Wednesday, 1 January 2014

AHMED RASHAD ALI BINGWA WA PROPAGANDA ZA UKOMBOZI WA AFRIKA SEHEMU YA PILI

Ahmed Rajab (aliyekaa kitako) na Abdilatif Abdallah wakiwa Leipzig Ujerumani



Ilikuwa nia yangu yangu kungoja kidogo kabla sijaweka kipande kingine cha Ahmed Rashad Ali.

Lakini leo asubuhi nikapokea ujumbe wa maandishi kwenye simu yangu kutoka kwa kaka yangu Ahmed Rajab akisema kuwa anasubiri kipande kingine cha Ahmed Rashad apate kusoma.

Kwa heshima ya kaka yangu Ahmed sina budi lazima nikiweke hapa apate kusoma yeye na wasomaji wengine. Nitakuwa mtovu wa adabu kumchelewesha. Dunia ina mengi. Nikiwa kijana mdogo nilipokelewa na Ahmed Rajab London na akanifanyia makubwa. 

Allah atamlipa Insha Allah. 

Kaka yangu Ahmed kanionyesha mengi katika dunia ya uandishi na yeye mwenyewe akapata kutumia baadhi ya maandishi yangu katika gazeti lake maarufu Africa Analysis. Akanitia katika ulimwengu wa undishi ambao sikujua kama upo. 

Akanipeleka BBC Idhaa ya Kiswahili na nikafanyiwa usaili na Neville Harmes , mzee wa Kiingereza aliyekuwa Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC...akanipeleka kwa jamaa wengi kunijulisha hapo London.

Kafanya haya yote wakati akiwa wala hanijui vyema. Haya yote illikuwa barua tu ya mkono iliyomfikia kutoka Dar es Salaam iliyoandikwa na nduguye Ahmed Maulid akimwambia,''Mpokee huyu ndugu yetu.'' 

Hapa panatosha hiki ni kisa cha kujitegemea iko siku In Sha Allah nitakieleza kwa kirefu. 

Ahmed Rajab huniita mimi mdogo wake na kwa hakika Ahmed Rajab ni kaka yangu.

Nakuwekeeni hapa chini picha ambayo mimi naipenda na kila nikiitazama humkumbuka kaka yangu Ahmed Rajab.

Kwa heshima yake nakiendeleza kisa cha somo yake Ahmed Rashad Ali.


Studio za BBC Glasgow Scotland   June 1991 nikifanya kipindi kiitwacho
''Barua Kutoka Glasgow''



















AHMED RASHAD ALI BINGWA WA PROPAGANDA ZA UKOMBOZI WA AFRIKA 
SEHEMU YA PILI

Mr. Money alikuwa muongeaji mzuri na hidaya hii ilikuwa muhimu sana kwake kwa kupata taarifa ambazo aliziwasilisha kwa British Resident. Mazungumzo nyumbani kwa Mr.Money yalikwenda hadi usiku sana na walikuwapo watu wengine. Katikati ya mazungumzo Bamanga akatoka akaenda Raha Leo kuangalia endapo mpango ulikuwa ukiendelea kama walivyopanga. Bila kificho Bamanga akawa nae anagawa makaratasi. Bamanga alikuwa mtu jasiri. Huwezi kuwa mwana masumbwi ikiwa si  jasiri. Bamanga alikuwa haogopi kitu. Historia inasema kuwa Bamanga aliwahi hata kutupiana ngumi na Karume. Alikuwa mashuhuru Zanzibar kwa ajili ya ustadi wake katika ulingo. Watu wengi usiku ule walimwona akigawa yale makaratasi. Alipomaliza kugawa akaenda nyumbani lakini mapema asubuhi akaonekana anagawa makaratasi sokoni pakijulikana kama Soko Muhogo. Alipomaliza kasi ile akawa bado amebaki na makaratasi mengine haya akendanayo kwa mama yake aliekuwa akiishi nje ya mji kuyahifadhi. Inasemekana ilikuwa dhamira yake kuyagawa kwa watu hapo baadae. Haukupita muda kwa Bamanga kukamatwa. Kukamatwa kwake kukaipa vyombo vya usalama njia. Serikali ilijua Bamanga  hakuwa na akili ya kuweza kuandika shairi kama lile. Hapakuwa na shaka yoyote kuwa kulikuwa na mtu nyuma ya Bamanga. Siku iliyofuatia Rashad alikuwa mahakamani akisikiliza kesi kwa ajili ya kipindi katika radio. Wakati ule Rashad alikuwa ameajiriwa na Idara ya Habari kama mtangazaji Sauti ya Zanzibar. Kituo hiki kilikuwa kimeanzishwa mwaka wa 1951.

Rashad aliarifiwa kuwa alikuwa anatakiwa kwa haraka sana ofisini. Alipofika akaitwa ndani kwenye ofisi ya mkubwa wake.  Mle ndani akapewa mahubiri makali na afisa wa kikoloni. Alipewa mhadhara kuhusu hali ya usalam na tabia ya upole ya visiwani na watu wake. Akawekea mtego kuhusu nafasi iliyokuwa mbele yake kama kijana mdogo nafasi ambayo inaweza kuharibika kwa vitendo vya kijinga kwa kukaidi utawala wa sheria na mamlaka. Afisa yule baada ya kumaliza mhadhara wake akamuonyesha Rashad ile karatasi. Rashad aliichukua ile karatasi akaanza kuisoma kwa taratibu kama vile ndiyo kwanza anaitia machoni. Alikataa kuhusika na ile karatasi. Rashad akakamatwa pale pale.

Kesi ikaenda mahakamani. Bamanga na Rashad wakashitakiwa kwa kusambaza makaratasi ya uchochezi. Inasadikiwa hii ndiyo ilikuwa kesi ya kwanza ya uchochezi Zanzibar.

Mwanasheria wa Kiparsii, Parves Talati alimtetea Rashad. Rashad alishinda kesi ile. Talati na Rashad walikuwa wamesoma darasa moja.Talati alikuwa mwanasheria a kuheshimika na alipata kuchaguliwa kuwa Meya wa Zanzibar. Talati alijitolea kuwatetea washitakiwa hawa wawili bure. Alimwambia Rashad katika kesi hii watu muhimu ni mashahidi ambao walimuona Bamanga akigawa yale makaratasi ya uchochezi. Alimwambia Rashad kuwa hao ndiyo wenye kubeba hukumu ya kesi ile. Mdahoma ndiye alikuwa muendesha mashataka.

Hakimu alikuwa anafahamiana na Rashad. Walikuwa pamoja katika kamati nyingi za michezo na walikuwa hawakubaliani katika mengi. Rashad wakati wote alikuwa akipingananae. Kabla ya kesi kuanza hakimu akirejea katika migongano na misuguano baina yao alimwuliza Rashad kama alikuwa na pingamizi yoyote kwa yeye kuwa hakimu katika kesi yake. Rashasd akasema hana kipangamizi kwa yeye kusimamia kesi yake.

Kesi ikaanza na kila shahidi aliyesimama alipohojiwa na mshtakiwa alikataa kumwona Bamanga kwa macho yao akigawa yake makaratasi. Walipoonyeshwa taarifa zao ambazo walikuwa wameweka sahihi zao wakikubali kuwa walipokea makaratasi kutoka kwa Bamanga walisema walilazimishwa na askari kusema hayo waliyosema.

Hakimu alipokuja kutoa hokum yake aliwakemea askari kwa kushindwa kufanya upelelezi sawasawa na kwa kuwalazimisha mashahidi kutoa ushahidi wa uongo mbele ya mahakama. Aliitupa kesi ile nje ya mahakama na kuwavua Bamanga na Rashad na makosa waliyoshitakiwa. Hata hivyo Rashad akafukuzwa kazi kwa kwa utovu akiwa mfanyakazi wa serikali na kwa ajili hiyo kutoajiriwa tena katika serikali ya Zanzibar. Juu hayo hakuweza tena kuishi Zanzibar kwa kuwa ametuhumiwa kama mkomunisti. Rashad ikabidi sasa ahame Zanzibar kwa sababu mfumo ambao yeye alikuwa akiupinga kwa kificho sasa ulikuwa ukimpiga vita vya wazi. Walikuwa wamejaribu mbinu za kuhamasisha umma lakini watu wa Zanzibar kwa wakati ule walikuwa bado hawajawa tayari. Rashad alidhani kuwa kwa kuwa mbinu kama zile zilifanikiwa vizuri India zingeweza kuwa kufanya kazi hata Zanzibar. Mwamko wa umma ambao Bamanga  alidhani ungetokea haukutokea. Lakini nini hasa matokeo ya mkasa huu ambao kwa upande mmoja ulikuwa msiba na mwingine kichekesho. Si kama kila kitu kilikuwa bure. Kulikuwapo na mafanikio. Iliwadhihirikia watawala kuwa Zanzibar ilikuwa inabadilika na hali si shwari. Kwa wale ambao hadi pale walikuwa hawajajiingiza katika siasa walitambua kuwa umma ulikuwa unasubiri uongozi uliokuwa makini.

