Bi. Titi Mohamed (1926-2000)
Utangulizi



| Bi. Titi Mohamed |

Ni vigumu kusema ni lini nimekuja kumfahamu Bi. Titi Mohamed. Nimefumbua macho nikikuwa katika mitaa ya Dar es Salaam ya miaka ya 1950 na 1960 nikimuona na kumfahamu kuwa huyu ndiye Bi. Titi. Mwanamke shupavu na kiongozi wa TANU. Haikunipitikia kwa wakati ule nikiwa bado kijana mdogo wakati mwingine nikimuona katika mikutano ya TANU pale Mnazi Mmoja au Jangwani kuwa ipo siku nitakaa nitafiti historia ya mashujaa wa uhuru wa Tanganyika na Bi. Titi awe mmoja wa mashujaa wangu ambao nilataka sana kuandika maisha yao. Siku moja tu kabla ya kifo cha Bi. Titi nilikuwa nikihojiwa na mwanafunzi wa kike wa Kitaliana kutoka Chuo Kikuu cha Napoli, Italia ambae alikuwa akifanya utafiti kuhusu nafasi ya wanawake katika harakati za kudai uhuru wa Tanganyika. Binti huyu alikuwa alinihoji kuhusu Bi. Titi na akataka kujua kwa nini hatajiki katika historia ya TANU na kwa nini wanawake wenzake aliokuwa nao katika harakati za kudai uhuru wanaonekana kutopenda kueleza habari za Bi. Titi. Nilimfahamisha binti yule kuwa sisi Watanzania tuna historia rasmi ya uhuru wa Tanzania ambayo tunatakiwa kuienzi. Historia hiyo inaanza na Mwalimu Nyerere na kuishia na Mwalimu Nyerere. Historia hiyo imewatoa wazalendo wengi katika historia pamoja na Bi. Titi. Binti huyo alikuwa na masikitiko kuwa wakati alipofanya mipango ya kutaka kwenda kumuhoji Bi. Titi akamkuta mgonjwa kwa hiyo hakuweza kufanya mahojiano. Nilimfahamisha mtafiti huyu yale niliyokuwa nayajua kuhusu Bi. Titi kisha tukaagana. Siku ya pili nikapata habari kuwa Bi. Titi amefariki.
Kama alivyokuwa akisema mwenyewe marehemu, ‘Yote kuhusu mimi yameshaandikwa
nyie waandishi wa leo mtaandika nini ?’ Ni kweli Bi. Titi kaandikwa sana
lakini waliomuandika hawakummaliza, kwa kuwa hawakummaliza ndiyo maana na
mimi nimepata nguvu ya kuweza kumuandika lau kama kwa muhtasari. Kwa hakika
wengi wa waandishi hao walikuwa wageni ; na wale waandishi wazalendo
walipomwandika Bi. Titi
walimwandika kwa mtazamo wa agenda zao na vilevile bila kuwa na ujuzi wa
historia ya Dar es Salaam katika miaka ya 1950. Wageni walimtazama Bi. Titi kwa
jicho la ugeni mimi nataka kumwandika Bi. Titi kama alivyokwenda na
historia ya kudai uhuru. Nataka kumueleza
Bi. Titi tokea mwanzo alipokuwa na Mwalimu Nyerere. Nyerere akibandua hatua
yake unyayo wa Bi. Titi unafuatia. Nataka kumuandika Bi. Titi jinsi alivyopanda
kutoka msichana mdogo wa Ki-Dar es Salaam akiwa na miaka 26 hadi kufikia
umaarufu mkubwa kabisa. Kisha ghafla nyota yake ikachujuka akaanguka na
akaishia kufungwa kifungo cha maisha kwa kosa la uhaini ambalo hadi kufa kwake
alikana kuhusika. Nataka kumuandika Bi. Titi jinsi alivyotoka kifungoni akiwa
fukara mali yake yote imepotea na jinsi alivyoyakabili maisha ya upweke na
kutengwa. Nataka kumuandika Bi. Titi jinsi kwa ufundi mkubwa na subra ya hali
ya juu alivyomtegemea Mungu kama nilivyopata kumsikia akisema na Mungu akaitika
dua zake na kamrudishia siyo mali zake tu bali hata na hadhi yake. Mtaa
aliopewa kwa heshima yake ambao alinyang’anywa ukaja kurudishwa jina lake. Na
wale waliomfanyia khiyana ile wakiwa wa hai na hawana uwezo wa kufanya lolote.
Vipi Bi. Titi akaja kuuguzwa na kuzikwa na walewale watu waliolitangazia taifa
kuwa alikuwa msaliti na ta’azia zao baada ya kifo chake zikajaa maneno ya
kumsifu. Ilikuwaje ikawa hivyo?
Nikiwa mtu mzima nilifanyiwa miadi na Ally Sykes ya kuzungumza na Bi. Titi katika ya miaka ya 1990 nyumbani
kwake Upanga. Baada ya kusalimiana na kuniuliza nilikotoka nilimfahamisha
wazazi wangu. Nilishangaa kuwa alikuwa anamfahamu baba yangu vizuri sanahata
akanieleza wajihi na umbo lake. Nilimfahamisha kuwa nilikuwa nataka kuandika
maisha yake. Bi. Titi akanikatalia kwa njia ya kistaarabu kabisa. Kwa hekima
kubwa sanaaliweza kunitoa katika mazungumzo ya harakati za siasa za kudai
uhuru na akaelekeza fikra zangu katika senema ya watoto Cinderella niliyokuta
akitizama pamoja na wajukuu zake. Kwa wale ambao walikuwa karibu na Bi. Titi
watakuwa wanajua jinsi alivyokuwa fasaha wa kuzungumza na jinsi alivyokuwa
hodari wa kushinikiza hoja zake. Niliishia kunywa soda na kutazama ile senema
katika TV kisha tukaagana. Lakini kwangu mimi nilikuwa nimefarajika sana.
Miaka michache iliyopita rafiki yangu mmoja alikuwa anamuoa binti ya ndugu yake
Bi. Titi na harusi hii ilifanyika nyumbani kwa Bi. Titi Temeke. Hali
niliyomkutanayo pale Upanga ilikuwa tofauti sanana nilivyomuona Upanga
mara tu alivyotoka kifungoni. Lakini kabla
sijaondola Bi. Titi alinifahamisha kuwa hazina yake ya nyaraka za wakati wa
kudai uhuru pamoja na picha zake nyingi za kihistoria zilichukuliwa na
askari wapelelezi wakati walipokuja kufanya upekuzi katika nyumba yake kwa
ajili ya tuhuma za kupindua serikali zilizokuwa zimemkabili katika miaka ya
1970. Nilisikitishwa na hili kwa kuwa nilijua yeyote atakaekuja kuandika habari
za Bi. Titi atakuwa amekosa zana za kumsaidia kumwandika mama huyu kwa usahihi.
Bi. Titi Mohamed alihutubia mkutano wake wa mwanzo katika viwanja hivyo na
hii ilikuwa hata kabla hajakutana na Julius Nyerere. Ilikuwaje Bi. Titi
akahutubia mkutano wa TANU kabla hata hajakutana na Nyerere au hata kabla
Nyerere mwenyewe hajafahamika kwa watu wa Dar es Salaam ?
Bi. Titi
Mohamed, Schneider Abdillah Plantan, John
Hatch na TANU - 1955
Historia ya Bi.
Titi inaanza na historia ya mwanzo kabisa ya TANU na historia ya TANU na ya Bi.
Titi haijakamilika kama hajatajwa Schneider Abdillah Plantan mtoto wa
Affande Plantan. Affande Plantan alikuwa mamluki wa Kizulu aliyekuja na Von
Wissman pamoja na askari wengine wa kukodi kutoka kijiji cha Kwa Likunyi - Imhambane, Mozambiquekuja
kupigana na Abushiri bin Salim bin Harith aliyekuwa Pangani na Chifu wa Wahehe
Mkwawa aliyekuwa na ngome yake Kalenga. Wazalendo hawa waliokuwa wanapinga
utawala wa Wajerumani Tanganyika. Halikadhalika historia ya TANU itakuwa
haijakamilika kama hujautajwa uwanja wa Mnazi Mmoja mbele ya Chuo cha
Watu Wazima. Hapo ndipo kilipokuwa kilinge cha TANU. Lakini mwaka 1955
wakati TANU inaanza kufanya mikutano yake chuo hicho kilikuwa bado
hakijajengwa. Sehemu ile ya
mbele ulikuwa ni uwanja tu uliojaa mchanga. Watoto walikuwa wakicheza mpira na
kwa wakati fulani ulipata kutumika kama uwanja wa mikutano wakati makuli wa
bandari ya Dar es Salaam chini ya chama chao Dockworkers Union walipokuwa
wanapambana na dhulma za Waingereza. Uwanja ule ulikuwa ndiyo mahali
walipokutana makuli na kufanya mikutano yao ya wazi. Mikutano ya siri ilikuwa
katika bonde la Msimbazi shambani kwa Mohamed Abeid. Uwanja wa Mnazi Mmoja
ndipo mahali Muislam wa kwanza Mzungu kutembelea Tanganyika katika miaka ya
1940, Dr Shadrack alipofanya mhadhara wake kuwahutubia Waislam wa Dar es
Salaam. Mkalimani wake akiwa Mzee Kleist Sykes. Uwanja huu ndiyo watoto
wa Dar es Salaam walipokuwa wakicheza Idi El Fitr baada ya mfungo wa Ramadhani
na kusheherejea Idi Kubwa (Idi El Haj). Kwa ujumla mambo mengi ya watu wa Dar
es Salaam yalikuwa yakifanyika pale. Haikustaajabisha basi kuwa watu wa Dar es
Salaam walifanyia mikutano ya mwanzo ya TANU katika Uwanja wa Mnazi Moja. Ni
katika uwanja huu ndipo Bi. Titi alipoanza kuwahamasisha Watanganyika, wake kwa
waume wajipinde waung’oe ukoloni katika ardhi ya Tanganyika chini ya TANU. Sasa
turudi kwa Schneider Plantan.
Schneider Plantan alikuwa mmoja wa wanachama wa African Association. Kaka yake Mwalimu Thomas Plantan alipata
kuwa rais wa TAA. Shneider alikuwa mmoja wa wazee wa TAA ambao walishirikiana
na wanasiasa vijana waliochukua uongozi wa TAA mwaka 1950 wakiwa na nia ya
kuigeuza TAA kuwa chama cha siasa kamili. Mdogo wake, Ramadhani Mashado Plantan
ndiye aliyekuwa akiipa TAA nguvu ya propaganda kupitia gazeti lake Zuhra alilokuwa
akilimiliki na kulichapa mwenyewe. Schneider aliwachukulia Waingereza kama adui
zake. Katika vita ya Kwanza ya Dunia (1914-1918) Schneider alipigana dhidi ya
Waingereza chini ya uongozi wa Von Lettow Vorbeck, mkuu wa majeshi ya
Wajerumani katika Afrika ya Mashariki. Katika vita ile alikuwa na ndugu yake
Kleist Sykes. Katika vita ya Dunia ya Pili Shneider alikuwa akipita katika
mitaa ya Dar es Salaam akishawishi kusambaza chuki dhidi ya Waingereza
waliokuwa ndiyo watawala wa Tanganyika na kuwashawishi wananchi wamuunge mkono
Hitler na Mussolini dhidi ya Waingereza. Wakati yeye anafanya haya mdogo wake,
Ramadhani Mashado Plantan akawa ameanzisha kijigazeti cha kurasa moja kikiitwa Dunia akawa
anafanya propaganda za chinichini dhidi ya Waingereza. Kwa ajili hii Schneider
alikamatwa na kuwekwa kizuizini Mwanza. Mwaka 1950 bila ya hofu Schneider
alisimama kidete katika mkutano wa TAA katika Arnautoglo akalazimisha mbele ya
ofisa wa Kingereza ufanyike uchaguzi ili uongozi mpya uingie wa vijana wengi
wao kutoka Makerere College uingie madarakani kuimarisha harakati dhidi ya
Waingereza. Uchaguzi huu ndiyo uliomuingiza madarakani Dr Kyaruzi kama rais na
marehemu Abdulwahid Sykes akiwa katibu. Huu ndiyo uongozi uliopanga mbinu za
kuunda TANU. TANU ilipokuja asisiwa mwaka wa 1954 Schneider alikuwa mmoja wa
wanachama wa mwanzo katika nia yake ile ile ya kupambana na Waingereza. Hii
ndiyo historia ya TANU. TANU haikuanza mwaka wa 1954 moto wake ulianza kuwaka
kwa chinichini miaka mingi nyuma kabla haujajitokeza. Mwanafunzi wa historia ya
Tanganyikia ni lazima azame katika utafiti wa watu walioishi kipindi kile ndipo
atakapopata ukweli wa mambo. Si kweli kama wanavyodai wana-historia wa sasa ati
TAA kilikuwa chama cha starehe.
Viongozi wapya
wa TAA walikuwa na uhusiano na Labour Party ya Uingereza. Ndani ya chama hiki
kulikuwa na wanasiasa waliojiita Fabian Society. Hawa walikuwa na mrengo wa
kushoto na licha ya kuelewana vyema na viongozi wa TAA halikadhalika waliunga
mkono juhudi za taa za kutaka kujikomboa na ukoloni. Mmoja wa viongozi hawa
John Hatch alikuja kutembelea Tanganyika kama mgeni wa TANU mara Juni 1955.
TANU ilifanya mkutano mkubwa sana Mnazi Mmoja na Hatch akawahutubia wananchi.
Inakisiwa takriban wanachama wa TANU na mashabiki wake jumla yao kiasi watu
elfu ishirini walijitokeza kwenye mkutano huo. Ali Mwinyi Tambwe alikuwa
mkalimani wa Hatch. Denis Phombeah pamoja na katibu mkuu wa TANU, Oscar Kambona
vilevile walihutubia halaiki ile. Hatch akiwa anaunga mkono ukombozi wa watu
weusi aligundua kuwa TANU haikuwa na tawi la akina mama. Katika dhifa ya chai
iliyoandaliwa na TANU kwa heshima yake, Hatch alilieleza tatizo hili kwa
Schneider Plantan na John Rupia. Hatch alimwambia Schneider kwamba ili kuwa na
chama chenye nguvu TANU isiwaache akina mama nyuma. Hatch alimwambia Schneider
kwamba huko Uingereza Labour Party kilikuwa kimejikita kwa wanawake kama moja
ya nguzo yake kuu.
Schneider
alimwendea Bibi Tatu binti Mzee akamwomba kuanzisha tawi la akina mama kwa
ajili ya TANU. Bibi Tatu binti Mzee alimpendekeza Bibi Titi Mohamed ndiye
afanye kazi hiyo kwa sababu ya tabia yake ya ucheshi na kupenda kuchanganyika
na watu na ukweli kwamba toka hapo alikuwa mwanachama wa ‘Bomba Kusema.’ Akina
mama hawa ndiyo chanzo cha Umoja wa Wanawake wa Tanganyika (UWT uliokuja
kuundwa mwaka 1962 na Bibi Titi Mohamed alichaguliwa mwenyekiti wake wa
kwanza). Fikra ya watu wengi ni kuwa Bibi Titi aliingizwa TANU na Nyerere.
Ukweli ni kuwa Schneider Plantan ndiye aliyemtia Bibi Titi katika siasa na Bibi
Titi alihutubia mikutano miwili baada ya ule wa Hatch mnamo Juni, 1955 kabla
hajakutana na Nyerere. Bibi Titi alijiunga na TANU pamoja na mumewe Bwana Boi
Selemani na wote waliingizwa TANU na Schneider Plantan. Boi Seleman ni mwenye
kadi ya TANU namba 15 wakati ambapo Bibi Titi, kama ilivyokwishaelezwa kadi
yake ni namba 16.
| Kulia Bi Titi Mohamed, Clement Mtamila, Sheikh Suleiman Takadir na Julius Nyerere Nyuma ya Nyerere Mama Maria Nyerere, Rajab Diwani na John Rupia |
Vikundi vya
taarab mjini Dar es Salaam na nyimbo zao, vyama vya wanawake wa mjini kama Saniyyat
Hubbi, Goodluck, Coronation,‘Bomba Kusema’ na vikundi vya lelemama
ambavyo vilikuwa na udugu na vikundi vya taarab kama Al-Watan au Egyptian,vilitoa
mchango mkubwa sana katika kuwaamsha watu kuiunga mkono TANU. Waliounganisha na
kuviongoza vyama hivi vya wanawake na harakati za kudai uhuru walikuwa Bibi
Titi Mohamed na Bibi mmoja wa Kimanyema, Hawa binti Maftah. Bibi Hawa binti
Maftah, kama kiongozi wa lelemama, alijulikana kwa jina la ‘Queen’. Hakuna hata
mtu mmoja Tanganyika nzima, mbali na Nyerere mwenyewe, aliyeweza kuifanya TANU
kuwa maarufu kama Bibi Titi Mohamed. Bibi Hawa Maftah ndiye aliyeiingiza kwa
mara ya kwanza nyimbo za lelemama ziimbwe katika mikutano ya TANU kama mbinu ya
kuhamasisha wananchi kukipenda chama. Vyama vya wanawake Nujum ul Azhar, Waridatil
Hubb na Egyptian Club vilivyokuwapo mjini Tabora
chini ya wanawake kama Nyange binti Chande na Dharura binti Abdulrahman. Vyama
hivi vya akina mama vilisaidia sana kuipa TANU nguvu katika Jimbo la Magharibi.
Muziki na ujumbe katika nyimbo zilizotungwa maalum kuinua mioyo ya wanachama wa
TANU vilikuwa na athari kubwa, hususani katika wakati ule ambapo serikali ya
kikoloni ilimpiga marufuku Nyerere kufanya mikutano ya hadhara. Ili kuepuka
kadhia hiyo TANU ilikuwa ikiandaa taarab na Nyere alikuwa akikaribishwa kama
mgeni wa heshima. Nyerere alikuwa akisimama kufungua hafla na katika kufanya
hivyo alisema maneno machache. Kwa namna hii ule moto wa kudai uhuru ulibaki
ukiwaka. Kwa njia hii Nyerere aliweza kuwasiliana na wananchi. Halikadhalika
kupitia taarab TANU ilikusanya fedha kwa ajili ya harakati. Kulikuwa na wimbo
mmoja wa lelemama ambao uligeuzwa kuwa kama ndiyo mwimbo wa Nyerere, mwimbo
huu na ulikuwa akiimbiwa yeye tu. Mwimbo huo ulikuja kuwa maarufu sana
kiasi kwamba ulipoimbwa katika mikutano ya TANU watu wote waliimba kwa pamoja.
Mashairi yake yalikuwa kama hivi: ‘Muheshimiwa nakupenda sana, wallahi sina
mwinginewe Insha Allah Mungu yupo, Tanganyika tutajitawala.’
Kwenye viwanja
vya Mnazi Mmoja mbele ya Princess Hotel. Kwenye jukwaa lililojengwa kwa miti walikuwa
wakikaa wale viongozi wa mstari wa mbele
ndani ya TANU - Nyerere rais wa TANU, Sheikh Suleiman Takadir, Mwenyekiti wa
Baraza la Wazee wa TANU, Bibi Titi Mohamed, John Rupia na Clement Mtamila.
Sahani ya santuri ilikuwa ikipigwa katika gramafoni kupitia kipaaza sauti.
Mwimbo uliokuwa ukipigwa ulikuwa wa Frank Humplink. Frank alikuwa kijana wa
Kichagga kutoka Moshi. [1] Baba yake alikuwa
Mzungu. Hamplink alikuwa mwimbaji na mpiga gitaa maarufu sana wakati ule
akipiga muziki wake na dada zake wawili Maria na Regina Humplink. Katika nyimbo
zake nyingi Frank alikuwa akiimba pamoja na dada zake. Mwimbo uliopendwa sana
na TANU na ndiyo uliokuwa ukipigwa katika kila mikutano yake yote na
uliosisimua wananchi ulikuwa na mashairi yafuatayo, ‘Uganda nayo iende,
Tanganyika ikichangamka, Kenya na Nyasa zitaumana’. Mwimbo huu ulikuwa
na ujumbe wa kisiasa kwa Waafrika wa Tanganyika. Ujumbe katika wimbo huo
ulikuwa kuwa, Tanganyika itakapoamka, kutakuwa vilevile na mapambano nchini
Uganda, Kenya na Nyasaland. Mwimbo huu ulikuwa ukivuma toka kwenye vipaza sauti
mfululizo kabla ya mkutano huku watu wakikusanyika viwanjani. Haikupita muda
mrefu serikali ya kikoloni ilipata maana halisi ya wimbo huo. Mara moja mwimbo
huo ukapigwa marufuku na serikali.[2] Serikali ya
kikoloni iliamuru kwamba mashairi ya wimbo huo yanachochea watu kuasi. Lakini
kabla ya mwimbo huo kupigwa marufuku ulipendwa sana na ukwa ukiombwa na
wasikilizaji na kupigwa katika kituo cha radio ‘Sauti ya Dar es Salaam’. Kituo
hicho cha radio kikaacha kupiga nyimbo hiyo. Huenda huu ulikuwa wimbo wa
kwanza kupigwa marufuku katika historia ya utangazaji Tanganyika. Kwa muda
mrefu sana mwimbo huu ulikuwa kama nyimbo rasmi ya TANU. Inaelekea uzalendo na
shauku ya uhuru ndiyo vitu vilivyomtia hamasa Humplink hata akatunga na kuimba
nyimbo hiyo.
Katika mikutano
ya TANU katika zile siku za mwanzo, kabla Nyerere au Bibi Titi kuhutubia umma,
Sheikh Suleiman Takadir alikuwa akisimama na kuomba dua. Kwa kawaida alikuwa
akisoma ghaibu Surat Fatihah, sura ya kwanza katika Qur’an Tukufu:
"Kwa jina la
Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu. Kila sifa njema ni milki
yake Mwenyezi Mungu, Mola wa Ulimwengu wote. Mwingi wa Rehema, Mwenye kurehemu.
Mfalme wa siku ya Hukumu. Wewe tu ndiyo tunayekuabudu na wewe tu ndiyo
tunakuomba msaada. Tuongoze katika njia iliyonyooka, njia ambayo umewaongoza
wale uliowaneemesha, si ya wale uliowaghadhibikia wala ya wale waliopotea."
Hii ni dua
ambayo kwa kawaida husomwa na Waislam kabla ya kuanza jambo lolote la kheri.
Wakati Sheikh Takadir akisoma dua hii watu walikuwa wima mikono yao juu
wakimshukuru Allah. Baada ya hapo Nyerere au Bibi Titi, kutegemea na ujumbe
maalum uliotaka kutolewa katika siku hiyo, alikuwa akisimama na kuhutubia.
Bibi Titi
alikuwa akijulikana kwa maneno yake makali wakati Nyerere alikuwa bingwa wa
fikra tulivu na utoaji wa ujumbe mzito. Sheikh Suleiman Takadir mwenyewe,
vilevile alikuwa msemaji mzuri sana. Ilikuwa kwa sababu hii na umri wake mkubwa
ndiyo alipewa heshima na wazee wa mji ya kuzungumza kwanza kabla ya yoyote
hajasema na kuomba dua, kisha kumtambulisha Nyerere kwa wananchi. Katika siku
hizo Nyerere alizoea kuvaa kaptura na soksi ndefu, mavazi yaliyopendwa na
walimu wa shule na hasa kivazi kilichopendwa na wale waliojiona wameelimika,
hususan watu wenye asili ya bara. Nyerere amenukuliwa akisema kuwa ilikuwa
Dossa Aziz ndiye aliyemtahadharisha kuwa maadam sasa anachanganyika na wazee
haitakuwa vyema kwake kuonekana amevaa kaptura.
Hotuba hii
aliyotoa Nyerere siku ile pale Mnazi Mmoja ambapo aliwaeleza watu kuhusu
safari yake kwenda Umoja wa Mataifa ilikuwa ndiyo mwanzo hasa wa historia mpya
ya Tanganyika. Kabla ya hapo Waafrika wa Tanganyika hawakupata kuonyesha shauku
na matumaini katika mustakbali wao. Katika viwanja vya Mnazi Mmoja Nyerere
aliwaeleza halaiki ya watu wenye furaha na waliokuwa wakimsikiliza kwa makini
kuwa miongoni mwa mataifa kumi na mbili yanayounda Baraza la Udhamini saba kati
yao yalitoa idhini kuwa muda wa utawala wa ndani wa Tanganyika utakapowadia,
Waafrika lazima wapewe nchi yao. Katika hotuba yake Nyerere alitilia mkazo sera
ya TANU kuhusu mahusiano mema baina ya Waafrika na watu wa mataifa mengine na
aliwaonya wanachama wa TANU ambao walikuwa wameanza kuwabagua watu wa rangi
tofauti kuwaambia kuwa hivyo haikuwa sawa. Alisisitiza juu ya umoja miongoni
mwa wananachi na hatimaye aliwadhihaki wasikilizaji kwa kuwauliza ikiwa
wangesubiri kwa miaka ishirini na tano kuwa huru. Halaiki hiyo ya watu kwa
pamoja ilipiga kelele, ‘hapana’. Wananachi kwa pamoja walijibu kwa sauti kubwa
wakisema walitaka uhuru kesho au kesho kutwa.[3]
Nyerere ambaye
alikuwa akiogopa kuchukua uongozi wa TANU tangu 1953 alikuwa amefarajika sana
na mshikamano huu ulioonyeshwa na wananchi. Sasa ilikuwa dhahiri kwake kwamba
rafiki yake Abdulwahid, Ally, Dossa Aziz, Rupia na uongozi mzima wa TANU pamoja
na lile Baraza la Wazee lilikuwa limemsafishia njia kuongoza harakati kwa niaba
yao. Lakini Padri Walsh na Wamishionari katika shule ya Mtakatifu Francis,
Pugu, walitazama harakati hizi kwa mtazamo mwingine kabisa. Wamishionari
hawakuweza tena kumvumilia Nyerere kuwa mmoja wa walimu katika shule yao.
Hatima ile ile iliyowasibu wazalendo wengine kabla yake sasa ilimkabili
Nyerere. Aliambiwa ama abakie mtumishi mtiifu wa kanisa au ajiuzulu; Kanisa
halikuweza kukaa kimya na kumuangalia Nyerere akiwatumikia mabwana wawili.
Nyerere
alilipeleka tatizo hili kwa Clement Mtamila, Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya TANU.
Mtamila aliitisha mkutano wa kamati kuu nyumbani kwake mtaa wa Kipata na TANU
ilijadili tatizo hilo. Miongoni mwa wajumbe wa kamati ile mbali na Rupia na
Kambona walikuwa Bibi Titi Mohamed na Bibi Tatu bint Mzee.[4] Kamati
Kuu ya TANU ilimshauri Nyerere ajiuzulu. Tafarani hii ilitokea wiki chache tu
baada ya kurudi kutoka Umoja wa Mataifa katika wiki za mwisho za mwezi Machi.
Tarehe 23 Machi, 1955 Nyerere alijiuzulu ualimu. Ilikuwa adhuhuri Nyerere
alipokuja Dar es Salaam kutoka Pugu, akiwa si mwalimu wa shule tena.
Inasemekana aliposhuka tu kwenye basi alikwenda moja kwa moja ofisini kwa
Abdulwahid katika soko la Kariakoo kumpasha habari rafiki yake. Nyerere alikaa
na Abdulwahid katika nyumba yake namba 78 Mtaa wa Stanley. Baadaye kidogo
Nyerere alirudi kijijini kwake huko Musoma. John Hatch alipokuja Dar es Salaam
kwa waliko wa TANU Nyerere alikuwa kwao kijijini. Tutaona hapo baadae kidogo
jinsi mgeni huyu Mwingereza alivyomgutusha Schneider Abdillah Plantan kuhusu
TANU kuwashirikisha wanawake katika harakati za kudai uhuru.
Wanawake na
Vyama Vya Lelemama Katika Harakati za Kudai Uhuru
Mwaka 1955 Bibi
Titi Mohamed na Julius Nyerere waliitika mwaliko na kuja Tabora. Mkutano
ulifanyika katika ile kilabu ya kandanda. Waliohudhuria mkutano ule walikuwa
Germano Pacha, Juma Mrisho, Shaaban Mohamed Silabu, Bilali Rehani Waikela,
Mohamed Mataka wakati ule akiwa muadhin wa Masjid Nur - msikiti
wa Wamanyema pale Tabora, Hassan Mohamed Ikunji, Ramadhani Mussa Wajaku, Swedi
Mambosasa, Said Ali Kiruwi na Hamis Khalfan. Uongozi wa kilabu ulimwambia
Nyerere na Bibi Titi kuwa kilabu hiyo ya kandanda ilikuwa ikitaka udugu
na TANU ili ifanye kampeni ya kuipatia TANU wanachama wengi. Uongozi huo wa
TANU kutoka makao makuu Dar es Salaam uliambiwa kuwa maadam kilabu hiyo ilikuwa
ikipendwa na kuungwa mkono na watu wa Tabora na ilikuwa maarufu sana, sifa hizo
zingeweza kutumiwa kwa manufaa ya TANU. Vilevile Nyerere alifahamishwa kuwa
kilabu hiyo ingependa kuvijumuisha vyama vitatu vya lelemama na vikundi vya
taarabu, Nujum ul Azhar, Waridatil Hubb na Egyptian
Club. Nyerere na Titi waliyakubali mapendekezo haya na usiku ule
akifuatana na uongozi wa kilabu Nyerere alizungumza na kikundi cha
watu waliyokusanyika nje ya nyumba ya kilabu juu ya hali ya Tanganyika katika
siku zijazo. Nyerere alikuwa amerudi Tabora ambapo alianza siasa kiasi cha
miaka minane nyuma. Jambo muhimu katika kipindi hiki pale Tabora ni kuwa wasomi
wa Makerere waliokuwa St. Mary’s School hawakuwapo katika harakati hizi na
katika mikakati iliyokuwa ikipangwa. Bibi mmoja wa Kiganda, Nyange bint Chande,
mwanachama wa moja ya vikundi vya lelemama mjini Tabora alijitolea nyumba yake
kama ofisi ya kwanza ya TANU katika Jimbo la Magharibi. Uchaguzi ulifanyika na
Shaabani Marijani alichaguliwa Mwenyekiti wa Wilaya na Idd Said Ludete Katibu
wa TANU. Bilali Waikela akawa mjumbe wa kamati. Kadi za kwanza za uanachama wa
TANU ziliuzwa ndani ya soko la Tabora na Amani Idd na Pacha, Katibu wa
Jimbo wa TANU. Pacha alikuwa na
lingo la kuni pale sokoni kama biashara yake. Baadae Amani Idd alisaidiwa kazi
hiyo ya kuuza kadi za TANU na Dharura bint Abdulrahman. Baada ya kufungua tawi
la TANU mjini Tanga, uongozi wa chama ulimwalika Julius Nyerere, Bibi Titi
Mohamed, John Rupia na Mbutta Milando kufanya ziara Tanga. Nyerere alifikia
nyumbani kwa Hamisi Heri. Ujumbe huu kutoka makao makuu ya TANU ulipata
makaribisho makubwa yaliyoandaliwa na vyama vya lelemama ambavyo kwa kawaida
vilikuwa vingi sana katika pwani ya Afrika ya Mashariki kutoka Mombasa nchini
Kenya hadi Mikindani, Tanganyika. Kiongozi wa akina mama hawa mjini Tanga
aliyesaidia kuieneza TANU alikuwa Bibi Mwanamwema bint Sultan, ndugu wa mbali
wa mwenyekiti wa TANU Tanga, Hamisi
Heri. Siku iliyofuata mabingwa wa hotuba wa TANU, Julius Nyerere na Bibi Titi
Mohamed walihutubia mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa Tangamano. Hii ilikuwa
hatua kubwa sana kwa TANU, na kwa harakati dhidi ya ukoloni pale Tanga.
Ilikuwa muda mrefu umepita tangu zile siku za zile siasa za wasomi katika Discussion
Group, kikundi cha majadiliano; na ile mizozo baina yao na ule uongozi
Waarabu katika TAA. Baada ya hapo, Mwalimu Kihere alichaguliwa kuwa Mwenyekiti
wa TANU Tanga badala ya Hamisi Heri na Amos Kissenge alichaguliwa katibu.
Abdallah Rashid Sembe mmoja wa wanachama waasisi wa mwanzo kabisa wa TANU
alichaguliwa kuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa ya TANU akiwakilisha Jimbo la
Tanga.
TANU katika Mombasa, Kenya, 1957
Mambo yalikuwa yanageuka dhidi ya Waingereza katika
makoloni yake yote Afrika ya Mashariki. Wazalendo walikuwa wakifanya harakati zao na kuvuka
mpaka mmoja wa nchi hadi mwingine bila matatizo. Ule wakati wa wao kusafiri kwa
kificho na kufanya mikutano yao nyakati za usiku mafichoni ulikuwa umepita.
TANU ilikuwa na nguvu ya sasa kuangali nje ya mipaka yake. Katika pwani ya
Kenya katika mji wa Mombasa, kijana mmoja kutoka Moshi, Ismail Bayumi,
aliyeajiriwa na Mombasa Municipal Council akivutika na mwenendo wa matukio ya
kisiasa kama yalivyokuwa yakitokea katika Afrika Mashariki, aliwashawishi
Watanganyika waliokuwa wakiishi na kufanya kazi Mombasa kuunda kile kilichokuja
kujulikana kama Mombasa TANU Club. Sheria ya Kenya haikuwaruhusu Watanganyika
kuunda chama cha siasa katika ardhi ya Kenya, kwa hiyo TANU Club ilisajiliwa
kama chama cha starehe na ilikuwa na ofisi zake katika Barabara ya Lohana.
Ismail Bayumi alichaguliwa rais wake wa kwanza. Lakini kwa hakika TANU Club
ilifanya kazi kama chama cha siasa kwa niaba ya TANU, KANU na KADU kwa kiwango
fulani. Wakati huo Jomo Kenyatta alikuwa Manyani akitumikia kifungo cha
miaka saba gerezani kwa kuhusika na harakati za Mau Mau.
Tom
Mboya aliitumia TANU Club kuifanyia kampeni KANU na kupigania kufunguliwa kwa
Kenyatta kutoka gerezani. Kote nchini Kenya KANU ilikuwa ikiibuka kama chama
cha wananchi wote. Wakati sera za KANU zilikuwa zile za mwelekeo wa
kuwaunganisha wananchi wote dhidi ya ukoloni, KADU chini ya Ronald Ngala, kwa
upande mwingine, ilikuwa na labda isemwe, ufahamu mfinyu, KADU ikifungamanisha
sera zake na siasa za ukabila na utawala wa majimbo. Kwa hiyo KADU ilikuwa
ikikusanya nguvu za upinzani wa makabila madogo dhidi ya KANU. KANU chini ya
Kenyatta, Jaramogi Oginga Odinga na Tom Mboya, ilichukuliwa kuwa ni chama cha
makabila mawili makubwa nchini Kenya, yaani Wakikuyu na Wajaluo ambayo
yakiachiwa kutawala yatameza makabila madogo. Nchini Tanganyika ambako
ushindani wa kikabila katika siasa haukuwepo, TANU Club ilijikuta kiitikadi
inapenda kuwa karibu zaidi na KANU kuliko KADU.
TANU
Club ilikuwa ikiandaa dansi katika Ukumbi wa Tononoka na dansi hizi zilikuja
kupendwa sana na wanasiasa wa Kenya. Ilikuwa chini ya pazia la sherehe hizi
katika Ukumbi wa Tononoka ndiyo wanasiasa wa Kenya na wale wa TANU Club
walipata nafasi kupashana habari namna TANU ilivyokuwa ikiendelea nchini
Tanganyika na nini TANU ingeweza kufanya huko Tanganyika ili kusaidia harakati
za kudai uhuru nchini Kenya. Baada ya TANU Club kufanikiwa sana huko pwani
uongozi wake uliamua kufungua tawi la TANU Club mjini Nairobi katika sehemu ya
Pumwani. Tom Mboya na Ronald Ngala walikuwa mstari wa mbele katika sherehe zote
za TANU Club, wakishiriki katika shuguli zake Mombasa na Nairobi.
Msukumo
mkubwa wakati ule nchini Kenya ilikuwa kufanya kampeni ya nchi nzima
kuwashinikiza Waingereza wamwachie huru Kenyatta aliyekuwa akichukuliwa na
wananchi wote kama kiongozi na nguvu ya umoja wa Waafrika wa Kenya. Katika
wimbi hili la kutaka Kenyatta afunguliwe kutoka gerazani, Tom Mboya alimdokeza
Ismail Bayumi kuwa TANU ingeweza kusaidia katika kampeni hii ya kuwashinikiza
Waingereza kumtoa Kenyatta kifungoni. Ismail alifikisha wazo hili makao makuu
ya TANU mjini Dar es Salaamkwa kupitia mtu maalum aliyekuwa akiwasiliana
na Tom Mboya na Nyerere kwa siri. TANU ilimtuma Bibi Titi Mohamed kwenda Kenya kuzitia
shime harakati za kufunguliwa Kenyatta. Wazalendo nchini Kenyawalikuwa
wameshindwa kabisa kuwaingiza wanawake ndani ya KANU hivyo kuzinyima harakati
za uhuru nguvu kubwa sanana ya kutegemewa ya akinamama. [5] Huko Mombasa TANU Club ilifikiria kuwa kumleta
Bibi Titi kuja Kenya kuifanyia kampeni KANU ilikuwa ni kitu kipya cha
kuwahamasisha wanawake ndani ya KANU na kwa hiyo kuongeza nguvu mpya na kutia
ari ya utaifa katika Kenya.
Bibi
Titi alikuja Mombasa na kufanya mkutano Ukumbi wa Tononoka. Kwa
kawaida kwa madhumuni ya kupata kibali mikutano hii ilikuwa inahesabiwa kama ni
mikusanyiko ya kufanya sherehe siyo mikutano ya siasa na ilikuwa ikifanyika
ndani. Lakini mkutano huu ulikuwa na umuhimu wake kwa sababu ya kuwako Bibi
Titi Mohamed mjini Mombasa. Wengi walikuwa wamemsikia Bibi Titi lakini
hawakuwa wamepata kumuona. Watu walijaa ndani ya ule ukumbi hadi nje
kuzunguka viwanja vya Ukumbi wa Tononoka. Kwa kweli kwa hali yoyote mkutano ule
usingeweza kuitwa kuwa ni mkutano wa wanachama wa TANU Club mjini Mombasa,
au hata mkutano wa TANU Club Kenyanzima, kwa sababu wanachama wa KANU
waliwazidi wanachama wa TANU Club kutoka Tanganyika.
Kenyailikuwa
bado haijaweza kumtoa hata mwanamke mmoja wa kiwango cha Bibi Titi. Kwa wakati
ule kumwona mwanamke wa Kiislamu amesimama bila baibui akihutubia halaiki ya
wanaume ilikuwa ni jambo la kushangaza sehemu za pwani, ambako wanawake
walitembea huku wamejifunika mabaibui na hawakutakiwa hata kufanya kazi
maofisini. Bibi Titi alifanya mikutano kule Mombasana Nairobiakiwasisitizia
watu wasikate tamaa wasimame pamoja hadi Kenyatta amefunguliwa kutoka gerezani.
Habari za mikutano hii iliandikwa kwa mapana na marefu na magazeti ya Mombasa Times na Taifa
Leo.
Miongoni
mwa Wakenya kule pwani waliyofanya kazi karibu sana na TANU Club
walikuwa Msanifu Kombo na Abdallah Ndovu Mwidau. Kombo na Mwidau kwa sababu ya
mchango wao kwa KANU kupitia chama chenyewe na kupitia TANU Club wakaja kuwa na
ushawishi mkubwa kwa Rais Kenyatta. Wazalendo hawa wawili baada ya uhuru wa Kenyawakawa
watu wenye sauti kubwa kule pwani. Hakuna mtu kutoka pwani alikuwa anaweza
kuteuliwa na kushika nafasi yoyote muhimu na Kenyatta bila Abdallah Mwidau na
Msanifu Kombo kumuunga mkono. Mara tu baada ya kufunguliwa kutoka gerezani,
Kenyatta alikwenda Mombasakutoa shukrani zake kwa Msanifu Kombo, Abdallah
Mwidau na TANU Club kwa msaada wao kwa KANU na kwa kufanya kampeni ya
kufunguliwa kwake. Mkutano ulitayarishwa kule Tononoka na Kenyatta alikuja
kutoa hotuba ya shukrani na kukutana na wanachama wa TANU Club.
Ujumbe
wa Nyerere mwenyewe kutoka makao makuu ulikuwa na watu wengi ambao wasingeweza
hata kidogo kusimama kamawagombea katika uchaguzi chini ya masharti yale.
Makao makuu ya TANU yalikuwa yanawakilishwa kwenye mkutano mkuu na Julius
Nyerere, Sheikh Suleiman Takadir, Bibi Titi Mohamed, John Rupia, Elias
Kissenge, Dossa Aziz, Julius Mwasanyangi, Michael Lugazia, Ramadhani Chaurembo,
Hussein Mbaruk, Clement Mtamila, Idd Tulio, Mzee Salum, Idd Faiz Mafongo, Idd
Tosiri, Haidari Mwinyimvua na Rajabu Diwani. Hii ilikuwa na maana uongozi wa
Waislam kule Dar es Salaam, Tanga, Tabora, Dodoma na mahala
pengine nchini Tanganyikausingeweza kusimama kama wagombea
uchaguzi ili wachaguliwe kuingia katika Baraza la Kutunga Sheria wala
wasingeweza kuwapigia kura wagombea wanaowataka. Kwa hiyo ilikuwa ni jambo la
wazi kabisa kuwa TANU ingesusia uchaguzi. Serikali ya kikoloni, ikishirikiana
na wamishionari, walikuwa wamewanyima Waislam elimu, sharti lile lile ambalo
sasa linawekwa kuwazuia Waislam kushiriki katika siasa. Mkutano wa Tabora
ulikuwa uamue ikiwa TANU itashiriki katika uchaguzi na kushindana na UTP au
ingesusia uchaguzi huo na hivyo kumpa mshindani wake mkubwa na hasimu wake
ushindi wa bure.
Hakuna
kumbukumbu zozote zinazoeleza mawazo ya Nyerere katika suala la kura tatu wala
hakuna nyaraka inayoweza kueleza kuwa alipata hata kuzungumza suala hili kwa
faragha pale makao makuu na viongozi wenzake kama Sheikh Suleiman Takadir,
Zuberi Mtemvu, Rajab Diwani, Idd Faiz, Haidar Mwinyimvua, Dossa Aziz au Bibi
Titi Mohamed. Kwa ajili hii ni vigumu kuweza kujua ni kwa kiasi gani Nyerere
alikuwa amejizatiti katika msimamo wa TANU kuingia katika kura tatu chini ya
masharti yale. Lakini ikiwa utafanya tathmini kutokana na hali ya hewa ya siasa
kama ilivyokuwa katika miezi ya mwisho ya mwaka 1958, si vigumu kuona kwa nini
Nyerere ilibidi afiche msimamo wake katika suala la kura tatu kama TANU
lilivyotwishwa na serikali. Nyerere alikuwa anafahamu hatari iliyokuwa
ikinyemelea TANU kutokana na kura tatu. Alijua wazi ili kukinusuru chama na
mgawanyiko kulikuwa na haja kubwa ya yeye kufanya uamuzi haraka na kwa makini
kabla ya kuenda kwenye mkutano Tabora.
Siku
kadhaa kabla ya kusafiri kwenda Tabora kwenye ule mkutano mkuu wa mwaka wa
TANU, Nyerere na Amos Kissenge, Kaimu Katibu Mwenezi wa TANU, walisafiri kwenda
Tanga kushauriana na uongozi wa Kamati Kuu ya Taifa ya TANU Tanga kuhusu
matatizo yaliyoletwa na uchaguzi wa kura tatu. Mkutano huu baina ya Nyerere,
Kissenge na ule uongozi wa Tanga ulikuwa wa siri sana. Tanga iliwakilishwa
na Hamisi Heri, Mwalimu Kihere, Abdallah Rashid Sembe, Ng’anzi Mohamed, Mustafa
Shauri na Abdallah Makatta. Nyerere alizungumza waziwazi na kwa ithibati ya
moyo wake. Nyerere alikiambia kikao kile kuwa amekuja Tanga kuomba wamuunge
mkono kwa sababu ilikuwa ni matakwa yake TANU lazima ishiriki katika ule
uchaguzi wa kura tatu uliokuwa unakaribia hata masharti yakiwaje. Nyerere
aliuambia uongozi wa Tanga uliokuwa ukimsikiliza kwa makini kuwa alikuwa
amekuja kwao kwa sababu watu wa Tanga wanajulikana kwa ufasaha wa lugha na kwa
uwezo wao wa kuzungumza vizuri. Nyerere alisema angehitaji hiki kipaji adimu
cha watu wa Tanga kuunga mkono msimamo wake huko Tabora. Nyerere alitoa hoja
kwamba TANU lazima iingie katika uchaguzi kwa sababu kuususia
ni sawasawa na kukipa chama hasimu, UTP ushindi bila jasho kuingia katika
Baraza la Kutunga Sheria. TANU ingedhoofika na hivyo ingekosa sauti katika
maamuzi yatakayotolewa na serikali katika siku zijazo.
Kufichuka
kwa msimamo wa Nyerere wa kutaka TANU iingie kaatika kura tatu kulishtua
uongozi wa Tanga. Majadiliano makali yalifuata uongozi wa Tanga ukionyesha
upinzani wao kwa msimamo wa Nyerere. Baada ya majadiliano ya muda mrefu Nyerere
alifanikiwa kuwashawishi wote wawili, Hamisi Heri na Mwalimu Kihere ambao ndiyo
walikuwa wapinzani wakubwa wa msimamo wa Nyerere na uchaguzi wa kura tatu.
Nyerere aliutahadharisha uongozi wa Tanga kuwa agenda ya kura tatu itakapokuja
anatabiri kupata upinzani mkali kutoka katika majimbo. Huko Tanga kwenyewe,
TANU ilikuwa ikikabiliwa na upinzani mkali kutoka UTP na serikali. Matawi
kadhaa yalikuwa yamepigwa marufuku. [6] UTP
ilikuwa na nguvu Tanga kwa sababu wanachama wake wengi walikuwa wakimiliki
mashamba ya mkonge katika jimbo hilo. Kwa ajili hii chama kilikuwa
kinaelemewa na mashambulizi kutoka wa wapinzani. Wakati huo Tanga ilikuwa
imetoa viongozi wenye uwezo lakini wote walikuwa wamehamishiwa makao makuu
mjini Dar es Salaam. Wapangaji mikakati wazuri kama Peter Mhando alikuwa
amehamishiwa Dar es Salaam na kutoka hapo alipelekwa Tabora ambako si
muda mrefu akafa. Elias Kissenge vilevile alihamishiwa makao makuu kushika
nafasi ya Katibu Mkuu wa TANU baada ya Oscar Kambona aliyekuwa ameshika nafasi
hiyo kwenda Uingereza kwa ajili ya masomo. Uongozi wa TANU Tanga hata baada ya
kujadili mbinu waliyopanga na huku Nyerere akielekeza mikakati ambayo Mwalimu
Kihere na Abdallah Rashid Sembe wataitekeleza Tabora, bado uongozi ule ulikuwa
na wasiwasi wa mafanikio ya mpango huo. Kwa ajili ya wasiwasi huu, viongozi wa
TANU wa Tanga walimuomba Nyerere wawe pamoja ili ifanywe tawaswilwaombe
msaada wa Allah awape ushindi dhidi yaa vitimbi vya Waingereza.
Maili
tatu kutoka Tanga kipo kijiji cha Mnyanjani ambako kulikuwako na tawi la TANU
lililokuwa na nguvu sana likiongozwa na Mmaka Omari kama mwenyekiti na Akida Boramimi
bin Dai akiwa katibu. Mmaka alikuwa kijana aliyekuwa akiendesha mgahawa pale
kijijini na Akida bin Dai alikuwa mwashi. Akida aliongoza tawi la vijana wa
TANU ambalo baadae lilikuja kujulikana kama Tanga Volunteer Corps
(TVC). TVC ilikuwa sawasawa na Bantu Group, ambayo wakati huo ilikuwa
imekwishaanzishwa huko Dar es Salaam na Tabora. Vikundi hivi mbali na kufanya
shughuli za propaganda na kuhamasisha wananchi halikadhalika viliifanyia TANU
ujasusi. Nyerere na Kissenge walichukuliwa hadi Mnyanjani na tawaswil ikasomwa.
Waliohudhuria kisomo hicho walikuwa Abdallah Rashid Sembe, Sheikh Dhikr
bin Said, Mzee Zonga, Hemed Anzwan, Salehe Kibwana aliyekuwa mshairi maarufu,
Akida Boramimi bin Dai na Mmaka Omari. Aliyechaguliwa kusoma Quran Tukufu
alikuwa mjomba wa Mwalimu Kihere, Sheikh Ali Kombora.
Mjadala wa Kura Tatu
Wasomi waliokuwa Dodoma, Tabora na Tanga walishindwa
kabisa kuunda chama cha siasa. Kazi hii ilitwikwa na kubebwa kwa mafanikio
makubwa na Waislam ambao hao waliokuwa na kisomo waliwaona ni wachache wa
elimu. Hadi kufikia mwaka wa 1958, TANU ilikuwa na nguvu na ilikuwa ipo
takriban kila jimbo nchini Tanganyika na ilikuwa sasa inatarajia kushiriki
katika uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia. Hapakuwa na shaka yoyote kuwa TANU
ingesusa kushiriki katika uchaguzi wa kura tatu kwa sababu ya masharti ya
kibaguzi yaliyowekwa na serikali ya kikoloni. Waafrika hawakuweza kutimiza
masharti yale hasa Waislam ambao ndiyo walikuwa mstari wa mbele katika harakati
za kumng’oa Mwingereza kutoka Tanganyika. Hii ilimaanisha kuwa Waislam
waliokuwa viongozi katika TANU wasingeweza kusimama wapigiwe kura kuingia
katika Baraza la Kutunga Sheria na halikadhalika halaiki ya Waislam waliokuwa
katika harakati za siasa wasingeweza halikadhalika hata kupata ile haki ya kupiga
kura.
Uchaguzi wa kura tatu ulikuwa ukizuia uongozi wa
kuchaguliwa na watu kuingia kwenye madaraka. Viongozi kama Sheikh Suleiman
Takadir, Fundi Mhindi, Omar Suleiman, Hamis Heri waliochaguliwa na watu
kidemokrasia kuongoza harakati dhidi ya mfumo dhalimu walikuwa wanapigwa
marufuku kushiriki katika mustakabali wa nchi yao kwa matakwa ya wakoloni tu
wala si kwa sababu yoyote ile ya msingi. Katika hali kama hii yale yote ambayo
Waislam waliojitolea mhanga kwayo, yalionekana kama yamepotea bure. Mara baada
ya kurudi kutoka Tanga Nyerere aliondoka kwenda Tabora akiongoza ujumbe mkubwa
sana kutoka makao makuu ndani yake wakiwemo: Sheikh Suleiman Takadir, Bibi Titi
Mohamed, John Rupia, Elias Kissenge, Dossa Aziz, Julius Mwasanyangi, Michael
Lugazia, Ramadhani Chaurembo, Hussein Mbaruk, Clement Mtamila, Idd Tulio, Mzee
Salum, Idd Tosiri, Hadari Mwinyimvua, Rajab Diwani na wengine.
Katika miaka ya 1950 Tabora ulikuwa mji mdogo usiokuwa na
uwezo wa kuhimili ugeni kwa ujumbe mkubwa kama ule wa TANU ambao ulitoka
majimbo yote ya Tanganyika. Ofisi ya wilaya ya TANU, Tabora, sasa chini ya
uwenyekiti wa Mohamed Mangiringiri, fundi cherahani aliyeajiriwa na
mfanyabiashara wa Kiasia, G. B. Somji, iliwashirikisha wanachama wote na vyama
vilivyokuwa na udugu na TANU kwa kuwaomba wachange kwa ukarimu fedha ili
kufanikisha mkutano ule na vilevile wachangie chochote watakachoweza kutoa kwa
ajili ya kuwakimu wageni. Wanachama walitoa nyumba zao kwa ajili ya malazi ya
wajumbe, wengine walitoa vyakula, mablanketi, shuka, magodoro na samani. Wale
matajiri walijitolea fedha taslimu. Usalama wa wajumbe ulikabidhiwa kikundi cha
TANU Bantu Group. Ramadhani Abdallah Singo, [7] wakati
huo akiwa na umri wa miaka ishirini na nane na aliyekuwa na sifa ya ubabe na
Abdallah Saidi Kassongo, akiwa na umri wa miaka ishirini na nne wote wawili
wanachama wa Bantu Group walikabidhiwa kazi ya kumlinda rais wa TANU, Nyerere
mara tu atakapokanyaga ardhi ya Tabora.
Issa Kibira, mwanachama muasisi wa tawi la African
Association mjini Tabora na sasa mwanasiasa mkongwe na mwenye kuheshimiwa
alijitolea kumkaribisha Nyerere nyumbani kwake. Makamu wa rais wa TANU John
Rupia na Michael Lugazia walilala katika nyumba nyingine ya Kibira. Kijana
mmoja kwa jina Jaffari Idd alichaguliwa maalum kumpikia chakula Nyerere.
Mwaminifu kama alivyokuwa, Jaffari alilazimika kula yamini - kiapo cha
Kiislamu, kuwa hatashawishika kwa namna yoyote ile na katika hali yoyote
kumruhusu adui amshawishi kumtilia Nyerere sumu katika chakula. Jaffari
alikumbushwa na wale waliomlisha yamini kuwafikiria Waafrika milioni tisa
nchini Tanganyika waliokuwa wanamtegemea Nyerere kama mkombozi wao.
Mnamo tarehe 28 Januari, 1958 Nyerere na ujumbe wake
kutoka Dar es Salaam waliwasili Tabora kwa gari moshi. D.C. wa alikuwa
ameionya TANU mapema na katika wakati wa kutosha kabisa kuwa TANU isipeleke
zaidi ya watu wawili kumpokea Nyerere na ujumbe wake. Kwa hiyo TANU ilipanga
kumpokea Nyerere na wajumbe wengine Igalula, stesheni ndogo nje ya Tabora.
Kundi kubwa lililokusanyika Igalula lilimpokea Nyerere na ujumbe wa TANU
toka makao makuu kwa vifijo na nderemo. Baada ya hapo kundi lile la wananchi
lilimsindikiza Nyerere na ujumbe wake kwa maandamano makubwa hadi kwenye ofisi
ya TANU katika mtaa wa Usagara. Mwaka
1955 Nyerere na Bibi Titi walipokaribishwa Tabora na Young New Strong
Football Club hapakuwepo na kishindo chochote. Waliojua kuwa Nyerere
na Bibi Titi walikuwapo mjini walikuwa wale waliokutananao uso kwa uso. Safari
hii kuja kwa Nyerere Tabora kulikuwa ni ushindi kwa TANU na kishindo chake
kilisikika katika wilaya zote nane za Jimbo la Magharibi na nje ya mipaka yake.
Zaidi ya wajumbe mia moja na hamsini kutoka kila pembe ya Tanganyikawalikutana
Parish Hall, ukumbi wa Kanisa Katoliki kujadili uchaguzi wa kura tatu. Tabora
iliwakilishwa na Mzee Fundi Mhindi, Mohamed Mangiringiri na Dharura bint
Abdulrahman.
Ile
agenda ya uchaguzi wa kura tatu ilipoanza kujadiliwa, mkakati wa Tanga ukaanza
kutekelezwa. Nyerere aliyekuwa mwenyekiti wa mkutano aliomba amwachie kiti
Mwalimu Kihere ili apate fursa ya kushiriki katika mjadala na kutoa
mchango wake. Mara tu baada ya Mwalimu Kihere kuchukua kiti aliutuliza mkutano
na akamchagua Abdallah Rashid Sembe kuwa msemaji wa kwanza kamavile
walivyopanga kule Tanga majuma machache yaliyopita. Sembe alihimiza TANU
kushiriki katika uchaguzi. Kama vile Nyerere alivyotabiri mapema,
zogo kubwa lilizuka. Wajumbe walipiga makelele, wakagonga meza kwa hasira,
wengine wakawa wanaburuza meza na viti kwa fujo kudhihirisha hamaki zao.
Jumanne Abdallah, aliyekuwa akifahamika kwa umaarufu wa kuwa Kadiani na Bhoke
Munanka kutoka Jimbo la Ziwa walisimama na kumlani Sembe wakimwita msaliti.
Sembe alishikilia msimamo wake kuwa TANU ni lazima iingie uchaguzi unaokuja ili
ishinde uchaguzi na katika ushindi huo iwe na uwezo wa kufutilia mbali mfumo
huo wa kuchukiza. Nyerere alisimama na akamuunga mkono Sembe. Nyerere alitoa
hoja katika misingi hiyo hiyo kuwa ili TANU iweze kuondoa kura tatu ni lazima
kwanza iingie kwenye kura tatu. Wajumbe hawakuafikiana hoja ile. Wote
walishikilia msimamo wa TANU kususia uchaguzi. Hamaki za watu zilikuwa wazi
ndani ya ukumbi wa mkutano na Mwalimu Kihere aliahirisha kikao hadi siku ya
pili ili kuwapa wajumbe muda wa kutuliza hasira. Wajumbe walipokuwa
wanarudi kupumzika majumbani walikofikia, ujumbe wa Tanga, na hasa Sembe
aliyejiletea balaa kwa matamshi yake ndani ya mkutano aliamini kuwa ule mkakati
waliopanga na Nyerere ulikuwa unawageukia na kuwa msiba mkubwa na wa kutisha
kwake yeye mwenyewe binafsi na kwa chama.
Siku
iliyofuata ustadi wa Nyerere katika mjadala uliokuwa maarufu toka alikupokuwa
mwanafunzi Makerere College - ulitumika. Nyerere akizungumza kwa vitendawili na
methali, aliwauliza wasikilizaji wake, je, ingewezekana kwa mkulima mwenye
busara, aliyelima na kupanda shamba lake kwa taabu, angesita kuvuna mazao yake
kwa kuhofia kuchafua nguo zake, kwa sababu tu, ili afike shambani kwake itabidi
avuke mto wenye matope. Watu wangelimuonaje mkulima kama huyo? Nyerere
aliwaeleza wale wajumbe kuwa, TANU iko njia panda, ingekuwa kazi bure kwa
wakati huu kwa chama kususia uchaguzi baada ya kufanya kazi yote ile kwa shida
kubwa hadi kufika hapo walipofika. Kusuia uchaguzi ingekuwa ni kujiingiza
katika mtego. Adui angefurahi kuona imenasa katika mtego, TANU ikisimama
pembeni na UTP ikiingia katika uchaguzi na kuchukua viti vyote katika Baraza la
Kutunga Sheria. Serikali ya kikoloni ingefurahi sana kuona kitu hiki kinatokea. Hata hivyo agenda ya kura tatu ilibidi
ipigiwe kura. Kura ilipopigwa kundi la msimamo mkali waliotaka kuususia
uchaguzi walishindwa: kura thelathini na saba zilipigwa kuunga mkono kushiriki
uchaguzi wa kura tatu dhidi ya ishirini na tatu zilizotaka ususiaji. [8] Nyerere
na Sembe ambaye alihatarisha uhali wa yeye kuwapo katika TANU katika
suala la uchaguzi wa kura tatu walikuwa washindi.
![]() |
| Bi. Titi Mohamed na Julius Nyerere 1950s |
Baada ya kura kutangazwa Nyerere aliwaambia wajumbe wa
mkutano kutoka nje ili wapige picha ya pamoja. Wajumbe wachache sana walikubali,
wengi wao waliamua kukaa pembeni wasitokee katika picha kwa hofu ya kuandamwa
na serikali. Nyerere alitia sahihi Azimio la Tabora ambalo baadae lilikuja
kujulikana kama ‘Uamuzi wa Busara’; siku ile Nyerere alipokuwa akiweka sahihi
yake watu hawa wafuatao ndiyo walikuwa wamemzunguka: kwa upande wa kulia wa
Nyerere alikuwa amesimama makamu wa rais wa TANU, John Rupia; upande wake wa
kushoto alikuwepo Amos Kissenge; aliyekuwa kakaa nyuma ya Nyerere amevaa kofia
ya mkono, koti na kanzu alikuwa Mzee Jumbe Tambaza, mjumbe wa Baraza la Wazee
wa TANU, upande wake wa kuume alikuwa kijana Juma Selemani maarufu kwa jina la
lake la utani, ‘Juma Mlevi’, katibu wa TANU Bantu Group. Waliokuwa wamekaa
mwisho wa meza wakitazamana alikuwa Bibi Titi Mohamed kwa upande wa kulia
wa Nyerere na Sheikh Suleiman Takadir kwa upande wake wa kushoto.
| Bi. Titi Mohamed na Nyerere katika Tanganyika huru |
Mambo yakawa yamevurugika zaidi kwa kuwa rais wa EAMWS,
Tewa Said na makamo wake Bibi Titi Mohamed walikuwa katika baraza la mawaziri
la Nyerere na wakapoteza nyadhifa zao za ubunge katika uchaguzi mkuu wa mwaka
1965. Kwa ajili hii basi serikali ikawa inaeneza propaganda kuwa kwa kuwa Tewa
na Bibi Titi walikuwa katika uongozi wa juu wa EAMWS, walikuwa wanatumia nafasi
zao kujijengea himaya mpya kutoka kwa Waislam dhidi ya Nyerere. Viongozi hawa
ikawa lazima washughulikiwe na kuangamizwa. Mtu wa kufanya kazi hii hakuwa
mwingine ila Adam Nasibu katibu wa EAMWS Bukoba, mwalimu wa shule ya msingi
ambae elimu yake wala haikuwa kubwa. Adam Nasibu alikuwa tayari keshafanikiwa
kufanya mapinduzi dhidi ya rais wa EAMWS, Tewa Said Tewa. Kutokana na vitendo
vyake alikuwa ameidhihirishia serikali kuwa yeye angeweza kuwa mtumishi bora
kwa dola kuliko ule uongozi wa EAMWS uliokuwa pale makao makuu Dar es Salaam
ambao ulikuwa ukionekana umechoka.
Wakazi wa Dar es Salaam kila mwaka walikuwa wakifanya
maulidi katika viwanja vya Mnazi Mmoja kuadhimisha kuzaliwa kwa Mtume Muhammad
(SAW). Huu ndiyo toka asili ulikuwa uwanja ambao TANU ilifanya mikutano yake
yote wakati wa kupigani uhuru. Mwezi Juni 1968 maulidi mbili katika usiku mmoja
zilisomwa kuadhimisha kuzaliwa kwa Mtume (SAW). Maulidi moja ilisomwa
Mnazi Mmoja na nyingine Ilala. Chanzo cha haya yote ni kuwepo kwa kutoelewana
kati ya viongozi wa Waislam waliokuwa wanajiona kuwa ni ‘wazalendo’ wafuasi wa
TANU na wale na wale viongozi wa EAMWS ambao kambi nyingine ilikuwa ikiwaona
kama wapinzani wa TANU. Yale maulidi yaliyosomwa Ilala yalihudhuriwa na
viongozi wa EAMWS na yalipata watu wengi na yakafana sana ukilinganisha na yale
maulidi ya Mnazi Mmoja, ya wafuasi wa TANU. Uongozi wa TANU ulitishika na hali
hii iliyokuwa ikijitokeza kwa maana ilikuwa inaonyesha kuwa chama kilikuwa
kinapoteza wafuasi ambao walikuwa wakijiunga na kambi ya Tewa na Titi
iliyokuwa ikisemekana ipo dhidi ya Nyerere. [9]
Pambano
kati ya Nyerere, Tewa na Bibi Titi, 1968
Ili
tume ya uchunguzi ya Waislam iweze kufanya kazi yake vyema na bila upendeleo,
ilikuwa lazima ile tume ya Waislam iiombe serikali izuie propaganda iliyokuwa
ikiendeshwa na wale waliokuwa wamejitenga na EAMWS, wakitumia jukwa la radio ya
serikali na magazeti ya TANU. Tume ya Waislam ilikutana na Waziri wa Habari na
Utangazaji, Hasnu Makame, ofisini kwake tarehe 20 Novemba, 1968, kujadili
tatizo lile. [10] Hii haukusaidia kitu.
Propaganda dhidi ya uongozi wa EAMWS iliendelea kwa nguvu zote. Mashambulizi
kutoka pande tatu yaliyopangwa vyema yalikuwa kazini. Benjamini Mkapa akitumia
gazeti la Nationalistataandika habari yoyote ya Adam Nasibu, Martin
Kiama akitumia Radio Tanzania atatumia habari ile kama habari
muhimu katika radio na habari hiyo itatangazwa kutwa nzima huku ofisi ya rais
ikiwa kimya kwa fitna ile. Lile kundi la waliojitenga na umma wa Waislam Adam
Nasibu akiwa kama msemaji wao mkuu wakawa wakati mwingine kwa mastaajabu
makubwa wakawa wanakiuka hata misingi ya akida ya Tanzania, wakitoa madai ya
ubaguzi a rangi, wakikazania lazima EAMWS ivunjwe. Adam Nasibu alinukuliwa na The
Nationalist akisema kuwa:
Waislam
lazima wafahamishwe kwa nini East African Muslim Welfare Society iwe na katiba
ambayo inaendana na mwelekeo wa nchi. Hatujui nafasi ya Aga Khan katika nchi
yetu na ndiyo maana tunamkataa. [11]
Lakini
cha kushangaza zaidi ilikuwa ule ukimya wa serikali kuhusu matakwa ya kundi la
Adam Nasibu lililokuwa likidai kuwa Waislam wachanganye dini na siasa katika
suala hili, wakati ilikuwa ikijulikana wazi kuwa kufanya hivyo ni mwiko mkubwa
katika siasa za Tanzania. Haya yote mbali, lile la kushangaza hasa na
kitu ambacho kilikuwa kigeni katika Tanzania ilikuwa yale madai ya kuingiza
ubaguzi wa rangi katika siasa za Tanzania. Ilikuwa inastaajabisha kuona
magazeti ya TANU yaliyokuwa na sifa ya kuheshima haki za binadamu yakichapisha
na kuzipa uzito wa hali ya juu habari za kundi dogo la Waislam waliokuwa
wanawalaumu Waislam wenzao wa Kiismailia kwa kutozaliwa weusi. Miaka kumi
iliyopita watu wa Tanganyika, Waislam wenyewe waliokuwa ndiyo walioanzisha na
kuijenga TANU, walipambana vikali dhidi ya siasa za kibaguzi za Zuberi Mtemvu
na chama chake cha African National Congress. Mtemvu alishindwa na matokeo yake
ikawa Tanganyika kuwa na serikali ya watu wote isiyobagua rangi na ikitawala
raia wa rangi zote kwa misingi ya haki. Kwa ajili hii nchi ikawa haina msuguano
kwa ajili ya ubaguzi wa rangi. Haya matokeo mapya yalikuwa hayaendani na
misingi ya TANU.
Ilipofikia
hali hii, rais wa EAMWS, Tewa Said Tewa na makamo wake Bibi Titi Mohamed,
waliamua kulipeleka suala hili kwa Juluis Nyerere, Rais wa Tanzania na
mwenyekiti wa TANU, chama tawala. Watu hawa walikuwa wakichekeana jino pembe.
Lakini ili tuelewa chanzo cha uadui huu inatulazimu turudi nyuma hadi mwaka wa
1963, katika siku za mwanzo za uhuru, katika mkutano wa Halmashauri Kuu ya TANU [12]uliofanyika Ukumbi wa Karimjee.
Kama
ilivyokwishaelezwa hapo mwanzoni kuwa mwaka 1963 ulikuwa mwaka wa mambo mazito.
Ilikuwa ndiyo mwaka ambao Kanisa Katoliki liliteua wagombea wake wapambane na
wagombea wa TANU waliokuwa Waislam katika uchaguzi wa serikali za mitaa kule
Kigoma na Bukoba. Ulikuwa ndiyo mwaka ambao Rais wa TANU, Nyerere alipombana na
EAMWS kupitia Bilali Rehani Waikela. Mwaka wa 1963 ndiyo ulikuwa mwaka ambao
Halmashauri Kuu ya TANU ilivunja Baraza la Wazee wa TANU lililokuwa
limetawaliwa na Waislam kwa madai kuwa baraza hilo lilikuwa ‘likichanganya dini
na siasa’. Mwaka 1963 ulikuwa mwaka muhimu kwa Halmashauri Kuu ya TANU kwa
sababu ilikuwa mwaka ambao ilifanya maamuzi nyeti ya kidini. Mwaka ule Bibi
Titi na Nyerere walishambuliana kwa maneno ndani ya Halmashauri Kuu yA TANU
kuhusu jambo jingine tena la dini lililokuwa likihusu EAMWS.
Wanakamati
wawili wa Halmashauri Kuu ya TANU, Selemani Kitundu na Rajab Diwani, waliiomba
Halmashauri Kuu ya TANU imjadili Aga Khan na nafasi yake kama patroni wa EAMWS.
Kitundu na Diwani walidai kuwa wana habari Aga Khan anataka kuitawala
Tanganyika kupitia Waislam na EAMWS. Kwa ajili hii basi wakapendekeza EAMWS
ifungiwe. Nyerere aliwaunga mkono Selemani Kitundu na Rajab Diwani. Bibi Titi
akasimama kishujaa dhidi ya Diwani, Kitundu na Nyerere, akasema hakuna kati yao
aliyekuwa na haki ya kuifungia jumiaya yoyote ya Waislam. Kama walikuwepo watu
ndani ya EAMWS ambao walikuwa wanakwenda kinyume na sheria basi watu hao
wapelekwe mahakamani na sheria ichukue mkondo wake. Bibi Titi akaendelea na
kusema kuwa EAMWS imekuwepo kabla ya TANU na siku zote imekuwa ikitoa huduma
kwa Uislam. Inasemekana hasira zilipanda na kukawa na kutoleana maneno kati ya
Bibi Titi na Nyerere. Bibi Titi akamwambia Nyerere yeye hamuogopi yeyote ila
Allah.
Tuhuma
zile dhidi ya Aga Khan na EAMWS hazikuweza kuthibitishwa na Halmashauri Kuu ya
TANU ikaliacha jambo lile kwa wakati ule. Lakini Nyerere alikuwa amefedheheka.
Kuanzia hapo akajenga chuki dhidi ya Bibi Titi na kumweka Rajab Diwani na
Selemani Kitundu karibu yake. Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1965 Bibi Titi na
Tewa wakapoteza viti vyao kwa watu ambao walikuwa hata hawafahamiki – A.M.
Mtanga na Ramadhani Dollah. Iliaminika kuwa Nyerere alikuwa anahusika na
kuanguka kwa Bibi Titi na Tewa. Kuanzia hapo mambo yakawa dhahiri. Nyerere
alikuwa amewatangazia vita wote wawili, Bibi Titi na Tewa. Nyerere alikuwa sasa
ana imani kuwa wale maadui zake wawili walikuwa wamekwisha kisiasa. Lakini
kilichokuwa kkimuudhi Nyerere zaidi ilikuwa taarifa ambazo alikuwa akizipata
kuwa Tewa alikuwa akipewa mapokezi makubwa sana na Waislam katika ziara zake
huko mikoani kama rais wa EAMWS. [13] Sasa
mwaka wa 1968, Bibi Titi na Tewa walipokwenda kumuona Nyerere kuhusu jambo
lililokuwa linawahusu Waislam, Nyerere alikuwa amejitayarisha vyema. Kiwanuka
ameueleza mkutano huu vizuri sana:
…Viongozi
hawa wawili wa Waislam walimueleza Mwalimu masikitiko yao jinsi radio ya
serikali na magazeti ya TANU yalivyokuwa yakiandika habari kuhusu matatizo yale
ya Waislam. Walidai
kuwa TANU ilikuwa ikichanganya dini na siasa. Waliokuwa wakimtahadharisha
kuhusu jambo hilo hawakuwa wengine ila marafiki zake wa zamani na wa
kutumainiwa, Tewa na Bibi Titi. Marafiki wa kutumainiwa kwa sababu ilikuwa Titi
aliyemuunga mkono Nyerere katika siku za mwanzo za TANU, pale Suleiman Takadir
– mmoja wa wazee wa TANU – aliposema kuwa TANU ilikuwa na Ukristo kama Mwalimu
na Rupia, rais na makamo wake walivyokuwa Wakristo. Yeye mwenyewe akiwa
Muislam hasa, aliipatia TANU ushindi kwa kuthibitisha kuwa Tanzania, Tanganyika
kama ilivyokuwa ikijulikana wakati ule, ilikuwa mbele, na Uislam unafuata
nyuma. Leo, alikuwa anazungumzia jambo ambalo yeye mwenyewe alilishinda katika
miaka ya 1950. Jibu walilopata kutoka kwa Mwalimu lilikuwa la kusisimua.
Mpashaji wangu habari anasema lilikuwa jibu la mkato. ‘Mmeamua kunipiga vita,
jiandaeni.’ [14]
Mwalimu Nyerere alikuwa anawaambia Tewa Said Tewa na Bibi
Titi Mohamed uso kwa macho wajiandae kwa kile kilichokuwa dhahiri: vita ya
msalaba dhidi ya umoja wa Waislam. Sheikh Suleiman Takadir aliyaona haya na
aliiomba TANU toka mwaka wa 1958 pawepo na uhakika kuwa Wakristo ambao walikuwa
wanapanda migongo ya Waislam na kuchukua uongozi hawatakuja kuwafanyia uadui
Waislam pale Waislam watakapokuwa sasa wanataka kugawana madaraka ya kuongoza
nchi sawa na Wakristo baada ya uhuru. Tewa Said Tewa, muasisi wa TANU, waziri
katika serikali ya kwanza ya uhuru, balozi katika Jamuhuri ya watu wa China na
Rais wa baraza la Tanzania la EAMWS, pamoja na Bibi Titi, mwanamke
aliowakusanya wanawake wote nyuma ya Mwalimu Nyerere na TANU, walikuwa
wakisemwa na Nyerere kama vile watoto wadogo wa shule waliokuwa watukutu kwa
sababu tu, walikuja kumfahamisha Rais kuhusu kukiukwa kwa maadili ambayo
ilihitaji yeye ashughulikie mara moja na kutoa uamuzi.
Ulipofika mwezi Oktoba, ‘mgogoro’ ukachukua mwelekeo mpya
pale Makamo wa Rais wa Tanzania, Abeid Amani Karume, alipoishambulia EAMWS kuwa
ni chombo cha unyonyaji. [15] Kutokea
hapo Karume akawa anafanya mashambulizi na kutoa shutuma kwa EAMWS, wakati
mwingine akijaribu kufafananisha uhusiano wa EAMWS na Waislam katika mtazamo wa
Ki-Marxist, akidai kuwa jumuiya ile kilikuwa ‘chombo cha makabaila wakubwa na
kilikuwa chini yao kikiwanyonya watu wa chini’. [16] Mgogoro
ulipozidi kukua mashambulizi yakahama sasa kutoka EAMWS na kuhamia kwenye
mafunzo ya msingi katika Qur’an Tukufu. Katika mkutano wa hadhara Zanzibar,
Karume alitoa changamoto kwa Muislam yeyote ajitokeze bila ya woga kupinga
kauli zake mbili kuwa ‘Hakuna tofauti kati ya Uislam na Ukristo’, na ‘Kufunga
siyo lazima’.
Lakini juu ya mashambulizi dhidi ya uongozi wa
Waislam kutoka serikalini, Nyerere alikuwa hana uwezo wa kumgusa Mufti
Sheikh Hassan bin Amir. [17] Sheikh Hassan bin Amir alikuwa na nguvu
sana kiasi cha kwamba si Nyerere au yeyote yule kuweza kumgusa kwa wakati ule.
Sheikh Hassan alikuwa kwenye siasa kabla ya vijana waliokuwa katika TANU na
nafasi yake katika umma wa Kiislam na uzalendo wake ulikuwa hauna shaka. Sheikh
Hassan bin Amir aliingizwa TAA kwa mara ya kwanza mwaka 1950 na Abdulwahid
Sykes akiwa mwanakamati katika Kamati ndogo ya siasa ya TAA. Kwa ajili hii
basi, akawa mmoja wa wale waliotia sahihi ile memoranda iliyotayarishwa na TAA
kwenda kwa Gavana wa Tanganyika, Edward Twining kuhusu mabadiliko ya katiba ya
Tanganyika. TANU ilipoasisiwa, Sheikh Hassan bin Amir alikuwa akikiwakatia watu
kadi za TANU msikitini huku akidarsisha. Baadhi ya wanachama shupavu wa TANU
ambao Sheikh Hassan bin Amir aliwaingiza katika TANU ni Sheikh Mussa Rehani
ambae alipewa kadi yake ndani ya msikiti Kigoma. Wakati Nyerere alipokuja TAA
Dar es Salaam mwaka 1953, alimkuta Sheikh Hassan bin Amir mwenyeji katika
siasa. Baada ya uhuru Sheikh Hassan bin Amir alijiuzulu siasa, kutokana na
kauli yake alisema kuwa, ili awatumikie Waislam vyema.
Nyerere alifahamu fika kuwa haitakuwa rahisi kwake
kumweka Sheikh Hassan bin Amir kizuizini kama alivyofanya kwa Waislam wengine.
Sheikh Hassan bin Amir alikuwa ndiyo Mufti wa Tanganyika na Zanzibar na kwa
ajili hii alikuwa na hadhi kubwa katika umma wa Waislam. Halikadhalika haikuwa
rahisi kwa yoyote kumkiuka Sheikh Hassan bin Amir na kuchukua uongozi wa
Waislam.
![]() |
Bi. Titi Mohamed na Nyerere
Katika Miaka Yao ya Mwisho Duniani |
![]() |
| Titi Mohamed na Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi |
| Bi. Titi Mohamed na Kanyama Chiume na mkewe |
[1]Frank
Humplink ingawa baba yake ni Mzungu lakini katika mazungumzo yake na mwandishi
mara kadhaa bila ya dhamira alijinasibisha na Uchagga kuliko Uzungu. Kwa ajili
hii mwandishi ameamua kumtabulisha kamaMchagga.
[2]Mwandishi
alipomuhoji Frank Humplink kuhusu nyimbo ile alimfahamisha kuwa serikali
iliagiza askari waingie nyumba hadi nyumba kusaka ile santuri na ilipokutwa
ilivunjwa.
[3]Angalia Zuhra, 30
Machi, 1955.
[4]Angalia
barua katika TNA /57/A. 6/23.
[5]Angalia
Maria Nzomo, ‘Kenya: The Women’s Movement and Democratic Change’ in Lernado A.
Villon & Philip A. Huxtable, (eds.) The African State at a Critical
Juncture: Between Disintegration and Reconfiguration (Lynne &
Rienner, Colorado, 1998), uk. 167. Inasadikika kuwa wapo wanawake ambao
walishiriki katika harakati za ukombozi wa Kenya katika Mau Mau
lakini walioshika madaraka hawataki kuwapa hadhi wanazostahili kama mashujaa
wa uhuru. Halikadhalika shujaa kama Dedan Kimathi hajapewa heshima anayostahili
kama mzalendo aliyepigania uhuru wa Kenya na akanyongwa na wakoloni
wa ajili hiyo. Hadi leo kaburi lake badolipo ndani ya jela
aliyonyongewa. Kwa habari zaidi angalia, Willy Mutunga, Constitution
Making From The Middle Civil Society and Transition Politics in
Kenya, 1992 – 1997, SAREAT, Nairobi, 1999 uk. 1.
[6] Matawi ya TANU yaliyopigwa marufuku
yalikuwa: Korogwe, Handeni, Lushoto na Pangani. Kwa maelezo ya kina
angalia, Ulotu Abubakar Ulotu, Historia ya TANU, Kilimanjaro
Publications, 1980, uk. 77-87.
[7] Nyerere
alipokwenda Tabora mwaka 1988 kuadhimisha miaka thelathini ya ‘Uamuzi wa
Busara’, Ramadhani Abdallah Singo akiwa mtu mzima wa makamo alimuuliza Nyerere
vipi chama kimekuwa mwizi wa fadhila kwa kuwasahau wazalendo waliopogania uhuru
wa Tanganyika. Nyerere kuanzia pale kila alipokwenda aliwasifia mashujaa
waliopigania uhuru na akaagiza chama iwatafute viongozi waliokiongoza chama
kati ya mwaka 1954-1958. Hadi Singo na Kassongo wanafariki hakuna chochote
kilichofanyika.
[8] Kuna
utata katika kura zilizopigwa. Iliffe, A Modern History... akimnukuu
Martin Lowenkopf ‘Political Parties in Ugandaand Tanganyika’, M.Sc.
(Econ.) Thesis, University of London, 1961 amenukuu kura
thelathini na saba kuunga mkono kushiriki na ishirini na tatu zilipinga.
Abdallah Rashid Sembe alipohojiwa na mwandishi tarehe 6 Julai, 1988 alitoa
idadi ya kura kuwa thelathini na mbili ziliunga kushiriki na ishirini dhidi
yake. Hassan Issa, ‘Safari ya Tabora’ Taarifa ya mkutano wa mwaka 1958
uliofanyika toka tarehe 21/1/1958 mpaka tarehe 25/1/1958 TANU 51, CCM
Archives, anatoa idadi ya kura thelathini na saba kushiriki na kumi na moja
dhidi yake. Kwa maelezo zaidi juu ya Mkutano wa Tabora angalia Iliffe, ibid. uk.
556-557.
[9] Nyerere
alizidi kutishika pale mara baada ya maulidi yale yaliyofanikiwa, mwezi Julai,
1968 Tewa akifuatana na masheikh wawili, Athumani Manzi na Sheikh Minshehe
Mgumba akafanya safari ya kutembelea Dodoma, Kongwa, Mpwapwa, Kondoa,
Tabora na Kigoma. Huko kote Waislam walikuwa wakijitokezakwa wingi kumpokea
kiongozi wao. Tabora ulifanyika mkutano mkubwa uliohutubiwa na Sheikh Jumanne
Biasi na Rehani Bilali Waikela. Kigoma Tewa alifanyiwa mapokezi makubwa
akasindikizwa na magari hadi Ujiji msafara ukiongozwa na Sheikh Khalfani
Kiumbe. Katika ziara hizi Tewa alikuwa akifungua shule zilizokuwa zimejengwa na
EAMWS. Ilikuwa Kigoma ndipo Tewa Said Tewa alipoonyeshwa barua kutoka kwa Adam
iliyoambatanishwa na miniti za mkutano kati ya Sheikh Abdallah Chaurembo na
Sheikh Ramadhani Chaurembo akiuandikia uongozi wa EAMWS Kigoma akiwaomba
Waislam wajitoe kutoka EAMWS kwa sababu ilisoma maulidi Ilala. Aliporudi Dar es
Salaam Tewa aliufahamisha uongozi wa makao makuu kuhusu barua ile.
[10] Barua ya Mwenyekiti Halmashauri ya Uchunguzi
Mogogoro ya Waislam kwa Waziri wa Habari na Utangazaji, 21 Novemba, 1968.
[11] The Nationalist, nukuu kutoka kwa
Kiwanuka, uk.81.
[12] Maelezo kutoka mwanakamati wa Halmashauri Kuu ya
TANU ambae ameomba jina lake listiriwe.
[13] Mwezi Novemba 1967 Tewa Said Tewa alikuwa
amefanya ziara ya Mwanza na Bukoba iliyokuwa na mafanikio makubwa kwa
kuwa alifanya majadiliano na viongozi wa Waislam wa huko kama Sheikh Amin
Abdallah wa Mwanza, Sheikh Ali Migeyo na Sheikh Suedi Kagasheki wa Bukoba.
[14] Kiwanuka, uk.2-3.
[15] Ibid., p.81
[16] The Standard, 9th November
1968 nukuu kutoka Kiwanuka p. 81. Vilevile angalia The Standard, 20
November 1968.
[17] Sheikh Hassan bin Amir alianza kukosana na
serekali mara tu baada ya uhuru pale Kanisa Katoliki ilipotoa vitu vya
kukumbuka uhuru vilivyokuwa vimenakshiwa na picha za Kikristo. Sheikh Hassan
bim Amir alikereka na hili na hasa pale George Kahama, Waziri wa Mambo ya
Ndani, alipokwenda Italia kuweka uhusiano baina ya Tanganyika na Vatikano.
Kuanzia hapo, Sheikh Hassan bin Amir, kupitia Daawat Islamiyya na kwa kupitia
wanafunzi wake waliokuwa wameenea nchi nzima alianza kuandika khutba za
Ijumaa na kuzisambaza katika misikiti ya nchi nzima na khutba hizo zikawa
zinasomwa katika sala ya Ijumaa. Ujumbe wake kwa Waislam ulikuwa Waislam
watumie fursa iliyoletwa na uhuru kwa kujielimisha ili wagawane madaraka sawa
na Wakristo katika kuiendesha nchi. Sheikh Hassan bin Amir akaanzisha mfuko wa
elimu ambao Waislam walitakiwa kuchanga fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule. Kwa
ajili ya kuingia kwake kati pale Nyerere alipotaka kuivunja EAMWS, Sheikh
Hassan bin Amir akaonekana ni kikwazo kwa Ukristo kuukalia juu Uislam.



No comments:
Post a Comment