Fikra Gani Ilikuwapo kwa Waafrika Waasia na Wazungu Kabla
ya Kuundwa kwa TANU?
Kwa hakika ni kitendawili kikubwa ikiwa utakaa chini na
kuwaza kuhusu historia ya TANU. Wanahistoria wetu wamepwapuuza kabisa wazalendo
waliokuwakatika harakati kabla ya Nyerere. Binafsi nimeulizwa maswali mengi
katika kila muhadhara niliofanya ndani na nje ya nchi kuhusu mchango wa Nyerere
katika kuunda TANU. Wanataka kujua palipitika nini hata ikawa TANU inanasibishwa
na Nyerere peke yake? Wakati mwingine hutoa jibu na wakati mwingine nikiwa
nimechoka husema swali hilo lielekezwe kwenye CCM (Chama Cha Mapinduzi) kwa kuwa wao
ndiyo warithI wa TANU. Kama wamerithi TANU basi watakuwa wamerithi na historia
yake. Miaka michache iliyopita palikuwa na mjadala mkali sana katika Jamii
Forum kuhusu hili. Nimepita katika kumbukumbu zangu na nimekuta jibu
nililotoa kwa mmoja wa wanajamvi wa JF. Ningependa na wasomaji wangu nanyi
muone nilisema nini.
Hali ya TAA Makao Makuu New Street, 1950
Kueleweka kwa nini Abdulwahid alimuunga mkono Nyerere
inahitajika uchambuzi kuelewa siasa za mfumo wa kikoloni katika Tanganyika.
Mwaka wa 1951 Abdulwahid Sykes na Hamza Mwapachu walipokuwa wakishughulika
kuifufua TAA, walijiwa na Ivor Bayldon, [1] Brig. Scupham na V.M.
Nazerali kuombwa kuunga mkono kuundwa kwa chama cha kisiasa kitakachojumuisha
Watanganyika wa rangi zote. Hawa walikuwa wajumbe wa Baraza la Kutunga Sheria.
Bayldon alikuwa mlowezi tajiri kutoka Nyanda za Juu za Kusini na alikuwa
amehamia Tanganyika kutoka Afrika ya Kusini. Wajumbe wa Kiafrika wa Baraza la
Kutunga Sheria walioliunga mkono wazo hili walikuwa Chifu Kidaha Makwaia na
Liwali Yustino Mponda wa Newala [1].
Watu wengine mashuhuri walioshauriwa na kuombwa kuunga mkono chama hiki
walikuwa: Dr Joseph Mutahangarwa, Chifu Abdeli Shangali wa Machame, Chifu Mkuu
Thomas Marealle wa Marangu, Chifu Adam Sapi Mkwawa, Chifu Haruna Msabila
Lugusha, Dr Wilbard Mwanjisi, Abdulkarim Karimjee, Dr Vedasto Kyaruzi, Liwali
Juma Mwindadi, H.K. Viran, Stephen Mhando, Ally Sykes na Dossa Aziz [1].
Huu ulikuwa mchanganyiko wa Wazungu ambao tangu hapo
walikuwa raia wa daraja la juu, baadhi yao kama Bayldon walikuwa walowezi;
machifu kama vile Marealle, Waafrika
wasomi kama Mwapachu; tabaka ya
wafanyabiashara wa Kiasia kama Karimjee na watu wa mjini kama Dossa Aziz na
Juma Mwindadi. Wote hawa walikuwa
viongozi waliokuwa na wafuasi katika jumuiya zao. Katika barua Nazerali
aliyomtumia Ally Sykes miaka miwili baada ya kudhihiri kuwa chama kile
walichokusudia kisingeweza kuundwa, Kwenye sehemu moja alikuwa na haya ya
kueleza: ëHaja kubwa ilikuwa kuandaa kikundi cha watu walio wakweli, waaminifu
na wenye imani katika maendeleo ya watu katika nchi yetu, pamoja na fursa sawa
kwa wote.
Abdulwahid wakati huo akiwa katibu pamoja na wanachama wa
TAA wasingeweza kukubali wazo kama hilo. Ingawa kwa kiasi fulani malengo ya
chama hicho kilichokusudiwa yalionekana yanafanana na malengo ya wananchi hivyo
kudhihirisha barabara kile ambacho TAA ilikuwa ikikipigania, Waafrika
wasingeweza kuachia azma ya wa Tanganyika kwa dhamira njema ya wasiokuwa
Waafrika na ambao walikuwa wakishirikiana bega kwa bega na serikali ya
kikoloni. Ilikuwa dhahiri kuwa Wazungu na Waasia nchini Tanganyika hawakutaka
kukubali kuwa Tanganyika kwa hali yoyote ile ilikuwa nchi ya Waafrika. Kwa TAA
kukubali kuundwa chama cha siasa kitakachojumuisha mataifa yote, kulikuwa sawa
na kuyaweka maslahi ya Waafrika chini ya watu wachache. Miaka michache nyuma
wazo kama hilo chini ya kile kilichojulikana kama Capricon Society lilianzishwa
na wakoloni katika maeneo ya Tabora ambako kulikuwa na idadi kubwa ya Waafrika
wasomi, wengi wao wakiwa Waalimu. Imani ya Capricon Society ilifungamana na
dhana ya ëuhuru kwa Waafrika waliostaarabikaí. Stephen Mhando aliyekuwa Dar es
Salaam na akiwasiliana na George Magembe mjini Tabora alituma barua kwa uongozi
wa TAA huko akiwatahadharisha juu ya mtego wa na Capricon. Ilikuwa dhahiri kuwa
Tanganyika wakati ule ilikuwa ikitafuta mwelekeo wa kisiasa na haikuwa TAA peke
yake iliyokuwa ikishughulika kutaka kuonyesha njia.
Mara baada ya Nyerere kuchukua uongozi wa TAA chama
kikaanza kusinzia, ushupavu na bidii iliyokuwepo wakati wa uongozi wa Abdulwahid vilitoweka. Kwa hakika
ilikuwa wakati mmoja tukatika historia ya Dar es Salaam ambapo mkristo Erikah
fia, alikamata bendera dhidi ya serikaly ya kikoloni. Nyerere alikuwa akikaa
nje ya mji na alikuwa akija Dar es Salaam mwishoni mwa juma tu. Kwa kiasi
fulani hii iliathiri shughuli za chama. Kwa muda wanachama walionekana kama
wamepoteza hamu ya chama. Wajumbe wa kamati ya utendaji mara nyingine
hawakutokea kwenye mikutano ijapokuwa Dossa aliwapitia majumbani kwao na gari
yake kuwachukua.
Dossa anakumbuka kuwa alikuwa akisimama nje ya nyumba ya
mwanakamati na kupiga honi. Mtoto au mke wa mwanakamati angetoka mlangoni kutoa
habari kuwa hakuwapo, katoka ilhali yupo ndani. Kwa muda kidogo ilionekana kama
Nyerere alikuwa kikwazo cha maendeleo ya TAA. Na huu ndiyo ulikuwa mwendo wa
TAA, nguvu yake ilikuwa ikitegemea uwezo wa viongozi wake. Awamu ya kwanza ya
uongozi wa Kleist Sykes na Mzee Bin Sudi katika makao makuu TAA ilipiga hatua
kubwa. Vivyo hivyo katika zama za Ali Juma Ponda na Hassan Suleiman katika tawi
la Dodoma, TAA ilikuwa ikisikika sana na uongozi wake uliheshimiwa hata nje ya
Tanganyika. Abdulwahid alikuwepo kama makamu wa rais lakini alipendelea kumwona
Nyerere akiendesha ofisi na kufanya maamuzi yake mwenyewe kama rais. Akakihofia
kufa kwa chama, Abdulwahid aliwataka shauri viongozi wenzake wa ndani katika
TAA - Ally, Dossa, Tewa na Rupia kuwa kipi kifanyike ili kudhibiti hali ile
iliyojitokeza. Ilikuwa dhahiri tatizo lilikuwa ni katika kubadilisha uongozi.
Wanachama walikuwa hawana imani na uongozi mpya katika ngazi ya juu. Hili
linaweza kueleweka ikifikirika kuwa ilikuwa ni miaka mitatu tu huko nyuma
wakati Abdulwahid na Dr Kyaruzi walikifufua baada ya kupoteza mwelekeo baada ya
Vita Kuu ya Pili. Iliamuliwa kuwa wazee Waislam wa mjini Dar es Salaam waombwe
kumuunga mkono Nyerere.
Wazee walifatwa na wakaelezwa kuwa uongozi wa TAA ulikuwa
umemkubali Nyerere kama rais wa chama kama sehemu ya mpango wa kuigeuza TAA
kuwa chama cha siasa cha umma Abdulwahid
aliwaeleza wazee, miongoni mwao masheikh, kuwa nchi ilikuwa katika awamu yake
ya mwisho ya harakati ambayo ilihitaji kuungwa mkono na kila Mwafrika wa
Tanganyika bila kujali dini yake wala kabila. Hawa wazee walikuwa wanachama wa
TAA lakini vilevile walikuwa wanachama au viongozi katika vyama vyao vya
kikabila kama vile Batefera Union chama cha Wamanyema kilichokuwa kikiongozwa
na Mzee bin Sudi, na Zaramo Union chini ya uongozi wa Makisi Mbwana. Baadhi ya
wanachama waliokuwa katika vyama hivi walikuwa vilevile wanachama wa Al
Jamiatul Islamiyya. Abdulwahid aliwaambia wazee kuwa makao makuu ya TAA
yaliwahitajisana kuunga mkono chama, pamoja na wasomi kama Julius Nyerere
waliochukuliwa kuwa watiifu kwa utawala wa kikoloni. Hawa wanaodhaniwa kuwa watiifu kwa utawala wa
kikoloni ndiyo wanaofaa sana kugeuzwa waipinge serikali inayowadhulumu
wananchi.
Wazee waliafiki ushauri huu na wakaanza kumjenga Nyerere
kama kiongozi wa kuwasemea na kuwaunganisha Waafrika wote wa Tanganyika.
Mwanafunzi mmoja wa Mufti Sheikh Hassan bin Amir anakumbuka kuwaona Abdulwahid,
Dossa Aziz na Nyerere mara kadhaa katika miaka ya mwanzoni ya 1950 wakija
kuonana na sheikh katika madrassa yake Kariakoo, Amani Street, nyumba nambari
36. Kwa kawaida Abdulwahid, Dossa Aziz na Nyerere walipokuja kumwona Mufti,
Sheikh Hassan Bin Amir alikuwa akivunja darsa na kuwapa ruhusa wanafunzi wake
ili upatikane utulivu wa maongezi. Kwa kawaida mashauriano yalikuwa yakifanyika
mle mle ndani ya madrasa, Abdulwahid, Dossa na Nyerere wakiwa wamekaa chini
kwenye jamvi wamekunja miguu. Wazee wengine mashuhuri waliomuunga mkono Nyerere
walikuwa Sheikh Suleiman Takadir mwanachuoni wa Kiislamu aliyeelimika sana,
akijulikana zaidi kwa jina la utani ëMakariosí, Jumbe Tambaza, mzee aliyekuwa
akihodhi ardhi kubwa pale mjini; Mshume Kiyate, mzee muuza samaki aliyekuwa na
kipato kizuri; Mwinyijuma Mwinyikambi, mzee aliyekuwa na viunga vya minazi na
miembe; Rajabu Diwani, seremala hohe hahe lakini aliyejaaliwa ufasaha mkubwa wa
kuzungumza; Makisi Mbwana, kiongozi wa Wazaramo mjini Dar es Salaam; Sheikh
Haidari Mwinyimvua, fundi cherehani na mtu mwadilifu; Iddi Faizi Mafongo na Idd
Tosiri ndugu wawili Wamanyema na binamu wa Sheikh Mohamed Ramia wa Bagamoyo
Khalifa wa tariqa ya Qadiriya. Iddi Faizi akiwa mweka hazina wa Al Jamiatul
Islamiyya na Iddi Tosiri mwanachama shupavu); Iddi Tulio, mzee mwenye heshima
zake, Mashado Ramadhani Plantan, mhariri na
mmiliki wa gazeti la Zuhra na kaka yake Schneider Abdillah Plantan,
watoto wa Affande Plantan na wazee wengine wengi wa mjini.
1 comment:
Sheikh Mohamed said hongera kwa kutuletea Blog yenye manufaa kwa wote. Sisi tuliokuwa mbali na nyumbani tumeikubali na imeleta picha kamili ya hadithi tulizokuwa tukihadithiwa na mama zetu. Simulizi kama za historia ya fikra za Waafrika, Waasia na Wazungu kabla ya kuundwa kwa TANU zimeleta kumbukumbu za hao watu waliyowataja. Majina ya mababu kama Abdulwahid na Ally Sykes, Hamza Mwapachu, Liwali Yustino Mponda, Mzee Tewa, Mzee Dossa, Mzee Rupia, Makisi Mbwana, Chifu Thomas Marealle, Chifu Haruna Msabila Lugusha leo hii yameleta furaha na simulizi nyingine nyingi hapa nyumbani. Shukran. Ali K, Dronten, The Netherlands.
Post a Comment