Lakini Bamanga na Rashad walishinda vipi kesi ile? Kinyume cha mambo ni kuwa si askari waliowatisha mashahidi. Alikuwa Bamanga ndiye aliyewatisha mashahidi. Miongoni mwa mashahidi alikuwa mtu mmoja akiitwa Mwanjia yeye ndiye hasa alikuwa mwenye ushahidi mkubwa katika kesi ile. Kabla ya kesi kuanza akiwa nje ya mahakama Mwanjia alifuatwa na mtu ambae hajapata kumuona hata siku moja. Yule mtu akatoa bisu kubwa kutoka kwenye kanzu yake akamwonyesha Mwanjia. Akamwambia endapo atatoa ushahidi mahakamani ambao utamkandamiza Bamanga basi ajihesabu keshakufa. 

Rashad hakukubali kushindwa.  Alijua kuwa mapambano lazima yaendelee liwalo na liwe. Aliandika barua ya kurasa sita kwa Gamala Abdel Nasser wa Misri akamwomba kazi katika radio ya Misri iliyokuwa ikimilikiwa na  serikali ili autangazie ulimwengu dhulma inayofanywa na Uingereza katika Afrika ya Mashariki. Katika  barua ile Rashad akamweleza Nasser kuwa asimwandikie Zanzibar ila kupitia ubalozi wa Misri Bombay kwa taarifa za  safari yake kwenda Misri. Rashad akiandamwa na shutuma za ukomunisti alikuwa akifuatiliwa. Hakuweza sasa kusafiri kupitia Kenya ambayo ilikuwa koloni la Mwingereza kule angeweza kukamatwa. Baada ya miezi kupita Nasser akamwandikia Rashad na akamwambia aende India ambako mipango ya safari yake ya Cairo itashughulikiwa na Ubalozi wa Misri Bombay. Rashad alisafiri kwa meli kuelekea India Novemba 1952 na baada ya kukaa pale kwa miezi mitatu wakati ubalozi unatayarisha mipango ya safari yake kwenda Cairo. Rashad aliondoka Bombay Februari 1953 kuelekea Cairo. Wakati Rashad akiwa Bombay alikutana na rafiki yake aliesomanae darasa moja Anjuman Islam High School Bombay katika miaka ya 1940 sasa mcheza senema maarufu Dilip Kumar. Wanaharakati wa HK Jimmy Ringo, Said Njugu na Bamanga baadae wakaja kuwa viongozi wa vyama vya wafanyakazi Zanzibar miaka ya mwisho ya 1950.

ZNP walifungua ofisi ubalozi Cairo juma la kwanza baada ya Zanzibar kupata uhuru na Ahmed Nassor Lemki Mwarabu mwenye asili ya Zanzibar akawa balozi na Ali Khamisi akawa First Secretary. Ali Khamisi alikuwa akikerwa sana na msimamo wa Ahmed uliokuwa dhidi ya Waafrika. Ahmed Lemki alizaliwa Zanzibar mwaka wa 1929 kutoka ukoo tajiri sana. Wazazi wake walimpeleka Misri kusoma akiwa na umri wa miaka kumi na alikaahuko kuanzia mwaka wa 1939 hadi 1951. Mwaka 1948 Lemki alikuwa katika mapambano dhidi ya uzayoni na akajiunga na vuguvugu lililokuwa likimpinga Mfalme Farouk. Alikamatwa na kuhukumiwa kifungo cha miaka miwili jela. Alikuwa mwandishi hodari na aliuwa na uwezo mkubwa katika mbinu za propaganda. Aliporudi Zanzibar akawa mwanachama wa Arab Association. Lemki alirudi Zanzibar mwaka 1953 na akaanzisha chama Zanzibar National Union (ZNU). Chama hiki hakikufuzu kwa kuwa wasomi waliokionga mkono wakijitoa baada ya serikali kutoa waraka ambao ulikuwa unazuia wafanyakazi wa serikali kujihusisha na siasa. Lemki akawa mhariri wa Al Falaq na hili lilikuwa gazeti lenye sauti. Mwaka 1954 Lemki na viongozi wenzake walikamatwa na kushtakiwa kwa kosa la ‘sedition’ na walipigwa faini kubwa sana.

Itaendelea...

No comments: