Tuesday, 7 January 2014

Mwalimu Athmani Khalfani Mrindoko Mwalimu wa Shule ya Msingi Lwande Kosa Lake Kusomesha Wanafunzi Qur'an na Kukataa Kuchakachua Mitihani



Mwalimu Athmani Khalfan Mrindoko
Mwalimu wa Shule ya Msingi Lwande
Al Shabab wa Kufikirika
Mwalimu Athmani Khalfani Mrindoko ni mwalimu wa shule ya msingi Lwande moja ya vijiji vilivyoshambuliwa kwa tuhuma za ugaidi.

Mwalimu Athmani ni mwalimu mwajiriwa na serikali kusomesha masomo ya kisekula lakini kwa mapenzi yake katika Uislam kwa kuwa walimu wa somo la dini ya Kiislam Shule za Msingi hakuna yeye hujitolea kuwasomesha wanafunzi hawa na kuwatungia mitihani.

Kisa chake ni kisa cha kusikititisha na kuhuzunisha.

Siku za nyuma Mwalimu Athmani alifatwa na walimu wenzake akaelezwa kuwa imetoka amri juu kuwa walimu washirikiane kuwafaulisha watoto darasa la saba kwa kuwakokotolea wanafunzi majibu ya mtihani wa mwisho wa darasa la saba ili kunyanyua ufaulu wa shule na hatimaye wilaya. 

Mwalimu Athmani akakataa hili kwa misingi ya Uislam kuwa hicho kitendo ni ghushi yaani udanganyifu.
Udanganyifu huu ukakwama na sababu ni yeye Mwalimu Athmani.

Hapa ndipo zilipoanza chuki dhidi yake.

Sasa lilipotokea sakata la Lwande askari waliovamia kijiji kwa madai ya kupambana na Al Shabab Mwalimu Athmani akakamatwa, kupigwa na kufunguliwa kesi ya kujeruhi Mahakama ya Handeni.

Mwalimu Athmani sasa hivi ni masikini.

Alipoachiwa gerezani kwa dhamana alikuta nyumba yake imevunjwa na vitu vyake vyote vimeibiwa.

Huyu ndiye ''gaidi'' anaeshirikiana na Al Shabab.

Mwalimu muadilifu anaesomesha watoto kitabu cha Allah.

Mwalimu Athmani Khalfan Mrindoko ''Al Shabab wa Kufikirika.''

Haya ni machache.
Yapo mengi katika dhulma hii ya kumfanya mtu akabubujikwa na machozi.

No comments: