimizwa kwa mikono ya maadui zake waliopinduliwa. Haikuwa hivyo.

Wale wajane na mayatima walililipiziwa kisasi na watu waliokuwa maadui wakubwa wa hao waliopinduliwa. Vipi Hanga kiongozi mkuu wa mapinduzi aje kuwa adui wa mapinduzi yenyewe kiasi cha kuwa hukumu ya kumtosheleza haikuwa kifo tu bali kifo cha kishenzi? Fikra za Hanga zilikuwaje pale alipokuwa peke yake ndani ya selo Ukonga Prison…usiku ukimpita bila ya hata lepe la usingizi akiwaza yanayomkabili. Nini kilikuwa kikimpitikia katika ubongo wake wakati wauaji wake walipomtoa katika selo yake na yeye akawakabili ilhali akijua kuwa walikuwa wamekuja kuitoa roho yake. Fikra yake ilikwenda wapi? Ilikwenda kwa Sultan Jamshid bin Abdullah na Masultani wengine waliopita ambao wameiaga dunia mikono yao ikiwa haina damu, au kwa Abeid Amani Karume aliyeingia madarakani kwa mapanga ya Wamakonde wakata mkonge kutoka Sakura na Kipumbwi? Fikra ya Hanga ilielekea wapi? Kwa Nyerere aliyemsaliti?

Hakika ni wazi hakutegemea mapinduzi aliyoyaasisi yangemgeukia na kuwa sababu ya yeye kutolewa roho kwa kuuliwa kishenzi. Jambo la kusikitisha ni kuwa hadi pale alipokamatwa na kuwekwa jela Ukonga na kufikishwa mbele ya mkutano wa hadhara na kuadhiriwa na Julius Nyerere tayari alikuwa keshapoteza kila kitu achilia mbali dira ya mapinduzi aliyokusudia ingeongoza Zanzibar. Hanga hakuwa kamwe na uwezo wa kumfanya Karume lolote kwani Karume tayari alikuwa chini ya mbawa za Nyerere, ngome ambayo Hanga asingeweza kuitikisa achalia mbali kuibomoa. Muungano baina ya Tanganyika na Zanzibar ilikuwa hirizi tosha ya kumkinga Karume. Katika mkasa wa kuuliwa kwa Hanga ndipo msemaji mmoja akasema, “Maiti toka makaburini mwao walionyesha ujuzi wa kufanya miujiza na uchawi wao kwani laiti kifo cha Hanga kingesababishwa na wale waliyopinduliwa kisasi chake kingekuwa cha kutisha. Ilibidi Hanga kwa miujiza ya maiti zile auliwe na wale wale aliowaweka madarakani watu ambao hapakuwepo na sababu ya wao kumuona adui. Halikudondoka chozi kwa kifo cha Hanga. Kila aliyepata mnong’ono wa kuuliwa kwake alikuwa kimya kama vile ile taarifa ya kifo haimuhusu.” 


Hebu tumsome Dk. Ghassany ameandika nini katika kitabu chake Kwaheri Ukoloni Kwaheri Uhuru kuhusu Hanga wakati yuko nyumbani kwa Oscar Kambona anajitayarisha kurejea Tanzania:


''Nnavokumbuka mimi Oscar akatwambia sikilizeni bwana. Mimi nimekwiteni hapa mje mseme na ndugu yenu na mzee wenu huyu, Abdalla Kassim Hanga amekuja hapa na anataka kurudi nyumbani. Hajataja pahala. Na mimi nimemkataza. Nimemwambia huu si wakti mzuri ni bora yeye asiende. Ama angelibaki huko huko West Africa anokotoka kwa mkewe, au abaki hapa London lakini kakataa, anataka lazma arudi. Na mie na hofu maisha yake kuwa akifika kule hatoweza kupata salama. Kwanza kuwa yeye amefikia kwangu, anajulikana yeye na mimi ni rafiki, Nyerere atajuwa zaidi/uzuri hayo kuwa mimi tangu tuko kule tunasikilizana mimi na ndugu huyu Abdalla. Kwa hali hiyo mimi namwambia. Na yeye Abdalla anasema hana ugomvi na Nyerere.

Sasa mimi nimekwiteni mzungumze naye, mseme naye. Akatuchukuwa akatupeleka kwenye chumba akasema “Abdalla, hebu zungumza nao hawa jamaa wamekuja kukuamkia.” Tukaingia sie chumbani akatuacha mimi na Ahmed [Rajab] na Abdalla. Peke yetu watu watatu. Ndivo navokumbuka mie na ndivo anavokumbuka Ahmed [Rajab].
Ahmed Rajab 
Mimi sikumbuki ile nilikwenda railway station. Kile mimi sijakumbuka. Kama ulivosema, mimi nyumba nilikuwa naijuwa, sina haja ya Kasembe kunpeleka. Lakini inaweza kuwa nimekwenda mimi na Kasembe kumpokea Ahmed Rajab. Yeye Ahmed kafkiri tu na mie ni mgeni. Hajajuwa kuwa mimi na Kambona tunajuwana na jirani, na nyumba yangu mie na yake si mbali.

Ahmed Rajab ndo anosema, tumefika alofunguwa mlango ni Oscar Kambona, na akatuonyesha chumba. Hajaeleza nini Kambona katwambia. Lakini mimi nakumbuka Kambona katwambia kwanza, “semeni naye.” Yeye kazungumza moja kwa moja, sisi tumekaribishwa tumekwenda kwa Abdalla. Yeye Ahmed amekumbuka mambo mimi sijayakumbuka. Kwa sababu, kasema tulipofika Abdalla Hanga katwambia skizeni: nyinyi ni vijana, watoto kwa sasa, lakini kesho nyie ndo mtakuwa viongozi. Nna maneno nnataka kukwambieni. Tukawa sasa tumekaa tunamsikiliza nini atasema.

Anasema nataka kukwambieni juu ya habari ya mapinduzi yetu ya Zanzibar. Kuna mabaya ambayo tuliyafanya na kabla sijasema lolote nnakutakeni jambo moja muhimu mlikumbuke. Msije mkakubali kufata siasa za ukabila.4 Siasa za ukabila ndizo zinotuletea matatizo na ndizo zitozidi kutuletea matatizo. Hilo ni jambo la mwanzo ambaye yeye Hanga katwambia. Akasema mimi (Hanga) nilivoondoka Zanzibar kupelekwa Dar es Salaam, kuwa Waziri wa kule, badili ya kuwa Vice-President [Makamo wa Rais] huku na Mzee Karume, alivopelekwa bara, anasema jambo moja katika mambo aloyafanya ni kuwasaidia Wazanzibari walokimbia kutoka Zanzibar wakakaa pale, wale ambao wataalamu, kuwatafutia kazi. Akataja majina. Akamtaja Maalim Salim Sanura, na akawataja wengine, mimi siwakumbuki. Kuwatafutia kazi na wakapewa kazi serkalini. Hata ikafika akaanza kusemwa, akalaumiwa, kuwa Abdalla, mbona unakwenda kinyume sasa? Hawa si ndo tuliowapinduwa, mbona wewe sasa hapa unawasaidia? Unawapokea? Akasema bwana, hapa mimi naona ni Mzanzibari tu hapa. Hawa wote ni Wazanzibari bwana. Na hawako nchi nyengine. Wako na sisi pamoja hapa. Kwa hali hiyo yeye anasema ule ndo uzi anataka sisi tuufate. Tusibaguwane.

Jambo la pili akasema, sisi Mungu atusamehe, tumefanya mambo mengi ambayo mabaya, tumedhulumu, tumechukuwa watoto na wake za watu, na Mwenye Enzi Mungu ndiye anojuwa. Basi mimi namuomba Mweye Enzi Mungu anisamehe na ninajuta kwa haya nlioyafanya. Ahmed Rajab akamuuliza suala. Akamwambia, mzee, lakini wewe na Janab [Babu] mnaskizana vipi kisiasa? Akamwambia, mimi na Babu sote wawili ni Marxists lakini Babu si tishio kwa Karume. Mimi ndo tishio. Mimi ndo ni tishio juu ya Karume, lakini Babu is not [si tishio]. Hiyo tafauti yangu mimi na Babu, anasema. Kwa Unguja. Sasa ndio tukamuuliza, Vipi ikawa wewe ndo tishio? Yeye Ahmed Rajab ndo anamuuliza.

Rome ilijaribu kuingia kati katika ugomvi wa Oscar na Nyerere na ilishindwa. Kambona alinieleza. Hata makanisa yamejaribu. Ugomvi ulikuwa mkubwa na hiyo akijuwa yeye zaidi Kambona ndo mana akahofu Abdalla asirudi. Ile imani yake ilikuwa kubwa kuwa Nyerere hatomdhuru. Na yeye akiona watu wangapi wamepotea lakini hajafikiria atakuja kuwa yeye.

Tukasema naye tukamwambia kweli hayo maneno anayoyasema Oscar inaonyesha ni bora usirudi kwa sasa. Akasema hapa kuna mambo mawili. Moja, kuna kutosikilizana baina ya Oscar Kambona na Mheshimiwa Nyerere, Raisi Nyerere. Sasa huyu bwana akisema mimi nisirudi anazungumzia kule kutosikilizana baina yake yeye na Raisi Nyerere. Sasa anahisi mie nikirudi labda kwa sababu mimi nimefikia kwake au ni rafki yake Nyerere anaweza akachukuwa hatuwa. Mimi nimeshafanya kazi na Nyerere na namjuwa uzuri mzee Nyerere, mimi na yeye hatuna ugomvi wowote. Abdalla Kassim Hanga anasema kuwa yeye na Nyerere hawana ugomvi. Na yeye ikiwa anarudi harejei kwa Zanzibar. Atarudi anakwenda zake akakae nyumbani Dar es Salaam. La pili alisema, kuna ukweli wa kuwa mimi na Mzee Abedi Amani Karume kuwa hatuskizani na kusema kweli si makosa yangu. Akasema Abdalla, jambo dogo sana limemfanya Mzee Abedi anichukie mimi hata ikawa mimi nikienda Zanzibar sasa siwezi kukaa nikalala Zanzibar. Lazima siku ileile nirudi Dar es Salaam.

Na hili jambo anasema, mimi nilivokuwa niko Tanzania Bara na Dar es Salaam ni mmoja katika Mawaziri, nilikuwa nnakwenda Zanzibar mara kwa mara. Na nikenda nikifia katika nyumba ilioko Migombani ambayo niliwahi kukaa nilivokuwa Makamo wa Raisi. Wakati mmoja nafikiri baada ya mapinduzi, President wa Zanzibar alikuwa ni Karume na Makamo alikuwa Hanga. Sasa ile nyumba ya Migombani ikawa yeye bado Hanga hajairejesha serikalini kila akienda Zanzibar anafikia pale. Siku katika siku alizokuweko pale anasema yeye kaja kafikia nyumbani pale Migombani na kila akenda watu wakipata habari kuwa Abdalla kaja, watu, jamaa, ndugu na marafiki, walikuwa wanakwenda kumuona na kuzungumza naye, na wengineo wanakuwa nayo mahitajio yao wanakwenda kumuomba awasaidie. Sasa sku moja hiyo Mzee Karume anatokea njia ya uwanja wa ndege kwenda zake mjini akapita pale Migombani akaona magari, akauliza. Kuna nini hapa, mbona magari mengi? Akaambiwa basi lazim Mzee Abdalla Kassim Hanga kaja. “Ala, sasa yeye kila akija lazma iwe namna hii?” Akaambiwa, yeye akija watu wanakuja hapa kumuamkia na kuonana naye. Basi jambo hilo anavosema Abdalla Kassim Hanga ndilo liloanzisha ugomvi baina yake na Mzee Karume. Karume akawa hataki tena na ikawa na yeye Abdalla akenda Zanzibar hafikii tena katika nyumba ile. Akakataa kabisa.

Lakini inaskitisha kuwa tangu wakati ule yeye yupo pale London habari zishafika Cairo. Walioko Cairo maambassador wa pale wameshapeleka habari Tanzania kwa Mzee Nyerere. Ikawa serikali ninavosikia wamekaa wakimngojea arejee tu. Yeye Hanga hajajuwa, wala sisi hatujajuwa.'' 


Ukimsoma Dk. Ghassany anavyoeleza jinsi Hanga alivyoonywa asirejee Tanzania na yeye akakaidi unaweza kusema kuwa kifo kilikuwa kinamwita. Hebu sikiliza na kisa hiki kilichotokea uwanja wa ndege wa Dar es Salaam siku Hanga alipotua kutoka London kwa Egypt Air. Mpashaji habari wangu anasema:

''Wakati ule mimi nilikuwa meneja wa shirika moja la ndege. Nilikuwa uwanjani nikamuona Bi. Mkubwa. Huyu alikuwa mkewe Hanga, mwanamke wa Kingazija. Nikamuuliza mbona yuko pale akanambia kuwa alikuwa amekuja kumpokea Hanga. Nilishtuka sana. Mimi ni Mzanzibari na nikijuana na Hanga kwa miaka mingi na nilikuwa nasikia mengi. Hanga alipofika nilikwenda kumlaki na tukatoka sote nje ya uwanja na hapo nikamualika yeye na mkewe chakula cha mchana hapo hapo uwanja wa ndege. Wakati tunatoka nje ya uwanja nilimuuliza Hanga iweje karejea nchini wakati kama ule. Hanga akanijibu kuwa hapana kitu. Mimi sikuridhika. Tulipomaliza kula na tukawa tanazungumza nilitaka kwa mara nyingine niufungue moyo wangu kwa Hanga. Sikumbuki nilifanya nini lakini niliweza kumtoa mkewe pale mezani tukabaki sie wawili, mimi na Hanga. Hapo nikamwambia Hanga kuwa ni vyema kama akirejea London na ndege ile ile aliyokujanayo. Hanga hakuniskiliza. Jioni mimi nikamtafuta Ali Nabwa wakati ule anafanyakazi Tanganyika Standard. Nikampa habari kuwa Hanga yuko mjini. Tulimtafuta mji mzima mwisho tukampata Oyster Bay kumbe kafikia kwenye nyumba ya Kambona. Tukaja hadi Magomeni kwa Maalim Matar tukafanya dua. Ali Nabwa kumbe alikuwa amewaambia Tanganyika Standard wasubiri habari muhimu wachelewe kidogo kuchapa gazeti. Siku ya pili Tanganyika Standard ikachapa habari ukurasa wa mbele kuwa Hanga amerejea nchini. Haikuchukua siku Hanga akakamatwa.''


Ali Nabwa


Maalim Mohamed Matar

Kutoka kushoto kwenda kulia ni Abdulaziz Twala (Msaidizi Waziri katika Ofisi ya Rais), Aboud Jumbe (Waziri wa Siha na Majumba), Hasnu Makame (Waziri wa Fedha na Maendeleo), Othman Shariff (Waziri waElimu na Mila), Abdulrahman Babu (Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara), Abeid Karume (Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar), Abdallah Kassim Hanga (Makamu wa Rais), Saleh Saadalla (Waziri wa Kilimo), Idris Abdul Wakil (Waziri wa Kazi, Njia na Nguvu za Umeme) na Hassan Nassor Moyo (Msaidizi Waziri wa Kazi, Njia na Nguvu za Umeme).Abdalla Kassim Hanga

Thursday 26 December 2013






Mohamed Omari Mkwawa (Tindo) mwanamapinduzi aliyesahauliwa,  mwamasishaji, mpelelezi, mtekelezaji mipango ya upigaji kura Zanzibar 1963, mwanamapinduzi Zanzibar 1964,  askari wa msituni wa Afro Shirazi Party, mvushaji askari mamluki wa Kimakonde na makabila mengineo kwenda Zanzibar kupiga kura na kushiriki katika mapinduzi akiwa amekishika kitabu Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru!




Mmoja wa washirika wa Mohamed Omari Mkwawa alikuwa Victor Mkello.


Photo

Kassim Hanga ni huyo aliyekaa chini ya jukwaa kavaa miwani. Aliyevaa sare ya polisi ni Hamza Aziz kushotoni kwake ni Andrew Shija aliyevaa pama. Aliyekaa mbele ya Kassim Hanga ni Omari Londo. Nyerere ndiye huyo katika ulingo akihutubia.  Hapo ni Mnazi Moja. Baada ya mkutano huu Hanga alirejeshwa Zanzibar na huko akauawa mwaka 1967 au 1968

Utangulizi
Kwa kipindi kirefu historia ya mapinduzi ya Zanzibar ilikuwa ni ile historia rasmi ambayo imeathiri historia nyingi Afrika. Viongozi wa Afrika wanapenda ile historia itakayowakweza na kuwaonyesha wao katika mwanga wa kupendeza. Vinginevyo historia hiyo haitakiwi. Wazalendo wenyewe hawakuwa na hamu ya kuandika historia hii na watu wa nje walioandika historia ya mapinduzi ya Zanzibar hawakupata kuifanyia haki historia ya Zanzibar labda kwa ugeni wao na kwa kuyaamini maelezo yaliyokuwa “wazi” kwa wakati ule, mfano mkubwa ukiwa ni kule kuamini kuwa mapinduzi ya Zanzibar yalipangwa na makomredi wa Umma Party.

Hapajakuwapo udanganyifu mkubwa katika uandishi na utafiti kama huu. Dkt Ghassany amekiweka chano uwanjani bila kawa. Akizungumza na Abdushakur Aboud wa Sauti ya Amerika Dkt Ghassany amesema kuwa historia ya Zanzibar ni historia ya kujijuwa maisha yake akiwa mjukuu wa babu wa mababu Muomani na mabibi wa Kimanyema na Kimwera– mchanganyiko wa damu ya Kiarabu na Kiafrika. Hii kwa hakika ndiyo historia ya wananchi wa Zanzibar. Ni tabu sana kumpata huyo Muarabu Zanzibar kila umuonae Muarabu basi ana mjomba na shangazi Mwafrika. Maadui wa Zanzibar wakiweka mkazo katika ubaguzi wa rangi na kuwafitinisha Wazanzibari. Ukweli huu ndiyo chanzo cha matatizo yote yaliyoikumba Zanzibar toka vyama vya siasa vilipoanza katika miaka 1950 na matatizo yaliyosababisha mauaji ya mwisho yakiwa mwaka 2001.

Mohamed Omari Mkwawa
Mwaka 1995 wakati wa uchaguzi wa kwanza wa vyama vyingi Tanzania nilibahatika kufuatana na mgombea urais wa CUF Prof. Ibrahim Haruna Lipumba katika kampeni za uchaguzi katika mikoa ya Kilimanjaro na Tanga. Prof. Lipumba alifanya mkutano mkubwa sana Tangamano kiasi cha kuishtua CCM. Baada ya mkutano ule Prof. Lipumba na ujumbe wake walialikwa nyumbani kwa mama mmoja akijulikana kama Mama Ummie (sasa ni marehemu) ambako walifanyiwa dhifa kubwa. Kote tukipita mitaa ya Tanga msafara wetu ulikuwa ukishangiliwa kwa nguvu sana. CUF ilikuwa imeingia Tanga kwa kishindo kikubwa.

Mimi kazi yangu ilikuwa kuangalia niliyokuwanayaona na kupiga picha. Kwa hakika nilikuwa nikishuhudia historia ikijiandika. Historia ambayo ilikuwa imeshahibiana sana na ile ya wakati wa kudai uhuru wa Tanganyikakatika miaka 1950. Lakini ninalotaka kusema si hili bali ni picha ambayo niliipiga ndani ya nyumba ya Mama Ummie. Picha hii ilikuwa inamuonyesha mzee mmoja wa makamo aliyevaa fulana ya CUF mbele ikiwa na picha ya Prof. Lipumba. Mzee huyu alikuwa amekaa nyuma ya Prof. Lipumba. Kwa wakati ule picha hii haikuwa na maana yoyote kwangu na hata nilipokuwa naitazama mara kwa mara sura yake si iliyokuwa inanivutia bali ile fulana ya CUF aliyovaa ambayo ilikuwa na picha ya rafiki yangu Prof. Lipumba.

Mungu ana mipango yake. Mihangaiko ya kutafuta riziki yakanihamishia Tanga na nikawa karibu sana na baadhi ya viongozi wa  CUF na wanachama wake. Sasa hapa ndipo nilipokujakuonana uso kwa uso na mzee yule kwenye picha yangu niliyoipiga hata kwa wakati ule ilikuwa miaka mingi iliyopita. Jina la huyu mzee wangu ni Mohamed Omar Mkwawa.  Ilikuwa katika barza yetu ya kawaida  ya kunywa kahawa na kula pweza huku tukijadili historia ya Tanzaniaambako siku moja Mzee Mkwawa alinambia, “Mohamed nataka nikuambie kitu. Unajua mimi nimehusika sana katika mapinduzi ya Zanzibar?”

Nilimuangalia Mzee Mkwawa kwa makini. Fikra yangu ya utafiti na uandishi ishashtuka haipo tena usingizini. Mzee Mkwawa aliendelea, “Mimi ndiye niliyekuwa nikiwavusha Wamakonde kutoka Kipumbwi kwenda Zanzibarkuipigia kura ASP na wakati wa mapinduzi mie ndiye niliyewavusha Wamakonde kwenda kuipindua serikali ya Jamshid.” Sasa moyo wangu ukaanza kudunda kwa nguvu. Naisemesha nafsi yangu, “Huyu mzee anajua uzito wa maneno haya?” Tuishie hapa. Kuanzia siku ile nikawa sasa namtazama Mzee Mkwawa kwa jicho jingine na heshima yangu kwake ikawa imepanda maradufu. Nilikuwa nimeshatambua kuwa Mzee Mohamed Omari Mkwawa alikuwa mmoja wa wanamapinduzi waliosahaulika katika historia ya Tanganyika na Zanzibar. Juu ya hayo nilishangazwa na kitu kimoja. Iweje leo huyu mwanamapinduzi wa ASP ambae Abeid Amani Karume alimpa jina la “Tindo” kwa ujasiri wake amekuwa mstari wa mbele CUF chama ambacho kinanasibishwa na Hizbu hasimu mkubwa wa ASP?


Dr Harith Ghassany
Nilikutana na Dr Harith Ghassany mwaka 1999 nyumbani kwake Maskati, Oman. Naikumbuka siku ile kama jana vile. Kanipeleka kwake mwenyeji wangu Farouk Abdulla lakini kabla ya kunipeleka nilikuwa nimeshalisikia jina lake mara nyingi sana pale Maskati kila nikikutana na jamaa wenye asili ya Tanzania jina lake litaibuka. Katika fikra yangu ikanijia kuwa Dkt Ghassany atakuwa ni mtu mzima. Sielewe kwa nini nilipata picha hii. Tulipopiga hodi na akatokea Dkt Ghassany kuja kutufungulia mlango nikapata mshangao mkubwa.

Aliyekuwa mbele yangu alikuwa ni kijana mdogo sana tofauti na nilivyodhani. Kwa njia ya utani hata kabla sijatoa salamu. Nikamgeukia Farouk nikasema, ”Ah! Dkt Ghassany, Dkt Ghassany, Dkt mwenyewe ndiye huyu?” Mila na tamaduni za watu wa pwani wakikutana hazipishani. Maskhara ni dalili ya mapenzi. Dkt Ghassany pale pale alipokea yale maskhara na akajibu, ”Bwana  wangu we wanakutisha bure kwani we ulidhani litakuwa jitu kubwa?” Urafiki na udugu wetu umedumu hadi leo na ndipo katika mazungumzo aliponifahamisha kuwa anataka kuandika historia ya kweli ya mapinduzi ya Zanzibar. Hapo ndipo nilipomjuvya kuhusu Mzee Mkwawa na nikamuomba aje Tanga amuhoji.

Kitu kimoja mashuhuri kwa mashujaa wa harakati za siasa katika Tanzania ni kuwa takriban wote wana hali ngumu sana za maisha. Sikujua vyema hali ya Mzee Mkwawa hadi nilipofika nyumbani kwake na Dkt Ghassany. Utu uzima na udhaifu wa maisha ulikuwa umempiga barabara. Nilimjulisha Dkt Ghassany kwa Mzee Mkwawa na kuwaacha waendelee na maongezi yao. Niliporudi mchana kumchukua Dkt Ghassany rafiki yangu alinambia nimuache nije jioni kumfuata. Niliporudi jioni nilimkuta Dkt Ghassany amechoka na uso umesawijika. Tukiwa ndani ya  gari yangu tunaondoka nikamuuliza kulikoni. Dkt Ghassany akanambia maneno ambayo hadi leo yamebaki kichwani mwangu, ”Mohamed ufunguo wa kitabu changu anao Mzee Mkwawa na kama nisingeonana nae utafiti wangu wote wa kabla ungelikuwa hauna maana yoyote.”

Dkt Ghassany alikuwa amechukuliwa na Mzee Mkwawa katika safari ya zaidi ya nusu karne. Mzee Mkwawa akimshika mkono kwanza kumpeleka Pemba ambako akiwa kijana wa kiasi cha miaka 25 akifanya kazi ya uashi. Huo ndio ulikuwa wakati wa siasa za ASP na Hizbu zimepamba moto. Mzee Mkwawa alikuwa mmoja wa wachezaji wa ngoma ile hata kama alikuwa anatoka Tanganyika. Dkt Harith akavushwa na kuletwa pwani ya Kipumbwi na Sakura ambako Mzee  Mkwawa alikuwa akisimamia kambi ya mafunzo iliyokuwa msituni ya wakata mkonge wengi wao wakiwa Wamakonde, kambi ambayo ilitoa askari waliotumika kuipindua serikali ya Mohamed Shamte 12 Aprili 1964.

Dkt Ghassany hakuwa amejitayarisha kwa haya. Alishangwazwa na uwezo wa kumbukumbu wa Mzee Mkwawa, akitaja majina na mahali na akirudia mazungumzo neno kwa neno kati yake na maofisa wa serikali ya Tanganyika kutoka vyombo vya usalama waliomtia katika operesheni maalum ya kuipindua Zanzibar kutoka Tanganyika. Majina ya Abdulla Kassim Hanga, Jumanne Abdallah, Ali Mwinyi Tambwe, Victor Mkello, Oscar Kambona na wengine yakawa yanadondoka moja baada ya lingine. Taarifa hizi ndizo zilizommaliza Dkt Ghassany na kumsawajisha uso.

Mimi binafsi nilipigwa na butwaa. Nilibaini kama alivyobaini Dkt Ghassany kuwa Mzee Mkwawa alikuwa hazina na tulikuwa tumevumbua mgodi wa dhahabu. Kazi yetu sasa ilikuwa kuchimba tu. Kumekuwa na uvumi kwa miaka mingi katika duru za wanasiasa wapya na wa zamani na katika wanafunzi wa historia ya Tanzania na Mapinduzi ya Zanzibar kuwa Ali Mwinyi Tambwe alihusika sana katika kupinduliwa kwa serikali ya Zanzibar lakini hakuna aliyejuwa ni kwa kiwango gani na alihusika vipi. Lakini zito ni kuwa yeye mwenyewe akiudhika sana mtu akimuuliza habari zile. Kwa nini ilikuwa hivyo? Kitabu cha Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru cha Dkt Ghassany kilikuja kutoa majibu. Hakuna binadamu apendae historia yake ihusishwe na mauaji na dhulma na kufutwa kwa nchi yake.

Kwa kipindi cha takriban miaka saba Dkt Ghassany alikuwa akija Tanga kwa mahojiano na Mzee Mkwawa na katika kipindi hicho Mzee Mkwawa alitupeleka Kipumbwi na Sakura na kutuonyesha sehemu zile ambazo walikuwa na kambi na wakifanya mazoezi ya kivita na matumizi ya silaha. Mkahawa ambao wale wakata mkonge walikuwa wakila chakula cha usiku kabla ya kuvushwa kwa vyombo vya bahari kwenda Unguja bado upo hadi leo ingawa kwa sasa kijumba kile hakitumiki tena kama mkawaha. Endapo itakuja siku serikali ya Zanzibar itataka kuhifadhi historia ya Mapinduzi ya Zanzibar bila shaka moja ya vitu vitakavyokuwa katika makumbusho ni picha ya hicho kibanda.

Victor Mkello
Kipumbwi haijabadilika iko kama vilevile iliyokuwa miaka ya 1960. Kipumbwi imebaki vilevile kama kijiji cha uvuvi. Mzee Mkwawa alitupeleka hadi sehemu ambapo bahari imeingia katika kijiji lakini sehemu hiyo imefunikwa na mikoko mingi na vichaka. Tuliingia ndani na kuangalia mandhari ya pale mahali. Hakika pale palikuwa sehemu nzuri ya kujificha. Leo imekuwa sehemu hii ni maarufu kwa watu wa magendo.  Mzee Mkwawa alitueleza kuwa hapo ndipo walipojificha na ndipo walipopandia vyombo vyao kwa usiri mkubwa wakati wote wakiwa wamevaa nguo matambara na kofia za makuti kama wavuvi. Tanga ilikuwa kituo muhimu cha kufanikisha mapinduzi ya Zanzibar. Haikuwa bure kuwa Ali Mwinyi Tambwe, Jumanne Abdallah na Victor Mkello walikuwa hapo na wala haistaajabishi kwa Dkt Ghassany kutueleza kuwa vinara wa mapinduzi kwa upande wa bara, Mkello na wenzake, walisubiri taarifa za mapinduzi katika mkesha ndani ya ofisi ya TANU Tanga.

Napenda kukiri kuwa sikupata kushiriki kama msikilizaji wa mahojiano wakati wa utafiti wa Kwaheri Ukoloni Kwaheri Uhuru. Kazi yangu kubwa sana ilikuwa kufungua milango na kumwendesha daktari. Kwa ufupi kazi yangu ilikuwa kumwekea mwandishi mazingira mazuri ili kazi yake iwe nyepesi. Kwa hakika ilikuwa kazi ambayo na mimi vilevile nilisoma, kujifunza mengi na kupata faida kubwa. Katika haya nakumbuka sakata la kumtafuta Victor Mkello. Leo si wengi wanaomjua Victor Mkello au hata kupata kusikia jina lake likitajwa. Lakini kwa sisi tuliokuwa wadogo tukiwa shule katika miaka ya 1960 Mkello alikuwa hapungia katika magazeti ya Ngurumo na Mwafrika. Mzee Mkwawa ndiye aliyetusaidia kumtafuta alipo. Victor Mkello ndiyo aliyekuwa ”Amiri Jeshi Mkuu” wa lile jeshi la Wamakonde lililokuwa na makao yake makuu katika mashamba ya mkonge ya Sakura na Kipumbwi. Bila ya kupata kauli ya Mkello kitabu kisingeweza kuandikika.

Ilichukua muda kuweza kumpata. Kwanza tulikwenda Muheza ambako ndiko kwao. Huko tukaambiwa kuwa hakuwapo hapo bali kwa muda mrefu alikuwa Tanga. Mwishowe tulimkuta nyumbani kwake Nguvumali. Mkello alikuwa katika kitanda cha mauti. Kisukari kilikuwa kikimla kiwiliwili chake. Hakuwa anaweza kunyanyuka kitandani wala kukaa. Kwa hakika alikuwa anasikitisha. Huyu hakuwa Victor Mkello niliyekuwa namsoma katika magazeti wala yule ambae Mzee Mkwawa alikuwa akituelezea. Mtu mjanja aliepambana na Magiriki wamiliki wa mashamba ya mkonge akitetea haki za Waafrika katika miaka ya 1960. Huyu kwa kweli hakuwa yule Victor Mkello aliyekuwa akisaidiana na TANU na Mwalimu Julius Nyerere kupigania uhuru wa Tanganyika. Hiki mbele yetu kilikuwa kivuli chake. Hapakuwa na wasiwasi wowote Victor Mkello alikuwa akisubiri malaika wa mauti amtembelee na yeye hilo alikuwa akilijua fika.

Victor Mkello na Mzee Mkwawa wanamapinduzi waliofutwa katika historia walitazamana na wakasalimiana kama vile hakuwapata kujuana. Jicho la Mkello lilikwenda kwa Dkt Ghassany kisha likaangukia kwangu kisha likarudi kwa mwanamapinduzi mwenzake Mzee Mkwawa. Baada ya utambulisho uliofanywa na Mzee Mkwawa nilihisi woga na wasiwasi kwenye sura ya Victor Mkello. Hakuwa anaamini kuwa Dkt Ghassany katoka Maskati kwa ajili ya utafiti wa historia na hili lilijidhihirisha alipofunua kinywa kuzungumza. Victor Mkello alikuwa na hisia kuwa alifuatwa kukamatwa kwa vifo vya Waarabu vilivyotokea Zanzibar wakati wa mapinduzi ili apelekwe Mahakama ya Kimataifa. Baadae Dkt Ghassany alinifahamisha kuwa jinsi Waingereza walivyomueleza katika taarifa zao za siri ambazo yeye alizisoma London zimeafikiana kabisa na jinsi alivyomuona pale. Waingereza walimsifia Mkello kwa kusema kuwa alikuwa bingwa wa kuteleza kama samaki ndani ya maji.

Kufupisha maelezo. Ilichukua karibu miaka mitatu kwa Victor Mkello kukubali kuzungumza kuhusu mapinduzi ya Zanzibar. Dkt Ghassany akienda Maskati na kurudi Tanga na kila akienda kwa Victor Mkello, Mkello hakuwa tayari kueleza kile alichokijua kuhusu mapinduzi ya Zanzibar. Kila nilipokwenda na Dkt Ghassany kumuona Mkello hali yake ilikuwa inazidi kudidimia. Sasa alikuwa kakatwa mguu mmoja kwa ajili ya kisukari. Ilikuwa katika hali ile katika siku zake za mwisho ndipo siku moja alipomwambia Dkt Ghassany aje siku ya pili na yeye atazungumza na angependa azungumze mbele ya mkewe ili amkumbushe pale atakapokuwa kasahau kitu.

Hapa ndipo ilipo moja ya sehemu tamu kabisa ya kitabu hiki Kwaheri Ukoloni Kwaheri Uhuru. Victor Mkello Amiri Jeshi Mkuu wa Mamluki wa Kimakonde alizungumza. Mimi sikushiriki katika mazungumzo yale nilijiweka pembeni ili Mkello azungumze na Dkt Ghassany kwa utulivu. Nilikuwa nimeegesha gari yangu karibu ya msikiti jirani ya nyumba ya Mkello nikimsubiri daktari akamilishe upasuaje mgonjwa apate nafuu. Mwendo wa Dkt Ghassany wa kudunda alipokuwa ananijia pale nilipoegesha gari ulidhihirisha furaha yake.

Haukupita muda mrefu baada ya mazungumzo yale na Dkt Ghassany, Victor Mkello akaaga dunia kimya kimya. Hakuna mtu aliyejua kifo chake kama ilivyokuwa vifo vingi vya mashujaa waliopigania uhuru wa Tanganyika. Hakuna hata gazeti moja lililotoa taazia yake wala hotuba hazikusomwa kaburini kwake. Mkello aliondoka katika historia ya Tanzania kimya kama jinsi mamluki wake walivyokuwa wakiingia Zanzibar kimya kimya usiku mkuu  na kwa siri, mapanga yao makali ya kukata mkonge yakiwa chini ya nguo zao za ndani yakisubiri kuivamia Zanzibar na kuua watu wasio na hatia. Kazi hii kwao haikuhitaji mafunzo kwani  mafunzo walikuwanayo muda mrefu katika kazi yao ya kukata mkonge katika mashamba ya mkonge ya Tanga. Pigo moja lilitosha kuangusha chini jani zito la mkonge seuze kiungo cha binadamu.

Kwaheri Ukoloni Kwaheri Uhuruni kitabu kilichoandikwa kwa staili ya pekee wahusika wenyewe wa matokeo katika mapinduzi kujitolea kueleza kile kilichotokea katika mapinduzi, kabla na baada yake. Kuanzia mipango ya kuangusha serikali ya Zanzibar hadi katika kuwaua wale waliokujakushukiwa kuwa ni maadui wa mapinduzi hadi kufikia hata kuweka wazi jinsi walivyoshiriki katika mengi ya kusikitisha kupelekea hata msomaji kujiuliza kwa nini hawa watu baada ya miaka yote hiyo kupita wameamua kueleza yote hayo. Vipi Abdallah Kassim Hanga, Othman Shariff, Mdungi Ussi, Jaha Ubwa, Abdulaziz Twala na wengineo walivyouliwa, nani alitoa amri ya mauaji, nani aliwauwa na katika mazingira gani. Kifo cha Karume mwenyewe kwa mtutu wa bunduki hakikuwekewa pazia na chanzo cha kuamuliwa kuwa auawe ni tofauti ya kilichozoeleka kuelezwa. Karume hakuuawa na ”wapinga mapinduzi” kama ilivyozoeleka kuelezwa katika historia rasmi.

Kwa kumaliza tusubiri mapitio ya kitabu hiki na ni wazi kuwa wasomaji watapata mengi ya kuelimisha na kuhuisha. Tunategemea wasomi wa somo la historia watakaopitia kitabu hiki watatufanyia hisani kubwa kwa kuwaleta katika picha wahusika wakuu wa mapinduzi – Mwalimu Julius Nyerere – fundi mkuu mwenye kishindo kikubwa lakini hakisikiki, mkono wake wa chuma hauonekani, uso wake nyuma ya pazia, Abdallah Kassim Hanga – kiongozi hasa na mpangaji wa mapinduzi, Victor Mkello – mtumishi wa Hanga na Nyerere  bila ya yeye mwenyewe kujua kati ya hao wawili nani aliyekuwa bingwa kumshinda mwenzake katika mchezo mchafu wa siasa ya kuiuwa Zanzibar na Wazanzibari na wengineo.

Lakini juu ya hayo yote mipango hii ilikuwa ni ya akina Nyerere, Hanga na Mkello pekee? Dkt Ghassany anaeleza nini kuhusu mkono wa Waingereza, Algeria, Misri, Wachina, Warusi, Marekani na Mayahudi? Nini kilichowasukuma hao wote katika mapinduzi ya Zanzibar? Nini kilimsukuma Nyerere, kuwapindua Waislam walioupigania Uhuru wa Tanganyika na baadae kuwapinduwa Waislam walioupigania Uhuru wa Zanzibar na kuendelea kuwadhibiti hata baada ya kuipindua Zanzibar? Nini kilichowasukuma Waingereza na Wamerekani kuachia mapinduzi yafanyike? Lakini kubwa zaidi kipi kilichowasukuma Wayahudi kuingia na kusaidia mapinduzi, ni ile chuki yaoya asili dhidi ya Waarabu au kulikuwa na jengine ambalo liliwatia khofu? Na kwanini kitabu kiitwe Kwaheri Ukoloni Kwaheri Uhuru: Zanzibarna Mapinduzi ya Afrabia? Kitabu kina majibu ya haya maswali mengine ambayo bado hayajaulizwa na chemchemu mpya za utafiti.

Dkt Ghassany anastahili pongezi kubwa sanakwa kuinusuru historia ya mapinduzi ya Zanzibarna kuwaamsha Wazanzibari na Watanganyika toka lepe zito la usingizi ili wajitambue na wamjue adui yao. Anastahiki pongezi kubwa zaidi si kwa kukiandika kitabu cha Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru bali kwa kutumia mrengo usiokuwa na mrengo. Huna pa kumuweka Dkt Ghassany na baada ya kumaliza kukisoma kitabu ukaridhika napo. Kamautafikiria kuwa kitabu ni cha CUF basi baada ya kusoma mpaka mwisho utavunjika moyo. Kama utamtumbukiza ndani ya CCM basi ataelea. La kama unataka upae nje ya masunduku na mapakacha basi utamuona katulia ndani ya uhuisho wa umoja wa Zanzibarna Tanganyika Mpya – Tanzania Mpya.

Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru ni ngoma nzito ambayo watu wameanza kuicheza hata mdundo haujaanza kupigwa! Tayari imeshaingia katika rikodi za Hansard za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tayari imeshasikika katika Sauti ya Marekani. Tayari daktari anafuatilia kwa karibu ukweli wa Maridhiano na kuwa kwa mara nyengine tena ukweli wake umeshaanza kupotoshwa na waroho na tayari historia mpya na kubwa zaidi hata kuliko ile ya Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964 imeshaanza kuvurugwa.

Watengenezaji wa filamu Hollywoodwana mtindo wa kumaliza senema zao za matokeo ya kweli kwa kueleza katika maandishi yale yaliyowafika wahusika wa kisa kilichotengenezwa hiyo senema. Huonyesha majina na mwisho wa hao wahusika, kama wahai, wako wapi, wamekufa na kama wamekufa ni kwa kuuliwa au kwa amri ya Mungu nk. Katika Kwaheri Ukoloni Kwaheri Uhuru majina ya wahusika machache ambayo yametajwa katika makala haya yako kamahivi:

1.     Mohamed Omar Mkwawa:           Yu hai na anaishi Makorola Tanga
2.     Abeid Amani Karume:                            Ameuawa 1972
3.      Abdallah Kassim Hanga:             Ameuawa 1967/68
4.     Mustafa Songambele                      Yuhai anaishi Songea.
5.     Victor Mkello                                  Amekufa kifo cha kawaida
6.     Ali Mwinyi Tambwe                      Baada ya mapinduzi alikuja kuhusika katika mchakato wa kuunda muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Amekufa kifo cha kawaida.
7.     Jumanne Abdallah                         Alitumikia serikali kwa muda mrefu hadi alipofariki kifo cha kawaida
8.     Oscar Kambona                              Aligombana na Nyerere na akakimbia nchi mwaka 1967 na kwenda kuishi uhamishoni Uingereza
9.     Kuna vigogo kadhaa ambavyo viko hai na kwa sasa wameomba majina yaoyahifadhiwe.

17 Ramadhani 1431

28 August 2010

Photo

Ali Mwinyi Tambwe na Abeid Amani Karume



Abdalla Kassim Hanga

Kuwa Hanga ndiye aliyekuwa kinara wa Mapinduzi ya Zanzibar hili si jambo lenye utata tena. Ikiwa hivyo ndivyo Hanga hatoweza kuutua mzigo wa roho zilizopotea katika mapinduzi hayo. Ikiwa Hanga atalaumiwa kwa vifo vya maelfu ya Wazanzibari nani alaumiwe kwa umauti uliomfika Hanga tena kwa kuuliwa kishenzi kwani hapana neno zaidi ya hilo linaloweza kutosheleza kuelezea jinsi Hanga alivyouliwa. Kichekesho kikubwa ni kuwa wale waliopoteza roho kwa hiyo kutangulia mbele ya haki, yao yalikuwa yamekwisha. Lakini kwa wale wajane na mayatima waliobakia nyuma wakihangaika, kifo cha Hanga na wenzake katika wale waliofanikisha mapinduzi kuuliwa kwao kulikuwa muujuza wa aina yake, uchawi usioelezeka nani fundi wake. Ilikuwa vigumu kueleza. Ingeeleweka vyema endapo kisasi cha kuitoa roho ya Hanga kingetimizwa kutoka katika mikono ya maadui zake waliopinduliwa. Haikuwa hivyo.

Wale wajane na mayatima walililipiziwa kisasi na watu waliokuwa maadui wakubwa wa waume na baba zao waliopinduliwa. Vipi Hanga kiongozi mkuu wa mapinduzi aje kuwa adui wa mapinduzi yenyewe kiasi cha kuwa hukumu ya kumtosheleza haikuwa kifo tu bali kifo cha kishenzi. Fikra ya Hanga ilikuwaje alipokuwa peke yake ndani ya selo Ukonga Prison…usiku ukimpita bila ya hata lepe la usingizi akiwaza yanayomkabili. Nini kilikuwa kikipitika katika ubongo wake wakati wauaji wake walipomtoa katika selo yake na yeye akawakabili ilhali aikijua kuwa walikuwa wamekuja kuitoa roho yake. Fikra yake ilikwenda wapi? Ilikwenda kwa Sultan Jamshid bin Abdullah aliyempindua na kwa Masultani wengi waliopita ambao wameiaga dunia mikono yao ikiwa haina damu au kwa Abeid Amani Karume aliyeingia madarakani kwa mapanga ya Wamakonde kutoka Tanganyika, wakata mkonge kutoka Tanganyika wakifanya kazi mashamba ya Sakura na Kipumbwi? Fikra ya Hanga ilielekea wapi? Kwa Nyerere aliyemsaliti?

Hakika ni wazi hakutegemea mapinduzi aliyoyasisi yangemgeukia na kuwa sababu ya yeye kutolewa roho kwa kuuliwa kishenzi. Jambo la kusikitisha ni kuwa hadi pale alipokamatwa na kuwekwa jela Ukonga na kufikishwa mbele ya mkutano wa hadhara na kuadhiriwa na Julius Nyerere tayari alikuwa keshapoteza kila kitu achilia mbali dira ya mapinduzi aliyokusudia ingeongoza Zanzibar. Hanga hakuwa kamwe na uwezo wa kumfanya Karume lolote kwani Karume tayari alikuwa chini ya mbawa za Nyerere ngome ambayo Hanga asingeweza kuitikisa achalia mbali kuibomoa. Muungano baina ya Tanganyika na Zanzibar ilikuwa hirizi tosha ya kumkinga Karume.

Katika mkasa wa kuuliwa kwa Hanga ndipo msemaji mmoja akasema, “Maiti toka makaburini mwao walionyesha ujuzi wa kufanya miujiza na uchawi wao kwani laiti kifo cha Hanga kingesababishwa na wale waliopinduliwa kisasi chake kingekuwa cha kutisha. Ilibidi Hanga kwa miujiza ya maiti zile auliwe na wale wale aliowaweka madarakani watu ambao hapakuwepo na sababu ya wao kumuona adui. Halikudondoka chozi kwa kifo cha Hanga. Kila aliyepata mnong’ono wa kuuliwa kwake alikuwa kimya kama vile ile taarifa ile ya kifo haimuhusu.


10 February 2010
Kutoka Kushoto: Farouk Abdullah, Mwandishi, Sheikh Ali Muhsin na Sheikh Abdallah Muhsin
Muscat, Oman 1999
Mzee Mkwawa Akionyesha Kitabu cha Historia ya Mapinduzi ya Zanzibar 

Mwandishi akifanya mahojiano ya televisheni  (TV Imaan) na aliyekuwa katibu wa kwanza wa
 Baraza la Mapinduzi  Zanzibar  Salim Rashid 
Aliyevaa shada la maua ni Mohamed Abdulrahman Babu, pembeni yake Ali Muhsin Barwan na mwisho
ni Mohamed Shamte 
Waliokaa kushoto ni Abdallah Kassim Hanga akifuatiwa na Abeid Amani Karume